10/26/2004

KIMULIMULI NYUMA YANGU -2

Hii ni sehemu ya pili ya habari niliyoiita "Kimulimuli nyuma yangu." Kama hukusoma sehemu ya kwanza, isome ndipo umalizie kusoma hii. Niliiandika jumapili ya tarehe 18 mwezi huu.
**********************************************************************************
Basi tarehe 18 nikaelekea mahakamani. Kwanza nilifikiri kuwa nilitakiwa niende asubuhi saa nne. Nikampigia rafiki yangu mmoja simu kumuuliza jinsi ya kufika Mahakama ya Manispaa. Mimi huwa sipendelei sana kwenda katikati ya mji. Sifahamu sana barabara za mjini. Kati ya vitu vinavyonifanya nisiwe na tabia ya kwenda katikati ya mji ni jinsi barabara zake zilivyo. Huwa zinanichanganya sana maana nyingi haziruhusu magari kupishana. Ni barabara za magari yanayoelekea upande mmoja. Halafu kingine ni polisi. Mjini pale kila kona kuna gari la polisi. Sipendi kukutanakutana na polisi hata kidogo. Wananiudhi sana na magari yao yenye ving'ora na vimulimuli. Sehemu za kupaki pia ni chache na ghali.

Basi mshikaji wangu Manley akanipa maelekezo ya jinsi ya kufika mahakamani. Kisha akaniuliza, "Unatakiwa saa ngapi?" Nikamwambia, "Nadhani ni saa nne asubuhi." Akacheka na kuuliza (huwa anapenda kuniita profesa maana aliwahi kuwa mwanafunzi wangu), "Profesa, unadhani au una uhakika?"

Nikaamua niitazame tena tiketi yangu. Kumbe mahakamani nilitakiwa saa saba mchana. Nikaamua kurudi nyumbani nikale na kutazama kituo cha luninga cha C-Span ambacho hakina matangazo hata siku moja. Saa sita na kitu hivi nikaondoka zangu. Nimezunguka mjini kama dakika 20 nikitafuta mahali pa kupaki gari karibu na mahakamani. Mwishoni nikaamua kupaki karibu na maktaba kwenye makutano ya Michigan na Adams. Nikaweka hela za kupaki za saa moja.

Nilishasahau kuwa ninaishi kwenye nchi yenye hofu ya kuvamiwa na jamaa zake yule bwana mwenye madevu anayeishi mapangoni kule Afghanistan. Basi nikakuta kuna mashine za kutazama kama mtu amebeba silaha. Nikaambiwa nitoe kila kitu mfukoni na kuweka ndani ya bakuli la rangi ya kahawia. Baada ya kuonekana kuwa sina chochote cha kutishia usalama nikaruhusiwa kuingia.

"Naelekea mahakama namba nne." Namweleza binti aliyeko mapokezi. "Mahakama namba nne imehamia namba sita." Ananiambia. "Chukua lifti hadi gorofa ya nne." Ananielekeza. Ninapoifika mahakama namba sita nakuta imeshehena watu. Nachungulia kutazama sehemu ya kukaa. Jaji anasema, "Wenye majina yanayoanza na A hadi M wabaki hapa, waliobaki waende gorofa ya pili mahakama namba 2." Baadhi ya watu wanaondoka. Najivuta na kuketi. Mahakama inaanza shughuli zake. Watu wanaitwa mmoja mmoja. Wanaokuja hapa wote wana makosa ya barabarani. Jaji anakusome shtaka na adhabu yake na kukuuliza kama unakiri. Ukikataa kosa unapewa siku nyingine. Ukikubali unasomewa adhabu. Kama ni faini unaambiwa ulipe. Kama ni kifungo anakuuliza kama unaelewa kuwa ukikubali kosa utafungwa, na kuwa unaweza kufungwa kuanzia siku hiyo.
"Kosa lako la kuendesha bila leseni linaweza kukupeleka jela miezi sita pamoja/au faini ya dola 1000. Una haki ya kutafuta wakili." Jaji anasema. Wakati huo mimi ninajiuliza nitafikiwa saa ngapi? Nilidhani kuwa nitakaa mahakamani kama saa moja hivi. Matokeo yake nilikwenda kuweka hela zaidi kwenye mita ya nilikopaki gari mara tatu. Toka saa saba niliondoka mahakamani saa kumi jioni. Nilipofikiwa nilikuwa nimechoka hasa.
"Desanyo Maka," Jaji aliniita. Watu wengi wanashindwa kutamka Ndesanjo na Macha wanadhani inatamkwa Maka. "Nipo." Nikaitikia na kwenda kizimbani.
"Una kosa la kupita kwenye taa nyekundu na kuendesha bila kuvaa mkanda. Una hatia au huna hatia?" Alinisome shtaka na kuniuliza.
"Nina hatia kwa kosa la kwanza la kupita kwenye taa nyekundu ila sina hatia ya kutokuvaa mkanda." Askari aliyenikamata alidhani kuwa sikuvaa mkanda maana baada ya kunisimamisha, niliingiza mkono mfukoni ili kutoa leseni ya udereva, nikaweka simu mfukoni na kutoa kamba ya kusikilizia masikioni na kuweka mfukoni, alipoona ninajigusagusa akadhani kuwa ninakazana kufunga mkanda.

Ingawa nimetoka kwenye nchi ambayo watu wengi wanaamini kuwa ukifunga mkanda utashindwa kuruka wakati wa ajali, ninapoingia ndani ya gari jambo la kwanza ni kufunga mkanda. Nimekutana na watu wengi Tanzania wanaosema, "Ukifunga mkanda ni rahisi kufa wakati wa ajali!"

Jaji akaniuliza kama nina bima ya gari. Nikamwonyesha. Akasema, "Una hatia ya kupita kwenye taa nyekundu, unatakiwa ulipe faini ya dola 100. "Utalipa leo au siku nyingine?" Jaji akaniuliza. Nikajibu kwa uchungu, "Leo." Dola 100! Shenzi taipu!

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com