12/31/2004

UNAJUA HAYA KUHUSU MWAKA MPYA?

Watu wengi hudhani kuwa mwaka mpya wa kirumi husherehekewa na watu wote duniani. Wafuasi wa imani ya Bahá'í , kwa mfano, wanasherehekea mwaka mpya Machi 21 (siku hiyo huitwa NaW Ruz. Kalenda ya Ki-Bahá'í ina miezi 19 yenye siku 19. Imani ya Bahai ilianzishwa na Bahá'u'lláh. Wachina nao wana mwaka mpya wao. Sijui kama unajua kuwa miezi ya kichina ni majina ya wanyama. Kongoli hapa kwa undani zaidi. Nchini Thailand, mwaka mpya uitwao Songkran husherehekewa Aprili 13 hadi 15 kwa kurusha maji. Mwaka mpya wa Kikeltiki, Samhain, husherehekewa mwezi wa Novemba. Kalenda ya Kirumi ya zamani ilikuwa na miezi 10, na mwaka mpya ulianza Machi Kwanza.

Kalenda inayotumika katika nchi nyingi hivi sasa ni Kalenda ya Kiregori ambayo ilichukua nafasi ya Kalenda ya Juliani. Kanisa Katoliki lilipendelea kubadilisha kalenda ya Juliani kwasababu kadhaa, mojawapo ikiwa ni kufanya waumini wa kikristu washerehekee pasaka karika siku iliyokubaliwa na Baraza la Nikea. Huko Abisinia (Ethiopia) mwaka mpya (enkutatash) ulisherehekewa mwezi wa tisa tarehe 11. Kumbuka kuwa Abisinia iko nyuma miaka saba na miezi nane ya kalenda ya Kiregori (Giriligoloyo kwa wale waliosome Song of Ocol and Lawino) inayotumika katika nchi nyingi duniani hivi sasa. Kalenda ya Ethiopia ina miezi 13. Waislamu nao wana kalenda yao ambayo inafuata majira ya mwezi badala ya jua kama ilivyo kalenda ya kirumi. Kalenda hii ni pungufu kwa siku 11 tofauti na ile inayofuata majira ya jua. Mwaka mpya kwenye Uislamu huwa ni mwezi wa pili. Mwaka 2005 kwenye kalenda ya Kiislamu ni mwaka 1426. Mwaka wa Kiislamu unaanza toka pale mtume Muhammada na wafuasi wake walipokimbilia Medina toka Maka (mwaka 632 katika kalenda ya kirumi).

MWAKA MPYA!

Sherehe za mwaka "mpya" wa kirumi kule mtaani kwangu najua kama kawaida zilipamba moto kwa mayai viza na baruti. Sijui kama umewahi kupigwa na mayai viza. Mayai yaliyooza. Usiombe. Zaidi ya mayai viza, kuna wimbo maarufu (mchanganyiko wa kichagga na kiswahili) ambao nimekuwa nausikia kichwani kama vile niko nyumbani. Wimbo huu ni wa kuamsha wale waliolala wakati wa kupiga madebe na kurushiana mayai viza. Kaka yangu, Walter, kanikumbusha huu wimbo hivi majuzi:
Mwaka mpya Eeeeeee
Mwaka mpya kure ipfo mba
(yaani: toka huko ndani)
Lekana na kitara kyo (yaani: achana na kitanda hicho)
Mwaka mpya Eeee

Nilitaka sana kupiga madebe ila nikawa na hofu ya kuitiwa askari na majirani! Unajua tena nchi za sheria kali.

UNAMFAHAMU PHILLIP EMEAGWALI?

Kama hujawahi kumsikia huyu bwana, nenda hapa. Hata kama unamfahamu, nenda hapo kisha soma hotuba zake (hasa iitwayo African History: Lost, Stolen, or Strayed na pia The Mis-Education of the African). Kuna nyingine inaitwa How To Reverse the Brain Drain.

RAIS WA TANZANIA 2005 ATAKUWA MTU MWENYE UPELE!

Eti rais wa Tanzania 2005 atakuwa na nywele fupi wastani, pua yenye kuonekana, na upele! Sio utabiri wangu bali wa yule mtabiri maarufu Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein. Utabiri kamili huu hapa.

12/29/2004

WAAFRIKA 100 MAARUFU

Jarida la New African liliandaa orodha ya Waafrika 100 maarufu duniani katika toleo lake la Agosti/Septemba 2004. Tazama orodha yenyewe kwa kwenda hapa, hapa, hapa, na hapa.

MSIKILIZE JOE TUNGARAZA

Niliwahi kukutaka utege sikio kusikiliza kipindi cha AFROWORLD kinachoendeshwa na Mtanzania Nambiza Joe Tungaraza (DJ Joe) toka Australia kupitia Radio Adelaide 101.5 kila jumamosi. Masaa niliyoweka wakati ule ni ya Australia, ambapo ni saa 10:30 usiku hadi saa sita usiku. Leo naweka masaa ya sehemu nyingine ili muweze kukifuatilia. Hiki ni kipindi cha matukio na muziki kuhusu Waafrika (Afrika na Ughaibuni). Muziki aina mbalimbali kama Makossa, Zouglou, Rhumba, Kwaito, Rai, Highlife, Reggae, African hiphop unatumbuizwa. Na pia mjadala wa matukio ya kisiasa, kijamii, kitamaduni, na kiuchumi yanayohusu Waafrika.
Unachotakiwa kufanya ni kwenda kwenye tovuti ya Radio Adelaide kila jumamosi: www.radio.adelaide.edu.au na ukishafika hapo kongoli palipoandikwa "Listen Online."

Masaa ndio haya (shukran Tunga):
Walioko Marikani: Midwest/East Coast: Saa 1 asubuhi.
West Coast: Saa 10 alfajiri.
Johannesburg: Saa 8 mchana.
DarEsSalaam: Saa 9 Alasiri.
London: Saa 6 mchana.
Amsterdam: Saa 7 mchana.
Oslo, Stokholm, Copenhagen : Saa 7 mchana.
Helsinki: Saa 8 mchana.

AFYA: KUNYWA MAJI

Kuna rafiki yangu anapenda sana masuala ya afya na uhai. Kanikumbusha kuwa ni vyema nikawa pia najadili mambo hayo hapa bloguni. Hatuwezi kuwa kwenye mapambano dhidi ya utumwa wa fikra, udhalimu, na ufisadi wa watawala wetu bila kuwa watu wenye afya. Leo nitazungumzia maji.
Ninafahamu watu wengi sana ambao hawana tabia ya kunywa maji hadi wasikie kiu. Au wakiwa na kiu watakunywa sumu kali iitwayo soda. Au watakwenda baa kupata "udirinki." Maji ni muhimu sana kwa afya yako. Kwanza kabisa usifikiri kuwa kazi ya maji ni kukata kiu. Ukisikia kiu ujue kuwa mwili wako umeishiwa maji kiasi ambacho umeamua wenyewe kukushtua. Kiu ni njia ya mwili kukwambia, "Rafiki, mbona umenisahau?" Kwa maneno mengine, hutakiwi uwe na kiu hata siku moja. Kunywa maji hata kama huna kiu ili usipate kiu hata siku moja. Kwa siku usikose si chini ya bilauri nane. Ukitaka kujua maji yalivyo muhimu mwilini, fahamu mambo haya:
Asilimia 70 ya mwili ni maji, asilimia 70 ya ubongo ni maji, asilimia 80 ya damu ni maji.

WANABLOGU NA TETEMEKO LA BAHARINI (TSUNAMI)

Umuhimu wa blogu unajionyesha hivi sasa kutokana na maafa yaliyotokana na tetemeko la baharini (tsunami) huko Asia. Wana blogu hawako nyuma. Soma habari hii. Mwanablogu huyu kaweka na picha za video. Ukienda hapa utaona pia picha na video za maafa haya.

12/28/2004

UTUMWA NA BIASHARA YA UTUMWA

Kuna tovuti hii nzuri mno ya chuo kikuu cha Stanford kwa wale wanaofuatilia masuala ya utumwa, biashara ya utumwa, na malipo kutokana na madhara ya biashara hiyo (reparations). Kongoli hapa

KWANINI KAZI HAZIPATIKANI BONGOLAND?

Niliipata barua pepe iliyonipa jibu la swali hilo hapo juu zamani kidogo. Nikaibandika pembeni ya meza yangu. Kila mara nikawa nikiisoma na kuitafakari. Ni barua pepe ambayo imekuwa ikizunguka kwa muda kwenye mtandao. Huenda uliwahi kuipata. Siwezi kujua mwandishi wake hasa ni nani. Ila ninachojua ni kuwa kilichomo ndani yake sio mzaha. Ukiisoma unaweza ucheke. Hakuna ubaya. Ila tafakari undani wake.

Ninajiuliza maswali haya kila mara: Ni lini Tanzania itaachwa kuitwa nchi masikini? Ni lini Tanzania itaacha kuwa nchi
inayoendelea na kuwa nchi iliyoendelea? Hivi hiyo siku itakaa ije?

Kuna wakati huwa ninasita kusema kuwa Tanzania ni nchi inayoendelea. Kuendelea sio neno tu. Kuendelea ni hali ambayo unaweza kuipima. Karibu kila kipimo cha maendeleo ukikitumia, unaona kuwa Tanzania inarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa mfano siku zinavyokwenda wastani wa umri wa Mtanzania kuishi hapa duniani unapungua. Yaani kama wewe ni mtanzania unayeishi Tanzania, mauti utaikaribia kwa haraka sana! Najua inatisha, nisiseme?

Kwahiyo utaona ingawa inachukuliwa kuwa mataifa hapa duniani yamegawanyika kati ya yale
yanayoendelea na yaliyoendelea, ukweli ni kuwa kuna mataifa mengine yasiyoendelea, yaliyosimama na yanayorudi nyuma!

Haya, turudi kwenye swali la msingi. Kwanini ajira ni vigumu kupatikana Bongoland? Isome barua pepe ninayoizungumzia upate jibu la kwanini hakuna ajira Tanzania:
George Chege amepunguzwa kazi hivi karibuni. Amepania kutafuta kazi nyingine kwa udi na uvumba. Ameamshwa asubuhi ya leo na mlio wa saa ya mezani. Ni saa 12 alfajiri. Saa yake ya mezani imetengenezwa nchi Japani. Anaamka na kuweka maji ya chai katika jiko lililotengenezwa China huku akinyoa ndevu zake kwa mashine ya kunyolea iliyotengenezwa Hong Kong.

Anapomaliza kuoga kwa sabuni iliyotengenezwa Kenya, anavaa shati lililotengenezwa Uingereza na suruali ya dengirizi iliyotengenezwa Marekani na viatu vya Kimarekani vilivyotengenezwa na wafanyakazi wa ujira mdogo huko Vietnam. Anakunywa chai kwenye meza iliyoagizwa toka Dubai na kula mayai yaliyokaangwa katika kikaangio kilichotengenezwa India. Sahani, kijiko na kikombe anavyotumia vimetoka China.

Anafungua redio yake kisasa iliyotengenezwa Taiwan huku akifungua kitabu chake cha kumbukumbu kilichotengenezwa Italia ili aweze kupanga ratiba yake ya siku kwa kalamu toka Uingereza.

Anapomaliza kupanga ratiba yake ananyanyua simu yake ya mkononi toka Japan na kuondoka kuelekea kwenye kituo cha basi ambako anapakia basi lililotengenezwa Japan na kununuliwa Dubai.

Jioni inapowadia anarudi nyumbani akiwa mchovu kabisa. Anaketi kwenye viti vilivyotengenezwa Singapore na kuanza kutazama kipindi cha luninga kilichotayarishwa Marekani kwenye luninga iliyotengenezwa Taiwan. Wakati akitazama luninga anajiuliza sababu inayofanya iwe vigumu kwake kupata kazi. Haelewi.
** (Usisahau kuwa hata jina lake, George, limeagizwa toka Ulaya).

SAMAHANINI

Wazalendo wote, wana wa nchi, wazawa, wana mapinduzi, wakereketwa, wafurukutwa, wana ngangari, wana ngunguri, wana apollo (kule Mererani), vijana wa kule kwa mzee Jomo na "baba" Moi (sasa?), marastafari, vizabizabina, bila kumsahau mshikaji Joji Dabliyuu Kichaka, Wana mageuzi na mageuzo, wapiga debe, majangili yanayovaa kofia ya "uongozi," makaburu wanaoitwa "wawekezaji," polisi wanaokamata wahalifu huku nao ni wahalifu, wahubiri wanaotangaza wokovu wakati tunahitaji mapinduzi, mahakimu wanaohukumu wala rushwa huku nao wanakula rushwa (mbele, nyuma, kushoto, na kulia)...bila kuwasahau wana mapanga sha sha sha...! NIMERUDI. Samahanini kwa ukimya.
Bado siamini kuwa wale jamaa wenye ngozi isiyo na kemikali za melanin (Wayoruba wa Nigeria huwaita, "watu waliochubuka") waliomuua dada yetu wameachiwa!
Hiyo baadaye. Ngoja nitafute kitu cha kwanza cha kukupa. Nina mambo yamejaa vyungu kumi na mbili. Nitaanza kupakua chungu namba saba.

12/24/2004

UNAMJUA JOHN PILGER?

Kama humjui John Pilger usiseme kwa sauti watu wakusikie! Kongoli hapa na hapa umjue.

SIMU YA INTANETI YA BURE

Umeisikia Skype? Simu ya bure ya Intaneti. Piga kokote duniani. Usitoe hata "sumni." Jaribu ujionee mwenyewe. Bofya hapa.

WALE WAZEE WA MAHISIA YA REGE

Wale wazee wa mahisia. Wale wazee wa marege nendeni hapa. Kula muziki tani yako. Jaribu kusikiliza rege "roots" nzito hasa za Steel Pulse na Groundation.

DUA LANGU LITASIKILIZWA?

Kuna siku nilisema kuwa ningekuwa na uwezo ningefanya binadamu waweze kuendesha magari wakiwa wamelala! Hii ingenisaidia usiku wa leo wakati nikielekea Vermont, mwendo wa masaa kumi na kitu...kama hakutakuwa na theluji. Kumbe kwa uwezo wa teknolojia huenda ikawezekana siku moja. Tazama hapa.
Kingine nilichosema ni kuwa ningekuwa na uwezo ningefanya binadamu tuweze kusoma tukiwa usingizini! Na pia ningeongeza masaa ya siku, yaani siku iwe na masaa zaidi ya 24.
Usishangae mbona mawazo ya ajabu ajabu namna hii, ukiwa ughaibuni lazima mawazo kama haya yakujie!

ANGEKUWA NI KABWELA/MZALENDO MWENZETU...

Kawaida sina tabia ya kuapa. Lakini leo naapa. "Hakya" nani vile...nikatike kichwa (Nalamba udongo na kulamba kidole kisha kukielekeza mawinguni tunakoamini ndio aishipo muumba). Angekuwa ni kabwela, mlalanjaa, ngozi nyeusi, mzawa, mzalendo kama wewe na mimi ametuhumiwa kuua angeonja joto ya jiwe lupango hadi amani ipatikane Mashariki ya Kati.
Faili lingepotea.
Tungeambiwa, "ushahidi unaendelea" kwa miaka mitano hata kumi.
"Vizibiti" vingepotea.
Baadhi ya mashahidi wangetoweka.
Wengine wangekufa.
Mara hakimu angefiwa.
Mara angepata dharura.
Mwendesha mashtaka angeumwa. Angepona. Angeumwa. Angepona.
Mwendesha upelelezi angehamishwa kituo.
Mwendesha upelelezi mpya angehitaji nusu mwaka au mwaka mzima kupitia kesi....
Ingekuwa balaa, nuksi, mkosi, bahati mbaya, uzembe, utumbo, ubadhirifu, rushwa, ufisadi ...taja mengine.
Huyo ni mwenzetu.
Lakini wanapokuwa ni wale jamaa tunaowaabudu ambao mungu, yesu, na malaika wanafanana nao, na hata miti ya krisimasi tunaiwekea pamba ili iwe kama hali yao ya hewa ilivyo (hali yao ya hewa ina uungu fulani...!).
Akiwa ni jamaa mwenye damu ya jamaa waliomhadaa Mangungo wa Msovero...
unajua kitakachotokea.
Kama hujui...Hebu tazama.

12/23/2004

WALE WA MAREGE

Wale wazee wa hisia wanaopenda kula marege (hasa wachagga na vishuu wote wa Arusa) waende hapa watasikiliza miziki hadi watakoma

BURNING SPEAR ANAULIZA...

Nakumbuka ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya tisini nilipomuona babu Burning Spear kwenye video kwa mara ya kwanza. Sitasahau. Wimbo ulioningia ambao alikuwa akiuimba kwa hisia huku akizunguka huku na kule jukwaani ni ule anaouliza, "Unakumbuka enzi za utumwa?" Nami nakwambia kama hukumbuki, unapaswa kukongoli hapa.

ULIKUWA UNAJUA?

Je unafahamu kuwa krisimasi nchini Abisinia (Ethiopia) husherehekewa tarehe 7 Januari? Krisimasi nchini humo huitwa Ganna.
Labda ulikuwa pia hufahamu kuwa mwaka mpya nchini humo ambao huitwa Enkutatash, husherehekewa tarehe 11 Septemba. Absisinia hufuata kalenda ya Juliani ambayo ina miezi kumi na mbili ya siku 30 na mwezi mmoja (wa kumi na tatu) wenye siku tano! Kalenda hii, Juliani, iko nyuma kwa miaka saba na miezi nane ya kalenda ya Kiregori ambayo hutumiwa na mataifa mengi duniani.

KWANZAA HAPA MARIKANI NI KUANZIA TAREHE 26

Sikukuu ya Kwanzaa kwa watu weusi walioko tumboni mwa jitu (beast) ambayo pamoja na mambo mengine inatukuza kiswahili inasherehekewa kuanzia tarehe 26 mwezi huu hadi tarehe kwanza Januari. Kwa maelezo zaidi na historia ya sherehe hii ya watu weusi kongoli hapa na hapa.

SERA KUHUSU ZANA MPYA ZA MAWASILIANO NA HABARI

Kama unapenda kufuatilia mambo ya sera bofya hapa.

UNAPOSHEREHEKEA SIKUKUU USIYOJUA HISTORIA YAKE...

Wakati ukisherehekea sikukuu hii ya... "kuzaliwa kwa nani vile?." usisahau kufuatilia mahesabu ya "wanaokombolewa" kwa mabomu ya jeshi la "mkristo aliyeokoka" Joji Dabliyuu Kichaka. Bofya hapa.

BLOGU: BAGHDAD INAWAKA MOTO

Mwanablogu wa Baghdad Burning anamshauri baba wa krisimasi, Santa, akienda Iraki asisahau kuvaa fulana ya kuzuia risasi...

UNAFAHAMU CHANGAMOTO YA STOCKHOLM?

Bofya hapa.

12/22/2004

NANI KASEMA UCHAGUZI MARIKANI UMEMALIZIKA?

Unadhani uchaguzi uliofanyika hapa marikani tarehe pili mwezi uliopita umemalizika? Kule jimbo la Washington bado kura zinahesabiwa! Kama huniamini kongoli hapa.

MBONA HUMPENDI PAKA WANGU?

Nimekutana na rafiki abdulahi yangu toka nchi fulani ya Afrika Magharibi. Katika kujuliana hali maana hatujaonana muda kidogo, kanieleza kisanga kilichomkumba. Kisanga kinatokana na Amanda, binti wa kitasha ambaye wameanza naye urafiki muda si mrefu.
Ilianza hivi: Baada ya kupigiwa simu Abdulahi aliaacha shughuli zake na kufunga safari kwenda kumtembelea. Simu ilipoita subuhi siku hiyo alikuwa anaingia duka la Wakorea wanakouza vyakula toka Afrika Magharibi. Akacheki aliyepiga simu: Amanda. Akashangaa maana muda si mrefu katoka kwake alikokuwepo toka jana yake jioni. Akaipokea. Amanda akamtaka aende mara moja.
"Kuna nini."
"We njoo." Amanda akajibu huku sauti ikibadilika kama ya mtu anayekaribia kulia.
"Si uniambie." Abdulahi akasisitiza.
Wapi.
Lazima aende.
Basi huyo akaondoka zake hadi kwa Amanda. Kufika mlangoni anamkuta Amanda macho yamemvimba. Mara anaanguka kilio kama kuna msiba. Mshikaji haelewi ni kitu gani kinaendelea. Baada ya kumbembeleza kwa kama dakika 20 hivi, Amanda akaanza kuongea. Abdulahi hakuamini alichokuwa akisikia.
Amanda ana huzuni kwa muda mrefu. Ameitunza huzuni moyoni mwake kama yai. Leo kashindwa kuvumilia. Ameipasua.
"Kwanini humpendi paka wangu?"
Kwanza kabisa Abdulahi alihisi labda kawa kiziwi. Haiwezekani aliyosikia ndio yaliyotoka mdomoni mwa Amanda. Yaani usumbufu wote huo na kulia kote chanzo ni paka?
Amanda ana paka mmoja mweupe, mnene wa wastani. Virgo ndio jina lake. Kama unataka kukosana naye sema jambo lolote baya kuhusu paka wake. Au usimjali. Mahusiano na paka wake ni kama vile mahusiano kati ya binadamu na binadamu. Anamkumbatia, anapiga naye soga, anambusu, anacheza naye, anampapasa, anamwogesha, n.k. Toka wafahamiane, Abdulahi hajawahi kumgusa Virgo, wala kumzungumzia. Ni kama vile huwa hamuoni. Kumbe kosa. Amanda amekuwa akimtazama tu. Akiteseka.
"Utanipendaje mimi bila kumpenda paka wangu?" Amanda anauliza.
"Kwani umesikia namchukia paka wako?"
"Humchukii. Sijasema unamchukia, nasema humpendi." Amanda machozi yanazidi kumbubujika.
"Unataka ninfanyeje ndio ujue kuwa nampenda?"
"Mbona hujawahi kusema lolote kuhusu Virgo. Hutaki hata kumshika. Virgo kwako ni kama vile hayupo hapa ndani."
"Hiyo ni hofu yako tu mimi napenda mnyama wa aina yoyote." Abdulahi akasema kwa sauti isiyo na ushawishi. Kukawa na ukimya. Kisha akauliza, "Kitu gani kinakufanya udhani kuwa simpendi paka wako?"
Hapa ndio bomu kubwa zaidi likadondoshwa. Abdulahi hajapona hadi unaposoma kisa hiki.
Amanda akiwa bado analia akajibu, "Mbona hujamnunulia hata zawadi ya krisimasi?"
Abdulahi kimya. Wewe unadhani angesema nini? Hana la kusema zaidi ya kushangaa. "Wenzetu wana tamaduni tofauti sana." Ndio maneno yake ya mwisho wakati tunaagana baada ya kumuuliza, "Utamnunulia paka zawadi gani ya krisimasi?"
Ninashangaa kuwa toka anihadithie kisa hiki hadi dakika hii mbavu zangu bado ziko imara. Hasa ukimjua Abdulahi ndio hutamaliza kucheka na kumcheka.

CUBA YAJIBU MAPIGO YA MARIKANI

Mzozo unaotokana na Marikani kuweka mapambo ya krisimasi na nambari 75 (inayowakilisha wafungwa 75 wa kisiasa nchini Cuba) nje ya ofisi zake mjini Havana unazidi kunoga. Cuba imejibu mapigo. Jionee kwa macho yako.

DAUDI NA GOLIATI?

Mwaka mmoja na miezi saba iliyopita Joji Dabliyuu Kichaka alitangaza kuwa vita ya "kuwakomboa" Wairaki imemalizika. Kwa "mahesabu" ya jeshi la Marikani linalodaiwa kuwa ndio namba moja duniani kwa uwezo wa kivita, mwezi Aprili mwaka jana vita vilikuwa viishe, na mwezi huu majeshi hayo yalikuwa yaondoke na kuwaachia Wairaki nchi yao ili "wajitawale" wenyewe. Lakini matokeo yake (yaani ya "vita kuisha" na majeshi ya Marikani kuondoka baada ya ushindi) ndio haya hapa.

SIKILIZA HII

Kituo cha Murchison na idara ya masomo ya Waafrika katika chuo kikuu cha toledo, wametoa wimbo mmoja unaotokana na semina ya kila jumatano ya nadharia na fikra kuhusu mapinduzi ya zana mpya za habari na mawasiliano (inaongozwa na Dr. Abdul Alkalimat ambaye nilimzungumzia hivi majuzi). Isikilize hapa. Kituo cha Murchison, pamoja na mambo mengine kinajihusisha na juhudi za kutumia zana za mawasiliano kama nyenzo ya ukombozi wa wanyonge. Maudhui ya wimbo huu yanagusia jambo hilo.

FUNGUA MACHO

Fungua macho kwa kusikiliza shairi la Krs-One kwa kwenda hapa. Maneno ya shairi lenyewe haya hapa (sikiliza huku unasoma maneno yenyewe maana ni muhimu kuelewa kila anachosema).

NDIO MAANA TUNAPINGA HUKUMU YA KIFO

Hivi huyu bwana angekuwa amehukumiwa kitanzi, sindano ya sumu, au kiti cha umeme...na akawa tayari ameuawa. Angefukuliwa? Watu wangemuombea afufuke kama Lazaro? Au? Miaka 17 jela bila kosa! Nenda hapa.

12/21/2004

HIVI KILA NIJUACHO NI UONGO?

Hawa jamaa wananichezea shere au ni kweli? Eti wanasema kila nijuacho ni uongo mtupu. Tazama mwenyewe...

BABA AKIFARIKI...

Rafiki yangu, John Hill, kanishtua kweli. Hivi majuzi nilimuuliza, "Hivi unafanya nini mwisho wiki?" Akaniambia kuwa anakwenda kumtembelea baba yake. Akaongeza, "Nikimtembelea huwa tunacheza pool na kutazama mpira kwenye luninga."

Akanyamaza kidogo kisha akasema, "Baba yangu ana hela nyingi sana na ameshazeeka. Najua atafariki wakati wowote. "
Nikashtuka. "Unasema baba yako atafariki?!"
"Ana shinikizo la damu. Amelazwa hospitali mara mbili hivi karibuni. Hana muda mrefu. Baba yake, yaani babu yangu, alikufa kwa shinikizo la damu...akifariki nitarithi hela zake na pikipiki zake mbili. Ana hela nyingi sana benki."
Nilibaki mdomo wazi. Alikuwa anaongea kama vile ni jambo la kawaida. Bado ninaisikia sauti yake kichwani mwangu. Sijammaliza.

BARUA PEPE NA BARUA KONOKONO ZINAPOKUTANA

Tazama teknolojia hizi mbili zinavyosaidiana. Kongoli hapa.

BLOGU NA ELIMU YA JUU: HUDHURIA DARASA BURE

Kuna darasa ambalo litaendeshwa kwa kutumia blogu katika chuo kikuu cha Stanford. Kutakuwa na video kwa wale ambao watahudhuria kwa mtandao. Blogu ya darasa hilo hii hapa na muhtasari wake huu hapa.

JINSIA NA TEKNOLOJIA MPYA ZA MAWASILIANO NA HABARI

Kuna ripoti hapa kuhusu mahusiano kati ya jinsia na zana mpya za habari na mawasiliano. Wale wanaofuatilia masuala ya jinsia au mabadiliko ya kijamii yanayoletwa na teknolojia mpya kama intaneti watafaidika kwa kuisoma.

12/19/2004

BLOGU YA K.Y. AMOAKO

Namna gani katibu mkuu wa Tume ya Uchumi ya Afrika (Economic Commission for Africa - ECA), K.Y. Amoako? Ameisahau blogu yake?

KOMPYUTA ZA MKONONI NA DEMOKRASIA AFRIKA

Tarakilishi za mkononi zinatumika kujenga mazingira ya uchaguzi wa huru na haki nchini Rwanda. Habari kamili hapa.

KWENYE WATU KUMI...

Jabali la muziki, Marijani Rajab, aliposema kuwa kwenye watu kumi binadamu ni mmoja alikuwa amekosea? Ukisoma kisa hiki utapata jibu.

JUMAPILI NI JUMASABA?

Leo ni jumapili (hapa Marikani)...wakristo (ukitoa Wasabato) wanadai kuwa leo ni siku ya saba ya juma, kwahiyo ndio siku ambayo mungu wa kiyahudi, yehova, alipumzika baada ya uumbaji. Kwa uelewa wangu wa kiswahili nilijua kuwa jumapili ni siku ya pili maana jumamosi ni siku ya kwanza (yaani mosi = moja/kwanza) na jumatatu yaani kesho ni siku ya tatu. Sasa sielewi jumatatu itakujaje baada ya siku ya mwisho ya juma ambayo ni siku ya saba. Ukifika mwisho wa juma (yaani saba) si unaanza moja? Kama jumapili ni siku ya saba, siku inayofuata ni siku ya kwanza. Sasa kwanini uanze na TATU? Labda ni hili tatizo langu la hisabati, nilizoambiwa na mwalimu Kisanga nikiwa kidato cha kwanza kuwa "mwandiko wangu unaonyesha kuwa hisabati zinanipiga chenga" na pia nilizofeli toka kidato cha pili!
Najua Waislamu wanatabasamu na kusema, "Si unaona. Sisi tunasali ijumaa ambayo ni siku ya saba maana siku inayofuata jumamosi au jumakwanza/jumamoja ni siku ya kwanza." Waislamu wanafurahi kweli mtu ukiwagonga Wakristo, wakristo nao hivyo hivyo, ukigonga waislamu wanatabasamu.

Hii ni moja ya tofauti kati ya dini za asili za Afrika na dini za kuletwa na wakoloni, mabwana biashara utumwa, "mabedui" wenye majambia kiunoni na kurani mkononi, n.k. Imani zetu za asili hazina ushindani. Kwa mfano, imani ya Kichagga haisemi kuwa kwakuwa Msukuma ana imani tofauti basi imani yake ni ya uongo. Wachagga wanaamini imani yao ni ya kweli, na ile ya Wasukuma (ingawa ni tofauti na yao) ni ya kweli pia. Lakini hizi dini za kuja zina mantiki tofauti. Nikiwa mkristo, ninatakiwa kuamini kuwa mwenye dini tofauti na yangu atakwenda motoni. Muislamu naye anatakiwa kuamini kuwa dini yake katika maelfu ya dini na imani duniani ndio ya kweli. Zote zilizobakia ni za uongo. Waafrika hatuna hiyo mambo ya dini za uongo za na kweli. Imani zetu zote (ingawa zinatofautiana kutokana na sababu za kihistoria, na kitamaduni) ni sahihi. Kwanza kuna watu wengi ambao hadi leo hawajui kuwa Waafrika tuna dini za kwetu. Ajabu kabisa. Ndio maana naamini kuwa mfumo wetu wa elimu unatakiwa kufutwa na kuanza upya. Elimu inapaswa kuelimisha sio kupotosha.

Ngoja niwagonge na Waislamu kidogo (tazama Wakristo wanatabasamu!): Ukiweza kutembelea Bwagamoyo, nenda kwenye jumba la watumwa walipokuwa wakirundikwa kabla hawajawekwa kwenye majahazi na kupelekwa Uarabuni kutumikishwa zaidi ya punda. Kisha tambua kuwa waliokuwa wakifanya biashara hiyo ya unyama uliokithiri ya kuuza, kununua na kutumikisha ndugu zako ndio walioleta dini ambayo uko tayari kutoana macho na jirani yako ukiitetea. Wakati ule walichukua ndugu zetu utumwani kimwili, safari hii wanakuchukua kiakili na kisaikolojia. Wamekufanya ukadhani kuwa Uislamu ni Uarabu. Tazama, ili uwe muislamu unachukua jina la kiarabu, unasali kiarabu, unavaa kiarabu ukienda swala, ukisali unaelekeza uso uarabuni, ukimnukuu mungu unabadili lugha toka kiswahili hadi kiarabu (utasikia mtu anasema, "Mnyazi Mungu alisema..." kisha anarukiwa kiarabu. Ina maana anapotamka maneno toka kinywani kwa mungu hawezi kutamka kwa lugha ya kiswahili au ya kabila lake maana mungu wake haongei kiswahili au kinyakyusa. Nasema kama mungu wako hajui lugha yako ya Kimanyema, usithubutu kunihubiria habari zake. SIMTAKI!), mungu kwenye dini yako (uislamu) ana majina 99 na yote ni ya kiarabu, kuhiji unapaswa kuondoka nje ya bara lako lenye maeneo mengi matakatifu unakwenda hadi uarabuni unakobusu jiwe na kumpiga shetani mawe kisha unarudi, manabii zako wote wametoka huko mashariki ya kati...
Bob Marley huyo anaimba: Wont you help me to sing, this song of freedom....Emancipate (jikwamue) yourself from mental slavery, none but ourselves can free our mind....

Ile makala ya Mwafrika Akutana na Muislamu/ Mwafrika Akutana na Mkristo inakuja. Lazima tuongee haya mambo. Hatuna muda wa kupoteza. Hatuna cha kuogopa. Hakuna wa kututisha. Hata wakitutangazia fatwa kama Salman hatuwezi kukaa kimya. Wakristo na waislamu wote wanahubiri kuwa dini zetu za asili ni ushirikina na ushenzi, sisi tukiwasema wao wanakuwa mbogo. Sisi hatutatumia mapanga wala mawe. Hatutakuwa na hasira wala chuki. Tutajadili kwa uwazi, upendo, na ukweli. Historia ni historia.

MABISHANO YA ALI MAZRUI NA HENRY GATES, JR.

Filamu ya Wonders of the African World ilileta mabishano na mijadala mizito mizito kati ya wanahistoria, wana taaluma, waandishi, n.k. Mabishano makali kati ya Ali Mazrui na Henry Lous Gates (mtengenezaji wa filamu hiyo na mwalimu katika chuo kikuu cha Harvard) yalisambaa kila kona ya mtandao wa tarakilishi (kama yalivyokuwa mabishano kati ya Ali Mazrui na Wole Soyinka ambayo nitayaweka hapa baadaye). Ingawa mabishano haya ya kitaaluma yaliyokea muda mrefu (mwaka 1999), masuala yanayozungumziwa yanahitaji kuwa katika mijadala na fikra za watu wanaotafuta ukweli juu ya historia na utamaduni wa watu weusi.

Chini ya uchambuzi wa Ali Mazrui, kuna uchambuzi wa Molefi Kete Asante, mmoja wa waanzilishi wa dhana AFROCENTRICITY. Pia kuna uchambuzi wa Tolber, Jr. na Martin Doudou. Baadaye nitaweka majibu ya Henry Gates kwa Ali Mazrui. Faidi uhondo wa elimu na maarifa kwa kwenda kwenye mabishano hayo hapa.

12/18/2004

JABALI AFRIKA

Jabali Afrika wamebadili tovuti yao. Watembelee hapa usikilize nyimbo zao (ingawa sio nyimbo nzima). Nilipenda sana albamu yao ya kwanza iitwayo Journey. Niliinunua mtaani pale Nairobi mwaka 2000 (Che Mundugwao, Obati Masira, mpo wapi?...hakika Kisumu nitarudi tena). Toka hapo Jabali wameniingia sana. Nawafananisha na Sisi Tambala wa Tanzania. Albamu yao ya Rootsganza nimeinunua mwaka huu. Nimeipenda, ila sio sana. Wameingiza vinanda vinanda, magita, na sauti za watu wengine...sikuipenda sana. Lakini ni poa mtu ukiwa nayo. Nawapenda sana wanapoimba na ngoma peke yake. Nenda kwenye albamu ya Rootsganza, kongoli kwenye wimbo wa Maumau Chant usikie Nyabinghi ya nguvu na sauti ya mshairi Cosmas Sindani (nani ana habari zaidi kuhusu Cosmas Sindani?).


Hii timu inatafutwa na makachero wa "Sii Ai Ei" (naandika jina lao hivi ili wasinishtukie!). Yeyote anayewajua awaambie washushe hicho kibao, la sivyo "watashaa..."  Posted by Hello

MAPINDUZI YA HIP HOP DUNIANI

Wale wanaofuatilia masuala ya muziki wa rap unaosambaa dunia nzima kama chombo cha kuelimisha, kujieleza, kutetea, kupinga, kujipatia ajira, n.k nenda katika viunganishi hivi:
Afrika: http://www.africanhiphop.com/
Australia - http://www.ozhiphop.com/
Ulaya - http://www.ukhh.com/s
Amerika ya Kusini - http://www.realhiphop.com.br/

Kwa ajili ya masikio yako, nenda katika viunganishi hivi:
Afrika - http://www.africanhiphop.com/rumba-kaliplay.php?
Australia - http://www.ozhiphop.com/forum/forumdisplay.php?fid=24
Ulaya - http://www.ukhh.com/audio.html
Amerika ya Kusini - http://www.realhiphop.com.br/multimidia/radio/index.htm

USHAURI TOKA KWA BI. MTANDAO

Ukiniambia, nitasahau.
Ukinionyesha, sitaweza kukumbuka.
Ukinihusisha, nitaelewa.

UTANI, UTANI, MWISHOYE...

Utani, utani hivi hivi...mara imekuwa kweli. Kama unadhani naota, tazama hapa.

12/17/2004

MSIKILIZE NA KUMJUA MWALIMU NA RAFIKI YANGU: ABDUL ALKALMAT

Mtu aliyenipa msukumo wa kusoma, kutafiti, na hatimaye kufundisha juu ya maingiliano ya jamii na teknolojia mpya za habari na mawasiliano, ni Abdul Alkalmat. Alikalimat ni kati ya watu hapa Marekani ambao kila mara wananifanya nipate huzuni sana. Heshima na upendo walionao kwa Tanzania hakuna mfano. Sababu inayonifanya nihuzunike ni ukweli kuwa Tanzania wanayoizungumzia wanamapinduzi kama hawa imebaki kwenye majivu ya historia. Kwa mfano, katikati ya mwaka huu nilikutana na mshairi Nikki Giovani alipoongea na kusoma mashairi yake mapya hapa Toledo. Tukiwa tunaongea nje ya ukumbi wakati watu wakinywa divai na vitafunio, aliniuliza ninatoka wapi kutokana na lafudhi yangu. Nilipomwambia ninapotoka alitabasamu kwa furaha na kukumbuka alipoitembelea Tanzania na jinsi anavyoipenda. Moyoni nikajisemea, "Angejua Tanzania ya enzi zile imebaki moyoni na akilini mwa wanamapinduzi kama yeye." Niongeze, Nikki Giovani ndiye mwanamama aliyesema maneno haya kuhusu mwanamke mwenye uzuri wa asili: "...if I dreamed natural dreams of being a natural woman, doing what a woman does, when she's natural, I would have a revolution." (Mshairi huyu ana mchoro wa kudumu [tattoo] mkononi unaosema, "Thug Life," kwa kumbukumbu ya Tupac Amaru Shakur. Tupac alikuwa ana mchoro tumboni kwake wenye maneno haya. Hivi sasa Nikki Giovani anafanya kampeni ili picha ya Tupac iwekwe kwenye stampu za Marekani).
Kabla sijapotea njia, nirudi kwenye mada ya msingi. Alkalmat ndiye aliyenifanya nihamie hapa Ohio toka jimbo la Washington mwaka 2002. Baada ya kusoma kazi zake, niliamua kumwandikia barua pepe kumwambia kuwa nataka kusoma chuoni anapofundisha. Nilijua kuwa huyu ndiye mtu ninayetaka kufanya naye kazi hapa Ughaibuni. Nilimwambia kuwa nimetoka Tanzania. Nilijua kuwa nikitaja Tanzania nitakuwa nimemteka. Kama nilivyohisi, alinijibu baada ya dakika chache kwa kunipa namba yake ya simu na kunitaka nimpigie ili tuongee kabisa sio kuandikiana! Nilipompigia maneno ya kwanza toka kinywani kwake yalikuwa ya Kiswahili, "Habari Gani?" Alinisalimu. Kisha akaniuliza kwa kiingereza, "Nikusaidie vipi?" Hapo ndio ukawa mwanzo wa uhusiano wetu. Baada ya kumweleza ninachotaka aliniambia nimpe muda. Hutaamini. Haikupita siku niliandikiwa barua na rafiki yake mwingine ambaye hivi sasa kawa ndugu yangu kabisa (ambaye naye Afrika anaiabudu!) kuniambia kuwa kama nina alama za kutosheleza na barua za walimu toka chuo kikuu cha Dar Es Salaam za kuniunga mkono watanipa skolashipu! Dunia hii bado tuna watu weusi ambao hawajakata tamaa. Nawe usikate tamaa (ninatumia neno "nawe" maana sitegemei kuwa maadui zetu watakuwa wanasoma blogu hii. Kama wapo wakitoe haraka sana. Nikitema mate yakikauka wawe wameishia!)
Nakumbuka siku ya kwanza tunakutana ana kwa ana na Alkalimat, mwezi wa nane mwaka 2002 majira ya asubuhi, jengo la liitwalo chuo, nilikuwa kwenye maabara ya tarakilishi. Naye akawa anapita nje, aliponiona (ingawa hatukuwahi kukutana na wala hakuwahi kuona picha yangu) alisimama na kupunga mkono. Nikamwendea. Akaniuliza, "Wewe ni kaka toka Tanzania?"
Nikajibu, "Ndio. Umejuaje?"
"Huu ni wakati wa mapinduzi. Lazima uweze kumtambua mwanamapinduzi mwenzako. Tusipofahamiana tukiwa vitani tutauana."
Tulipofika ofisini kwake alianza kuwazungumzia akina Abdulrahaman Babu (mtazame Babu akinongonezwa jambo na Malcolm X), Issa Shivji, Mwalimu Nyerere, Wamba dia Wamba, n.k. Alianza kunihubiria juu ya mapinduzi makubwa ya kijamii, kisiasa, kisayansi, kitamaduni, na kitamaduni yanayoletwa na teknolojia mpya za habari na mawasiliano. Kuanzia hapo nikazama kabisa hadi kuja kuibukia kwenye tasnifu yangu iliyoitwa Political Use of New Information and Communication Technologies in Tanzania (ambaye yeye alikuwa mmoja wa wanakamati)...na pia kuibukia kwenye masuala ya blogu! Ukitaka kujua jinsi alivyo na upendo wa damu nyeusi, siku ya kutetea tasnifu yangu (maana alijua kuwa kuna watu walikuwa wamepania kuja kunitwanga maswali) aliniita ofisini kwake kunipa mazoezi. Si hivyo tu, alicheza faulo kidogo lakini katika dhana ya kutetea Uafrika, aliniambia maswali atakayoniuliza! "Nataka ujiandae vyema maana hawa maadui zetu wanatakiwa kujua kuwa hatuko hapa kucheza...tuna kazi ya kuokoa bara zima. Sio suala la mchezo. Lazima tusaidiane maana safari ni yetu wote." Aliniambia.
Ninapenda umfahamu zaidi Dr. Alkalmat ambaye upendo wake kwa watu weusi unanipa nguvu kila ninapokaribia kuanguka kwa majonzi ya jinsi watu wetu wanavyoangamia katika utumwa wa kimawazo na minyororo ya utegemezi. Kuna siku nitajadili kwa kina zaidi juu ya kazi zake zinazoendeleza na kuchangia harakati za watu weusi Ughaibuni na Afrika. Zaidi ya kuwa mwalimu wa masuala ya Afrika, Alkalmat ni msimamizi wa kundi la majadiliano kwenye intaneti kuhusu masuala ya watu weusi la H-Afro-Am ambalo unaweza kujiunga nalo. Ni mhariri wa tovuti za Malcolm X na eBlack Studies. Unaweza kumsoma hapa, na hapa. Kuna kitabu chake kipya hapa.
Ukitaka kumsikiliza, nenda hapa. Ukifika hapo teremka chini ya ratiba ya mkutano kisha utaona picha na jina lake. Kongoli umsikilize akihutubia mkutano wa cybernomads nchini Ujeremani.

AISEE...YAMETOKEA HUKO MEXICO

Maribel Dominguez amesajiliwa na klabu cha Celaya huko Mexico (inatamkwa Meiko).
"Nini cha ajabu?" Wajiuliza.
Tuliza ngoma. Maribel Dominiguez ni mwanamke na Celaya ni klabu cha wanaume kama ilivyo Yanga au Simba! Nenda hapa uhakikishe.

NITAKUPIGA PICHA

nitaleta
kamera,
nikupige picha,
niisafishe,
niiweke mkobani,
kila niendako
niwe nawe,
nikiwa na huzuni
majonzi na hasira,
nikutazame,

nitue moyo,
unipe furaha
kama kicheko chako
cha mvua ya radi
jumapili asubuhi.
- toledo, ohio, 2004

BINTI MTANZANIA AANZISHA GAZETI LA MTANDAONI

Binti Mtanzania, Lola Kingo, anayesoma chuo kikuu cha Harvard hapa Marekani ameanzisha gazeti la mtandaoni liitwalo Mimi. Hongera. Timua mbio. Mola akujazi.

12/16/2004

UNAJIJUA

Uliyenipa baadhi ya haya kwenye barua pepe yako unajijua. Umenikumbusha pia neno la kichagga lenye maana ya mbolea = sari.

Kwa Bibi = Uingereza
Unyamwezi = Marekani
Bondeni = Afrika Kusini
Wadanganyika = Watanzania

MAKALA MPYA

Nimepandisha makala mpya ambayo inafutana na ile ya Mapinduzi ya Umma Dhidi ya Dhuluma. Hii inaitwa: Unayetwangana naye ndiye mwenzako. Iko kwenye kona ya makala zangu, upande wa kuume, chini ya picha nilizoziweka hivi karibuni.

NINAREKEBISHA

Samahanini sana. Kuna watu wameniuliza juu ya viunganishi vya makala, tenzi, na hadithi za Freddy Macha. Tatizo sijui ni nini. Ninarekebisha.

NIMEONA MUSWADA WENYEWE

Nimeupata muswada anaoongelea Mtikila, ila kipengele cha rais kufukuza majaji bado sijakiona. Muswada huu hapa.

KUNA ANAYEWEZA KUTHIBITISHA MUSWADA HUU?

Kama kweli siri-kali ina mpango wa kupeleka muswada wa namna hii bungeni, nitaondoka hapa kwa miguu kurudi nyumbani. Naomba uthibitisho wa habari hii. Unajua wanasiasa kama Mtikila wakati mwingine wanaweza kututisha tu.

KONA YANGU AMERUDI....

Mwanablogu toka Bongo wa KONA YANGU, ndugu Mkina, amerudi. Kumbe alikuwa yuko vijijini. Nilipata wasiwasi. Habari yake ya waandishi na vitambi vya sambusa na manyama ya warsha, semina, makongamano, mikutano, nimeipenda maana huu mtazamo wa kuwa kitambi ni afya sijui tumeupata wapi. Kitambi ni mafuta mwilini yaliyojikusanya, yasiyo na kazi, yasiyotumika. Mtembelee hapa kupata vipande vyake.

12/15/2004

IKULU NAYO....

Ikulu nayo imelowana maji ya "uzima" toka kwa mabeberu. Bila kiingereza Watanzania tunaona kama vile hakifanyiki kitu. Hii ni tovuti ya ikulu ya Watanzania. Lugha wanayotumia wamesafiri hadi Ulaya kuazima....Ikulu ina kijarida chake, nacho sijui wanamwandikia Tony Blair na malikia Lizabeti au wanamwandikia Siwema, Mponjoli, Nyundo, Magire, n.k. Hivi ninakerwa peke yangu au kuna wengine? Isije ikawa ni mimi mwenyewe.

TUTASUBIRI HADI LINI?

Usishangae. Ndio tulivyo. Hatuoni umuhimu wowote wa kutunza urithi, historia, na utamaduni wetu. Wala hatujiulizi kwanini Waingereza wanatumia mamilioni ya pauni kuendeleza utamaduni na lugha yao kupitia British Council (sawa na british cultural center), Wajerumani wanatumia fedha kwa ajili ya Goethe Institut (ambayo ni german cultural center), Wafaransa wana Alliance Francaise (sawa na french cultural center), Wamarekani wana USIS. Kwanini wanaanzisha taasisi kama hizi na kuzisambaza dunia nzima? Kwanini mataifa "yaliyoendelea" sio tu yanasambaza bidhaa zao dunia nzima bali pia na tamaduni zao?

Kwa jinsi tulivyolala, wakati mwingine wanatumia taasisi hizi kutangaza na kuendeleza tamaduni zetu. Mchoraji na mchongaji maarufu kama George Lilanga (kazi zake zinauzwa hapa. ) anatangazwa na kuendelezwa na Alliance Francaise na mashirika na balozi za nchi za "wenzetu." Wasanii wa Kitanzania wanaotaka kufanya maonyesho ya kazi zao, hodi ya kwanza sio wizara ya utamaduni, au ofisi ya waziri mkuu, bali katika vituo vya tamaduni za nchi hizi za magharibi na balozi zao. Tumekwisha. Wasanii wengi, kwa uzoefu wao, wanakwambia kuwa ukitaka kufanya maonyesho ya kazi za sanaa (uchoraji, uchongaji, muziki, ngoma, n.k.) mbele ya kadamnasi inayojali, usiende kwa Watanzania wenzako. Nenda kafanye maonyesho hayo Alliance Francaise au British Council mbele ya wazungu. Sio kwa Watanzania wenzako. Ndio maana hutakiwi kushangaa kuwa gwiji la muziki wa asili duniani, marehemu Dr. Hukwe Zawose, hakuna aliyekuwa akijua kazi zake nchini Tanzania. Wenye santuri zake nchini Tanzania ni wazungu. Watanzania wengi wanadai kuwa walikuwa "wakimsikiasikia" !

Sio hivyo tu, ukiona kazi za wasanii wetu kama michoro ya tingatinga, vinyango vya wamakonde, shanga za kimasai, n.k. zimepamba ndani kwa mtu, basi jua mwenye nyumba sio Mtanzania. Sisi huwa hatupambi na kazi zetu za sanaa. Ukienda nyumba za mabeberu ndio utakuta mikeka, kanga, vinyago, tingatinga, n.k. Hata wanaouza vinyango pale Mwenge, jijini DSM, ndani kwao wamepamba kwa bidhaa za plastiki au udongo toka China au India! Wanaamini kabisa kuwa vinyago na kazi nyingine za kitamaduni ni vitu vya wazungu! Tukiona mtu amevaa mapambo ya kitamaduni na nguo za kitamaduni akilini mwetu tunajisemea, "Atakuwa msanii huyu."

Usishangae kuwa mwanzilishi wa Nyumba Ya Sanaa ni mweupe. Katoka kwao mbali kuja kutuanzishia "nyumba ya sanaa" zetu! Je unajua kuwa mwanzilishi wa makumbusho ya utamaduni wa Msukuma, Bujora, sio msukuma au Mtanzania? Unajua pia kuwa kati ya watu wanaosukuma harakati za kufanya kiswahili kipate hadhi ya juu katika mfumo wa elimu Tanzania ni mwingereza ambaye ana jina la Kinyamwezi? Unajua pia kuwa Mfuko wa Utamaduni Tanzania unapata fedha zake toka mataifa ya nje na sio serikali yetu? Mataifa haya yanatumia fedha za walipa kodi wao kuendeleza utamaduni wetu!
Tutasubiri wengine hadi lini? Lini tutajua kuwa utamaduni wetu ni wetu? Lini tutajua kuwa utamaduni wetu ni mzuri na unafaa kutunzwa, kuenziwa, na kuheshimiwa? Anza kujikomboa leo kwa kuondoa "takataka" za kichina ndani kwako. Tafuta kazi za sanaa; uchoraji, uchongaji, ufumaji, n.k. za Watanzania au Waafrika wenzako. Nyumba yako lazima iwe na sura yako kama Mwafrika. Tusipojijua kwenye dunia ya leo, tutabaki kuwa tegemezi kiakili, kiimani, kiuchumi, kisiasa, kinafsi, n.k. Jikomboe!

N'TAKUCHAPA! HUNICHAPI! N'TAKUCHAPA! HUNICHAPI!

Mwaka 1992. Shule ya sekondari ya Ilboru, Arusa. Nimejikalia zangu bweni la Mawenzi, mara naona miguu mirefu, miembamba ya mwalimu mkuu msaidizi inaingia bwenini na fimbo mkononi. Nikitoe au nibaki? Nilijiuliza. Kila upande nasikia kelele za miguu. Watoro wanakimbia na kuruka madirishani.
"Soo."
"Noma."
"Tuishie."
Watoro wanapeana taarifa za ujio wa Medukenya.
Nikajiuliza, "Kwanini nikimbie wakati sijafanya kosa?" Nikabaki. Akapita vyumba vvya chini kisha akaja juu. Akanikuta nimeketi kitandani. Sikumbuki nilikuwa nafanya nini. Akacharuka, "Wewe ndio unaongoza kundi la watoro sio?"
"Hapana." Nikamjibu.
"Hapana kivipi. Wenzako si hao wanakimbia huko nje?" Nikabaki kimya. Namtazama. Akanisogelea, akavuta sweta niliyokuwa nimevaa sehemu ya begani huku akiniamuru, "Twende ofisini ukanieleze vizuri."
Hao kiguu na njia hadi ofisini kwake.
"Jina lako nani tena?"
"Gregory"
"Una la kujitetea? Nikikuadhibu utasema nimekuonea?"
"Ndio utakuwa umenionea."
"Nimekuonea kivipi?"
"Sijafanya kosa lolote."
"Hebu acha masihara. Wewe umejificha kule Mawenzi wakati wenzako wako katika vipindivya dini kisha unasema kuwa huna kosa?" Alianza kupandisha mori. Mimi nimetulia tu.
"Sijajificha mwalimu."
"Wenzako wako wapi sasa hivi?" Aliniuliza huku akinionyesha ratiba inayoonyesha kuwa wakati huo ilikuwa ni vipindi vya dini.
"Mimi huwa siendi kwenye vipindi vya dini." Niliangusha bomu. Likatua kichwani kwake kwa kishindo kilichomyanyua toka kitini alikokaa na kuanza kunisogelea na fimbo yake tayari kunichapa.
"Naona tunataniana. Yaani unakiri kuwa mtoro sio leo tu bali siku zote!" Aliropoka.
"Mimi sio mtoro. Sihudhurii vipindi vya dini maana hakuna dini inayowakilisha mtazamo wangu wa kiimani." Bomu jingine. Hili lilimrudisha kwenye kiti.
"Gregory acha utundu wako. Kwani wewe sio mkristo?"
"Hapana mwalimu. Sina dini. "
Wakati huo nilikuwa mfuasi wa imani ya Kirasta ambayo niliichukulia kama mfumo wa maisha zaidi ya dini. Kwahiyo wakati wa vipindi vya dini nilikuwa najisomea Biblia mwenyewe. Nilikuwa bado niko katika safari ya utafiti na kujitafuta. Ila nilishaamua kuwa mimi sio mkristo. Kabla ya hapo nilikuwa Mluteri kutokana na sababu za kihistoria na kijiografia. Wamisionari toka Ujerumani walifika Old Moshi ambako wakazi wake wengi ni Waluteri. Ina maana ningezaliwa Rombo au Kibosho, uwezekano mkubwa ningekuwa Mkatoliki. Unaona jinsi dini zetu hizi tunazofikia hatua ya kutoana macho tumezipata kwasababu za kijiografia tu? Hatunazo kwakuwa tulitafiti na kuchambua na kusaka na kutafuta. Hapana, ni kutokana na tulipozaliwa. Ningezaliwa Zanzibar, uwezekano mkubwa ningekuwa Muislamu. Basi wakati huu nakutana na Medukenya nilikuwa kwenye safari hii muhimu sana ya kutafuta ukweli juu ya Mwafrika bila kupitia katika falsafa za walioleta utumwa na ukoloni (waarabu na wazungu).
"Huna dini kivipi? Kwani wazazi wako ni dini gani?" Aliniuliza.
"Wazazi ni Waluteri."
"Sasa inakuwaje unasema huna dini?"
Hapa alinipa nafasi ya "kumhubiria" na kuotesha mbegu ya ukombozi wa fikra.
"Imani na masuala ya kiroho sio mambo ya mkumbo. Haya ni mambo ya mtu binafsi. Wazazi wangu kuwa Waluteri haina maana kuwa lazima mimi nami niwe Mluteri."
"Dini ni ya wazazi wako." Aliniambia huku akionyesha kuwa na hamu ya kunisikiliza lakini wakati huo huo akitaka bado kuonyesha ubabe wa ki-ualimu.
"Nani kasema dini ni ya wazazi? Imeandikwa wapi?" Nilimuuliza kisha nikamwambia kuwa kama dini ni ya wazazi, basi wazazi wetu wameasi maana huko nyuma mababu zetu hawakuwa Wakristo au Waislamu. Kwahiyo kuna wakati ambapo wazazi wetu waliasi dini za wazazi wao na kufuata dini mpya zilizoletwa na wamisionari na mabwana wa biashara ya utumwa. Isitoshe, biblia ambayo yeye anaiamini inasema kuwa kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe.
Kijasho kilimtoka lakini hakutaka kuonyesha.
"Hizo fikra umepata huko mtaani zinakupotosha. Mtazamo huu unaweza hata kukuharibia maendeleo yao darasani." Aliniambia na kuniuliza dini yangu.
"Sina dini. Ila ninafuata mfumo wa maisha wa Kirasta ambao unajumuisha masuala ya imani juu ya mungu."
"Hebu shika chini. Urasta si uhuni tu wa huko mtaani? Hebu shika chini acha ukorofi wako. Uvivu umekujaa unatafuta njia za kuuhalalisha." Mara alinibadilikia. Kawa mbogo.
"Urasta sio uhuni mwalimu. Huu ni mfumo wa maisha unaomtazama Mwafrika, historia na utamaduni wake kama kielelezo kamili cha namna ya kuishi, kuabudu, kula, kutafakari, n.k."
"Nasema shika chini. Uhuni huo unauacha getini. Sio hapa."
"Hunichapi mwalimu. Urasta ni Uafrika. Sio uhuni. Kama ni uhuni mbona tunasoma biblia mnayosoma nyie?"
"Kama unasoma biblia si ungeenda kule chapel ukajiunga na wenzako?"
"Suala sio biblia. Suala ni tafsiri. Kama suala ni biblia si kusingekuwa na madhehebu mengi namna hii ya kikristo. Hawa waislamu wanasoma biblia."
"Gregory acha kupoteza muda. Shika chini."
"Huwezi kunichapa wakati sina kosa."
Mpaka wakati huu nilishajua kuwa nimeshinda. Alionekana kutaka kunichapa kama njia ya kutotaka kushindwa na mwanafunzi. Yeye ni mwalimu mkuu msaidizi, mtu mzima, na mrefu, atashindwaje na mwanafunzi? Kichwa kilikuwa kinanielemea kwa furaha. Sikujua nilipata wapi nguvu za kumjibu namna ile. Medukenya alikuwa akiongopeka. Sio kama Bino, mwalimu mkuu...ambaye naye tulikuja kushusha nguvu zake siku ile pale kwenye uwanja wa mpira wa shule ya msingi...kisa cha siku nyingine hiki (Hashimu, Isa, Mgeta, Mponezya, mnakumbuka?).
Mara akaweka fimbo chini na kuniambia niandike barua kwake kueleza msimamo wangu juu ya kuhudhuria vipindi vya dini. Barua hiyo hadi leo sijaiandika. Kilichofuata ni kuwa kila ijumaa wakati wa vipindi vya dini mimi nilikuwa naondoka zangu kupitia njia ya dukani kwa Kishuu (ingawa njia fupi ilikuwa ni ile ya kupitia Bino Road, ambayo wanafunzi hatukuipenda maana Bino alikuwa akiitumia) kwenda kwa Babu Fulani Mkushi Karudi, rasta aliyekuwa mhandisi wa ndege nchini Jamaika lakini akaamua kuondoka Babiloni kuja Sayuni kuwa mkulima na mtabibu wa kutumia vyakula. Babu alikuwa na misimamo mikali hasa. Alikuwa hagusi pesa, mara nyingi anakula chakula kibichi, nyumba yake haikuwa na mlango (mlango kazi yake nini?), nyumba yake ilikuwa imejengwa kwa nyasi....Fulani anahitaji kuandikiwa kitabu kabisa.
Toka siku ile Medukenya hakuwahi kuingia kwenye anga zangu tena.

HUU NDIO UKOMBOZI!

Marekani imekwenda Iraki kuwakomboa wananchi wa nchi hiyo maana inawapenda sana sana sana. Inawapenda sana ndio maana ililazimisha Umoja wa Mataifa kuiwekea nchi hii vikwazo ambavyo havikumuumiza Saddam na kundi lake bali wananchi wa kawaida. Inawapenda sana ndio maana ilikuwa ikimuunga mkono Saddam kwa muda mrefu na hata kumpa silaha, ujuzi, na fedha. Marekani inawapenda sana wananchi wa Iraki ndio maana Rumsfield alikwenda kumtembelea Saddam Hussein jijini Baghdad kama picha hii inavyoonyesha.
"Faida" za "ukombozi" huu ni nyingi sana: umeme hakuna, maji hakuna, wenye magari wanasubiri kwenye vituo vya mafuta zaidi ya wiki (katika nchi ya pili kwa wingi wa mafuta), raia wasio na hatia wanauwa bila huruma na pande zote (yaani Wamarekani na wale wanaowapinga Wamarekani), wananchi wamepoteza ndugu na jamaa zao na wanaendelea kuwapoteza, wengine wamepata ulemavu wa maisha, watoto hawaendi shuleni, madaktari na wasomi wengine wanakimbia nchi, misikiti, hospitali, na makaburi vimeteketezwa kwa mabomu, nyaraka mbalimbali na mali za kihistoria vimepotea, nyanja ya mafuta iliyokuwa inamilikiwa na umma imewekwa mikononi mwa makampuni ya Marekani kwa mikataba ambayo haikuwa na tenda wala ushindani (ilikuwa ni kupeana), unyama usio na kifani umefanywa na askari wa taifa hili la "kistaarabu" la Marekani dhidi ya wafungwa. Ripoti imetolewa jana kuonyesha unyama wa askari hawa wa Marekani. Bonyeza hapa uone "ukombozi" uliofanywa kwa miaka miwili nchini humo.

12/14/2004

NENO BUNGE

Kumbe neno "bunge" lilitoka kwa mshairi wa Tanga, Mwinyi Katibu Mohamed Amiri. Huyu bwana alianza ushairi mwaka 1940. Ndiye mtunzi wa shairi la ‘Utenzi wa Uhuru wa Tanganyika’ Na neno 'bunge" linatokana na utunzi wake.

UNAWEZA KUNISAIDIA?

Tafadhali sana nisaidie. Nashindwa kuelewa. Ziwa "Victoria" linafanya nini Tanzania? NInakubali kuwa nchi yetu ni masikini (ingawa kwa ni tajiri sana kimali asili), lakini umasikini wetu kiuchumi unatuzuiaje kuenzi watu wetu kwa kutumia majina ya mashujaa, manabii, wafalme, machifu, malkia, waliojazana katika historia ya nchi na bara letu? Ninaposema tujikomboe unadhani ninatania? Kulipa ziwa jina linaloendeleza heshima, utu, na utamaduni wetu tumeshindwa. Kama tumekosa majina ya maana usukumani na uhayani ikabidi twende hadi Uingereza.... mbona kuna kazi? Mko yatari tusaidiane kazi hii ya kurudisha historia, utamaduni, uhai na nafsi zetu zilizotekwa? Aliye tayari anyooshe kidole...kisha aje hapa bloguni tuhangaike naye.

BARUA TOKA LONDON: WATANZANIA TUNAJIFAHAMU?

Barua hii toka London ya Freddy Macha nimeipenda sana maana inaonyesha jinsi gani tunaumwa ugonjwa wa kutojipenda na kujifahamu. Ugonjwa huu madhara yake sio tu kwenye saikolojia yetu kama taifa, bali unajionyesha pia jkwenye nyanja nyingi kama ya uchumi. Tunadhani kuwa matatizo yetu kiuchumi, na pia kiutawala hayana uhusiano na kiwango cha utaifa na uzalendo tulichonacho. Kongoli hapa uisome. Usisahau kuwa makala na hadithi za Freddy Macha ziko hapa bloguni, chini ya makala zangu.

UTUMWA HIVI SASA NI HISTORIA?

Kama unadhani kuwa biashara ya utumwa hivi sasa ni historia, JIKOMBOE! Nambiza Joe Tungaraza kanitumia habari hii kuhusu utumwa huko Mauritania.
Wakati nikisoma habari hiyo, nilitembelea mjadala kuhusu utumwa katika tovuti ya BBC. Kuna bwana mmoja kanimaliza kabisa. Yeye anadai kila mtu, hata katika nchi za magharibi, ni mtumwa. Anasema kuwa minyororo huku Ughaibuni ni ya kisaikolojia. Haya ndio maneno yake:
We're all slaves, even in the western world. Why else would everyone spend their entire lives working away from their loved ones and family, only allowed to see them at evening time and the first thing in the morning if they are lucky. The only difference is that the chains in the western world are psychological ones. - Frank, USA.

Pia katika pitapita zaidi ndani ya tovuti hiyo nikakuta habari nyingine hapa kuhusu utumwa barani Afrika. Habari nyingine zaidi ziko hapa, hapa, na hapa.

Kuna habari nyingine hapa ya kusikitisha juu ya biashara ya kuuza watoto barani Afrika. Unaweza pia kutembelea tovuti ya shirika la Anti-Slavery International.

12/13/2004

UCHAGUZI MKUU GHANA NA TEKNOLOJIA

Matokeo ya uchaguzi mkuu uliomalizika karibuni huko Ghana yalikuwa yanatumwa papo kwa hapo kwa wapiga kura kupitia simu za mkono.

MKUTANO JUU YA INTANETI NA SIASA

Fuatilia mkutano uliomalizika katika chuo kikuu cha Harvard juu ya mtandao wa tarakilishi na siasa, ambapo masuala ya blogu yalijadiliwa. Katika mkutano huu, yule mwanadada wa Kenya, Ory, alitoa mada iliyoitwa Global Voices: Voices From the Kenyan Blogosphere.

12/12/2004

SHIRIKI KUTENGENEZA KAMUSI ELEZO

Mapinduzi ya zana mpya za mawasiliano na habari yanawezesha watu wa kawaida kufanya mambo ambayo hapo awali yalikuwa yakifanywa na watu wa tabaka la wasomi na matajiri. Kwa mfano, blogu inawezesha watu wote kuwa watoa na wapokea habari. Hapo awali wananchi wa kawaida tulikuwa tunameza kila tunacholishwa na vyombo vikubwa vya habari vinaomilikiwa na tabaka la matajiri na watawala. Leo hii, tumekuwa walaji na wazalishaji wa habari. Mwandishi Dan Gilmor katoa kitabu kinachoelezea kwa kina suala hili. Amekuja na dhana ya Uandishi wa Umma. Au Uandishi wa Wana wa Nchi. Kitabu chake kinaitwa We The Media: Grassroots Journalism By the People For the People. Unaweza kukisoma bure kikiwa mtandaoni au ukitaka kichape. Hakikisha umeongeza ukubwa wa herufi zake usije ukaumiza macho yako. Nenda hapa usome habari zaidi juu ya hii dhana ya Uandishi wa Wana wa Nchi. Tembelea OhMyNews ambao ni mfano mzuri sana wa mafanikio ya mapinduzi haya yanayofanya kila mwananchi kuwa mwanahabari.

Sijui kama unajua kuwa kamusi elezo (encyclopaedia) ambazo hapo nyuma zimekuwa zikiandikwa na "wasomi" zinapewa changamoto na kamusi elezo ambazo mtu yeyote yule anaweza kuandika jambo humo na hata kuhariri yaliyoandikwa na wengine! Wikipedia ni kamusi elezo maarufu hivi sasa mtandaoni. Wiki ni neno toka Hawaii lenye kumaanisha " haraka." Kuna Wiki pedia ya Kiswahili hapa (nakushauri ushiriki katika uandishi na uhariri wake) na hii hapa ni ya kiingereza. Ukiachilia mbali kamusi elezo ya mtandaoni (wikipedia) kuna kamusi ya maneno ya mtandaoni iitwayo Wikitionary. Hii nayo ni yetu wote. Kila mmoja anaweza kuandika, kuongeza, kupunguza, kusahihisha, kuhariri, n.k.

ITEMBELEE SERIKALI NA BUNGE LAKO

Hii ndio tovuti ya siri-kali yako: http://www.tanzania.go.tz/index2k.html
Na hili hapa ni bunge lako: http://www.parliament.go.tz/bunge/bunge.asp

Hakikisha una kamusi mkononi ndipo utembelee tovuti ya bunge. Wabunge wetu "tumewachagua" ili watuwakilishe sisi akina Magoti, Msechu, Kulusumu, Riziwani, Msembechu, Elibariki, n.k. lakini lugha wanayotumia ni ya akina Jones, McMurray, Phillips, na Howard. Hili ndio bunge letu. Linatuuza waziwazi, mchana wa jua la saa sita. Ukikutana na Pius Msekwa naomba unisaidia kumuuliza, tovuti ya bunge la Watanzania si inapaswa kuwa katika lugha inayotumiwa na Watanzania wote? Au tovuti hii imeundwa kwa ajili ya "watawala wapya" wanaotawala kwa kidhibiti-mbali:

NINGEKUWA NA UWEZO...

Hivi majuzi nilisema kuwa ningekuwa na uwezo nigefanya binadamu tuweze kuendesha magari huku tukiwa tumelala.
Leo ninaongeza: ningekuwa na uwezo ningeongeza masaa ya siku yawe zaidi ya 24!

WAGOMBEA URAIS WA MAISHA

Ukiwauliza viongozi wa juu wa vyama vya upinzani Tanzania wana mawazo gani juu ya Marais ambao katika historia wamewahi kujitangaza kuwa Marais wa Maisha (kama akina Bokassa, Banda, n.k.). Viongozi hawa wakiongozwa na Augustine Lyatonga Mrema (mzee wa "nji hii") , kufuatiwa na John Momose Cheyo (Bwana Mapesa), bila kumsahau Maalim Seif Hamad (anayedai kuwa watu wasio na ndevu makazi yao ni jikoni...) na wengine ambao hata ubalozi wa nyumba kumi hawawezi kupata...watakujibu kuwa Urais wa maisha ni udikteta. Urais wa maisha ni kinyume na misingi na kanuni za demokrasia.

Lakini wakati huo huo, viongozi hawa wamekuwa ni "wagombea urais wa maisha."
Sijui kama unaweza kunisaidia kidogo...siwaelewielewi hawa viongozi wa vyama vyetu.

SIKUJUA MUNISHI KAINGILIA SIASA NAMNA HII

Hivi unadhani Munishi amebaki kwenye kuimba na kurekodi kwaya? Mtembelee hapa ujionee mwenyewe.

UTACHAGUA KIDOLE AU PETE

Pete au kidole?...thubutu! Najua utachagua kidole. Lakini sio huyu mwanajeshi.

12/11/2004

YESU! KIIRU! BLOGU LAKI MBILI ZA WAIRANI!

Irani ni moja ya nchi ambazo teknolojia ya blogu imevaliwa njuga na wananchi wake. Hii ni nchi ambayo uhuru wa fikra, habari, na mawasiliano unawekewa vizingiti na utawala wa wanaojiita waislamu. Hivi karibuni niliandika juu ya wanablogu waliokamatwa kwa kutoa mawazo yao. Kuna zaidi ya blogu 200,000 (laki mbili) za Wairani. Kati ya hizo, 65,000 zinaandikwa kwa lugha inayozungumzwa na wengi nchini humo, Parsi. Lugha hii ndio ya nne kwa umaarufu katika ulimwengu wa blogu. Pamoja na kukamatwa kwa wanablogu wa nchi hiyo, blogu imebaki kuwa ndio chombo cha habari ambacho watawala wa nchi hiyo wameshindwa kukikaba koo kama vyombo vingine kama magazeti kama makala hii inavyotupasha. Wakati wenzetu Irani wana blogu laki mbili, Tanzania tuna blogu tatu. Na katika hizo, wanablogu wa Furahia Maisha Yako na Kona Yangu sijui nini kimewatokea. Wamekuwa kimya. Huyu wa Kona Yangu alikuwa anaandika juu ya mambo ya "wakubwa." Isije ikawa kaambiwa afunge domo lake kubwa! Unajua wa-twawala wasivyopenda kuambiwa ukweli. Kama wanavyotudanganya ili tuwape kula, nao wanataka tusiwape ukweli wa mambo. Wanataka tuwe waongo kama wao. Wanataka tufanye kati ya haya: 1. Funga domo! 2. Kama ukishindwa, ukiufungua usiseme ukweli hata kama hizi ni "zama za ukweli na uwazi." Kuna wakati niliuliza kama midomo hiyo wanayotumia kudanganya umma wanawezaje kuitumia makanisani na misikitini?

12/10/2004

KISWAHILI NA WAMAREKANI WEUSI

Mwezi huu Wamarekani weusi watasherehekea ile sikukuu ya Kwanzaa ambayo hutumia maneno mengi toka kwenye lugha yetu tunayoidharau ya Kiswahili. Pata undani wake hapa na hapa.

SULEIMANI NA "HEKIMA" ZAKE

Jina la mfalme Suleimani limenijia wakati nikivunjika mbavu nikifikiria jinsi ambavyo watu mtaani kwetu (Tanzania) na kwingine nchini wanavyoazima majina na kushindwa kuyatamka. Jina langu la zamani, Gregory, lilikuwa likitamkwa Kiregori! Nimemkumbuka jamaa mmoja mtaani anaitwa Selemani. Amenikumbusha habari za mfalme Suleimani wa kwenye biblia. Mfalme huyu anadaiwa kuwa alipewa hekima na mungu wa wayahudi, Yehova. Basi nikajiuliza: hivi hekima zake ndio zilimfanya akaamua kuwa na wake 300 na "nyumba ndogo" 700? Kwa ujumla, usije ukafikiri nimekosea, alikuwa na wanawake 1000. Ili uweke picha hii vizuri akilini mwako fanya mahesabu haya. Mwaka mmoja una siku 365. Yeye alikuwa na wanawake 1000!
Suleimani huyo...

KISA CHA STELA KIMENIKUMBUSHA...

Kisa cha Stela kimenikumbusha matukio mengi sana. Jana baada ya kuandika kisa kile nilimkumbuka Esta. Naye sijui anapumulia wapi siku hizi. Esta alianzana nami baada ya kusikia kwenye "bomba" kuwa niko na Stela. Stela, ingawa alichukuliwa na Frenki na kuniacha na majonzi, alikuwa kama vile ameniwekea sumaku. Esta alikuwa "mtalaamu" hasa. Alikuwa na marafiki kila upande. Ukilinganisha "utaalamu" wake kwenye haya mambo, mimi nilikuwa shule ya awali, naye alikuwa amehitimu chuo kikuu!

Sikumbuki alivyonipata. Nilishtukia tu ghafla ameshakuwa rafiki yangu. Nami nimeshakuwa wake. Unaona mwenyewe alivyokuwa matata. Bila kujielewa nikawa kwenye himaya yake. Na taarifa mtaani kwao na kwetu zikaenea, "Kregori anatembea na Esta...."

Esta ni yale macho. Uwiiii...n'tapiga mayowe miye. Unadhani nitakaa niyasahau? Macho yake yalikuwa meupe pe! Makubwa ya mviringo kama embe maji. Kilichonikata maini hasa ni jinsi alivyokuwa na tabia ya kuyalegeza hadi unaweza kudhani kuwa zimebaki sekunde tatu au nne kabla hayajaanguka. Unafungua viganja vya mikono tayari kuyadaka. Enzi hizo kulegeza macho ilikuwa iko kwenye fasheni. Alikuwa na tabia ya kulegeza macho kisha anatabasamu...meno nayo meupe kama weupe...Hasemi kitu. Ananitazama tu huku anatabasamu. Hakuwa na tabia ya kuongea sana. Sio kama Stela. Jana sikuwaambieni. Stela "ana mdomo." Pale umefika. Sio Esta. Yeye ni mrembuaji. Anaongea kwa macho na tabasamu. Nakumbuka pia kaka yake, tofauti na vijana wengi ambao wanaweza hata kuwapiga vijana "wanaomendea" dada zao, yeye alikuwa rafiki yangu kwa chati. Sio wa karibu sana, ila sio adui. Alikuwa na nidhamu fulani. Inawezekana ilitokana na kuwa kamanda wa chipukizi. Alisifika sana kwa hili.

Kuna wakati Esta alipomaliza shule alikuwa anauza kwenye kioski kimoja pale kituo cha mabasi Moshi mjini. Nikawa nikitoka maktaba (ambako palikuwa kama nyumbani kwangu...sikumbuki niliibaga vitabu vingapi!) naenda pale kioski. Kumtazama. Kumtamani. Kusuuza roho.

Kabla sijakaa na Esta vizuri, mara akatokea Adela.
Adelakwini.
Adela alikuwa anakaa pale jirani na kwa babu yangu. Nikiwa barazani kwa babu yangu ninaona nyumbani kwa akina Adela. Na wakati mwingine namuona Adela mwenyewe. Akijua nimeshuka kwa babu yangu atajipitisha pale nje kwao kila sekunde inapogonga. Naye alikuwa ana marafiki wengine ingawa alikuwa anakataa. Kila wakati namuona anaongea na wanaume tena wakubwa wakubwa. Nikimjia juu anasema, "Ah, yule mkubwa namna hiyo..."

Ukikutana na Adela mwambie kuwa najua alikuwa ananidanganya. Mdogo wake Adela, jina nimelisahau, alikuwa ananipenda sana. Alipenda niwe na dadake. Kila akiniona anasema, "Nikakuitie dada?" Au, "Dada amepandisha huko juu atarudi sasa hivi." Ataniambia hata kama sijamuuliza.

Lakini kulikuwa na kasheshe. Wote hawa walikuwa wanasoma shule moja. Na dada yangu alikuwa anawafundisha. Tena siku moja kukatokea ugomvi shuleni kuhusu mahusiano ya wavulana na wasichana. Majina yakatajwa. Jina langu halikukosekana. Jioni nimetulia nyumbani, washikaji wakaja mbio mbio kunipasha kabla dada yangu hajarudi toka kazini. "Wanafunzi wanaoenda disko pale kwa madigirii wametajwa na wavulana wanaoenda nao." Kama ni kwa madigirii lazima nitajwe. Nilikuwa sikosi.

Nilisubiri zaidi ya mwezi, mwezi na nusu, miezi miwili, mitatu, mwaka... dada yangu aniulize juu ya mahusiano yangu na wanafunzi wake lakini hakusema kitu. Alikuwa mkali kweli. Angejua alivyonitesa. Kila akinitazama au akiniita najisemea, "Mungu wangu, sasa ananiuliza." Wapi. Hadi leo hii hajagusia lolote. Nitamtumia kisa hiki kumkumbusha na kuumuliza kwanini hakuniuliza chochote?

Hasa hasa ninachotaka kusema ambacho nimekikumbuka kutokana na kuandika kisa cha Stela jana ni kuhusu timu ya mpira mtaani kwetu (Naona unakunja uso! Unataka stori za akina Esta na Adela?...Naweka akiba!) Basi siku moja tulikuwa na mechi kabambe na timu ya mtaa wa chini. Pale mtaani kwetu kulikuwa na mganga wa jadi. Tukaamua kumwendea. Tulikuwa tunasikia timu kubwa kama Yanga, Simba, Gor Mahia, Abaluhya (AFC Leopards), Nyota Nyekundu, n.k zinakwenda kwa wazee wa tunguri. Tukaona nasi twende tukachukue kizizi cha ushindi. Mganga yule akakubali. Akasema tutapata ushindi wa nguvu. Tusiwe na hofu. Akaanza manjonjo yake. Akaongeaongea kiarabu huku akirusharusha usinga huku na kule, akachoma ubani, kisha akatupaka mafuta na kitu cha rangi nyeusi (baadaye nilikuja kugundua kuwa kile kitu cheusi kilikuwa ni mkaa toka jikoni kwa mkewe! Yale mafuta huenda ilikuwa ni Vaseline Petroleum Jelly!). Akanipaka mimi zaidi maana nilikuwa ni mlinda mlango. Tulimpa pesa. Sikumbuki ilikuwa kiasi gani.

Basi tukaondoka zetu kwenda kuchukua ushindi wa nguvu dhidi ya timu yenye wachezaji wakali wa mtaa wa chini. Ndugu yangu, SIKU HIYO TULIPIGWA MABAO KAMA VILE TUMESIMAMA! Unajua timu zile za mtaani mnafungana hata magoli 100. Sikumbuki tulitiwa ngeu ngapi. Ninachojua ni kuwa tulifungwa idadi ya mabao ambayo kawaida washabiki husema, "Wamafungwa magoli yasiyohesabika."

Ilikuwaje tukafungwa wakati tulikuwa na kizizi? Tulitafuta jibu hatukupata. Baadaye nikahisi labda kwakuwa tulichezea kwenye uwanja wa kanisa hivyo "dawa" zile zikaisha nguvu kutokana na uwepo wa mungu.

Hivi mkaa unaweza kuzuia magoli? Yule mzee wa tunguri alitupata kisawasawa. Baadaye tulikuwa tukikutana naye anatabasamu tu. Hakutuuliza matokeo yalikuwaje. Kuanzia hapo tukaamua kurudia "vizizi" tulivyozoea ambavyo ni pamoja na betri za redio zilizoisha nguvu (unazipondaponda na kuziweka golini), ndulele (unazichimbia katikati ya goli), na kukunja "ngudo" mpira unapokaribia goli (ngudo ni kukunja vidole, kimoja juu ya kingine), na mambo yakiwa mabaya sana au wakati wa penati, tunabinya korodani zetu!

SHAIRI-ELEKTRONIKI: MAPINDUZI YANA RANGI...

*(unawe kubofya sehemu zenye rangi ya njano wakati wowote)
MAPINDUZI YANA RANGI

Mapinduzi!
Zinduka
Pindua
Badili.

Mapinduzi ni waridi
Lililochanua kule Jojia,
Eduard Shevardnadze
Virago alifungasha.

Mapinduzi ni kiludhu,
Kule Chekoslovakia
Wa-"twawala"
Moto uliwawakia.

Mapinduzi
Yana rangi,
Rangi yake ya machungwa
Tena ya Muheza
Yaliyokomaa,
Huoni
Kiev ni machungwa tupu?

Mwenye macho
Haambiwi tazama.

12/09/2004

TAFADHALI NAKUSIHI...

Mzalendo mwenzangu,
moja ya nguzo ya uzalendo ni maarifa. Kwa kuanza, kanunue au kaazime katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kisha isome. Tafadhali sana. Nakusihi.

HAYA NI MATUSI...

Hivi ndivyo wangesema mtaani, "Jamaa kafanya matusi ya nguvu..."
Duniani kuna mambo. Aliyetengeneza sinema ya The Passion of Christ, Mel Gibson, kanunua kisiwa!

MRUDISHO NYUMA WA "STELA YUKO WAPI?"

Mmoja wa wasomaji wa blogu hii kanikumbusha kasheshe iliyoambatana na kitabu cha Rosa Mistika. Simtaji jina. Kanikumbusha mbali. Haya ndio maneno yake:
"Maana ni kati ya Vitabu (yaani Rosa Mistika) vilivyokuwepo Nyumbani kwetu na nilipotaka kukisoma kile kitabu kilipotea katika mazingira ya utatanishi mpaka leo.Yaani dada wakubwa na kaka walikataza nisisome."
***************** ************************
Ndugu yangu, umenikumbusha mbali kweli. Nadhani vitabu vya David Mailu kama After 4:30 navyo vilitoweka "kinamna." Kaka na dada wakubwa walitaka kusoma wenyewe!

MAHOJIANO YA MWALIMU NYERERE

CHARLAYNE HUNTER-GAULT: You mentioned the one-party rule in your country where you were president for four terms during which time you promoted the principle of "Ujamaa," socialism, and you have acknowledged that it was a miserable failure. What lessons, in retrospect, do you draw from that and the kind of economies that African countries might more profitably pursue?
JULIUS NYERERE: Where did you get the idea that I thought "Ujamaa" was a miserable failure?
CHARLAYNE HUNTER-GAULT: Well, I read that you said socialism was failure; the country economically was in shambles at the end of the experiment.
JULIUS NYERERE: A bunch of countries were in economic shambles at the end of the 70s. They are not socialists. Now, today it needs so much courage to talk about socialism, therefore, perhaps we should change the phraseology, but you have to take in the values of socialism which we were trying to build in Tanzania in any society.
CHARLAYNE HUNTER-GAULT: And those values are what?
JULIUS NYERERE: And those values are values of justice, a respect for human beings, a development which is people-centered, development where you care about people you can say leave the development of a country to something called the market which has no heart at all since capitalism is completely ruthless, who is going to help the poor, and the majority of the people in our countries are poor. Who is going to stand for them? Not the market. So I’m not regretting that I tried to build a country based on those principles. You will have to--whether you call them socialism or not--do you realize that what made--what gave capitalism a human face was the kind of values I was trying to sell in my country.
CHARLAYNE HUNTER-GAULT: So what’s the answer? Because, with all due respect, the economy of Tanzania did not thrive under the socialism that you practiced. So what is the--what do you see as the answer for African countries which are still predominantly poor?
JULIUS NYERERE: The problem is not a question of socialism. You have to deal with the problem of poverty. You have to deal with the problem of poverty in your country, and your country is not socialist, or we’re in trouble. People in rich countries don’t realize the responsibility of handling poverty in countries like mine. But those countries will develop. Countries in Africa are poor, both capitalists and socialists, and today we don’t have a single one with these socialists.
CHARLAYNE HUNTER-GAULT: Finally, you’ve been critical of some western countries and their roles in Africa. At the same time you’ve called on western nations to help--I think your phrase was clean up the mess in Rwanda and Burundi. Can you explain what at least sounds like a contradiction?
JULIUS NYERERE: Well, I’m saying some of the problems we are now handling in Africa, some of the mess we’re trying to clean up in the continent we have inherited, the mess of the borders we have inherited.
CHARLAYNE HUNTER-GAULT: The colonial powers drew the borders.
JULIUS NYERERE: Yes. The colonial powers and some not colonial powers in Africa have supported regimes which are very corrupt on that continent. I think now they should stop backing up these corrupt regimes and let Africans in their own way try and establish regimes which can care about people. Some of the governments of the West, and including the United States, has really been very bad on our continent. They have used the Cold War and all sorts of things to back up a bunch of corrupted leaders on our continent. I think they should stop now and let the people of Africa sort out their own, their own future.
***********************************************************************************
Kama unataka kusoma au kusikiliza mahojiano kamili, nenda hapa.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com