12/09/2004

SIJUI STELA YUKO WAPI SIKU HIZI

Stela.
Stela alikuwa ndio demu wangu rasmi wa kwanza ukiachilia mbali wale waliokuwa wakubwa zaidi yangu waliokuwa wakinitania "mchumba, mchumba" nami nikawa ninaamini kuwa ni kweli!

Stela. Nakumbuka siku ile niliyomtamkia kwenye sikukuu ya ubarikio kwa jirani yao. Kabla sijamaliza kutamka akasema naye ananipenda. Nadhani sababu mbili zilichangia kufanikiwa kumpata: 1. Nilikuwa nasoma shule ya mjini (jambo lililokuwa linaonekana kuwa ni ujiko) 2. Dada yangu alikuwa ni mwalimu wake (kuwa na urafiki na mdogo wa mwalimu ilikuwa ni ujiko pia). Aliponikubalia tukaagana. Hatua ya kwanza nilifanikiwa. Ila baada ya hapo nilivurunda. Nilikuwa sijui msichana anapokubali kuwa rafiki yako kinachofuata ni kitu gani.

Kama ni kuongea tutakuwa tunaongelea nini? Vitabu? Alikuwa hapendi kusoma vitabu. Mimi nilikuwa nasoma vitabu viwili, viwili, hata vitatu kwa wakati mmoja. Tuongelee muziki? Hakuwa anapenda rege. Soka? Mchezo wa wanaume huo. Yeye si Yanga wala Simba. Mimi nilikuwa Yanga. Siku hizi sijui niko timu gani. Je Wili Gamba? Hakuwa amesoma Kufa na Kupona au Kikosi cha Kisasi wala hakuwa anasubiri kwa hamu kama mimi kitabu cha Hujuma. Akina Alfu Lela U Lela, Machimbo ya Mfalme Suleimani, Kisima cha Giningi, Uhuru wa Watumwa, Mwana wa Yungi Hulewa, Mzimu wa Watu wa Kale, Rosa Mistika (nilichokisoma nikiwa ndani ya shuka ili nisionekana) n.k alikuwa hajawahi kuvisikia.

Lakini kubwa zaidi lilikuwa ni mimi kutokujua unapokubaliwa na msichana ni kitu gani kinafuata. Basi nikawa jioni napita karibu na nyumbani kwao. Nakwenda. Narudi. Nakwenda. Narudi...hadi nitakapomuona. Hata kama nimeona unywele wake. Ninaridhika na kurudi nyumbani. Sikuwa nataka kuongea naye. Nilitaka tu kumuona. Kwanza, nilikuwa sijui tutaongea nini na pili, nilikuwa nina aibu sana.

Nakumbuka siku moja mama yake aliniona nikienda na kurudi. Akanisalimu, "Habari. Wewe si mtoto wa Macha?"

Nikasema, "Ndio." Sauti ilitoka kwa shida. Niliishiwa nguvu. "Anajua ninachofuata hapa?" Nilijiuliza.
"Unatafuta nini?" Aliniuliza.
Kama sio giza angeona uso wangu ukibadilika rangi na pengine mishipa ya uso ikichomoza. "Napita tu." Nilimjibu.
"Nilifikiri kuna kitu unatafuta maana nimekuona ukienda na kurudi...nikakutazama nikasema huyu si mtoto wa Macha? Nikajiuliza usiku wote huu anatafuta nini?"
Nilibaki kimya nikikenua meno yangu makubwa kama sijui nini.
"Haya Macha, usiku umeingia nenda nyumbani. Salimia nyumbani." Aliniambia.
Nikajiondokea. Siku hiyo sikumuona Stela wangu. Sikulala kwa raha.

Baadaye alikuja kujua ukweli akawa ananitania hata baada ya miaka mingi kupita. Akiniona ananiita kwa Kichagga, "Mii o mana." Yaani mume wa mwanaye.

Waswahili walisema kawia kawia....Ndivyo ilivyonitokea. Kutokana na uzembe uliotokana na kutokuwa na "utaalamu" wa kuwa na rafiki wa kike, Stela alitwaliwa na waliobobea kwenye fani. Nikaachwa njiani. Masikini, miye. Kosa langu? Kukosa "utaalamu." Stela alikuwa yu tayari. Alitaka. Mimi nilimfanya kama picha. Napita kwao, nikimuona nakwenda nyumbani nalala kama mtu aliyeshinda bahati nasibu ya mamilioni.

Sikumbuki habari zilinifikia vipi, ila niliambiwa Frenki (jina hili la kutunga) ndio "anamchukua." Roho iliniuma sana. Kila nikimuona alikuwa anazidi kupendeza. Alikuwa anapenda kucheka. Sijui alikuwa anacheka nami au ananicheka. Kila akiniona alikuwa hasemi kitu bila kutumia maneno haya, "Jamani Kiregori..." (Jina langu la zamani ni Gregory). Hapo alikuwa ananimaliza kabisa. Hasa neno "jamani" alivyokuwa akilitamka. Acha tu.

Frenki alijua kuwa Stela alikuwa wangu. Akawa anajiona mbabe kweli. Baadaye, sio kulipiza kisasi, nilikuja kumchukua rafiki yake wa kike wa muda mrefu. Frenki akawa mbogo. Tena rafiki yake huyo alinifuata mwenyewe. Akaunda njama na wenzake za "kunifungia kazi." Akawa anamwambia rafiki yangu mmoja wa karibu, "Yule mshikaji wako tukimuona pale mtaani tutamvunja zile fito zake." Tukawa hata hatusalimiani. Kisa hiki kinahitaji sura yake rasmi.

Stela.
Sijui Stela yuko wapi siku hizi.


Utashangaa. Hutaamini. Ingawa Stela alikuwa ni rafiki wangu wa kwanza, mtu wa kwanza kumpiga busu la "kifaransa" hakuwa yeye. Unadhani alikuwa ni nani? Amini usiamini. Alikuwa ni mdogo wake! Ndio, mdogo wake Stela. Yeye alikuwa mweusi kidogo, mnene kiasi, mfupi. Stela alikuwa mrefu wa wastani na sio mnene sana. Siku hiyo nilikuwa najipitia zangu karibu na kwao kwa matumaini ya kufufua penzi. Basi mdogo wake akatokea. Akaniuliza huku akicheka kama ninamtafuta Stela. Nikakubali. Akasema Stela anaishi Marangu. Mara akanishika mkono, akanivuta pembeni ya barabara huku akitazama huku na kule. Ilikuwa ni kama saa mbili usiku. Akaniuliza, "Unataka nini?" Nikawa sina jibu. Akanivuta karibu yake. Siku hiyo ndio ikawa siku ya kwanza kubusu msichana. Mdogo wake Stela!

Stela, uko wapi siku hizi?

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com