1/25/2006

Ujenzi wa Huduma cha Kublogu ya Kiswahili

Moja ya matatizo ya huduma za kublogu tunazotumia hivi sasa ni lugha. Huduma hizi zimetengenezwa kwa udhanifu kuwa watumiaji ni wazungumzaji wa Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kishirazi, n.k. Kiswahili hakipo. Tatizo jingine ambalo lipo katika huduma kama blogger.com (ambayo wengi tunatumia) ni kukosekana kwa muundo wa kupanga kazi tunazoandika katika makundi ya kimaudhui. Hili ni tatizo kubwa sana hasa kama mtu unapanga kublogu kwa muda mrefu.
Ina maana hapo baaadaye ukitaka kutafuta habari uliyoandika miaka mitatu iliyopita, itakupasa ukumbuke mwezi na tarehe ili uweze kuipata kwa urahisi. Kama hukumbuki uliandika mwezi gani itakubidi utumie muda mrefu kuisaka. Fikiria, je ikiwa imepita miaka saba? Lakini pia kuna suala la wasomaji kuja kwenye blogu yako na kutaka kusoma habari ulizoandika huko nyuma. Kama wanataka kusoma habari ulizoandika kuhusu utamaduni, watazipataje? Au hadithi. Au labda umekwenda kwenye blogu ya Michuzi baada ya miaka miwili, ukawa unatafuta picha ya jiji la Dasalama au ya Mwanza. Utaipataje hiyo picha? Namna rahisi ya kuipata picha hiyo ni kama amehifadhi picha zake kutokana na maudhui. Kwa mfano, maudhui yanaweza kuwa ni: utamaduni, siasa, michezo, uchaguzi, mikoani, Ughaibuni, Rais, Wabunge, Wanawake, Muziki, Historia, Hadithi, n.k.

Nikienda kwenye blogu ya Makene, nikataka kusoma mashairi yake. Bila kujua aliandika lini na mwezi gani itakuwa vigumu sana. Lakini akiwa na uwezo wa kupanga mambo kwenye blogu yake kutokana na maudhui, kila akiandika shairi analiweka kwenye maudhui ya kundi ya ushairi. Hivyo msomaji akienda hapo anabonyeza kwenye maudhui ya ushairi na kuweza kuona mashairi yake yote. Ukija kwangu ukataka kusoma mambo niliyoandika kuhusu utamaduni au kuhusu blogu, utapata tabu sana maana hakuna mpangilio wa kimaudhui. Kunapokuwa na makundi haya yaliyopangwa kimaudhui kunasaidia msomaji kuweza kupata habari ulizoandika huko nyuma kwa urahisi. Inakusaidia hata wewe mwenye blogu kujua mambo uliyoandika yako wapi. Tunapaswa kutatua tatizo hili. Tutalitatua.


Sasa rafiki yangu Chris wa NonProfit Design (bonyeza hapa uone blogu yake) na mimi tunalipatia tatizo la lugha kwenye huduma za kublogu dawa ya kudumu. Kwa kutumia huduma huria ya kublogu ya Wordpress, tunaunda toleo la Kiswahili. Wordpress tayari ina matoleo ya lugha kadhaa. Kiswahili kwa sasa hakimo. Uzuri wa Wordpress ni kuwa ni programu huria hivyo iko wazi kwa mtu yeyote kufanya chochote atakacho (iwapo una ujuzi sahihi).

Mwisho wa wiki Chris alinitembelea tukaa pamoja kwa siku mbili (alikuja na mbwa wake aitwaye IO). Tulitazama kwa undani jinsi ambavyo tunaweza kusaidia wanablogu wote wa Kiswahili kuhama toka walipo hivi sasa na kuweza kuwa na mpangilio wa mambo waliyoandika katika makundi ya kimaudhui na pia hatua za kufuata ili kujenga toleo la Kiswahili la Wordpress. Katikati ya kucheza na kodi za programu mbalimbali za tarakilishi, tulikuwa tukicheza mpira wa meza (ambapo nilimfunga mabao yasiyohesabika. Kama unabisha muulize! Richard Shilangale, unakumbuka kuwa wewe ndiye ulinifundisha kucheza mpira wa meza?). Pia tuliongelea masuala ya Creative Commons maana shirika lake ndilo linalojenga tovuti ya tawi la Creative Commons Tanzania na pia kuihifadhi tovuti hiyo. Bonyeza hapa usome aliyoandika mwenyewe kuhusu toleo la Kiswahili la Wordpress.

**Da Mija: wewe ndio umenikumbusha neno maudhui. Lilinitoka kabisa. Kila nikilitafuta neno linalonijia ni hadhira! hadhira na maudhui wapi na wapi?

3 Maoni Yako:

At 1/25/2006 10:09:00 AM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Basi utokwaji huo wa neno ulishanitokea kwenye mtihani...wee!!

 
At 1/25/2006 05:31:00 PM, Blogger John Mwaipopo said...

Nilipokuwa nikisoma habari hii nikawa najisemesha kuwa Ndesanjo kwa Kiswahili bomba mbaya. Kumbe baadhi ya maneno unayasahau hivi. 'hadhira' na 'maudhui' kweli mbali mbali.

lakini heri wewe ilikuwa kwenye matumizi kuliko Da'Mija ilipokuwa kasahau neno kwenye mtihani. Utaona hata kalamu ya moto ati!

 
At 1/26/2006 12:02:00 AM, Anonymous Anonymous said...

wordpress ya kiswahili ? hapo umetuwahi kaka . hongera kwa kazi hii njema

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com