1/20/2006

Creative Commons Tanzania!

Furaha niliyonayo sijui nifanye nini. Au niseme nini.
Ngoja nianzie mwaka jana mwezi wa sita: mwezi wa sita mwaka jana nilikwenda jiji la Egoli/Jozi (au Johannersburg, kama hujui), Afrika Kusini, kwenye mkutano wa Commons-Sense kwenye chuo kikuu cha Wits. Mkutano huu ulikuwa ni wa ufunguzi wa tawi la shirika la Creative Commons nchini Afrika Kusini. Bonyeza hapa usome hisia nilizopata nilipotembelea hapo kwa Madiba.

Creative Commons in vuguvugu linaloendeleza mfumo wa hatimiliki mbadala (kwa kiingereza: "copyleft" badala ya "copyright"). Kwahiyo badala ya kazi zilizoko chini ya hatimiliki kusema "Haki Zote Zimehifadhiwa" kama ambavyo mfumo wa hatimiliki uliozoeleka ulivyo, Creative Commons inatoa nafasi kwa wamiliki wa kazi mbalimbali kuweza kusema, "Baadhi ya Haki Zimehifadhiwa," au "Hakuna Haki Zilizohifadhiwa." Kimsingi, mfumo huu, tofauti na mfumo wa hatimiliki uliozoeleka ambao una kila chembe za falsafa za kibepari, umejengwa juu ya falsafa kama vile Ujamaa au Ubuntu. Msingi wa Ubuntu ni huu: mtu sio mtu bila watu. (bonyeza hapa kusoma kwa kifupi kuhusu ubuntu). Kwahiyo sio vigumu sana kwa Waafrika kuelewa mantiki ya vuguvugu kama Creative Commons. Afrika Kusini ndio nchi ya kwanza Afrika kuwa na tawi.

Vuguvugu la Creative Commons nimekuwa nikilifuatilia kwa muda mrefu. Nilipokwenda mkutano wa Afrika Kusini na kukutana na wanaharakati wengine wa vuguvugu hili na pia "baba" wa Creative Commons, Larry Lessig (bofya hapa kuna blogu yake) mwili mzima ulinisisimka. Kabla ya hapo nilikuwa nimewagusia marafiki zangu kadhaa Tanzania juu ya vuguvugu hili ila hakuna aliyeonekana kujali. Walinisikiliza tu. Nikawaacha. Sasa mwezi Septemba nikiwa njiani kwenda Helsinki, Ufini (ambapo ndipo nilikutana na Michuzi na blogu yake kabambe ilipozaliwa...blogu yake ina uraia wa Ufini!), nikiwa uwanja wa ndege Uholanzi nikakutana na Paul Kihwelo, ambaye zaidi ya kuwa mshikaji wangu, ni mkuu wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu Huria Tanzania. Tukaongea kidogo nikamgusia kuhusu Creative Commons na umuhimu wa kujenga vuguvugu lake Tanzania. Hatukuwa na muda wa kutosha. Tukakubaliana kuandikiana. Basi kukutana kwetu pale uwanja wa ndege kumezaa matunda. Na ndio furaha yangu niliyonayo. Paul ni kati ya watu ambao akikwambia kuwa atafanya jambo, ujue kuwa atafanya.

Ombi letu kwa ofisi inayoshughulikia uanzishwaji wa matawi ya Creative Commons katika nchi mbalimbali kutaka kuanzisha Creative Commons Tanzania limekubaliwa. Kwahiyo shughuli rasmi ya kujenga tawi la Creative Commons na kuwezesha wasanii, watunzi, shule, vyuo, wanasayansi, n.k. kutoa kazi zao kupitia Creative Commons imeanza. Paul Kihwelo ndio mwanasheria muongozaji wa zoezi zima la kuanzisha tawi lake nchini Tanzania. Zoezi hili litakuwa chini ya kitivo cha sheria, chuo kikuu huria (moja ya masharti ya kuanzisha tawi ni kuwa lazima kuwe na taasisi ambayo ndio itasimamia). Jumapili tutawasiliana na Paul kuhusu ujenzi wa tovuti maana katika masharti ya mradi huu ni kwamba lazima kuwepo na tovuti. Tayari kuna mashirika mawili ambayo yako tayari kutoa nafasi ya bure ya kuhifadhi tovuti yetu. Kesho ninakutana na Chris Blow wa shirika la NonProfit Design, ambaye yuko tayari sio tu kuhifadhi tovuti hiyo bali pia kuiunda.

Ukibonyeza hapa utaona jina la Tanzania tayari limeingizwa katika nchi ambazo ziko mbioni kuunda Creative Commons (Tazama upande wa chini sehemu isemayo: Upcoming Project Jurisdictions).

Watu wengi ukiongea nao kuhusu masuala ya faida ya kuwa na hatimiliki ya "baadhi ya haki zimehifadhiwa" au "hakuna haki zilizohifadhiwa" badala ya mfumo wa "hazi ZOTE zimehifadhiwa," mawazo yao yanakuwa yanakwenda tu kwenye masuala kama ya muziki. Vuguvugu kama la Creative Commons linagusa maeneo mengi sana kwenye jamii. Hasa maeneo yanayohusu maarifa na elimu. Mfumo wa hatimiliki uliopo hivi sasa unapendelea watu wahodhi maarifa na elimu wakati ambapo Creative Commons inataka kuachilia huru maarifa na elimu. Kutokana na Creative Commons, kuna vitabu ambavyo unaweza kuvipata bure. Bila hata sumni. Kwa mfano, bonyeza hapa upate kitabu kimojawapo.

Lakini pia Creative Commons inaachilia huru maarifa ya vyuo vikuu kwa ajili ya faida ya watu wote hata kama sio wanafunzi waliolipa ada wa chuo chenyewe. Kwa mfano, chuo cha MIT kimeweka masomo yake wazi mtandaoni kwa watu wote wanaotaka kufaidi bure. Bonyeza hapa.
Hata chuo kikuu cha Rice nacho kinaunga mkono vuguvugu hili. Bonyeza hapa. Blogu yangu iko chini ya Creative Commons. Huenda umewahi kuona nembo ya Creative Commons ukashindwa kujua inafanya nini hapa. Ni kwamba kazi zilizoko hapa haziko chini ya mfumo wa "haki zote zimehifadhiwa." Ina maana kuwa kama unataka kuzitumia (iwe ni picha, makala, kisa, shairi, n.k.) sio lazima uiombe ruhusu au unilipe.

Bonyeza hapa ukitaka kusoma zaidi juu ya Creative Commons (kwa kiinglishi).

4 Maoni Yako:

At 1/20/2006 10:10:00 PM, Blogger mwandani said...

endeleza mapambano. nashukuru kwa harakati unazofanya - kwa ajili ya wote

 
At 1/21/2006 01:56:00 AM, Blogger mark msaki said...

ni kweli, kwa ajili ya wote, lakini labda kabla sijaendelea..ni kweli kwamba hakimiliki zinadhibiti upatikanaji wa marifa kwa wengi wasio na uwezo....lakini ninaiona hii kuwa ni zaidi muhimu kuwawezesha sisi wa dunia ya mwisho kuenda sambamba na mabadiliko ya dunia kwani kutoa $ 30 kusoma karatasi bado ni ndoto. lakini swali langu wakati huo huo,,,ni nani atayekuwa anafadhili tafiti ikiwa mfumo wa hatimiliki kwa haki zote ukifa-yani utafiti usipoendeshwa kibiashara? ninaposema hivyo nitatoa mfano, kwa nchi kama SA utafiti unafadhiliwa na makampuni binafsi kwa tanzania ni serekali...lakini ni serekali hiyo hiyo imekuwa ikilalama haina hela za utafiti...na ndio maana watafiti wa nchi zetu nyingi hukimbilia ughaibuni ambako kuna vyombo na ugharimiwaji wa tafiti zao - wanawezeshwa!....kwa upande wa pili utafiti chini ya hatimiliki umefanya piracy ya indigenous people's knowledge sehemu nyingi..anyway, labda niisome vizuri hii habari nijue vyema ugharimiaji utakuwaje...

 
At 1/21/2006 08:22:00 AM, Blogger Ibrahim M. Bwire said...

Ndesanjo, nakuunga mkono na juhudi pevu uzifanyazo. Mimi niko Tanzania na kilio changu ni Mawazo hakiki nayaita akili pevu, fikra pevu. Ni wazo pekee ndio mtaji wa mwanadamu. wako wanaofikirifikiri tu na hao ni wepesi wa kuona kila kitu ni kigumu. Naamini kuwa fikra zinajenga uhai na uhai unajenga utu ,utu uajenga heshima, heshima inajenga maendeleo.Nakutia moyo na wanamtandao wote nawaomba wakuunge mkono.Viva Ndesanjo na creative commons, Viva Tanzania

 
At 1/21/2006 01:36:00 PM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Shukrani nzito zimwendee Paul Kihwelo. Huyu bwana ana mtazamo ambao ni tofauti sana na watu wengi. Yeye sio mzungumzaji. Ni mtendaji. Anafanyia mambo kazi. Wazo hili alilichukua na kulifanyia kazi kwa muda mfupi sana. Na tena ameshakutana na baadhi ya watu ambao ni mhimili wa creative commons (alipokuwa Uingereza hivi karibuni). Ninavyoandika sasa ninajadili na rafiki yangu Chris kuhusu tovuti ya vuguvugu hili. Mark ameuliza maswali mazuri sana ambayo nitayajibu vyema kwenye ukurasa wa mbele.

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com