Hukujua Kuwa Michuzi Anaimba Sauti ya Nne?
Michuzi sio tu ana ujuzi wa kupiga picha bali pia ni mwimbaji mashuhuri sana hasa akiwa nchi za nje. Katika picha hii Watanzania tuliokuwa katika mkutano kuhusu utandawizi na demokrasia katika jiji la Helsinki, Ufini mwezi Septemba, tunatumbuiza. Siku hii ilikuwa ndio mwisho wa mkutano. Tukiwa katika tamasha la kuaga wana mkutano, Mama Maria Shaba ghafla alitufuata mimi na Michuzi nje. "Watanzania lazima tuwakilishe."Nikamuuliza, "Tuwakilishe vipi?"
Akasema, "Toka tuje wanaoimba na kutumbuiza ni Wafini, kwani sisi hatuna sauti? Lazima tukaimbe."
Basi akatukusanya Watanzania mmoja mmoja. Hakuna kukataa. Hao jukwaani. Mnajua tuliimba wimbo gani? Buni....tuliimba Malaika. Michuzi akiwa ndio sauti ya nne. Katika picha unamuona Mama Shaba akiwa ameshika kipaza sauti. Pia unaweza kumuona Mama Mwingira wa Tango kushoto kwa Maria Shaba. Mimi nadhani nilikuwa naimba sauti ya 60! Baada ya kumaliza wimbo wa Malaika, tuliaga jukwaa, huku tukishangiliwa kwa nguvu, kwa wimbo wa Bob Marley: Get Up, Stand Up. Wimbo huu ndio wimbo rasmi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.











