1/28/2006

Mawaziri Kuapa kwa Biblia na Kurani: Imani tumezibebabeba tu?

Wiki iliyopita, kwa ajili ya ukurasa wangu katika gazeti la Mwananchi, niliandika makala kuhusu mawaziri wapya kuapa kwa kutumia kitabu "kitukufu" na "kitakatifu" baada ya kuteuliwa. Soma baadhi ya hoja nilizotoa dhidi ya tendo la kuapa:

Baada ya rais mpya kuteua baraza jipya la mawaziri, kilichofuata kilikuwa ni tendo la kula kiapo. Tukio hili limezungumzwa sana mtaani hasa kutokana na kitendo cha Kingunge Ngombale Mwiru (nitampa zawadi ya jina zuri) kuapa kwa kunyoosha mkono bila kushika kitabu "kitukufu" au "kitakatifu" (kurani au biblia) kama wengine walivyofanya.

Wakati ambapo kwa watu wengi kuapa bila kutumia kitabu cha dini ilikuwa ni habari kubwa, kwangu mimi kitendo cha wafuasi wa Isa/Yesu kuapa ndio ilikuwa habari kubwa kabisa. Ni habari ya binadamu kuwa na tabia ya kufanya mambo kutokana na mazoea bila kutafiti kwa kina juu ya usahihi wa jambo lenyewe. Ni tabia inayotokana na utamaduni wa kuiga mifumo ya sheria, utawala, na demokrasia ya nchi nyingine tukidharau uwezo wetu wa kuunda mfumo wetu wenyewe.

Tendo la mawaziri kuapa wakitumia kitabu kitakatifu au kitukufu hatujaanzisha sisi. Utamaduni wa mashahidi kuapa mahakamani kwa kutumia vitabu hivyo hatujauanzisha sisi. Tumeiga toka kwa wengine kama ambavyo tumeiga karibu kila kitu.

Kwanini habari kwangu sio Kingunge kuapa mikono mitupu bali Wakristo na Waislamu kuapa? Jibu la swali hili liko katika kitabu cha Matayo, mlango wa 5, aya ya 33 hadi 37. Katika aya ya 34 Yesu/Isa anakataza wafuasi wake (Waislamu na Wakristo ni wafuasi wake) kuwa wasiape kamwe.

Hivi ndivyo asemavyo toka aya ya 33 hadi ya 37: "Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana. Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Ukisema, `Ndiyo`, basi iwe `Ndiyo`; ukisema `Siyo`, basi iwe kweli `Siyo`. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu."

Anasema kuwa ingawa huko nyuma kuna manabii waliwaambia wanadamu kuwa wanaweza kuapa, yeye anabadili na kusema kuwa usiape kamwe. Hii haikuwa kwa mara ya kwanza kwa Yesu/Isa kutengua mafundisho ya zamani. Unakumbuka, ingawa iliandikwa “jino kwa jino, jicho kwa jicho,” yeye alikuja na kusema geuza shavu. Mchukie adui yako akabadili kwa kutuambia kuwa tuwapende na tena tuwaombee. Aligeuza sheria ya kupiga mawe hadi kuwaua wanaokamatwa katika uzinzi. Alibadili sheria kuhusu talaka. Alibadili maana ya kuzini kwa kusema kuwa hata ukitamani umeshazini.

Nimetoa mifano hii kukupa picha kidogo ya baadhi ya mambo aliyobadili likiwemo suala la kiapo. Anatuambia kuwa kipimo cha ukweli wa kauli yetu isiwe ni kiapo. Anasema ukisema “ndiyo” iwe “ndiyo” na ukisema “hapana” iwe “hapana.” Ukisema utatii katiba na kutumikia wananchi, basi tii katiba na kutumikia wananchi. Hakuna la kuongeza wala kupunguza. Sema ukweli na simama kwenye hiyo kweli, usianze kuingiza jina la Mungu ili kutufanya tuone kuwa unayosema ni kweli.

Nimekuwa najiuliza kwanini wafuasi wa Mwalimu huyu wamekuwa hawafuati mafundisho yake? Je inawezekana kuwa ufuasi wao ni wa jina tu na sio imani ya dhati na uelewa wa mafundisho yake? Amesema waziwazi usiape. Wewe unaapa, tena kwa kutumia kitabu chenye maneno yake yanayokukataza. Je hili ni tatizo la kufuata tamaduni za wengine bila kuhoji? Au ni tatizo la kuwa wafuasi wa Isa/Yesu bila kusoma mafundisho yake?

Lakini tukiacha hoja hii ya kuwa Isa/Yesu amekataza wafuasi wake kuapa, kuna hoja nyingine ambayo niliwahi kuitoa huko nyuma. Nitairudia kwa kifupi. Haiwezekani kutumia Kurani au Biblia kuapa kuwa utalinda katiba ya nchi ukitegemea kuwa Mungu atakubariki na kukusaidia ili utimize kiapo hicho. Kwa sentensi chache sana nitakueleza ni kwanini kisha nitakuacha ili iwe tafakari yako siku hii ya mungu jua (ndio maana ya jumapili).

Kurani na Biblia zinasema kuwa Mungu ametoa amri kumi. Amri ya kwanza inasema, “Mimi ni Bwana Mungu wako usiwe na miungu wengine ila mimi.” Hili sio ombi. Inaitwa amri. Anasema wazi kuwa anataka umwamini na kumwabudu yeye tu. Yeye Yehova/Allah. Tuje kwenye katiba yetu: katiba yetu inatoa uhuru wa kuabudu. Ina maana kuwa unaweza kuabudu Mungu mmoja au miungu 10, hutakuwa umevunja sheria ya nchi. Sio hivyo tu, unaweza pia kutokuwa na imani yoyote na usiwe umevunja sheria ya nchi.

Kwa maneno mengine, wakati Yehova/Allah anakwambia, “Niabudu mimi” katiba inasema “Abudu chochote kile.” Je Mungu aliyekupa AMRI ya kumwabudu yeye tu, anaweza kukubariki ili uendeleze katiba inayosema abudu chochote kile? Yaani Mungu atakuwa anakubariki ili uendeleze mwongozo ambao unawapa wanadamu ruhusa ya kuvunja amri yake ya kwanza. Tena amri hii sio ya kumi bali ni ya kwanza. Kama katiba ingesema mwamini mungu mmoja ambaye ni Yehova/Allah, basi nisingeshangaa iwapo waumini wa Kikristo na Kiislamu wangekuwa wanamuomba mungu awasaidie kuilinda hiyo katiba. Lakini katiba haisemi hivyo. Inapingana kabisa na mafundisho ya Allha na Yehova. "Usiwe na miungu mingine ila mimi" sio sawa na kusema kila mtu ana haki na uhuru wa kuamini atakacho.

Kwahiyo kitendo cha kutumia kitabu kinachokutaka uwe na Mungu mmoja kuapa kuwa utalinda katiba inayokuruhusu uwe na mungu yoyote, mmoja au miungu wengi, au hata usiwe na imani kabisa, n.k. kinaonyesha kuwa huenda imani zetu tumezibebabeba tu. Au tumebebeshwa.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com