12/15/2004

HUU NDIO UKOMBOZI!

Marekani imekwenda Iraki kuwakomboa wananchi wa nchi hiyo maana inawapenda sana sana sana. Inawapenda sana ndio maana ililazimisha Umoja wa Mataifa kuiwekea nchi hii vikwazo ambavyo havikumuumiza Saddam na kundi lake bali wananchi wa kawaida. Inawapenda sana ndio maana ilikuwa ikimuunga mkono Saddam kwa muda mrefu na hata kumpa silaha, ujuzi, na fedha. Marekani inawapenda sana wananchi wa Iraki ndio maana Rumsfield alikwenda kumtembelea Saddam Hussein jijini Baghdad kama picha hii inavyoonyesha.
"Faida" za "ukombozi" huu ni nyingi sana: umeme hakuna, maji hakuna, wenye magari wanasubiri kwenye vituo vya mafuta zaidi ya wiki (katika nchi ya pili kwa wingi wa mafuta), raia wasio na hatia wanauwa bila huruma na pande zote (yaani Wamarekani na wale wanaowapinga Wamarekani), wananchi wamepoteza ndugu na jamaa zao na wanaendelea kuwapoteza, wengine wamepata ulemavu wa maisha, watoto hawaendi shuleni, madaktari na wasomi wengine wanakimbia nchi, misikiti, hospitali, na makaburi vimeteketezwa kwa mabomu, nyaraka mbalimbali na mali za kihistoria vimepotea, nyanja ya mafuta iliyokuwa inamilikiwa na umma imewekwa mikononi mwa makampuni ya Marekani kwa mikataba ambayo haikuwa na tenda wala ushindani (ilikuwa ni kupeana), unyama usio na kifani umefanywa na askari wa taifa hili la "kistaarabu" la Marekani dhidi ya wafungwa. Ripoti imetolewa jana kuonyesha unyama wa askari hawa wa Marekani. Bonyeza hapa uone "ukombozi" uliofanywa kwa miaka miwili nchini humo.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com