1/28/2006

Zaidi juu ya Creative Commons: kitabu cha bure na zoezi la pekee la kuhariri

Huu ni mmoja wa mifano ya faida za Creative Commons. Majuzi kimetolewa kitabu cha kufundisha watu wa nchi zinazoitwa "zinazoendelea" juu ya ujenzi wa mtandao usiwaya (wireless network kwa kimombo). Kitabu hiki kimetolewa chini ya nembo ya Creative Commons. Kinapatikana bure. Na kuwakuwa kiko chini ya Creative Commons, mtu yeyote yule anaruhusiwa kukitoa kitabu hiki katika lugha yoyote ile (na hata kuongeza mambo ambayo anaona ni muhimu ila hayako katika kitabu mama). Yote hii unaruhusiwa kufanya bila kuomba ruhusa kwa mtu yeyote kwa masharti kuwa kitabu hicho usikitoe kwa minajili ya kibiashara na pia lazima toleo lako liwe chini ya Creative Commons. Kitabu chenyewe ukibonyeza hapa utakipata. Hapa kuna ukurasawa wa "wiki" wa kitabu hicho.

Kuna mfano mwingine wa mabadiliko makubwa yanayojitokeza kutokana na teknolojia mpya na vuguvugu kama la Creative Commons. Mwaka 1999, Larry Lessig, mwanzilishi wa vuguvugu hili, alitoa kitabu kizuri sana kiitwacho Code and Other Laws of Cyberspace. Hili lilikuwa ni toleo la kwanza. Toleo la pili, yaani Code v. 2, ni muendelezo na upanuaji wa hoja na uchambuzi ulioko katika toleo la kwanza. Kwa staili ya ki-Creative Commons, toleo hili la pili badala ya kuandikwa na Larry Lessig peke yake kama ilivyo kawaida katika nyanja ya vitabu, toleo hili linaandikwa/linahaririwa na watu mbalimbali. Ina maana kuwa hata wewe unaweza kushiriki katika kuandika toleo la pili la kitabu hiki. Bonyeza hapa uone zoezi hili la kipekee.

2 Maoni Yako:

At 1/29/2006 06:38:00 AM, Blogger Hector Mongi said...

Nashukuru kwa habari hii. Nimekiona kitabu hicho na naamini ni kizuri sana kwa jumuiya ya wanamtandao. Hata hivyo kwa vile kuna nafasi ya kuhariri, basi wataalamu wa mambo haya wajitokeze kuwezesha watu wa kawaida watakaokisoma wakielewe. Tunafuatilia kwa karibu kuanzishwa kwa tawi la creative of commons hapa Tanzania.

 
At 1/30/2006 04:12:00 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Kuanzishwa kwa Creative Commons Tanzania kutasaidi kuwezesha vitabu kama hivi vinavyotolewa chini ya nembo ya Creative Commons (baadhi ya haki zimehifadhiwa au hakuna haki zilizohifadhiwa) kutafsiriwa na kusambazwa bure. Nitatafuta vitabu vya masuala ya kilimo vilivyoko chini ya Creative Commons kwa ajili ya mtandao wenu.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com