1/29/2006

Blogu Mpya, Nguvu za Teknolojia Mpya, na Kadhalika

Kasri la Mwanazuo katuletea mwanablogu mpya. Juhudi zake nazipongeza. Mwanablogu huyo ni Mustapha ambaye amekuja na Hotspot. Mkaribishe na uwe unamtembelea. Bonyeza hapa uende nyumbani kwake. Kuja kwa Mustapha kumetokea dakika chache kabla sijakaa chini kuandika kifupi juu ya masuala ya teknolojia na vyombo vya habari. Huwa sichoki "kuhubiri" juu ya masuala haya kwani mapinduzi ya teknolojia ya habari, mawasiliano, na maarifa yananikuna sana. Mapinduzi haya faida zake kwa nchi kama zetu unaweza usizione lakini ukiwa unatazama mbali na una uwezo wa kuona "picha kamili" utajua kuwa mapinduzi haya yatabadili mambo katika nchi zetu kwa kiasi kikubwa. Kama sio sasa, ni hapo baadaye kidogo.

Moja ya mambo ambayo yanabadilika kutokana na teknolojia mpya ni mahusiano kati ya magazeti na wasomaji. Mahusiano kati ya wahariri, waandishi, na wasomaji wao. Kwa miaka mingi magazeti yamekuwa ni chombo cha habari cha mstari mmoja ulioonyooka ambapo habari, maarifa, na elimu vinatoka katika vyombo hivyo na kwenda kwa wasomaji. Mahusiano kati ya magazeti na wasomaji ni mahusiano kati ya mtoaji na mpokeaji. Magazeti yanatoa habari na maarifa, sisi wasomaji tunapoke. Wasomaji ni walaji. Barua za wasomaji tunaweza kusema kuwa ndio njia kuu ya kufanya mahusiano kati ya magazeti na wasomaji kuwa ya nipe nikupe. Magazeti yanatuambia jambo nasi tunapata nafasi ya kujibu, kuhoji, kuuliza, kusahihisha, kupongeza, n.k kupitia barua za wasomaji. Pia tunaweza kuandika kukemea jambo au kumtaka kiongozi afanye au aache kufanya jambo fulani. Zaidi ya hapo wasomaji hatuna sauti. Sisi ni magolikipa.

Kama hujawahi kufanya kwenye magazeti hutajua kuwa ni barua chache sana ambazo wasomaji wanaandika zinapata nafasi ya kusomwa na wahariri na kuchapishwa gazetini. Nyingi huishia kapuni. Na wakati mwingine, "barua za wasomaji" huandikwa na waandishi wa habari wenyewe! Kuna mambo ya ajabu sana ndani ya vyombo vya habari (ndio maana wakati mwingine mimi huviita vyombo vya uongo). Unaweza kusoma habari isemayo, "wananchi wengi waliohojiwa na gazeti hili..." ukaamini kabisa kuwa wananchi wengi waliohojiwa kumbe "wananchi" hao wako kichwani mwa mwandishi. Hajaenda kokote, hajahoji mtu yeyote.

Tofauti na magazeti-jadi ambapo msomaji ni msomaji, mtandao wa tarakilishi (Intaneti) umeleta jambo jipya. Mtandao huu, baadhi ya watu wanauita: soma-andika. Mtandao wa tarakilishi umejengwa kwa namna ambayo inaruhusu mtu kusoma na pia kuandika. Kwa mfano, kama umesoma jambo hapa kwenye blogu ukawa hukubaliani nalo au hukuelewa unaweza kuandika kupinga au kutaka ufafanuzi. Walaji na wazalishaji wanakuwa kitu kimoja. Wasomaji wanakuwa waandishi, waandishi wanakuwa wasomaji (wanasoma yaliyoandikwa na wasomaji wao). Mahusiano ya vyombo vya habari mtandaoni na wasomaji yanabadilika na kuwa ya mistari miwili ya nipe nikupe.

Ngoja nikupe mfano mdogo wa jinsi teknolojia inabadili mambo. Nimekuwa nikiandika magazetini rasmi toka mwaka 1992/93. Toka wakati huo hadi majuzi nilikuwa siwezi kujua wasomaji wangu wanawaza nini, ukiachia mbali wale ambao nilikuwa nakutana nao ana kwa ana. Lakini nilipoanza kuweka anuani yangu kwenye makala zangu nikaanza kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na wasomaji wangu. Wasomaji wananiuliza maswali kutaka ufafanuzi, wananipa mapendekezo ya makala za kuandika, wananiunga mkono, wananishushua, wananiponda, wananikumbusha ahadi nilizoweka za kuandika kuhusu jambo fulani, n.k. Nimeandika makala nyingi kutokana na mapendekezo ya wasomaji. Hili ni badiliko kubwa sana.

Blogu zinatuwezesha kwa kiasi kikubwa kufanya mambo ambayo yamekuwa hayawezekani katika magazeti-jadi ya kuuzwa mtaani. Huku bloguni tunaandika. Wasomaji wetu nao wanaandika. Mara yanatokea majadiliano. Sio mtu mmoja tu anawaambia wengine ambao wanasoma bila kuwa na uwezo wa kujibu, kuunga mkono, au kuuliza maswali. Hapana. Blogu inawezesha nyanja ya habari kutoka kwenye zama za wasomaji kuwa kama watu wasio na mawazo, habari, au fikra. Watu wanaopaswa kusoma tu, kupokea bila kutoa. Tunatoka kwenye zama hizo na kuingia kwenye zama ambazo nyanja ya habari inakuwa ni aina fulani ya majadiliano. Mazungumzo. Nipe, nikupe. Mzalishaji ni mlaji na mlaji ni mzalishaji. Kila mtu anakuwa mwanahabari. Hili ndio linafanya blogu kupata umaarufu kwa haraka. Siku hizi zinatolewa hadi skolashipu kwa ajili ya kublogu. Sio mchezo. Bonyeza hapa uione (lazima uwe mwanafunzi wa chuo kilichopo Marekani).

Katika kujaribu kubadili mahusiano kati yake na wasomaji, kwa kutumia teknolojia mpya, magazeti kadhaa yanafanya majaribio ya aina mbalimbali. Kwa mfano, gazeti la Wisconsin State Journal linatumia wasomaji wake kuamua habari zipi ziwekwe ukurasa wa mbele. Wasomaji wanapiga kura. Bonyeza hapa usome kuhusu jaribio hili. Mwaka jana gazeti la Seattle Post-Intelligencer lilianzisha jaribio ambalo tahariri inaandikwa na wahariri wa gazeti hilo na wasomaji wake. Kongoli hapa na hapa kwa undani. Kuna gazeti kama News and Record ambalo limeanzisha ukurasa uitwao Town Square katika tovuti yake ambapo wasomaji wanapewa nafasi ya kuandika habari wenyewe. Bofya hapa uwatazame. Magazeti mengi yanachofanya hivi sasa ni kuwa na waandishi wao ambao wanakuwa na blogu. Blogu hizo zinakuwa ni uwanja wa majadiliano kati ya gazeti na wasomaji wake. Ukiachilia mbali maagazeti hayo, teknolojia mpya zimezalisha miradi mipya kabisa kwenye nyanja ya habari. Kwa mfano, kuna Wikinews, mradi ambao habari zinaandikwa na wasomaji. Zinaandikwa na mtu yeyote. Tazama hapa. Halafu kuna jamaa walioanzisha mradi kabambe wa uandishi wa umma huko Korea ya Kusini, Ohmynews. Ohmynews ina habari ambazo zinaandikwa na wananchi. Wasomaji wakisoma habari wakaipenda wanaweza kumlipa aliyeandika habari hiyo. Bonyeza hapa utazama toleo la kiingereza la Ohmynews.

Kwa ufupi, nilikuwa namkaribisha Mustapha , kumpongeza Kasri kwa kutuletea huyu ndugu, na kusema kuwa tunalofanya kupitia katika blogu zetu hizi ni sehemu ya mapinduzi ambayo yanabadili kabisa mahusiano kati ya watoa habari na wapokeaji.

5 Maoni Yako:

At 1/30/2006 08:18:00 AM, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

Ndesanjo, tunaomba usiache kututia hamasa mara kwa mara maana kila mara wanablogu wapya huingia ukumbini basi ni vyema kwamba kila saa hamasa juu ya ajira hii binafsi iwe inatolewa....keep it up MWANA WA MFALME WA BLOGU!

 
At 1/30/2006 08:46:00 AM, Blogger mwandani said...

Na ni nani atakeyeutonya umma
Kwamba uhuru wa kutoa hoja umekuwa sawa na masihara tu,

Makampuni yanatuendeshea nchi
Makampuni hayo hayo yanatutengenezea vichwa vya habari.

Kwani hivi ni vyombo vya habari au vya kupindisha mawazo?
Je, ushindi ni ushindi au ni makosa mengine ya jinai?

Na ni nani atakayeutonya umma…
Kwamba hizi ndio nyakati tunazoishi

- wimbo wa Willie Nelson

Saa nyingine hukumbuka mistari ya nyimbo kusapoti hoja

 
At 1/30/2006 09:04:00 AM, Blogger boniphace said...

Naungana na Mark kuhusu mawazo ya makala hii. Kuna haja makala kama hizi kuendelea kuandikwa na ikibidi kutanuliwa. Huu ni mtindo bora wa kuwaelimisha watu katika kufungua Magazeti Tando yao. Naamini mapinduzi ya habari yanakuwa katika spidi ya kutia matumaini.

 
At 1/30/2006 04:21:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Ndesanjo,
Mabadiliko unayoyazungumzia hapa ni ya kweli kabisa na yananipa mwanga wa huko niendapo hata kama hapa nilipo "tanesco" wamezima umeme wao.Kutanuka kwa nyanja ya habari kuna maanisha uhuru mpya wa kuwaza na kufikiri.Siku hizi tunajua mambo ambayo kamwe wenzetu wazungu wasingetaka tujue.Interneti na upanukaji wa habari ni mtego kwa vizazi vyote.Ni dunia ambayo nadhani mungu aliidhamiria tangu uumbaji.

 
At 2/01/2006 10:00:00 AM, Blogger boniphace said...

Ndesanjo kuna wachungaji watatu wameingia kwa mpigo pale kwangu naomba pia ili nawe uwakaribishe. Kwa kasi hii sijui na bado tunaendelea.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com