12/06/2004

DUNIA INA AMANI...ZIMEMTOKA NINI?

Nasikia eti yule jamaa mwenye madevu anayeishi mapangoni kule katika nchi inayoongoza hivi sasa kwa kuzalisha majani ya coca yanayotengenezea cocaine, anafurahia sana kazi kubwa anayoifanya Joji Dabliyuu Kichaka ya kumzalishia makuruta wa kupigana katika jihadi aliyoitangaza dhidi ya Marekani na maswahiba wake. Uvamizi wa Iraki umezalisha magaidi kwa kasi kubwa kuliko kipindi chochote katika historia. Kwahiyo, bwana madevu na wenzake wameweza kubana matumizi maana fedha zinazotumika kuzalisha kizazi kipya cha magaidi ni zile za walipa kodi wa Marekani zinazofikia dola bilioni nne kila baada ya siku 10.

Wakati huo huo Joji Kichaka bado yu ndotoni. Wakati Wairaki zaidi ya 70 na Wamarekani 11 wameuawa hadi mwisho wa wiki, na ubalozi wa Marekani nchini Saudi Arabia, ambao uko chini ya ulinzi mkali, umevamiwa na magaidi wasio na woga waliouingilia "mchana mchana" wakiwa na bunduki za rashasha na maguruneti, Joji anadai kuwa eti baada ya kutolewa kwa swahiba wao wa zamani madarakani, Saddam Hussein (yule mwandishi wa kitabu cha Zabina and the King), dunia imekuwa ya amani sana. Labda dunia anayozungumzia ni pale nyumba nyeupe anapoishi. Kwa wakazi wa mji kama Fallujah ambao umekuwa ni mahame kuwaambia kuwa eti dunia imekuwa na amani zaidi kutokana na kuangushwa kwa Saddam, wataona kama unahitaji kupelekwa Milembe ukatazamwe kama kuna "nati" imechomoka. Tazama yanayotokea Darfur, Kongo, Chechnya, na kwingineko...hiyo amani anayozungumzia huyu kibaka wa kura sijui iko wapi.Wairaki hivi sasa hawathubutu kwenda kusali, kusimama kwenye makundi makundi, kupeleka watoto wao shule, kwenda kazini, n.k. Wanaishi katika hofu ya mabomu ya kutengwa barabarani, mabomu ya wanaojitoa mhanga, n.k. Mambo yote haya walikuwa wakiyasikia kwenye "bomba" kuwa yanayokea kwa Waisraeli, na Wapalestina. Sasa yamewafika. Kichaka anadai, "Dunia imejaa amani maana Saddam hayuko madarakani." Hazimo nini?
Anajisifu eti kutokana na uvamizi wa Afghanistani, wananchi wa nchi hiyo, hasa wanawake, wameweza kupiga kura kidemokrasia kwa mara ya kwanza. Lakini hatuambii kuwa baada ya kuondoka siri-kali ya wafuga ndevu kama beberu, Watalibani, nchi hiyo imekuwa ndio namba moja kwa uzalishaji wa majani ya coca yanayouzwa kwa watengeneza madawa ya kulevya.

Haya, "turudi nacho" (wachagga tumezoea kusema hivi), anaposema kuwa wanawake wameweza kupiga kura, mbona Saudi Arabia ambayo ni swahiba wa Marekani bado hairuhusu wanawake kupiga kura? Mbona hatusikii matamko na vitishoi vya kuitaka iwaruhusu mara moja? Mbona Bush na mkewe wanakubali kupokea zawadi wanazopewa na familia ya kifalme ya nchi hiyo isiyo na hata tone moja la misingi ya demokrasia Marekani inalazimisha nchi nyingine kuwa nayo? Cuba imewekewa vikwazo. Kisa? Sirikali yake ni ya kidikteta. Wananchi wake hawana uhuru wa kisiasa na mawazo. Sawa. Je Saudi Arabia? Je Pakistani ambayo Rais aliyekuwa hapa majuzi alichukua madaraka kwa nguvu dhidi ya kiongozi aliyechaguliwa kwa kura?

He, jamani, unafiki ndio nguzo kubwa katika siasa za Marekani. Na unafiki huo na kiburi ndivyo vitamwangusha kwa kishindo cha tembo, pwa!

Marekani kaja juu, "Ooh, Irani isiruhusiwe kuwa na silaha za nyuklia." Ni kitu gani kinawapa majirani zake Irani: India, China, Pakistan, Israeli, haki ya kuwa na silaha hizo lakini Irani?
Wakati huo huo Marekani inalalama juu ya Irani kuwa na mpango wa kutengeneza silaha hizo, yenyewe inaendelea kuzipika tena kwa wingi na sasa inaamua kuzihamishia huko angani kabisa. Yaani hawana hata aibu, kwani wakimuomba mungu wao wanatazama huko angani, na sasa wanaamua kupeleka silaha zao huko. Yasije yakatokea kama yale yaliyoko kwenye ile hadithi ya kutunga ya mnara wa babeli! Niishie hapa. Nilikuwa napunguza "stimu" ya mahasira yangu juu ya Dabliyuu Kichaka.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com