12/06/2004

KRISIMASI

"Vipi krisimasi mwaka huu?"
"Umeshanunua zawadi za krisimasi?"
"Una mpango gani wa krisimasi?"
"Hivi wewe unasherehekea krisimasi?"
"Umenunua kadi za krisimasi?"

Haya ni maswali ambayo ninaulizwa na marafiki, wanafunzi, na watu wengine mbalimbali ninaokutana nao. Badala ya kuwajibu moja kwa moja, nina kawaida ya kuwauliza maswali mengi tu. Kwa mfano, jana nilikutana na marafiki zangu wawili ambao waliniuliza kama nitasherehekea krisimasi. Nikawauliza, "Ninyi mtasherehekea?" Wakajibu, "Ndio."
Nikawauliza, "Hivi mara ya mwisho kushika Biblia, wala sio kuisoma, bali kuishika tu, ni lini?" Wakatazamana, wakacheka. Hawakumbuki. Waliisoma zamani sana.
Nikawauliza, "Hivi kwenye agano jipya kuna vitabu vingapi vinavyozungumzia maisha ya Yeshua (Yesu) toka kuzaliwa kwake hadi kufa?" Wakasema hawajui.
Nikawauliza, "Hivi Yeshua alikufa akiwa na miaka mingapi?" Hawakumbuki.
"Je alitupa amri gani mpya juu ya zile kumi ambazo Musa alizichukua kutoka Misri na kudai kapewa na Mungu mlimani?" Hawajui. Ila wakashtuka, "Unasema Musa alichukua amri kumi toka Misri?"
"Tutazungumzia hilo baadaye. Nijibuni kwanza. Je kitabu kipi ndani ya biblia kinasema kuwa Yeshua alizaliwa tarehe 25 Desemba?" Hawana uhakika kama krisimasi iko kwenye biblia.
"Je, ni kitabu gani cha historia nje ya biblia kinachosema kuwa kuzaliwa kwa Yeshua kulikuwa na tarehe 25 Desemba?"
"Hatujachunguza sana historia hiyo." Wakanijibu.
"Je nini historia ya Krisimasi?" Jibu hawana.
"Je krisimasi ya kwanza ilianza lini?" Hawajui.
"Je mnajua kuwa krisimasi ilikuwepo kabla ya kuzaliwa kwa Yeshua?" Hawajui. Wanashangaa.

Nikapumua. Nikamaliza kwa kuwauliza, "Sasa kama hamjui yote haya? Hamsomi mafundisho ya Yeshua na wala hamjui mbele wala nyuma juu ya historia ya krisimasi, na biblia hamjui inafunguliwa vipi, NI KWA NAMNA GANI MNAWEZA KUSEMA KUWA MNASHEREHEKEA KRISIMASI?"

Marafiki zangu hawa kama walivyo watu wengi wanachosherehekea ni "mkumbo wa kadamnasi" uitwao krisimasi kwa madai kuwa ni sherehe ya kuzaliwa kwa Yeshua. Kipindi chote hiki cha mwezi wa 12, watu wanazungumzia hii sherehe na kununua kadi na zawadi na kupamba kwa taa za kila rangi ila hakuna anayemzungumzia Yeshua. Ukisubiri hadi tarehe 26 Desemba ukawauliza watoto krisimasi ni sherehe ya nini, watakwambia ni sherehe ya baba wa krisimasi (father christmas) ambaye ni mzee mmoja mweupe, macho ya bluu, na nyewele nyeupe ambaye anawapa watoto zawadi za peremende, pipi, na lawalawa ambazo huharibu meno yao!
***************************************++***************************************
NB: Unaweza kusoma makala niliyoandika, nadhani mwaka jana, iitwayo KRISIMASI BILA YESU iliyoko katika kona za makala zangu.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com