10/17/2004

KIMULIMULI NYUMA YANGU

Nimemaliza kukata kona ya barabara ya Upton kuingia barabara ya Bancroft. Nadhani ni saa tatu usiku. Nasikiliza zangu muziki wa Fela Kuti. Anaimba wimbo wake uitwao Mwalimu Usinifundishe Upuuzi. Fela! Nashindwa kummaliza.... Basi mara naona gari nyuma yangu yenye kimulimuli. Nafyonza, "Polisi huyo. Nimefanya nini?" Napunguza mwendo, naashiria kuingia upande wa kulia. Ninahamia upande wa kulia kisha nasimamisha gari. Polisi anasimama nyuma yangu. Nabaki ndani ya gari. Inapita kama dakika mbili hivi askari ananijia na kugonga dirishani huku mkono mmoja uko kiunoni penye bastola. Nashusha kioo. "Naomba leseni ya udereva." Ananiambia. Ninampa. "Una leseni ya jimbo la Washington, una mpango wa kurudi Washington au kuwa hapa?" Namwambia kuwa sina uhakika ila sitakuwepo Ohio kwa muda mrefu. "Kama utaendelea kuishi hapa lazima uombe leseni ya Ohio." Namwitikia. Anaichukua na kurudi garini kwake.

Nasubiri. Fela bado anaimba wimbo ule ule. Unajua nyimbo za Fela zilivyo ndefu. Wakati fela anarekodi na kampuni kubwa kwa mara ya kwanza, aliambiwa na kampuni hiyo, Polygram, kuwa lazima apunguze urefu wa nyimbo zake. Fela akagoma. Mpaka leo ana nyimbo ambazo ni zaidi ya dakika 30 tofauti na nyimbo nyingi za wanamuziki wengine ambazo huwa ni dakika tatu, nne, au tano. Ninaposikiliza nyimbo za Fela, kama leo hii, ninazidi kuelewa kwanini aligoma kufupisha nyimbo zake. Nyimbo za Fela ukizipiga kwa dakika tano itakuwa ni kama mtu mwenye njaa aliyepewa nusu kijiko cha chakula akipendacho. Nyimbo za Fela ni kama safari ndefu yenye matukio ya kufurahisha, kufikirisha, na kuchangamsha. Mrindimo wa ngoma, magitaa yanayopigwa kwa kurudiarudia kodi moja au mbili, kwaya ya matarumbeta yanayopayuka juu ya kinanda na gitaa la besi linalotembea kwa kuyumbayumba kwa madaha.

Askari amerudi. Ananikabishi leseni yangu na kipande cha karatasi. "Nenda mahakamani tarehe 18 mwezi huu. Umepita kwenye taa nyekundu na hukuwa umefunga mkanda."
"Sikufunga mkanda? Mbona sikuelewi?"
"Utakapokwenda mahakamani utajitetea. Asante." Anaondoka.
Kuhusu taa nyekundu sina uhakika kama nilifanya kosa. Ninadhani kama unatokea Upton na taa ni nyekundu, unaweza kuingia Bancroft kama hakuna gari lolote. Tarehe 18 ni wiki ijayo. Tusubiri. Mambo ya kwenda mahakama ya mtu mweupe siyapendi kabisa. Hata hivyo sina la kufanya. Ingekuwa nyumbani tukio hili lingemalizika kwa kuingiza mkono mfukoni.

Binadamu watu wa ajabu sana. Ukitoa rushwa unalalamika kuwa rushwa imekithiri. Ukikutana na mtumishi wa umma anayejali nidhamu ya kazi bado unaudhika!
Nasubiri wiki ijayo nitakueleza.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com