12/09/2005

Mungu Wabariki Viongozi wa Afrika! Ati Nini??

Wakati ambapo Tanzania haijawahi kutawaliwa, tunaambiwa kuwa tarehe kenda Desemba ni sikukuu ya uhuru wa Tanzania! Sasa katika kukumbuka siku hii, Mti Mkubwa (Fidelis Tungaraza), ambaye tunamfahamu kwa changamoto zake, anatupa tafakari kuhusu wimbo wetu wa taifa. Je ni kweli tunataka mungu awabariki viongozi wa Afrika kama tusemavyo tunapoimba wimbo huo? Soma aya toka kwa Fidelis. Nimezipata toka kwenye waraka pepe aliotuma kwa watu kadhaa akiwemo mwanablogu Da Mija. Nabandika hapo chini:


"Miye naupenda sana wimbo wa taifa wa Tanzania (Mungu Ibariki Afrika). Wimbo huu siye Watanzania tumeukopa toka Afrika ya Kusini. Nyimbo hii ni nzee sana ilitungwa kunako mwaka 1897 kwa hiyo una miaka takribani mia moja na kumi na moja! (111)! Muziki wa nyimbo hii ni utunzi wa Hayati Enoch Sentonga, ambapo maneno yake yalitungwa na Hayati Enoch Sentonga na baadaye yakaja kukarabatiwa na Mshairi Samuel Mqhayi. Wimbo hatujaukopa Watanzania tu na Wazambia nao na wazimbabwe hali kadhalika. Lakini sijui kwa sabau gani Wazimbabwe waliuacha wimbo na kuchukua mwingine.

Wimbo huu huwa unanipa na kunitoa raha pale unapofika kwenye mstari wa WABARIKI VIONGOZI WAKE! Ukifika hapo huwa unanikumbusha sura za viongozi walionuna wakiwa wamesimama pale mein stend, neshino stedium, huku askari wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na chipukizi wa chama wakiwa wamekauka juani na saluti kali. Halafu na Watanzania wapenda amani na utulivu, wafanyakazi, wakulima na "wazururaji" wakiwa wametanda kwenye sehemu zingine za uwanja wakishiriki kwenye hiyo ghafla aidha kwa ridhaa zao au vinginevyo. Miujiza ya Tanzania Mei Dei au Saba Saba wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na hai skuli wote wanashiriki kikamilifu!

Turudi kwenye Mungu Ibariki Afrika, hususani pale kwenye mstari wa WABARIKI VIONGOZI WAKE. Hapo nadhani ndipo Watanzania tulipopewa uwezo wa pekee wa kuweza kumtia kizunguzungu Mwenyezi MUNGU! Maanake Mwenyezi Mungu akiwatazama hao viongozi tunaomuomba awabariki Mwenyezi Mungu mwenyewe anapata kizunguzungu. Lakini dua letu siyo kama linaishia kwa viongozi wetu wa Tanzania pekee yake bali tunawaombea na majirani zetu kama Waganda wakati ule wakiwa na Idd Amin Dada, Malawi na Dr Hastings Kamuzu Banda, Zaire na Mobutu Sese Seko Kuku Mbwendu wa Zabanga, viongozi wazalendo wa Wahutu na Watutsi wa Rwanda na Burundi, kina Alphonso Dhlakama kiongozi wa Chama cha RENAMO cha Msumbiji. Dua zetu pia zilikuwa zinawaombea kina Eyadema, Omar Bongo, Paschal Lisouba, Jean Baptist Bokassa, Macias Nguema, Mfalme Hassan, Jaffar Nimeir, Omar Bashir, na Hassan Tourabi, John Voster, Tommy Ndabaningi Sithole, Abel Muzorewa, Morgan Tsivangirai, Jonas Savimbi, Gatsha Mongasuthu Buthelezi, na wengineo wote wamo kwenye dua hiyo ya WABARIKI VIONGOZI WAKE.

Kesho 09 Desemba Watanzania tutaimba tena MUNGU IBARIKI AFRIKA, WABARIKI VIONGOZI WAKE, ....Wakati tukiimba hivyo tutazame jirani yetu Kenya. Tumuombe Mwenyezi Mungu AWABARIKI VIONGOZI WAKE(kuna neno nimetaka kulisema lakini nimelimezea)."

3 Maoni Yako:

At 12/11/2005 01:31:00 PM, Anonymous F. Massawe said...

"Wakati ambapo Tanzania haijawahi kutawaliwa, tunaambiwa kuwa tarehe kenda Desemba ni sikukuu ya uhuru wa Tanzania!" Hebu Ndesanjo toa ufafanuzi kidogo kuhusu hili. Kuna jambo linatia utata kidogo.

 
At 12/13/2005 02:51:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Ni kweli kabisa iliyotawaliwa ni Tanganyika si Tanzania. Hiyo ni mieleka tu ya maneno.

Da Mija.

 
At 12/13/2005 09:08:00 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Ndio Frank,
NI kweli kabisa Tanzania haikupata uhuru mwaka 1961! Soma makala iliyoko kwenye kiungo hiki hapa: http://h1.ripway.com/macha/GUMZOUHURU.doc

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com