6/05/2005

AFRIKA KUSINI, HISIA, MAJINA, N.K.

Nitakuwa nikiandika mambo kadhaa juu ya nchi ya Afrika Kusini. Baada ya kurudi toka kwa Mzee Madiba, nimekuwa nikiifikiria sana nchi ile. Nchi ilinipa hisia za ajabu ajabu sana. Nilifurahi mno kuwa Afrika, kuwa miongoni mwa watu wangu. Lakini wakati huo huo nchi ile ilinipa huzuni kubwa. Utajiri usio na kifano na umasikini wa kutisha vinatazamana uso kwa uso. Hakuna anayemwelewa mwenziye. Nadhani toka kuzaliwa kwangu sijawahi kuona utajiri namna ile (hata ukiiweka Marekani) na ufukara wa kutisha. Sina maana kuwa Afrika Kusini ndiko kwenye ufukara kuliko nchi nyingine duniani, nina maana katika nchi nilizotembelea sijawahi kuona ufukara kama ule.
Lakini kuna mambo ambayo yalinipa furaha. Moja kubwa ni ufahari walionao Waafrika Kusini juu ya utamaduni na historia yao. Ukienda mahakama ya katiba unakuta meza kuu ya majaji imepambwa na ngozi ya ng'ombe. Sherehe za kitaifa zinafunguliwa sio kwa sala za kikristo na kiislamu tu kama Tanzania, bali pia kwa sala toka kwa viongozi wa dini zetu za asili. Watambaji mashairi ya sifa hutumika katika matukio mbalimbali ya kitaifa (kwa waliofuatia sherehe za kuapishwa serikali mpya ya Mandela wanaweza kukumbuka). Timu yao ya taifa wanaiita Bafana Bafana (timu ya taifa ya Tanzania inaitwa Taifa Stars...neno "stars" sijui linafanya nini hapo!).
Baada ya kuondolewa kwa mfumo wa kinyama wa ubaguzi nchini Afrika Kusini, wananchi wa nchi hiyo waliamua kubadili baadhi ya majina ambayo yamebeba historia ya kibaguzi na unyama wa makaburu. Jiji la Pretoria ambapo ndipo makao makuu ya serikali mwishoni mwa mwaka huu litabadili rasmi jina lake na kuitwa Tshwane (ukitamka usitamke herufi "h". Inatamkwa "Tswane). Hili ni jina la mto unaokatiza katika jiji hilo. Inasemekana kuwa jina Tshwane lilitokana na jina la mtoto wa Chifu Mushi aliyekuwa akiishi maeneo hayo mwanzoni mwa miaka ya 1800. Neno hili linamaanisha, "Sisi ni ndugu." Jina "Pretoria" lilitokana na jina la kiongozi wa kikaburu, Andries Pretorius.
Jiji nililokuwa, Johannersburg, linajulikana pia kwa jina la eGoli. Neno hili la Kizulu linamaanisha, "Mahali penye dhahabu." Sijasikia kama kuna hatua za kutumia jina eGoli kama jina rasmi la jiji hili. Watu wengine hupenda pia kuliita jiji hili "Jozi."
Miji mingine ambayo iko mbioni kubadilishwa majina ni Durban: eThekwini. Jina hili linamaanisha ghuba. Pietersburg itakuwa Polokwane.
Kitongoji cha Alexandra nadhani kinatakiwa kubadili jina lake mapema iwezekanavyo. Jina hili linatokana na jina la mke wa kaburu Papenfus ambaye aliamua kuita eneo hili kwa jina la mkewe! Kitongoji hiki visa vyake hutavimaliza. Jina la kitongoji maarufu cha Soweto ambacho kina wakazi zaidi ya wakazi wote wa jiji la Dar Es Salaam linatokana na ufupisho wa jina lake la awali: South Western Township. Hefuri mbili za mwanzo katika maneno hayo matatu ndio zilizaa Soweto.0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com