12/08/2005

Tuzo ya Majimaji Yaenda kwa Jaji Mwalusanya

Jaji James Mwalusanya amepewa tuzo ya pekee ya Haki za Binadamu itolewayo na Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania. Tuzo hiyo inaitwa Maji Maji Human Rights Award. Jaji Mwalusanya ni kati ya majaji ambao baadhi huwaita "majaji wanaharakati." Mwalusanya ni jaji ambaye masuala ya haki za binadamu yalikuwa yakimgusa sana na alijulikana kwa tabia yake ya kutoogopa kutoa maamuzi yanayoendana kinyume na matakwa ya serikali. Hii ndio sababu iliyokuwa ikipelekea mchungaji Christopher Mtikila kuwa na tabia ya kupeleka kesi zake Dodoma badala ya Dar Es Salaam. Jaji Mwalusanya alikuwa akifanya kazi Dodoma.
Moja ya kesi kubwa ambazo Mwalusanya aliwahi kutoa maamuzi yake ni ile ambayo alitamka kuwa hukumu ya kifo inayokubalika katika sheria za Tanzania ni kinyume na katiba na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania tumetia saini. Ni Mwalusanya huyu pia ambaye katika kesi iliyofunguliwa na Mtikila aliamua kuwa ni kinyume na katiba ya Tanzania kwa wananchi kutakiwa kuomba ruhusa kwa Mkuu wa Wilaya (yaani kinara wa CCM) na polisi (yaani mkono wa udhalimu wa wa-twawala) ili kufanya mkutano wa hadhara. Hukumu hiyo unaweza kuisoma kwa kubofya hapa. Ni Mwalusanya pia ambaye alitoa hukumu katika kesi nyingine ya Mtikila kuwa ni kinyume na katiba kwa Mtanzania kutumia pasipoti ili kutembelea Tanzania! (enzi zile za kutumia pasipoti kwenda Zanzibar). Pia ndiye aliyeamua kuwa ni halali na ni haki ya kikatiba kwa raia yeyote yule kugombea nafasi yoyote ya uongozi bila kuwa mwanachama wa chama chcochote. Hukumu hii iliwafanya watwawala kukimbilia bungeni kwenda kuipinga.
Pamoja na tangazo la tuzo hii na pia pongezi kwa Kituo cha Haki za Binadamu kutambua mchango wa Jaji Mwalusanya katika ujenzi wa demokrasia nchini Tanzania, ninatumia wasaa huu kuuliza swali ambalo linaweza kuwa limeshachosha baadhi yenu. Mimi halijanichosha. Kisa cha kuita tuzo hii Maji Maji Human Rights Award ni nini? Kwanini isingeitwa Tuzo ya Haki za Binadamu ya Majimaji? Au ikiitwa "award" ndio inakuwa na nguvu zaidi?
Dakika chache zilizopita nimetembelea tovuti ya Kituo cha Haki za Binadamu...kwanza jina lao hasa ni Center for Human Rights...nilitaka kutazama kama wamebadili lugha ya kigeni waliyokuwa wakiitumia. Wapi! Ugonjwa ule ule. Ukisoma malengo ya hawa wapigania haki (sijui kwanini hawapiganii haki za kitamaduni) utaona kuwa wanasema kuwa wanatetea na kuelimisha wanyonge na masikini kuhusu haki zao za msingi. Lakini wakati huo huo tovuti yao inatumia kiingereza tena cha mabomba makali makali. Wanafikiri Maimuna ataelewaje haki zake kama wanamwelimisha kwa lugha asiyoielewa? Halafu watabaki wakidai Watanzania hawajui haki zao...watazijuaje kama inabidi waende kwanza kwenye madarasa ya lugha za kigeni?
Pamoja na kuwaunga mkono katika jitihada zao za kutoa huduma za kisheria na elimu ya katiba kwa Watanzania, ningependa kuona wakitumia tovuti yao kuelimisha na kutoa msaada wa kisheria kwa Watanzania wa kawaida na sio Waingereza au Wakanada. Wafaye hivyo kwa kutumia lugha ambayo tunaitumia majumbani, mitaani, kwenye mabasi, sokoni, kwenye harusi, misiba, n.k. Lugha tunayoitumia asubuhi, mchana, jioni. Lugha hiyo ni Kiswahili.
Bofya hapa utembelee tovuti yao.

4 Maoni Yako:

At 12/09/2005 09:41:00 AM, Blogger Jeff Msangi said...

Pongezi kwa mheshimiwa Jaji.Pia nakubaliana na wewe kuhusu matumizi ya lugha ya kituo cha kutetea haki za binadamu.Ni jambo la msingi sana kuangalia hadhira yako kabla ya kutengeneza makabrasha na vipeperushi vya matangazo ikiwemo mtandao.Huenda wanadamu wanaoongelewa hapa sio babu yangu na bibi yangu kule Kilimanjaro."Wanadamu" hawa nadhani ni wale ambao tayari wanazijua baadhi ya haki zao za msingi.Kituo kinafanya kuwakumbusha tu pale wanapoonekana kuzisahau.Tusubiri,labda watatujibu.

 
At 12/13/2005 04:04:00 AM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Mimi naona tuanze kuwaandikia moja kwa moja kuwauliza kwanini wanatumia kiingereza kuwaandikia waswahili, je wanajua madhara yake?

 
At 12/13/2005 09:48:00 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Inanishangaza sana. Haki wanazopigania ni za watu wa kawaida, kama wanavyodai, lugha wanayotumia sio ya hao watu wa kawaida. Labda tuwaandikie kama Mija ulivyosema.

 
At 12/26/2005 07:26:00 AM, Blogger Kaka Pori said...

Mimi ni nafanya kazi katika kituo hicho kwa kujitolea. Bila ya shaka (kwa maana mimi si msemaji wa kituo) kuna jitihada zinafanyika katika kuweka kurasa za tovuti hiyo katika lugha ya kiswahili pia.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com