12/12/2004

SHIRIKI KUTENGENEZA KAMUSI ELEZO

Mapinduzi ya zana mpya za mawasiliano na habari yanawezesha watu wa kawaida kufanya mambo ambayo hapo awali yalikuwa yakifanywa na watu wa tabaka la wasomi na matajiri. Kwa mfano, blogu inawezesha watu wote kuwa watoa na wapokea habari. Hapo awali wananchi wa kawaida tulikuwa tunameza kila tunacholishwa na vyombo vikubwa vya habari vinaomilikiwa na tabaka la matajiri na watawala. Leo hii, tumekuwa walaji na wazalishaji wa habari. Mwandishi Dan Gilmor katoa kitabu kinachoelezea kwa kina suala hili. Amekuja na dhana ya Uandishi wa Umma. Au Uandishi wa Wana wa Nchi. Kitabu chake kinaitwa We The Media: Grassroots Journalism By the People For the People. Unaweza kukisoma bure kikiwa mtandaoni au ukitaka kichape. Hakikisha umeongeza ukubwa wa herufi zake usije ukaumiza macho yako. Nenda hapa usome habari zaidi juu ya hii dhana ya Uandishi wa Wana wa Nchi. Tembelea OhMyNews ambao ni mfano mzuri sana wa mafanikio ya mapinduzi haya yanayofanya kila mwananchi kuwa mwanahabari.

Sijui kama unajua kuwa kamusi elezo (encyclopaedia) ambazo hapo nyuma zimekuwa zikiandikwa na "wasomi" zinapewa changamoto na kamusi elezo ambazo mtu yeyote yule anaweza kuandika jambo humo na hata kuhariri yaliyoandikwa na wengine! Wikipedia ni kamusi elezo maarufu hivi sasa mtandaoni. Wiki ni neno toka Hawaii lenye kumaanisha " haraka." Kuna Wiki pedia ya Kiswahili hapa (nakushauri ushiriki katika uandishi na uhariri wake) na hii hapa ni ya kiingereza. Ukiachilia mbali kamusi elezo ya mtandaoni (wikipedia) kuna kamusi ya maneno ya mtandaoni iitwayo Wikitionary. Hii nayo ni yetu wote. Kila mmoja anaweza kuandika, kuongeza, kupunguza, kusahihisha, kuhariri, n.k.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com