12/22/2004

MBONA HUMPENDI PAKA WANGU?

Nimekutana na rafiki abdulahi yangu toka nchi fulani ya Afrika Magharibi. Katika kujuliana hali maana hatujaonana muda kidogo, kanieleza kisanga kilichomkumba. Kisanga kinatokana na Amanda, binti wa kitasha ambaye wameanza naye urafiki muda si mrefu.
Ilianza hivi: Baada ya kupigiwa simu Abdulahi aliaacha shughuli zake na kufunga safari kwenda kumtembelea. Simu ilipoita subuhi siku hiyo alikuwa anaingia duka la Wakorea wanakouza vyakula toka Afrika Magharibi. Akacheki aliyepiga simu: Amanda. Akashangaa maana muda si mrefu katoka kwake alikokuwepo toka jana yake jioni. Akaipokea. Amanda akamtaka aende mara moja.
"Kuna nini."
"We njoo." Amanda akajibu huku sauti ikibadilika kama ya mtu anayekaribia kulia.
"Si uniambie." Abdulahi akasisitiza.
Wapi.
Lazima aende.
Basi huyo akaondoka zake hadi kwa Amanda. Kufika mlangoni anamkuta Amanda macho yamemvimba. Mara anaanguka kilio kama kuna msiba. Mshikaji haelewi ni kitu gani kinaendelea. Baada ya kumbembeleza kwa kama dakika 20 hivi, Amanda akaanza kuongea. Abdulahi hakuamini alichokuwa akisikia.
Amanda ana huzuni kwa muda mrefu. Ameitunza huzuni moyoni mwake kama yai. Leo kashindwa kuvumilia. Ameipasua.
"Kwanini humpendi paka wangu?"
Kwanza kabisa Abdulahi alihisi labda kawa kiziwi. Haiwezekani aliyosikia ndio yaliyotoka mdomoni mwa Amanda. Yaani usumbufu wote huo na kulia kote chanzo ni paka?
Amanda ana paka mmoja mweupe, mnene wa wastani. Virgo ndio jina lake. Kama unataka kukosana naye sema jambo lolote baya kuhusu paka wake. Au usimjali. Mahusiano na paka wake ni kama vile mahusiano kati ya binadamu na binadamu. Anamkumbatia, anapiga naye soga, anambusu, anacheza naye, anampapasa, anamwogesha, n.k. Toka wafahamiane, Abdulahi hajawahi kumgusa Virgo, wala kumzungumzia. Ni kama vile huwa hamuoni. Kumbe kosa. Amanda amekuwa akimtazama tu. Akiteseka.
"Utanipendaje mimi bila kumpenda paka wangu?" Amanda anauliza.
"Kwani umesikia namchukia paka wako?"
"Humchukii. Sijasema unamchukia, nasema humpendi." Amanda machozi yanazidi kumbubujika.
"Unataka ninfanyeje ndio ujue kuwa nampenda?"
"Mbona hujawahi kusema lolote kuhusu Virgo. Hutaki hata kumshika. Virgo kwako ni kama vile hayupo hapa ndani."
"Hiyo ni hofu yako tu mimi napenda mnyama wa aina yoyote." Abdulahi akasema kwa sauti isiyo na ushawishi. Kukawa na ukimya. Kisha akauliza, "Kitu gani kinakufanya udhani kuwa simpendi paka wako?"
Hapa ndio bomu kubwa zaidi likadondoshwa. Abdulahi hajapona hadi unaposoma kisa hiki.
Amanda akiwa bado analia akajibu, "Mbona hujamnunulia hata zawadi ya krisimasi?"
Abdulahi kimya. Wewe unadhani angesema nini? Hana la kusema zaidi ya kushangaa. "Wenzetu wana tamaduni tofauti sana." Ndio maneno yake ya mwisho wakati tunaagana baada ya kumuuliza, "Utamnunulia paka zawadi gani ya krisimasi?"
Ninashangaa kuwa toka anihadithie kisa hiki hadi dakika hii mbavu zangu bado ziko imara. Hasa ukimjua Abdulahi ndio hutamaliza kucheka na kumcheka.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com