12/10/2004

KISA CHA STELA KIMENIKUMBUSHA...

Kisa cha Stela kimenikumbusha matukio mengi sana. Jana baada ya kuandika kisa kile nilimkumbuka Esta. Naye sijui anapumulia wapi siku hizi. Esta alianzana nami baada ya kusikia kwenye "bomba" kuwa niko na Stela. Stela, ingawa alichukuliwa na Frenki na kuniacha na majonzi, alikuwa kama vile ameniwekea sumaku. Esta alikuwa "mtalaamu" hasa. Alikuwa na marafiki kila upande. Ukilinganisha "utaalamu" wake kwenye haya mambo, mimi nilikuwa shule ya awali, naye alikuwa amehitimu chuo kikuu!

Sikumbuki alivyonipata. Nilishtukia tu ghafla ameshakuwa rafiki yangu. Nami nimeshakuwa wake. Unaona mwenyewe alivyokuwa matata. Bila kujielewa nikawa kwenye himaya yake. Na taarifa mtaani kwao na kwetu zikaenea, "Kregori anatembea na Esta...."

Esta ni yale macho. Uwiiii...n'tapiga mayowe miye. Unadhani nitakaa niyasahau? Macho yake yalikuwa meupe pe! Makubwa ya mviringo kama embe maji. Kilichonikata maini hasa ni jinsi alivyokuwa na tabia ya kuyalegeza hadi unaweza kudhani kuwa zimebaki sekunde tatu au nne kabla hayajaanguka. Unafungua viganja vya mikono tayari kuyadaka. Enzi hizo kulegeza macho ilikuwa iko kwenye fasheni. Alikuwa na tabia ya kulegeza macho kisha anatabasamu...meno nayo meupe kama weupe...Hasemi kitu. Ananitazama tu huku anatabasamu. Hakuwa na tabia ya kuongea sana. Sio kama Stela. Jana sikuwaambieni. Stela "ana mdomo." Pale umefika. Sio Esta. Yeye ni mrembuaji. Anaongea kwa macho na tabasamu. Nakumbuka pia kaka yake, tofauti na vijana wengi ambao wanaweza hata kuwapiga vijana "wanaomendea" dada zao, yeye alikuwa rafiki yangu kwa chati. Sio wa karibu sana, ila sio adui. Alikuwa na nidhamu fulani. Inawezekana ilitokana na kuwa kamanda wa chipukizi. Alisifika sana kwa hili.

Kuna wakati Esta alipomaliza shule alikuwa anauza kwenye kioski kimoja pale kituo cha mabasi Moshi mjini. Nikawa nikitoka maktaba (ambako palikuwa kama nyumbani kwangu...sikumbuki niliibaga vitabu vingapi!) naenda pale kioski. Kumtazama. Kumtamani. Kusuuza roho.

Kabla sijakaa na Esta vizuri, mara akatokea Adela.
Adelakwini.
Adela alikuwa anakaa pale jirani na kwa babu yangu. Nikiwa barazani kwa babu yangu ninaona nyumbani kwa akina Adela. Na wakati mwingine namuona Adela mwenyewe. Akijua nimeshuka kwa babu yangu atajipitisha pale nje kwao kila sekunde inapogonga. Naye alikuwa ana marafiki wengine ingawa alikuwa anakataa. Kila wakati namuona anaongea na wanaume tena wakubwa wakubwa. Nikimjia juu anasema, "Ah, yule mkubwa namna hiyo..."

Ukikutana na Adela mwambie kuwa najua alikuwa ananidanganya. Mdogo wake Adela, jina nimelisahau, alikuwa ananipenda sana. Alipenda niwe na dadake. Kila akiniona anasema, "Nikakuitie dada?" Au, "Dada amepandisha huko juu atarudi sasa hivi." Ataniambia hata kama sijamuuliza.

Lakini kulikuwa na kasheshe. Wote hawa walikuwa wanasoma shule moja. Na dada yangu alikuwa anawafundisha. Tena siku moja kukatokea ugomvi shuleni kuhusu mahusiano ya wavulana na wasichana. Majina yakatajwa. Jina langu halikukosekana. Jioni nimetulia nyumbani, washikaji wakaja mbio mbio kunipasha kabla dada yangu hajarudi toka kazini. "Wanafunzi wanaoenda disko pale kwa madigirii wametajwa na wavulana wanaoenda nao." Kama ni kwa madigirii lazima nitajwe. Nilikuwa sikosi.

Nilisubiri zaidi ya mwezi, mwezi na nusu, miezi miwili, mitatu, mwaka... dada yangu aniulize juu ya mahusiano yangu na wanafunzi wake lakini hakusema kitu. Alikuwa mkali kweli. Angejua alivyonitesa. Kila akinitazama au akiniita najisemea, "Mungu wangu, sasa ananiuliza." Wapi. Hadi leo hii hajagusia lolote. Nitamtumia kisa hiki kumkumbusha na kuumuliza kwanini hakuniuliza chochote?

Hasa hasa ninachotaka kusema ambacho nimekikumbuka kutokana na kuandika kisa cha Stela jana ni kuhusu timu ya mpira mtaani kwetu (Naona unakunja uso! Unataka stori za akina Esta na Adela?...Naweka akiba!) Basi siku moja tulikuwa na mechi kabambe na timu ya mtaa wa chini. Pale mtaani kwetu kulikuwa na mganga wa jadi. Tukaamua kumwendea. Tulikuwa tunasikia timu kubwa kama Yanga, Simba, Gor Mahia, Abaluhya (AFC Leopards), Nyota Nyekundu, n.k zinakwenda kwa wazee wa tunguri. Tukaona nasi twende tukachukue kizizi cha ushindi. Mganga yule akakubali. Akasema tutapata ushindi wa nguvu. Tusiwe na hofu. Akaanza manjonjo yake. Akaongeaongea kiarabu huku akirusharusha usinga huku na kule, akachoma ubani, kisha akatupaka mafuta na kitu cha rangi nyeusi (baadaye nilikuja kugundua kuwa kile kitu cheusi kilikuwa ni mkaa toka jikoni kwa mkewe! Yale mafuta huenda ilikuwa ni Vaseline Petroleum Jelly!). Akanipaka mimi zaidi maana nilikuwa ni mlinda mlango. Tulimpa pesa. Sikumbuki ilikuwa kiasi gani.

Basi tukaondoka zetu kwenda kuchukua ushindi wa nguvu dhidi ya timu yenye wachezaji wakali wa mtaa wa chini. Ndugu yangu, SIKU HIYO TULIPIGWA MABAO KAMA VILE TUMESIMAMA! Unajua timu zile za mtaani mnafungana hata magoli 100. Sikumbuki tulitiwa ngeu ngapi. Ninachojua ni kuwa tulifungwa idadi ya mabao ambayo kawaida washabiki husema, "Wamafungwa magoli yasiyohesabika."

Ilikuwaje tukafungwa wakati tulikuwa na kizizi? Tulitafuta jibu hatukupata. Baadaye nikahisi labda kwakuwa tulichezea kwenye uwanja wa kanisa hivyo "dawa" zile zikaisha nguvu kutokana na uwepo wa mungu.

Hivi mkaa unaweza kuzuia magoli? Yule mzee wa tunguri alitupata kisawasawa. Baadaye tulikuwa tukikutana naye anatabasamu tu. Hakutuuliza matokeo yalikuwaje. Kuanzia hapo tukaamua kurudia "vizizi" tulivyozoea ambavyo ni pamoja na betri za redio zilizoisha nguvu (unazipondaponda na kuziweka golini), ndulele (unazichimbia katikati ya goli), na kukunja "ngudo" mpira unapokaribia goli (ngudo ni kukunja vidole, kimoja juu ya kingine), na mambo yakiwa mabaya sana au wakati wa penati, tunabinya korodani zetu!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com