12/15/2004

TUTASUBIRI HADI LINI?

Usishangae. Ndio tulivyo. Hatuoni umuhimu wowote wa kutunza urithi, historia, na utamaduni wetu. Wala hatujiulizi kwanini Waingereza wanatumia mamilioni ya pauni kuendeleza utamaduni na lugha yao kupitia British Council (sawa na british cultural center), Wajerumani wanatumia fedha kwa ajili ya Goethe Institut (ambayo ni german cultural center), Wafaransa wana Alliance Francaise (sawa na french cultural center), Wamarekani wana USIS. Kwanini wanaanzisha taasisi kama hizi na kuzisambaza dunia nzima? Kwanini mataifa "yaliyoendelea" sio tu yanasambaza bidhaa zao dunia nzima bali pia na tamaduni zao?

Kwa jinsi tulivyolala, wakati mwingine wanatumia taasisi hizi kutangaza na kuendeleza tamaduni zetu. Mchoraji na mchongaji maarufu kama George Lilanga (kazi zake zinauzwa hapa. ) anatangazwa na kuendelezwa na Alliance Francaise na mashirika na balozi za nchi za "wenzetu." Wasanii wa Kitanzania wanaotaka kufanya maonyesho ya kazi zao, hodi ya kwanza sio wizara ya utamaduni, au ofisi ya waziri mkuu, bali katika vituo vya tamaduni za nchi hizi za magharibi na balozi zao. Tumekwisha. Wasanii wengi, kwa uzoefu wao, wanakwambia kuwa ukitaka kufanya maonyesho ya kazi za sanaa (uchoraji, uchongaji, muziki, ngoma, n.k.) mbele ya kadamnasi inayojali, usiende kwa Watanzania wenzako. Nenda kafanye maonyesho hayo Alliance Francaise au British Council mbele ya wazungu. Sio kwa Watanzania wenzako. Ndio maana hutakiwi kushangaa kuwa gwiji la muziki wa asili duniani, marehemu Dr. Hukwe Zawose, hakuna aliyekuwa akijua kazi zake nchini Tanzania. Wenye santuri zake nchini Tanzania ni wazungu. Watanzania wengi wanadai kuwa walikuwa "wakimsikiasikia" !

Sio hivyo tu, ukiona kazi za wasanii wetu kama michoro ya tingatinga, vinyango vya wamakonde, shanga za kimasai, n.k. zimepamba ndani kwa mtu, basi jua mwenye nyumba sio Mtanzania. Sisi huwa hatupambi na kazi zetu za sanaa. Ukienda nyumba za mabeberu ndio utakuta mikeka, kanga, vinyago, tingatinga, n.k. Hata wanaouza vinyango pale Mwenge, jijini DSM, ndani kwao wamepamba kwa bidhaa za plastiki au udongo toka China au India! Wanaamini kabisa kuwa vinyago na kazi nyingine za kitamaduni ni vitu vya wazungu! Tukiona mtu amevaa mapambo ya kitamaduni na nguo za kitamaduni akilini mwetu tunajisemea, "Atakuwa msanii huyu."

Usishangae kuwa mwanzilishi wa Nyumba Ya Sanaa ni mweupe. Katoka kwao mbali kuja kutuanzishia "nyumba ya sanaa" zetu! Je unajua kuwa mwanzilishi wa makumbusho ya utamaduni wa Msukuma, Bujora, sio msukuma au Mtanzania? Unajua pia kuwa kati ya watu wanaosukuma harakati za kufanya kiswahili kipate hadhi ya juu katika mfumo wa elimu Tanzania ni mwingereza ambaye ana jina la Kinyamwezi? Unajua pia kuwa Mfuko wa Utamaduni Tanzania unapata fedha zake toka mataifa ya nje na sio serikali yetu? Mataifa haya yanatumia fedha za walipa kodi wao kuendeleza utamaduni wetu!
Tutasubiri wengine hadi lini? Lini tutajua kuwa utamaduni wetu ni wetu? Lini tutajua kuwa utamaduni wetu ni mzuri na unafaa kutunzwa, kuenziwa, na kuheshimiwa? Anza kujikomboa leo kwa kuondoa "takataka" za kichina ndani kwako. Tafuta kazi za sanaa; uchoraji, uchongaji, ufumaji, n.k. za Watanzania au Waafrika wenzako. Nyumba yako lazima iwe na sura yako kama Mwafrika. Tusipojijua kwenye dunia ya leo, tutabaki kuwa tegemezi kiakili, kiimani, kiuchumi, kisiasa, kinafsi, n.k. Jikomboe!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com