10/31/2004

KITABU CHA MAUAJI YA MWEMBECHAI

Nimerudia kukisoma tena kitabu cha Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania kilichoandikwa na Hamza Mustapha Njozi na kupigwa marufuku na kiranja mkuu mtawala wa Tanzania Benjamin Mkapa. Sielewi hata kidogo sababu ya siri-kali ya Tanzania kukipiga marufuku. Hebu nawe kipitie kwa kubonyeza hapa.

UNGO NA UNUNUZI WA NDEGE YA RAIS

Kuna mjadala mtamu sana unaendelea juu ya ununuzi wa ndege ya Rais wa Tanzania. Nadhani ili watu wengi wafaidike na mjadala wenyewe, nitaweka maoni ya watu mbalimbali waliochangia na wanaoendelea kuchangia ndani ya blogu hii. Mjadala ni moja ya nguzo za demokrasia: Kujadili, kushawishiana, kukubaliana, kukataa kukubaliana, n.k.
Sijachangia lolote katika mjadala huu. Nina swali dogo ambalo ninatafuta jibu lake kabla sijaingia rasmi mjadalani. Hivi kwanini wachawi wa Tanzania wasisaidie taifa letu kwa kumpatia Rais ungo wa kusafiria?

BUSH NA KIINGEREZA

Rais mwizi wa kura, Joji Kichaka, anaandamwa na wapinzani wake kwa tuhuma kuwa hana kitu kichwani. Wanadai huyu jamaa shuleni mambo yalikuwa hayapandi hata kidogo. Moja ya vielelezo vya kuwa yeye ni mbumbumbu ni madai kuwa katika mjadala wa Urais alikuwa amevaa kidude cha mtandao usiwaya (wireless) ili awasiliane na mshauri wake Karl Rove, ambaye alikuwa akimnong'onezea majibu!
Wanadai pia kuwa ingawa Kiingereza ni lugha pekee anayoijua, lugha hii inampa tabu sana. Katika mjadala wake wa mwisho wa mwongo mwenzake wa chama cha Democratic, John Kerry, Bush alisema "internets" wakati ambapo neno internet halina wingi kwahiyo huna haja ya kuongeza "s" kama alivyofundishwa akiwa mtoto!
Ukitaka kuona picha ya kidude cha mtandao usiwaya alichovaa Joji Kichaka, kongoli hapa.

10/30/2004

SOMA MAKALA MPYA MBILI

Nimeweka makala mpya mbili kwenye kona ya makala zangu ambayo iko mkono wa kuume chini ya picha yangu. Makala hizi ni Dini na Utu (sehemu ya kwanza na ya pili). Kwahiyo ni vyema ukaanza kusoma namba moja kisha namba mbili. Makala hizi niliziandika kwa ajili ya safu yangu kwenye gazeti la Mwananchi, Gumzo la Wiki, kila jumapili. Karibu uzisome.

UNARUHUSIWA KUCHEKA

Hii nayo nimeipata toka blogu ya Furahia Maisha Yako ya Dennis Mponji:
JE WAJUA?
KWA MUJIBU WA UTAFITI ULIOFANYWA NA ASASI MOJA ISIYO YA KISERIKALI (NGO), IJULIKANAYO KAMA MKAKA FOUNDATION UMEGUNDUA YAFUATAYO:
1. ZAIDI YA ASILIMIA 89.76 YA MA BARMAIDS HAPA DAR ES SALAAM NI WENYEJI WA MKOA WA TANGA,YAANI WAZIGUA,WABONDEI,WASAMBAA NA WADIGO! TANGA KUNANI PALEEEE?
2. ZAIDI YA ASILIMIA 92 YA MA HOUSE GIRLS HAPA DAR ES SALAAM NI WENYEJI WA MKOA WA IRINGA YAANI WAHEHE. NYIKA VIPI HII KITU, MNOGEGE MNOFWELA?
3. ZAIDI YA ASILIMIA 78 YA WAUZA KAHAWA NA MAJI KWENYE MIKOKOTENI NI WENYEJI WA MKOA WA DODOMA YAANI WAGOGO. BABA MALECELA CIGWEMISI NI AJE?
4. ZAIDI YA ASILIMIA 96 YA WAVUNJA MAWE NA KOKOTO HUKO KUNDUCHI, TEGETA NI WENYEJI WA MKOA WA KIGOMA YAANI WAHA, HE BURAZA K NI AJE?
5.ZAIDI YA ASILIMIA 70 YA POMBE YA CHIBUKU INAYOZALISHWA KIWANDANI HUNYWEWA NA MAKABILA YA WANDAMBA,WARUGURU,WAPOGORO NA WANGONI WAISHIO MAENEO YA KIGOGO,MSIMBAZI MISSION, MBURAHATI NA TANDALE UWANJA WA FISI!
6.ZAIDI YA ASILIMIA 70 YA WASAMBAZAJI WA MAYAI YA KUKU WA KISASA HAPA DAR ES SALAAM NI WENYEJI WA MKOA WA MARA, WA KABILA LA WAKURYA, WAISHIO HUKO KIPUNGUNI NA GONGO LA MBOTO!

MCHUANO WA MAJINA!

Nimepata habari hii toka kwenye blogu mpya ya Mtanzania iitwayo Furahia Maisha Yako. Anasema kuwa orodha hii ni ya majina ya walioingia raundi ya pili katika mchuano wa wenye majina yasiyo ya kawaida. Kweli kuna majina hata mimi ninayetetea umuhimu wa kuwa na majina ya asili yamenitoa jasho nene. Orodha hii hapa:
1. Ndugu TAMPERA NGUNAMABWOKO-Muhitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari ya wavulana Tabora mwaka 1992.
2. Ndugu GOGOMOKA MISALABA-Muhitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari Minaki mwaka 1998.
3. Ndugu ABDALLAH NYUNDO KICHECHE-Mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Minaki mwaka 2002
4. Ndugu MASANINGA SUMAKU POMBOJOLOWE a.k.a PUMBU-Dereva wa mabasi ya Hood
5. Koplo RUBYENEKO MUGANYIZI BYOMBARIRWA-Mpishi mkuu wa kikosi cha 34 cha Jeshi (34 KJ), Mbeya.
6. Ndugu TAKOTAKO WA PUMBUJE a.k.a AKANANA-Muuza miwa na maji baridi maarufu pale magomeni makutano ya barabara za Rashid Kawawa na Morogoro
7. Mheshimiwa NJENGAFIBILI MWAIKUNGILE-Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania
8. Mheshimiwa JOHN POMBE MAGUFULI-Waziri wa Ujenzi Tanzania
9.Ndugu TUNTUFYE MWAIKIMBA a.k.a KIMBA-Fundi majiko maarufu Railway Gerezani Dar es Salaam
10. Ndugu BENADETTA TYETYETYE-Muhitimu wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2001 fani ya sayansi ya jamii (BA)

10/29/2004

TOVUTI YA HIP HOP SUMMIT TANZANIA NA KISWAHILI

Desemba mwaka huu wana Hip Hop wa Tanzania watafanya mkutano mkubwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee. Kwa habari zaidi tembelea tovuti yao kwa kubonyeza hapa. Nimepata tarifa hizi toka kwenye blogu mpya ya Furahia Maisha Yako.
Wale tunaona kuwa lugha yetu ya Kiswahili ina umuhimu sana katika ujenzi wa taifa na utamaduni wetu, tunashindwa kuelewa kwanini Watanzania wamelewa namna hii huu mvinyo wa utumwa wa kifikra. Wazo la Hip Hop Summit na tovuti yao ni zuri mno. Ninawapongeza. Kutumia muziki na falsafa nzima ya hip hop kama moja ya njia ya kupambana na tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania ni wazo la kuungwa mkono na kila mtu. Lakini swali langu kila siku ni hili: kama unaanzisha jambo kwa ajili ya Watanzania kwanini unatumia lugha ya watu wengine?? Hili ni swali la msingi. Nimetembelea hii tovuti ya hip hop summit nikajiona kama ninasoma jambo linalohusu Marekani, Canada, au Uingereza. Kumbe ni jambo linalotuhusu Watanzania. MOja ya madhumuni ya hip hop summit ni kuwaunganisha watu wote wanaohusika katika nyanja ya muziki huu, kubadilishana mawazo na kutazama jinsi ambavyo muziki unavyosaidia kuondoa tatizo la ajira na umasikini Tanzania. Kama nia yao ni hii, kwanini webu yao wameandika kwa kiingereza? Kwanini wameita Hip Hop Summit? Hao vijana wanaowazungumzia ambao hawana ajira na masikini wanatumia lugha gani katika maisha yao ya kila siku? Mara nyingi vyama, mashirika huanzishwa kwa ajili ya wafadhili, kutokana na sababu hii utaona majina ya mashirika au vyama hivyo ni ya kiingereza (lugha inayotumiwa na hao wafadhili). Nimetembelea tovuti yao kutafuta kiswahili bila mafanikio. Tukumbuke kuwa wanamuziki ndio watatumia uwezo na ubunifu wao kutuondoa katika utumwa wa fikra. Ukombozi wetu na mapambano dhidi ya umasikini Tanzania mwanzo wake ni kwenye fikra.

Tafadhali nenda kwenye hii webu. Waandikie hawa mabwana. Waombe watumie lugha yetu ya Kiswahili. Hii lugha haina mapungufu yoyote. Ni lugha nzuri. Ni lugha ya maendeleo. Ni lugha inayotumiwa na walalanjaa ambao hip hop summit inataka kuwasaidia. Msaada wao uanze kwenye fikra zetu. Watusaidie tujue kuwa uhai wa taifa uko kwenye utamaduni na historia yake. Tafadhali fanya hivi. TUJIKOMBOE!

MTANZANIA MWINGINE KATIKA ULIMWENGU WA BLOGU

Pamoja na kubanwa na shughuli nyingi, zikiwemo za uchaguzi wa Urais wa hapa Marekani, nimeona ni vyema nichukue nafasi hii kutangaza kuwa kuna Mtanzania mwingine, Dennis Mponji, ambaye ameingia kwenye ulimwengu wa wana blogu. Blogu yake iitwayo FURAHIA MAISHA YAKO inaungana na blogu nyingine mpya ya Mtanzania Simon Mkina iitwayo KONA YANGU. Niliwahi kusema kuwa Wakenya kwa upande wa Afrika Mashariki ndio ambao wako mbele sana katika ku-blogu. Ninafurahi ninapoona Watanzania nao wanaanza kutumia teknolojia hii rahisi na nyepesi kujifunza kuwasiliana, kupeana taarifa, kutoa mawazo yao bila kuwa chini ya uangalizi wa mtu yeyote. Kongoli hapa kuiona blogu ya Furahia Maisha Yako. Bado iko kwenye ujenzi, siku zinavyokwenda itazidi kubadilika. Pia kama hujatembelea blogu ya Kona Yangu ambayo iko kwenye safu ya blogu za Wana Afrika Mashariki upande wa kuume ndani ya blogu hii, kongoli hapa uitembelee.

Iwapo kuna mtu yeyote anayetaka kuwa na blogu au ana maswali yoyote juu ya blogu (yawe ni maswali ya kitaaluma, kitaalamu, au vinginevyo) wasiliana nami nitafanya niwezalo kukusaidia. Niandikie: ughaibuni@yahoo.com au kama uko Marekani unaweza kuongea nami: 419-699-8085.

10/26/2004

KIMULIMULI NYUMA YANGU -2

Hii ni sehemu ya pili ya habari niliyoiita "Kimulimuli nyuma yangu." Kama hukusoma sehemu ya kwanza, isome ndipo umalizie kusoma hii. Niliiandika jumapili ya tarehe 18 mwezi huu.
**********************************************************************************
Basi tarehe 18 nikaelekea mahakamani. Kwanza nilifikiri kuwa nilitakiwa niende asubuhi saa nne. Nikampigia rafiki yangu mmoja simu kumuuliza jinsi ya kufika Mahakama ya Manispaa. Mimi huwa sipendelei sana kwenda katikati ya mji. Sifahamu sana barabara za mjini. Kati ya vitu vinavyonifanya nisiwe na tabia ya kwenda katikati ya mji ni jinsi barabara zake zilivyo. Huwa zinanichanganya sana maana nyingi haziruhusu magari kupishana. Ni barabara za magari yanayoelekea upande mmoja. Halafu kingine ni polisi. Mjini pale kila kona kuna gari la polisi. Sipendi kukutanakutana na polisi hata kidogo. Wananiudhi sana na magari yao yenye ving'ora na vimulimuli. Sehemu za kupaki pia ni chache na ghali.

Basi mshikaji wangu Manley akanipa maelekezo ya jinsi ya kufika mahakamani. Kisha akaniuliza, "Unatakiwa saa ngapi?" Nikamwambia, "Nadhani ni saa nne asubuhi." Akacheka na kuuliza (huwa anapenda kuniita profesa maana aliwahi kuwa mwanafunzi wangu), "Profesa, unadhani au una uhakika?"

Nikaamua niitazame tena tiketi yangu. Kumbe mahakamani nilitakiwa saa saba mchana. Nikaamua kurudi nyumbani nikale na kutazama kituo cha luninga cha C-Span ambacho hakina matangazo hata siku moja. Saa sita na kitu hivi nikaondoka zangu. Nimezunguka mjini kama dakika 20 nikitafuta mahali pa kupaki gari karibu na mahakamani. Mwishoni nikaamua kupaki karibu na maktaba kwenye makutano ya Michigan na Adams. Nikaweka hela za kupaki za saa moja.

Nilishasahau kuwa ninaishi kwenye nchi yenye hofu ya kuvamiwa na jamaa zake yule bwana mwenye madevu anayeishi mapangoni kule Afghanistan. Basi nikakuta kuna mashine za kutazama kama mtu amebeba silaha. Nikaambiwa nitoe kila kitu mfukoni na kuweka ndani ya bakuli la rangi ya kahawia. Baada ya kuonekana kuwa sina chochote cha kutishia usalama nikaruhusiwa kuingia.

"Naelekea mahakama namba nne." Namweleza binti aliyeko mapokezi. "Mahakama namba nne imehamia namba sita." Ananiambia. "Chukua lifti hadi gorofa ya nne." Ananielekeza. Ninapoifika mahakama namba sita nakuta imeshehena watu. Nachungulia kutazama sehemu ya kukaa. Jaji anasema, "Wenye majina yanayoanza na A hadi M wabaki hapa, waliobaki waende gorofa ya pili mahakama namba 2." Baadhi ya watu wanaondoka. Najivuta na kuketi. Mahakama inaanza shughuli zake. Watu wanaitwa mmoja mmoja. Wanaokuja hapa wote wana makosa ya barabarani. Jaji anakusome shtaka na adhabu yake na kukuuliza kama unakiri. Ukikataa kosa unapewa siku nyingine. Ukikubali unasomewa adhabu. Kama ni faini unaambiwa ulipe. Kama ni kifungo anakuuliza kama unaelewa kuwa ukikubali kosa utafungwa, na kuwa unaweza kufungwa kuanzia siku hiyo.
"Kosa lako la kuendesha bila leseni linaweza kukupeleka jela miezi sita pamoja/au faini ya dola 1000. Una haki ya kutafuta wakili." Jaji anasema. Wakati huo mimi ninajiuliza nitafikiwa saa ngapi? Nilidhani kuwa nitakaa mahakamani kama saa moja hivi. Matokeo yake nilikwenda kuweka hela zaidi kwenye mita ya nilikopaki gari mara tatu. Toka saa saba niliondoka mahakamani saa kumi jioni. Nilipofikiwa nilikuwa nimechoka hasa.
"Desanyo Maka," Jaji aliniita. Watu wengi wanashindwa kutamka Ndesanjo na Macha wanadhani inatamkwa Maka. "Nipo." Nikaitikia na kwenda kizimbani.
"Una kosa la kupita kwenye taa nyekundu na kuendesha bila kuvaa mkanda. Una hatia au huna hatia?" Alinisome shtaka na kuniuliza.
"Nina hatia kwa kosa la kwanza la kupita kwenye taa nyekundu ila sina hatia ya kutokuvaa mkanda." Askari aliyenikamata alidhani kuwa sikuvaa mkanda maana baada ya kunisimamisha, niliingiza mkono mfukoni ili kutoa leseni ya udereva, nikaweka simu mfukoni na kutoa kamba ya kusikilizia masikioni na kuweka mfukoni, alipoona ninajigusagusa akadhani kuwa ninakazana kufunga mkanda.

Ingawa nimetoka kwenye nchi ambayo watu wengi wanaamini kuwa ukifunga mkanda utashindwa kuruka wakati wa ajali, ninapoingia ndani ya gari jambo la kwanza ni kufunga mkanda. Nimekutana na watu wengi Tanzania wanaosema, "Ukifunga mkanda ni rahisi kufa wakati wa ajali!"

Jaji akaniuliza kama nina bima ya gari. Nikamwonyesha. Akasema, "Una hatia ya kupita kwenye taa nyekundu, unatakiwa ulipe faini ya dola 100. "Utalipa leo au siku nyingine?" Jaji akaniuliza. Nikajibu kwa uchungu, "Leo." Dola 100! Shenzi taipu!

NJIA YA MUONGO KUMBE NI NDEFU!

Hivi njia ya muongo ni fupi au ndefu? Kongoli hapa.

10/22/2004

TUTAMKUMBUKA SUPREME NDALA KASHEBA

Mwanamuziki Ndala Kasheba ameaga dunia. Nimeamua kwa wiki moja sitamsikiliza mwanamuziki yeyote zaidi ya Ndala Kasheba. Kasheba aliingia Tanzania miaka ya 60 akiwa na bendi ya Orchestra Fauvette. Kasheba pamoja na kuwa ndio mwanzilishi wa mtindo ambao bado ninaupenda ile mbaya, Dukuduku Yee!, ni mwanamuziki wa kwanza Tanzania kudonoa gitaa la nyuzi 12. Ni baada ya kuzindua gitaa hili pale viwanja vya Mnazi Mmoja miaka ya 80, marehemu Kasheba alipachikwa jina la Supreme. Siku hiyo alivunja gitaa lake la nyuzi sita na kulivaa gitaa la nyuzi 12 ambalo alikuwa "akilinyanyasa" hadi alipofariki.

Moja ya nyimbo za marehemu ambazo zimewahi kuvuma sana ni ule wa Dezo Dezo alioutunga akiwa na bendi yake ya Zaita Musica. Wimbo huu ulikuja kurekodiwa na Tshala Muana. Katika wimbo huu anasema:
"Ewe mtoto wa kike, acha umbeya, mbeya...nitakusemea..."
"Unapenda dezo dezo...sigara hutaki kuacha...eh bwana we yatakushinda."

Nyimbo zake nyingine ni Marashi ya Pemba, Chunusi, Marinella, Nimlilie Nani, na Sungura Weba. Santuri yake ya mwisho iliitwa Yellow Card. Hii pia ni santuri yake ya kwanza kutolewa nchini Marekani. Wimbo wa Yellow Card aliuimba kufuatia uvumi kuwa amefariki kwa ukimwi. Katika wimbo huu anasema: "...hata wewe ni marehemu mtarajiwa."

Mara ya mwisho kumuona akifanya onyesho la hadharani (live) ilikuwa ni mwaka 2002 pale kwenye bustani za Mnazi Mmoja. Alipanda jukwaani na King Kiki na Babu Seya. kati ya mwaka 1994-97 nilikuwa nikihudhuria maonyesho yake ya usiku kule Sinza (nimesahau jina la ile klabu) ambapo tulikuwa tukipeperusha kitambaa cheupe. Onyesho la mwaka 2002 lilinidhihirishia kuwa kwa upigaji wa gitaa Tanzania, marehemu Kasheba hakuwa na mfano. Huyu bwana alikuwa akidonoa nyuzi kama vile anakunywa chai barazani huku akitazama wacheza bao. Tutamkumbuka daima.
Ukitaka kusikiliza baadhi ya nyimbo zake au kununua CD yake (hasa kwa walioko Marekani)
kongoli hapa.

10/21/2004

BLOGU YA MTANZANIA

Mfanyakazi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Simon Mkina, ameingia kwenye ulimwengu wa blogu. Hadi hivi sasa Wakenya ndio wako mstari wa mbele katika matumizi ya zana hii mpya ya mawasiliano. Blogu za Wakenya ni za Kiingereza. Siku zinavyokwenda nina imani kuwa Watanzania wengi zaidi wataingia kwenye ulimwengu huu wa blogu ambao tunapashana habari na kuelimishana kwa njia rahisi na haraka. Kongoli hapa uone blogu ya Mkina.

BLOGU ZA WAAFRIKA MASHARIKI

Nimeweka kona ya blogu za Waafrika Mashariki. Wakenya wako mbele kidogo kwenye ulimwengu wa blogu (blogsphere). Nimeweka blogu nne kwa sasa ila bado ninapandisha nyingine zaidi. Jioni nitaweka moja ya Mtanzania aliyeko Dar. Blogu zenyewe ziko mkono wa kuume chini ya "archives."

NILIPOKWENDA MAHAKAMANI

Nimekuwa na pilikapilika za hapa na pale. Kwa siku mbili hivi sikuwepo hapa ndani ya blogu. Baadaye leo nitaendelea na kile kisa cha kusimamishwa na polisi kwa madai ya kutokutii taa nyekundu na kutokufunga mkanda. Tarehe 18 nilikwenda mahakamani saa saba mchana. Nitakueleza nini kilitokea. Sasa hivi ninakwenda kwenye maandamano dhidi ya mgombea mwenza wa Bush, mwizi na muongo aitwaye Dick Cheney. Kwahiyo tutaonana hapo baadaye.

10/17/2004

KIMULIMULI NYUMA YANGU

Nimemaliza kukata kona ya barabara ya Upton kuingia barabara ya Bancroft. Nadhani ni saa tatu usiku. Nasikiliza zangu muziki wa Fela Kuti. Anaimba wimbo wake uitwao Mwalimu Usinifundishe Upuuzi. Fela! Nashindwa kummaliza.... Basi mara naona gari nyuma yangu yenye kimulimuli. Nafyonza, "Polisi huyo. Nimefanya nini?" Napunguza mwendo, naashiria kuingia upande wa kulia. Ninahamia upande wa kulia kisha nasimamisha gari. Polisi anasimama nyuma yangu. Nabaki ndani ya gari. Inapita kama dakika mbili hivi askari ananijia na kugonga dirishani huku mkono mmoja uko kiunoni penye bastola. Nashusha kioo. "Naomba leseni ya udereva." Ananiambia. Ninampa. "Una leseni ya jimbo la Washington, una mpango wa kurudi Washington au kuwa hapa?" Namwambia kuwa sina uhakika ila sitakuwepo Ohio kwa muda mrefu. "Kama utaendelea kuishi hapa lazima uombe leseni ya Ohio." Namwitikia. Anaichukua na kurudi garini kwake.

Nasubiri. Fela bado anaimba wimbo ule ule. Unajua nyimbo za Fela zilivyo ndefu. Wakati fela anarekodi na kampuni kubwa kwa mara ya kwanza, aliambiwa na kampuni hiyo, Polygram, kuwa lazima apunguze urefu wa nyimbo zake. Fela akagoma. Mpaka leo ana nyimbo ambazo ni zaidi ya dakika 30 tofauti na nyimbo nyingi za wanamuziki wengine ambazo huwa ni dakika tatu, nne, au tano. Ninaposikiliza nyimbo za Fela, kama leo hii, ninazidi kuelewa kwanini aligoma kufupisha nyimbo zake. Nyimbo za Fela ukizipiga kwa dakika tano itakuwa ni kama mtu mwenye njaa aliyepewa nusu kijiko cha chakula akipendacho. Nyimbo za Fela ni kama safari ndefu yenye matukio ya kufurahisha, kufikirisha, na kuchangamsha. Mrindimo wa ngoma, magitaa yanayopigwa kwa kurudiarudia kodi moja au mbili, kwaya ya matarumbeta yanayopayuka juu ya kinanda na gitaa la besi linalotembea kwa kuyumbayumba kwa madaha.

Askari amerudi. Ananikabishi leseni yangu na kipande cha karatasi. "Nenda mahakamani tarehe 18 mwezi huu. Umepita kwenye taa nyekundu na hukuwa umefunga mkanda."
"Sikufunga mkanda? Mbona sikuelewi?"
"Utakapokwenda mahakamani utajitetea. Asante." Anaondoka.
Kuhusu taa nyekundu sina uhakika kama nilifanya kosa. Ninadhani kama unatokea Upton na taa ni nyekundu, unaweza kuingia Bancroft kama hakuna gari lolote. Tarehe 18 ni wiki ijayo. Tusubiri. Mambo ya kwenda mahakama ya mtu mweupe siyapendi kabisa. Hata hivyo sina la kufanya. Ingekuwa nyumbani tukio hili lingemalizika kwa kuingiza mkono mfukoni.

Binadamu watu wa ajabu sana. Ukitoa rushwa unalalamika kuwa rushwa imekithiri. Ukikutana na mtumishi wa umma anayejali nidhamu ya kazi bado unaudhika!
Nasubiri wiki ijayo nitakueleza.

10/16/2004

ETI MILA NA UTMADUNI VIMEKUFA?

Nani anasema kuwa hakuna mtu anayejali tena mila na utamaduni wa Mwafrika? Bonyeza hapa usome harusi ya kimila ya mtunzi Ngugi wa Thiong'o.

MUZIKI WA TANZANIA WAVAMIA KENYA

Unakumbuka jinsi michezo ya kuchekesha ya Kenya ilivyokuwa inawamaliza Watanzania? Sasa naona tumerudisha goli kwa bongoflava/hip hop. Kuna habari hii kwenye gazeti la Daily Nation. Iliandikwa mwaka jana, ila kwa taarifa nilizonazo bado muziki wa Tanzania unawazengua Wakenya hadi hivi sasa. Bonyeza hapa usome habari kamili.

10/14/2004

TOVUTI YA MUZIKI WA AFRIKA

Bonyeza hapa utembelee tovuti hii nzuri sana ya inayohusu muziki wa Afrika. Nimetembelea tovuti nyingi sana. Hii nimeipenda kichizi.

NDUGU ZETU WALIOKWENDA INDIA KARNE NANE ZILIZOPITA

Kuna ndugu zetu wako India. Walikwenda huko karne nane zilizopita. Wanapenda Kiswahili ambacho wanasema ni lugha ya mababu zao. Unafahamu haya? Nimekumbana na habari yao nilipotembelea blogu ya mwanafunzi Mkenya, Ory Okollah, aliyeko hapa Marekani: Kenyan Pundit (http://blogs.law.harvard.edu/ory/). Bonyeza hapa uisome habari nzima.

SIKU YA KUMUENZI NYERERE

Eti leo ni siku ya kumuenzi Mwalimu Nyerere Tanzania! Watu wanapumzika. Kisha? Kisha kesho wanakwenda kazini hadi mwaka ujao tena! Sijui ni watu wangapi wanamuenzi kwa dhati.

Mwezi wa saba mwaka huu niliandika kipande hiki juu ya Nyerere. Kwa heshima yake nitabandika tena ili ambao hawakupata kusoma wasome. Pia kama unataka kusikiliza hotuba zake, mwisho wa nukuu kuna sehemu ya kubonyeza ili umsikilize.

MWALIMU NYERERE AWAPASHA BENKI YA DUNIA
Mwaka 1999 Ikaweba Bunting alifanya mahojiano na Mwalimu Nyerere. Mahojiano hayo yalitolewa katika gazeti la New Internationalist. Nimependa sana jibu lake hili. Hivi ndivyo alivyosema:
"I was in Washington last year. At the World Bank the first question they asked me was `how did you fail?' I responded that we took over a country with 85 per cent of its adult population illiterate. The British ruled us for 43 years. When they left, there were 2 trained engineers and 12 doctors. This is the country we inherited. When I stepped down there was 91-per-cent literacy and nearly every child was in school. We trained thousands of engineers and doctors and teachers. In 1988 Tanzania's per-capita income was $280. Now, in 1998, it is $140. So I asked the World Bank people what went wrong. Because for the last ten years Tanzania has been signing on the dotted line and doing everything the IMF and the World Bank wanted. Enrolment in school has plummeted to 63 per cent and conditions in health and other social services have deteriorated. I asked them again: `what went wrong?' These people just sat there looking at me. Then they asked what could they do? I told them have some humility. Humility - they are so arrogant!"
Ndio Mwalimu huyo. Ukitaka mahojiano kamili kongoli hapa.
Ukitaka kusikiliza hotuba za Mwalimu Nyerere kongoli hapa.

10/13/2004

JINSI YA KUONDOA SERIKALI MADARAKANI

Nimekuwa nikiandika makala hii kwa muda mrefu. Ni makala inayoonyesha jinsi ambavyo watu wa kawaida wanaweza kuondoa watawala madarakani na kuweka viongozi/kujiongoza wenyewe. Nadhani nitaimalizia leo usiku na kuituma katika safu yangu ya gazeti la Mwananchi. Kabla ya mwisho wa wiki ijayo nitaiweka hapa ndani ya blogu. Nimemaliza kusoma kitabu kiitwacho: JINSI YA KUWATOA WANAUME WAZUNGU MAJUHA MADARAKANI. Kitabu hiki kimenitia moyo wa kumalizia makala yangu. Kitabu bomba sana hiki. Kwa walio Tanzania, fuatilia Mwananchi na walioko nje ya Tanzania, fuatilia blogu hii ili uweze kusoma makala hiyo. Nadhani ni jambo muhimu sana kujua jinsi ambavyo sisi watu wa kawaida tunaweza kuwaondoa madarakani watawala ambao wamezungukwa na kuta nene na polisi wa kuzuia fujo na jeshi ni kama misukule yao. Kama unamsikiliza Fela Kuti, kasikilize wimbo wake wa Zombie (Msukule). Alipoimba wimbo huu nchini Ghana, ilibidi serikali imtumie haraka sana. Wimbo huu unazungumzia askari kama tunaokumbana nao barabarani tunapoandamana. Utakuta tunatetea haki ambazo zinawajumuisha ndugu zao, wao wenyewe, majirani zao, shangazi zao, bibi zao, watoto wao, nchi yao, n.k. lakini kwakuwa eti wamepewa "amri" wanakurupuka na kuanza kutuangushia mkong'oto. Usikose makala hiyo. Lazima tujiongoze wenyewe. Nguvu za demokrasia ziwe mikononi mwetu. Kuna kanuni za umma kutwaa madaraka. Kwa maneno mengine nitakuwa nazungumzia jinsi ya kuleta mapinduzi. Najua CCM wanaamini kuwa wao ndio wana haki ya kuzungumzia mapinduzi. Wengine tukizungumzia tunaweza kukamatwa na kushtakiwa kwa uhaini. Sijui kwanini wanaongopa watu wa kawaida tukitumia neno hili. Tuna haki ya kusema kuwa tunataka mapinduzi. Kwani tunachotaka sio kitu kingine. Harambee!
"By Any Means Necessary." - Malcolm X.

RAIS JOJI KICHAKA ALIFICHA KIDUDE MGONGONI??

Leo mjadala wa tatu na wa mwisho wa wagombea wawili wa Urais, Kichaka (Bush) na Kerry, utafanyika. Toka walipokutana katika kiti moto cha raundi ya kwanza, kumekuwa na habari za kutatanisha juu ya kitu kilichokuwa kimetuna mgongoni mwa Rais Kichaka, ndani ya koti lake la suti. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa alikuwa amewekewa chombo cha kunasa mtandao usiwaya (wifi au wirelesss network) ili apewe majibu na mshauri wake mkuu, Karl Rove. Sikioni alikuwa ameweka kijitu kidogo cha kusikilizia. Moja ya mifano inayotumiwa kujenga hoja ya kuwa alikuwa akinong'onezewa na mshauri wake aseme nini, ni pale alipokuwa akiongea kisha akasema, "Ngoja, niache kwanza nimalize..." wakati ambapo hakuna mtu aliyesema lolote. Kila mtu alikuwa akimsikiliza, sasa alikuwa anamwambia nani asubiri kwanza amalize? Jambo jingine ni matumizi yake ya misamiati na mabomba makali makali ya Kiingereza ambayo sio kawaida yake. Wachambuzi wanazidi kudai kuwa Rais Kichaka alikuwa akitazama chini kimya kama mtu anayemsikiliza mtu mwingine, kisha ananyanyua kichwa na kushusha mapointi makali mno! Watu wanamshauri Kerry katika mjadala wao wa mwisho leo usiku kumpapasa Kichaka kabla ya kufanya lolote lile. Bonyeza hapa uone picha yake na kidude kilichotuna mgongoni mwake.

MKAPA, HUU NDIO UZAWA!

Baadhi ya Watanzania walipoanza kuhubiri uzawa, yaani umuhimu wa kuwawezesha Watanzania ili waweze kushiriki kikamilifu katika soko huria, uwekezaji, na ubinafsishaji; walionekana kuwa wanahubiri itikadi ya ubaguzi wa rangi. Idd Simba alipofikia hatua ya kuandika kabisa kitabu juu ya uzawa, chama chake, CCM, kilikuja juu na kusema kuwa hiyo siyo sera rasmi ya chama hicho.

Sasa leo nimepigwa na butwaa baada ya kusoma aliyosema Rais Mkapa (hivi nilitakuwa kusema Mheshimiwa? Sina uhakika, ila sina tabia ya kuita watawala Waheshimiwa. Waheshimiwa kwa lipi?) jana katika mkutano uitwao Annual Global African Business Titans jijini Dar Es Salaam. Aliyosema yote kwa neno moja tunaita UZAWA. Nasubiri CCM wamjie juu mwenyekiti wao. Nimefurahishwa na ujumbe alioutoa Mkapa. Ila ningependa kama angetumia muda huo kutupa ripoti, takwimu, na mifano ya sera na sheria ambazo serikali yake imepitisha kumsaidia huyu mzawa ili aweze kupambana na wafanyabiashara toka nje wenye mitaji mikubwa na uzoefu wa muda mrefu wa biashara ya kimataifa. Badala ya kutuambia kuwa "Tunapaswa kusaidia wazawa..." atuambie amefanya nini toka awepo madarakani kufanikisha analosema? Huu ndio ujumbe tunaoutaka. Soma aliyosema Mkapa kwa kubonyeza hapa.

IRANI, MAREKANI, NA NYUKLIA

Wakati Irani imezungukwa na nchi zenye silaha za nyuklia (Pakistan, India, Israel, China, n.k.) Marekani imetishia kutumia nguvu kama nchi hiyo itaendelea na mpango wake wa kutengeneza nyuklia. Hivi Wairani wenyewe wanasemaje juu ya nchi yao kutengeneza nyuklia? Bonyeza hapa uone mawazo ya wenyewe wenye nchi.


10/12/2004

SOMA MAKALA MPYA

Nimeweka makala mpya kwenye kona ya makala zangu, upande wa kuume, chini ya picha yangu. Kicha chake ni: Gurudumu Liko Wapi? Hii makala niliiandika siku za nyuma. Nimeifuma leo wakati nikitafuta nyaraka fulani muhimu. Ingawa nimebanwa na shughuli nimeamua kuipandisha ili upate kuisoma.

MREMA, MIWAYA, NA DIGRII

Augustino Lyatonga Mrema, mwenyekiti wa Tanzania Labour Party, amedai kuwa hana ngoma na kuwa maprofesa hapa Marekani walimzimia fegi na kubloo mapigo kwa jinsi alivyowashushia nondo. Habari kamili iko gazeti la Alasiri. Bonyeza hapa uisome. Mimi imeniacha hoi kwa kucheka.

10/11/2004

GOOGLE NA KISWAHILI

Webu ya utafutaji wa taarifa mbalimbali, google, ina ukurasa kwa Kiswahili. Bonyeza hapa.

10/10/2004

MAZINGIRA NA HATIMA YA TANZANIA

Kwa wale wanaopenda kufuatilia masuala mbalimbali ya mazingira nchini Tanzania (sheria, sera, uharibifu, uzembe, utafiti, n.k.) nenda katika webu ya jamaa wa LEAT: http://www.leat.or.tz/. Hawa mabwana wanafanya kazi nzuri sana. Nenda katika webu yao kajielimishe juu ya masuala ya mazingira nchini Tanzania. Jambo moja ambalo nadhani tunapaswa kuwauliza ni hili: hizi taarifa kwenye webu yao ni kwa ajili ya nani? Kama ni kwa ajili ya Watanzania, kwanini waandike kwa lugha ya watu wengine? Watanzania, ambao ndio wanapaswa kujua undani wa masuala ya mazingira yao, kupata taarifa sahihi ili waweze kushiriki katika harakati za utunzaji wa mazingira; lugha wanayoielewa ni Kiswahili. Wiki kadhaa zilizopita niliandika makala ambayo nitaiweka bloguni hivi karibuni ambayo kimsingi ilikuwa ikihoji mantiki ya waanzishaji wa vyama vya siasa au mashirika yasiyo ya kiserikali yenye majina ya Kiingereza. Tazama chama kama NCCR-Mageuzi, kwa mfano, sijui ni wakulima na wafanyakazi wangapi ambao chama hiki kinadai kuwatetea wanaoweza kusema kirefu cha NCCR. Nakumbuka kuna wakati chama hiki kilikuwa na mwenyekiti ambaye hakuwa anaweza kutamka vyema kirefu cha jina hili. Je ni wakulima na masikini wangapi wanaelewa maana ya maneno Tanzania Labour Party au Civic United Front. Ukiona majina ya mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya siasa unaweza kufikiri kuwa uko Uingereza au Australia. Huwezi kuanzisha chama au shirika kwa ajili ya Watanzania kisha ukakipa au ukalipa jina la kigeni ambalo Watanzania hao unaotaka kuwatetea au kuwaelimisha hawawezi kutamka wala kuelewa maana ya jina la chama au shirika lenyewe. Kuna sababu kuu mbili zinafanya jambo hili kutokea. Kwanza, kasumba ya kuamini kuwa jina la Kiingereza lina utamu zaidi maana hii ni lugha yenye hadhi zaidi duniani. Kiongozi yeyote mwenye fikra kama hizi anahitaji msaada wetu. Anahitaji kuongozwa na sio kuongoza. Sababu ya pili ni kuwa mashirika na vyama vinaanzishwa kwa ajili ya wafadhili. Kwahiyo majina yanachaguliwa toka kwenye lugha ambayo wafadhili wanaielewa. Ujumbe mkuu wa blogu hii ni kujikomboa. Lazima tupambane vikali na upuuzi huu. Mtu yeyote anayekuja kuomba kura kwako na chama ambacho jina lake linatumia lugha ya Kiingereza mwambie aende akashiriki uchaguzi wa Uingereza au Canada. Watanzania lugha yetu ni kiswahili. Hii ndio lugha ya walalanjaa. Ndio lugha ya wakulima na wafanyakazi wanaonyanyaswa na mfumo wa utawala wa watu wachache wenye fedha na elimu. Wenye fedha wanatumia uwezo wao kuturubuni na kuweka viongozi kwenye viganja vyao na wenye elimu wanatumia elimu yao na lugha ya kuja kutuweka kizani na kuendeleza ukoloni mamboleo huku wakishirikiana na watu wanaoitwa wafadhili. Upuuzi huu, utumwa huu wa kiakili ukome.

Kwahiyo ndugu yangu tembelea webu ya jamaa wa LEAT. Nakuomba utumie dakika chache kuwandikia na kuwataka waonyeshe heshima sio kwa mazingira tu bali pia kwa utamaduni wetu na lugha yetu. Waulize kama webu yao ni kwa ajili ya wafadhili na wazungu tujue. Ila kama taarifa zilizoko hapo ni kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania, basi watumie lugha ambayo wote tunaielewa vyema. Anuani yao hii hapa: leat@mediapost.co.tz . Ukiweza tuma kopi hapa: ughaibuni@yahoo.com
Unaweza pia ukawatumia kipande hiki kwa kubonyeza hapo chini kwenye alama ya kibahasha kisha uweke anuani yao hiyo hapo juu. Au unaweza kuwaandikia barua wenyewe. Taarifa zilizoko kwenye webu yao ni za muhimu mno ndio maana ninaona ni muhimu kwa lugha ya Kiswahili kutumika. Taarifa hizi zitakuwa na mafanikio zaidi zikitufikia kwa lugha tunayoijua. Lugha tunayoitumia asubuhi, mchana, na jioni. Hata hivyo, nawapongeza jamaa wa LEAT kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwakuwa masuala ya mazingira hayako kwenye kauli za wana si-hasa wetu ni vyema kukawa na makundi ya wana wa nchi kama LEAT yanayohamasisha na kutetea utunzaji wa dunia tuliyorithishwa na waliotutangulia ambao waliitunza na kuiheshimu... na hata kuiabudu!

10/09/2004

WIZI WA URITHI WA WAAFRIKA

Uingereza kama yalivyo mataifa mengine ya Ulaya yaliyoitawala Afrika bado inashikilia vitu vya kitamaduni na kidini walivyoiba toka Afrika. Vitu hivi wameweka kwenye majumba yao ya makumbusho bila aibu yoyote. Soma habari hii ya Waethiopia wanaopambana kurudisha urithi wao ulioibwa na Waingereza. Bonyeza hapa.

WANGARI MATHAI NA NISHANI YA NOBELI

Wangari Mathai, naibu waziri wa mazingira na kiongozi wa vuguvugu la ukanda wa kijani (green belt movement) amekuwa mwanamke wa kwanza kupata nishani ya Nobeli ya amani. Kuna baadhi ya watu ambao wamepinga kupewa nishani hiyo kwa mwanaharakati wa mazingira maana hawaoni uhusiano wa utunzaji wa mazingira na amani. Hawa ni watu wenye tafsiri finyu sana ya amani. Bonyeza hapa kusoma habari yake kwa undani.

10/08/2004

MJADALA WA URAIS

Leo kiti moto cha urais hapa Marekani kinaendelea. Kilianza ijumaa iliyopita. Leo wananchi wa kawaida ambao hawajaamua kuwa watampigia nani kura ndio watauliza maswali. Kambi ya Bush mwanzoni ilikuwa ikisita kushiriki kwa sababu zilizo wazi. Bush mambo hayapandi sana kichwani. Ana tabia ya kutunga sentensi mbovu, kupata kigugumizi, kujirudiarudia, n.k. Ninakwenda nyumbani kutazama huku nakula ugali wa maharage ya nazi.

10/07/2004

SOMA MAKALA MPYA

Nimeweka makala mpya kwenye kona ya makala zangu ambayo iko mkono wa kuume, chini ya picha yangu. Makala mbili mpya ni Kaombe Fedha kwa Ombaomba na Dini yake ni Kujitolea. Makala hizi mbili zimetoka hivi karibuni kwenye safu yangu ya kila jumapili katika gazeti la Mwananchi.

Tazama Video ya Billionaires For Bush

Kampeni za kisiasa kupitia mtandao wa tarakilishi zimepamba moto. Tazama video hii toka kwenye tovuti ya jamaa wanaojiita: Billionaires For Bush. Jina lao hili ni kejeli kwa Bush. Bonyeza hapa kutazama video hiyo.

KARIBU OBEY NKYA

Saa ya ukombozi....unakumbuka harakati za jeshini? Ile historia itabidi tuiandike siku moja.
Karibu sana ndani ya blogu. Masomo mema.

10/06/2004

UKIMWI NA AFRIKA

Afrika na ukimwi ni kama pacha katika fikra za watu wengi huku ughaibuni. Wanashindwa hata kuona wenzao wanaotokomea kwa gonjwa hili kwa kudhani kuwa ugonjwa huu (ambao wanadai umetoka afrika) unawamaliza Waafrika peke yao. Sasa jana kulikuwa na kiti moto cha wagombea umakamu wa Rais, Dick Cheney na John Edwards. Wakaulizwa juu ya athari za ukimwi miongoni mwa wanawake weusi. Muulizaji akasema wazi kuwa hataki wazungumzie Afrika, bali Marekani. Wapi! Jamaa hawa wote wawili wakaanza kuelezea jinsi ambavyo ugonjwa huu ulivyo na madhara katika mataifa ya Afrika na kwingineko katika uliwengu wanaouita wa tatu. Dick Cheney alipobanwa juu ya Ukimwi miongoni mwa wanawake weusi ambao ni rahisi kuupata ukilinganisha na wanawake wengine Marekani, alisema, "Sina taarifa hizi kuwa ukimwi ni tatizo kubwa kwa watu weusi hapa Marekani!" Yaani makamu wa rais mzima anajua zaidi tatizo la ukimwi na takwimu zake Afrika kuliko hapa Marekani.

Dick Cheney alibanwa na John Edwards pale alipoambiwa kuwa rekodi zinaonyesha kuwa alipiga kura ya kuzuia kufunguliwa kwa Nelson Mandela na pia kupinga kuwepo kwa sherehe ya kitaifa ya Martin Luther King. Maaluni mkubwa huyu....alikuwa akiunga mkono ubaguzi wa rangi Afrika Kusini sasa anajifanya eti anapenda haki za binadamu ndio maana anatuma majeshi huko Iraki yakawakomboe Wairaki.

BENDERA YA MARIKANI

Jana nilikuwa nazunguka kwenye maduka mbalimbali yanayouza beji na vitambaa vyenye bendera ya Marekani. Nilitaka kujua hii alama ya uzalendo uliojitokeza baada ya septemba 11, 2001 inatengenezwa wapi. Beji na vitambaa hivi vinatengenezwa China. Wachina wanafaidika na uzalendo wa Wamarikani!

SILAHA ZA SUMU

Ripoti ya jeshi la Marekani juu ya silaha za sumu nchini Iraki imetolewa. Ripoti hii sio tu inasema kuwa Saddam hakuwa na silaha za sumu, bali hakuwa na mpango wowote wa kuzitengeneza. Unakumbuka baada ya Bush na mabwana wa vita wenziye kugundulika kuwa walitudanganya kuhusu kuwepo kwa silaha hizi, walikuja na kisingizio kipya. Walisema. "Hatukusema kuwa Saddam alikuwa na silaha ila tulisema kuwa alikuwa na programu ya kutengeneza hizo silaha." Ripoti hii inmaonyesha kuwa sio silaha wala programu. Uongo mtupu. Na utawatokea puani.

10/04/2004

"UKOMBOZI" WA IRAKI

Kwa mujibu wa jirani yangu ambaye anafuatilia kwa karibu vifo na majeruhi huko Iraki, hadi jana tarehe 3, Oktoba, takwimu zilikuwa hivi:
Wairaki waliokufa: 12, 976
Wamarekani waliokufa: 1, 054
Wamarekani waliojeruhiwa: 7, 032

Sio rahisi kujua idadi kamili ya Wairaki waliouawa au kujeruhiwa. Idadi halisi ya waliokufa ni kubwa kuliko hii. Utaona kuwa jirani yangu hajaweza kupata idadi ya Wairaki waliojeruhiwa. Kama unakumbuka niliwahi kuandika kuhusu huyu bwana ambaye nje ya nyumba yake kuna bendera ya Marekani na Umoja wa Mataifa na mabango matatu yenye idadi ya waliojeruhiwa na kuuawa. Najua nikipita hapo baadaye leo nitakuta namba zimebadilishwa maana anafuatilia dakika hadi dakika. Wakiuawa watu huko jamaa anabadili tarakimu kwenye mabango yake. Kazini sijui anakwenda saa ngapi, au labda amestaafu.

10/02/2004

TUMERUHUSIWA NA NYERERE KUVUTA BANGI!!

Ingawa nimebanwa na shughuli kutokana na muda mfupi nilionao kabla ya kurudi Toledo, Ohio, habari hii nimeisoma muda mfupi uliopita nimeona niiweke hapa ili wale ambao hawajaisoma waisome. Imeniacha hoi kabisa. Bonyeza hapa ili upate uhondo wenyewe.
Nimekutana na mmasai mmoja, Kakuta Ole Hamisi, nilipotembelea soko la "kiboriloni" la Vermont. Hili ni soko la kila jumamosi. Lilianza mwaka 1974. Nilikuwa hapo na bwana Kakuta ambaye anapenda kuita wazungu, "mabeberu." Kama nilivyoahidi, katika makala yangu ya wiki hii gazeti la Mwananchi, nitazungumzia safari hii. Kwahiyo nitagusia habari za Kakuta na hili soko. Haya, bonyeza hapo juu usome kisa cha kabila la Wahadzabe ambao ukiwatembelea ni vyema ukakumbuka kuwapelekea zawadi ya bangi!

10/01/2004

SAFARI

Niko safarini. Nimeondoka Toledo jana. Nitarudi jumapili. Katika makala yangu, Gumzo la Wiki, katika gazeti la Mwananchi jumapili ijayo nitazungumzia safari yangu hii ambayo imenikutanisha na Wamarekani wanaojenga ujamaa kwa njia mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa maduka ya ushirika! Sina muda wa kutosha wa kuingia kwenye mtandao. Kwahiyo hadi nikirudi maeneo yangu ya kujidai, Toledo, ukae salama salimini.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com