6/30/2005

Edinburgh

Jana kutokana na harakaharaka nilikosea nikaweka kwenye blogu hii mambo niliyoandika kwa ajili ya blogu ya kiingereza. Kwa ajili ya rekodi nitaacha kama ilivyo. Tumewasili Uskochi kama saa moja lililopita. Baada ya kuingia mtandaoni ndio nimegundua kosa nililofanya. Lakini hakuna lililoharibika. Kinachofuata ni kutazama ratiba na ramani ya mji ili kupanga jinsi ya kufuatilia matukio yanayotokea hapa Uskochi kabla ya mkutano wa wezi wakuu duniani.


We are living for Edinburgh early tomorrow morning. We are all excited. The first thing I want to do when I get there is to look for anarchists! So when you see anarchists, look carefully you will see me blogging!

Kesho safari ya Edinburgh

Kesho asubuhi na mapema tunaondoka kwa treni kuelekea Edinburgh, Uskochi. Kule ndiko kuna kivumbi cha wezi wa mataifa nane na wanaharakati wanaopinga mpango wa nchi za kibepari kufanya dunia nzima kama mali yao binafsi kwa kutumia viini macho kama vile Tume ya Afrika inayoongozwa na mzungu!

Filamu za propaganda za wazungu

Ukienda hapa katika tovuti ya kundi la mataifa yanayoongoza kwa wizi duniani, G8, utakuta viungo kwa ajili ya filamu za propaganda za kuonyesha kuwa "misaada" toka kwa Waingereza inasaidia sana bara la Afrika. Sijui ni lini wataonyesha filamu kuhusu jinsi silaha toka Uingereza "zinavyoisaidia" Afrika.

Mahojiano na BBC (Go Digital)

Leo tumekutana na Paul Mason wa kipindi cha BBC kiitwacho Newsnight. Kazungumzia mkutano wetu naye kwenye blogu yake. Pia tumekutana na mwanablogu wa gazeti la The Observer, Rafael Behr. Kwa ujumla leo ilikuwa siku nzuri sana na isitoshe tumeshinda ofisini siku nzima, hakukuwa na harakaharaka za kukimbilia kwenye matreni na mabasi, jambo ambalo tumekuwa tukifanya toka niwasili hapa jumatatu. Baada ya dakika 20 hivi jamaa wa kipindi cha Go Digital cha redio ya BBC atawasili hapa ofisini kufanya mahojiano nami juu ya masuala ya kublogu Afrika na mengine kuhusu teknolojia mpya ya habari na mawasiliano. Muda mfupi uliopita nimetuma makala yangu ya kila wiki katika gazeti la Mwananchi. Makala hiyo, siwezi kuipandisha sasa kutokana na muda kuwa mdogo, nimeipa kichwa hiki: Afrika Itaendelezwa na Waafrika na Kudumazwa na Wazungu.

6/29/2005

Mama Claire Short

Hivi sasa ni saa nne kasoro usiku. Nimechoka kutokana na mizunguko ya leo. Tulikwenda kwenye ofisi za BBC Online na baadaye tukafanya mahojiano mazuri mno na mama Claire Short aliyejiuzulu toka serikali ya Blair kutokana na uvamizi dhidi ya Iraki. Kutokana na uchovu, na kutakiwa kuamka mapema mno kesho, sitaweza kuandika aliyosema mama huyu. Kaongea kweli. Kwa kifupi, kasema Tume ya Afrika na ripoti yake ni upuuzi mtupu! Kesho.

Kutoka London: Nasaha za Tariq Ali na wenzake

Jana, mimi na John Kamau wa Sunday Standard (Kenya) tulifanya mahojiano na Cliff Stone, mkurugenzi wa City Water aliyetimuliwa nchini. Mahojiano hayo yalipangwa na taasisi ya Panos London. Dhumuni kuu lilikuwa ni kupata taarifa toka kinywani mwake kuhusu mgogoro wa kampuni aliyokuwa akiiongoza na serikali ya Tanzania. Hatukumaliza mahojiano yenyewe, tutaendelea. Siku haijapangwa.

Katika mambo yote tuliyofanya jana, kubwa ni pale tulipokwenda ukumbi wa New Theatre wa London School of Economics kwenye mhadhara ulioitwa Make the G8 History. Nlifurahi sana kumsikiliza na kukutana na Tariq Ali, mwandishi wa habari, mtunzi, na mhariri wa jarida la New Left Review. Tariq ni mwandishi wa kitabu kiitwacho The Clash of Fundamentalisms. Wengine waliozungumza kwenye mhadhara huo ni mwandishi George Monbiot, na Mark Curtis.

Tariq Ali alizungumzia mada iliyoitwa Power and Resistance. Haya ni baadhi ya mambo aliyosema:
- Afrika haitakaa iondoke kwenye dimbwi la umasikini kwa kutumia misaada toka nchi za Magharibi
- Wanasiasa wa mrengo wa kulia na kushoto wana tofauti ndogo sana. Ukiwachambua kwa undani unakuta lao moja
- Marekani ni kati ya nchi zinazoongoza kwa rushwa duniani!
- Ili kuondokana na uchumi tegemezi Afrika iache kukimbilia nchi za Magharibi na ianze kushirikiana na nchi za Amerika ya Kusini
- Waafrika waache kutegemea tabaka la wasomi na matajiri wa Afrika na wanasiasa wa Magharibi

Mark Curtis alisema yafuatayo:
- Nia ya Uingereza katika mpango wake wa Afrika sio kuondoa umasikini bali kutengeneza njia kwa ajili ya makampuni ya Magharibi kuwekeza na kuiba utajiri wa Afrika
- Anashangaa sana waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, anaonekana kama vile ni mwokozi wa Afrika
- Ni ajabu kuwa Uingereza inajifanya ghafla kuwa inaipenda Afrika wakati ilikaa kimya wakati wa mauaji ya Rwanda, iliunga mkono ubaguzi wa rangi Afrika Kusini kwa miaka 50, ilimuunga mkono dikteta Idd Amin kwa mwaka mmoja na nusu, ina historia chafu sana kutokana na mateso ya Kinazi iliyowafanyia mashujaa wa kundi la Maumau nchini Kenya, na kitendo cha serikali ya Uingereza kukaa kimya wakati makampuni ya mafuta ya Uingereza yananyonya utajiri wa Nigeria na mabenki ya Uingereza yakificha fedha za watawala wala rushwa wan chi hiyo

George Monbiot alisema:
- Mwanamuziki Bob Geldof anashangaza baada ya kuwaambia wanamuziki wanaoshiriki kwenye tamasha la Live 8 kuwa wasimsakame mwizi namba moja duniani ambaye ni raisi wa Marekani, Joji Kichaka
- Wazungu nane (viongozi wa G8) wanajifanya kuwa wana uwezo wa kuondoa matatizo ya dunia nzima

Waandishi wa habari toka Kenya wafukuzwa Tanzania

Jamaa mmoja kanitumia habari hii muda sio mrefu. Imenishangaza. Soma mwenyewe.

6/28/2005

Nimewasili kwa Bibi

Niko kwenye mgahawa wa Copacabana nje ya hoteli ninayokaa katika mtaa wa Southampton. Ninaandika haraka kidogo maana muda si mrefu tutaondoka na waandishi wengine, ambao wanakunywa chai sasa, kwenda ofisi za Panos.
Niliwasili jana asubuhi hapa kwa Malikia Lizabeti, au kama vijana wa kijiweni wanavyopaita, 'kwa bibi.' Nimekutana na waandishi wengine walioko kwenye mpango huu wa shirika la Panos wa G8 Media Fellowship: Kamau, Machrine, na Maura. Salamatu toka Sierra Leone anawasili leo.
Jana tulipelekwa kutambulishwa kwa wafanyakazi wa Panos na baada ya mlo wa mchana tulihudhuria kikao cha wafanyakazi wa shirika hili, ambapo kulikuwa na ripoti kuhusu ushiriki wa Panos katika mkutano wa dunia wa masuala ya jamii-habari (world summit on information society). Baadaye tulikwenda ofisi za bunge kuoana na mbunge wa jiji la York, Hugh Bayley, ambaye ni mwenyekiti wa Africa All Party Parliamentary Group. Alitueleza kwa kifupi juu ya kazi na mafanikio ya kundi hili. Nitatoa maelezo yake kadri siku zinavyokwenda.
Leo tutakuwa na mjadala kuhusu agenda ya kundi la nchi nane (G8) na pia kutazama yaliyomo katika vyombo vya habari vya Afrika na Uingereza kuhusu mkutano wa G8 utakaofanyika mwezi ujao, ambapo moja ya agenda kuu ni suala la maendeleo ya Afrika. Tutakwenda katika ofisi za gazeti la Metro, ambalo liko mbioni kuanzisha blogu. Kuna watu kadhaa ambao kuna uwezekano wa kukutana nao leo, au siku nyingine, kutegemea na ratiba itakavyokuwa: Aubrey Meyer wa Global Commons Institute, John Hilary wa kundi la Chatham House, na waziri wa masuala ya maendeleo ya kimataifa, Hilary Ben.
Mchana nitakwenda kufanya mahojiano na mmoja wa wakurugenzi walitimuliwa nchini Tanzania, Cliff Stone, wa kampuni ya City Water iliyokuwa imepewa jukumu la kusambaza maji jijini Dar Es Salaam. Tutakutana katika ofisi za kampuni mama ya City Water iitwayo BiWater.
Ila tukio kubwa nadhani ni kesho tutakapozindua blogu mpya inatakayoendeshwa na waandishi toka Afrika. Anuani yake siwezi kuianika hapa sasa hadi izinduliwe rasmi.
Mengine baadaye.

Namba yangu London

Nimewasili hapa Landani (london) jana asubuhi. Wasomaji wangu walioko hapa wanaweza kuwasiliana nami kwenye namba hii: 0207 242-2828. Chumba changu ni nambari: 445.

6/26/2005

Naondoka kwenda kwa Malikia Lizabeti

Kama nilivyoeleza hapo nyuma, ninakwenda kublogu, pamoja na mambo mengine, mkutano wa nchi zinazoitwa "tajiri" kuliko zote duniani kule Uskochi. Nikiweka kituo sentensi ya mwisho hapa ninabeba begi, huyooo...

Kwahiyo ukisikia tena toka kwangu nitakuwa niko kwa Malikia Lizabeti, itakuwa ni siku ya jumatatu. Kwahiyo fuatilia mkutano huo na mambo mengine kama maandamano ya kupinga wezi hao wa mataifa nane, n.k. katika blogu hii. Mpaka tutakapoonana kesho, uhuru daima!

SHAIRI: NIANZE WAPI?

Kila mara
Ninakaa chini
Nikuandikie shairi
Mahiri
Wangu wa moyoni
Jua la asubuhi
Usiku wa mbalamwezi.
Kila mara ninapokaa
Chini
Nikuandikie shairi
Wangu azizi
Najiuliza
Pasi jibu
Nianze wapi?
Usiku nilikuwaza
Nikatamani
Utamke neno
Nami nijibu.
- Vermont, USA 2005

Mdahalo kuhusu Afrika na G8 redio ya BBC

Siku ya ijumaa na jumamosi, tarehe kwanza na pili mwezi ujao, Redio ya BBC itatangaza mdahalo uitwao: Je nchi za G8 zinaweza kuinusuru Afrika? Watakaoshirika katika mdahalo huo utakaofanyika katika ukumbi wa Africa Centre, jijini London, ni: Tajudeen Abdul-Raheem, Mkurugenzi wa Justice Africa na katibu mkuu wa Pan African Movement, Rosemary Museminali,balozi wa Rwanda Uingereza, James Shikwati, mwanauchumi toka Kenya, na Lord David Triesman, waziri mtarajiwa wa masuala ya Afrika.

Matangazo ya mdahalo huo yatarushwa siku ya ijumaa tarehe kwanza saa 1900 GMT, 2100 GMT, na 2200 GMT; na siku ya jumamosi tarehe pili saa 1100 GMT.

6/25/2005

Live 8: Kutazamwa na mabilioni ya watu

Onyesho la kuhamasisha juu ya umasikini barani Afrika, onyesho kubwa kuliko yote yaliyowahi kurushwa kwenye luninga na intaneti. Onyesho hili litapita hata idadi ya watu bilioni 3.9 waliotazama mashindao ya olimpiki kule Athens, Ugiriki.

6/24/2005

Tutakutana na George Monbiot

Waandishi tunaokwenda nchini Uingereza katika mpango wa shirika la Panos uitwao G8 Media Fellowship, tumefahamishwa kuwa asubuhi ya tarehe 5 mwezi ujao tutakutana na mwandishi na mtangazaji nimpendaye wa siasa za mrengo wa kushoto, George Monbiot. Monbiot huwa anaandika makala za kila wiki katika gazeti la the Guardian la Uingereza. Licha ya kuandika magazetini, Monbiot pia ni mtunzi wa vitabu kama vile The Age of Consent: A Manifesto for a New World Order, Captive State: The Corporate Takeover of Britain, Poisoned Arrows, na No Man’s Land (alichokiandika kutokana na ukachero alioufanya Kenya na Tanzania). Monbiot, ambaye ameishi na kufanya kazi Indonesia, Brazil, na Afrika ya Mashariki, ni mwalimu wa muda katika chuo kikuu cha Oxford Brookes. Tembelea tovuti yake kwa habari zaidi juu yake na makala na insha mbalimbali za upembuzi yakinifu.

Marekani, Marekani, Marekani...

Sirikali ya Marekani inayoongozwa na mwizi wa kura, Joji Kichaka, inanichefua kupita kiasi. Wakati wakianza kushawishi dunia bila mafanikio kuhusu uvamizi dhidi ya Iraki, moja ya sababu kuu walizotoa ni kuwa nchi hiyo imekuwa ikizuia wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukagua maeneo yanayoaminika kuwa yalikuwa yanatengeneza silaha za sumu. Watawala wa nchi hii wakauliza, "Kama Iraki haitengenezi silaha kwanini inakataza wakaguzi wa Umoja wa Mataifa? Kuna nini kinafichwa?"
Sasa kichekesho cha siasa za beberu huyu ni hiki: toka mwaka 2002 (leo ni 2005) Umoja wa Mataifa umekuwa ukiomba ruhusa toka sirikali ya Marekani ili wakaguzi wake waende wakatembelee wafungwa walioko ghuba ya Guatanamo. Hadi dakika hii Marekani haijakubali kuruhusu wakaguzi hao. Ni kitu gani kinafichwa?
Taarifa za mateso na unyama uliokithiri unaofanywa na Marekani dhidi ya wafungwa zinatisha. Majuzi tulisikia kuwa badala ya kutumia karatasi maalum za chooni, askari wa Marekani hapo Guantanamo walitumia Kurani. Hivi Marekani imeishiwa kiasi cha kushindwa kununua karatasi za chooni?
Kwanini wakaguzi wa Umoja wa Mataifa hawaruhusiwi? Ukweli ni kuwa wakaguzi hao wakiruhusiwa kuonana na wafungwa, habari za kuteswa kwao tukazisikia, dunia nzima itatambua kuwa sirikali ya Marekani haina tofauti yoyote na sirikali ya Taliban au ya huyo Saddam Hussein waliyemgeuka. Ukitaka kujua ukweli wa serikali hii tazama marafiki zake wakubwa: Saudi Arabia, Israeli, Equatorial Guinea, Pakistani, n.k. Usisahau pia kuwa sirikali za Taliban na Saddam Hussein zilikuwa ni maswahiba wa kufa na kuzikana na Marekani kwa miaka mingi. Ukitaka kumfahamu mtu kwa undani, tazama marafiki zake. Ndivyo hivyo hata kwa sirikali.

6/23/2005

Wanablogu Shirikini Kwenye Muhtasari

Kama nimekosea naomba nisahihishwe. Katika tafutatafuta nimeona kuwa tafsiri ya Kiswahiliya neno, survey, ni muhtasari.
Haya, kuna muhtsari kwa ajili ya wanablogu unaondeshwa na maabara ya chuo cha MIT. Tafadhali ukiwa na muda shiriki.
Wakati natembelea tovuti ya maabara hiyo nimekutana na habari hii kuhusu kompyuta za mapajani za dola 100!

6/21/2005

NINAKWENDA KUBLOGU MKUTANO WA G8

Waandishi saba wa Afrika, nikiwemo kati yao, tutakwenda Uingereza, pamoja na mambo mengine, kuhudhuria mkutano wa G8 utakaofanyika tarehe 6-8 mwezi ujao kule Uskochi. Safari yetu itakuwa ya wiki mbili (wiki moja katika jiji la London na wiki nyingine Edinburgh. Tutakuwa katika mpango uitwao G8 Media Fellowship wa shirika lisilo la kiserikali la Panos London. Waandishi wengine watakaoshiriki wametoka Kenya, Uganda, Malawi, Sierra Leone, na Msumbiji. Moja ya madhumuni ya mpango huu ni kuwawezesha waandishi wa habari toka Afrika kuweza kuwa na ufahamu zaidi juu ya masuala ya sera na mikutano ya kimataifa. Pia itawawezesha kuandika habari kuhusu mkutano huo kupitia mtazamo wa Waafrika wenyewe.
Tembelea shirika la
Panos kujua zaidi juu ya kazi zake.

*******************************************************************************

Maombi yangu ya visa ya kwenda Uingereza yamekubaliwa leo. Hivyo nitaondoka jumapili kwenda huko kwa Malikia Lizabeta. Nikiwa huko nitablogu hapa Jikomboe juu ya mkutano na matukio mengine yanayohusiana na mkutano wa nchi nane za kibepari. Pia shirika la Panos linatengeneza blogu maalum kwa ajili ya mkutano huo. Nikishapata anuani ya blogu hiyo nitaweka hapa.

Nikiwa ninablogu kwa Kiswahili kupitia Jikomboe,
Mshairi, mwanablogu toka Kenya anayeishi Uingereza amenieleza kuwa ana nia ya kutafsiri (nitakayokuwa naandika kwa Kiswahili) kwa kiingereza kwenye blogu yake. Namshukuru kwa uamuzi wake huo wa kujitolea.

6/19/2005

HUYU NI MMOJA WA WAJUMBE WA TUME YA "AFRIKA"

Mmoja wa wajumbe wa ile Tume ya Afrika ambayo mkuu na mwanzilishi wake ni Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, (sijui Blair alizaliwa kijiji gani Afrika hadi aanzishe tume ya Afrika), ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi. Kama tuna mtu kama Zenawi kwenye tume ya kujenga Afrika mpya, hiyo Afrika itakuwa na mito ya damu? Fuata viungo hivi usome unyama wa majeshi ya mjumbe huyu wa tume ya "kuiokoa" Afrika. Kongoli hapa, hapa, na hapa.

WAZUNGU NA AFRIKA: MAENDELEO YETU BILA SISI KUSHIRIKISHWA?

Soma uchambuzi uliofanywa na katibu mkuu wa Pan Africa Movement, Dakta Tajudeen Abdul-Raheem kuhusu juhudi za kuondoa umasikini Afrika bila kushirikisha Waafrika wenyewe. Anachozungumzia ndio hasa mchezo wa kuigiza unaoendelea huku duniani ukipigiwa makofi na vigelegele na viongozi wetu na suti zao wanaozunguka Ulaya na Marekani kunadi nchi zetu.

Blogu zilizopata tuzo ya Wanahabari Wasio Na Mipaka

Wanahabari Wasio na Mipaka wametangaza blogu zilizopata tuzo ya kutetea uhusu wa kujieleza. Blogu iliyoshinda toka Afrika ni hii hapa toka Morocco. Na hii ndio orodha ya blogu zote zilizopata ushindi. Wanablogu walioshinda watahojiwa hivi karibuni kupitia ukurasa wa mradi wa Global Voices.

UCHAGUZI WA IRANI, MGOMBEA MWENYE BLOGU NA KADHALIKA

Mwanablogu maarufu wa Iran anayeishi nchini Kanada, Hoder, yuko nchini Iran ambako alirudi hivi karibuni ili aweze kuandika juu ya uchaguzi huo. Pia mmoja wa wagombea urais nchini humo, Dakta Mostafa Moeen, ana blogu yake. Kulikuwa na hofu kuwa pengine mwanablogu Hoder angetiwa ndani kama wanablogu wengine ambao wako jela kutokana na kutumia blogu zao kupinga udhalimu wa serikali yao.

TEKNOLOJIA INAVYOSAIDIA WATU WA KAWAIDA AFRIKA

Msikilize Peter Day wa BBC akizungumzia jinsi ambavyo teknolojia mpya za mawasiliano na habari zinavyosaidia watu wa kawaida (kama wakulima na wafanyabiashara wadogo) katika bara la Afrika.

6/18/2005

DUNIA IMETUKOSA NINI?: Soma ripoti za PANOS

Utakuwa ukisikia sana masuala ya mazingira yakitajwa kwakuwa moja ya masuala ambayo wakuu wa nchi za kibeberu duniani watakayojadili mwezi ujao kule kwa Malikia Lizabeti ni mabadiliko ya mazingira. Shirika la Panos lina ripoti mbili toka kitengo chake cha mazingira. Hapa na hapa.

Gatua na Mashairi ya Kikuyu

Niliandika siku za nyuma juu ya CD mashairi ya Gatua wa Mbugwa iitwayo Maitu Ni Ma Itu Keri. Unaweza kuonja uhondo wa kazi yake, ingawa kwa sekunde kadhaa, kwa kukongoli hapa, hapa, na hapa. Huenda ukawa hufahamu kuwa Gatua ni yule bwana ambaye aliandika tasnifu yake ya shahada ya pili katika chuo kikuu cha Cornell kwa lugha ya Kikuyu! Unaweza kusikiliza zaidi hapa. Au kununua kabisa CD zake hapa.

6/17/2005

SKOLASHIPU KWA WANABLOGU/WAANDISHI AFRIKA

Mkutano uitwao Highway Africa wa mwaka huu unafanyika Septemba huko Grahamstown, Afrika Kusini. Kuna nafasi chache za skolashipu kwa waandishi walioko Afrika. Nadhani wanablogu walioko barani wanaweza kuomba nafasi hizo hasa kutokana na ukweli kwamba katika mkutano huo kuna msisitizo wa matumizi ya zana mpya za mawasiliano na habari. Mwisho wa kuomba ni tarehe 7 mwezi ujao. Nenda hapa kwa taarifa kamili za mkutano na maelezo jinsi ya kuomba. Wanasisitiza kuwa ukiomba lazima UWE MWANDISHI WA HABARI.

6/16/2005

SIKU KUKU WALIPOMTEMBELEA TONY BLAIR

Siku hiyo Tony hatakaa aisahau. Kama ni wewe kuku walikutembelea utasahau? Basi kuku walibisha hodi kwa Tony wakitetea haki za wafugaji kuku nchini Ghana. Na video ya ziara hiyo ya kuku iko hapa.

WANAMUZIKI WA AFRIKA KUTUMBUIZA KUPINGA UBEBERU

Mapema leo nilipoandika kwa kirefu na kuweka viungo mbalimbali kuhusu yanayofanyika na yatakayofanyika katika kuelekea mkutano wa nchi 8 kibeberu duniani, nilisema kuwa watu wengi hawaelewi kwanini tamasha la muziki la Live 8, ambalo nia yake ni kutetea Afrika linafanyika bila wanamuziki wa Afrika kushirikishwa. Sasa waandaaji wamegutuka. Wametangaza kuwa wanamuziki wa Afrika watatumbuiza siku ya tamasha hilo, ila katika ukumbi wao wenywe (!!!). Kati ya wanamuziki watakaoshiriki ni mwanamama toka Somalia. Maryam Mursal. Mursal aliwahi kupigwa marufuku kuimba nchini kwake Somalia baada ya kuisakama serikali. Hiyo ilikuwa ni kabla hajakimbilia Ulaya. Baada ya kuzuiwa kuimba alijipatia riziki kwa kuendesha teksi. Hii hapa ni historia yake fupi. Sikiliza mahojiano yake na redio ya NPR. Pia watakuwemo Angelique Kidjo wa Benin na Yossouf Ndour wa Senegal. Habari ya kuwepo kwa tamasha hilo la wanamuziki wa Afrika katika jiji la London iko hapa.

MKUTANO WA G8: JIELIMISHE...

Nitaandika sana kuhusu mkutano wa makabaila uitwa G8 unaofanyika mwezi ujao kule Uskochi. Mkutano huu ni muhimu kwetu kuufuatilia maana moja ya mambo makubwa wanayojadili ni suala la maendeleo Afrika . Mkutano huu ni muhimu kama mkutano huu mwingine utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Uingereza ndio itakuwa mwenyekiti wa mkutano wa mwaka huu wa mabepari. Wakati Marekani imechukua suala la ugaidi na “amani” Mashariki ya Kati kuwa kipaumbele katika sera zake za nje, Uingereza imechukua Afrika na masuala ya mazingira kuwa ndio vipaumbele vyake. Mkutano wa G8 kawaida huwa unajadili masuala ya sera zinazohusu mataifa hayo, ila mwaka huu suala la umasikini Afrika litakuwa mstari wa mbele kutokana na mtazamo wa kisera wa serikali ya Uingereza. Katika kufanikisha azma yake ya kuweka Afrika mbele katika sera zake, serikali hiyo ilianzisha Tume ya Afrika, ambayo rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ni mmoja wa wajumbe.

Mwezi wa tatu mwaka huu tume hiyo ilitoa ripoti yake (baadaye nitawapeni maoni ya watu mbalimbali juu ya ripoti hiyo ya tume ambayo waafrika “tumeundiwa.”


Serikali ya Uingereza pia itachukua ukuu wa Jumuiya ya Ulaya (kwa miezi sita) ambapo serikali hiyo ina nia ya kuweka suala la afrika na umasikini duniani kwenye meza ya majadiliano

Wakati hayo yote yanaendelea, mashirika yasiyo ya kiserikali, watu binafsi, wanaharakati, na vyama mbalimbali vimekuwa katika
kampeni kubwa ya kutaka umasikini duniani utokomezwe na kupinga unafiki, ulafi, na tamaa za nchi tajiri na makampuni makubwa ya kibepari


Huko Uingereza, mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa na kampeni motomoto iitwao “Fanya Umasikini Kuwa ni Historia” (Make Poverty History). Wako wanablogu kama huyu hapa ambao wameweka nembo ya kampeni hii kwenye blogu zao. Kampeni hii inatarajia kushirikisha watu zaidi ya laki mbili kwenye maandamano mwezi ujao huko Uingereza. Hapa kuna habari zaidi juu ya maadamano ya kupinga ubeberu.

Katika harakati hizi za kupinga ubeberu sanaa ya muziki itatumiwa katika miji ya London, Paris, Rome, Philadephia, na Berlin kama njia ya kuonyesha kuwa dunia imechoka na sera za ukandamizaji za mataifa makubwa. Utashangaa kuwa ingawa kampeni hii inafanyika hasa kwa ajili ya Afrika, hakuna mji wa Afrika utakaokuwa na tamasha hili na sijaona jina la mwanamuziki toka Afrika katika orodha ya watakaoshiriki. Kwa sasa niweke mawazo yangu pembeni maana nataka kukupa kwanza picha halisi ya kinachofanyika kisha baadaye tukae chini tujadili, tujiulize maswali, tukosoe, tuunge mkono, n.k.

Suala jingine kubwa litakalojadiliwa kwenye G8 ni mazingira. Katika kampeni zitakazofanyika kule Uingereza, kutakuwa na tukio la kutoa ripoti inayoitwa Afrika Inaungua (Africa is Burning) na masuala ya kampeni dhidi ya ubakaji wa dunia yetu. Katika shughuli zitakazokuwa zikifanyika katika kupinga ubepari na madhara yake kwa masikini na mazingira kutakuwa na kitu
kinaitwa Mbadala wa G8. Na pia kuwakuwa na wanaharakati wa mazingira watakaokuwa na “Tahadhari ya Mazingira.”

Pamoja na mpango wa serikali ya Uingereza kutaka nchi za Afrika zipewe misaada zaidi, ikiwa ni pamoja na kusamehewa madeni na kueleza kuwa nia yake ni kutaka kuona Afrika inaondokana na umasikini, bado sera zake zinazua mabishano, utata, mizozo, n.k. Kwa mfano, shirika la misaada la Action Aid, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, limetoa ripoti inayoonyesha kuwa sehemu kubwa ya misaada ya fedha huwa inaishia kurudi nchi za Magharibi na sio kusaidia nchi changa. Serikali ya Uingereza imepinga ripoti hiyo.

Moja ya mambo ambayo wanaharakati wanasema ni kuwa sera ya serikali ya Uingereza inataka nchi za Afrika zizidi kufungua soko lake na kubinafsisha kila kitu. Madhara na utata mzima wa zoezi la ubinafsishaji unaonyeshwa katika
sakata la kubinafisha maji Tanzania. Ubinafishaji huu ambao umeungwa mkono na Benki ya Wazungu ambao pia huitwa Benki ya “Dunia” umesimamishwa na serikali ya Tanzania

Hapa kuna mabadilishano ya barua kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali Uingereza na mshauri wa kampuni iliyopewa kazi ya kuhodhi maji wakati ambapo maji ni zawadi toka kwa Mola, Ruwa, Ngai, Mulungu, n.k.

Pia gazeti la The Guardian
lina barua ya siri iliyobambwa na waandishi ikielezea kuwa Jumuiya ya Ulaya ambayo inaendesha Mpango wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya nchi za Ulaya na Afrika ikimtaka waziri wa Uingereza anayeshughulikia mambo ya uchumi ya Jumuiya ya Ulaya, Peter Mandelson amshinikize Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, aache kuendeleza sera zinazipa serikali za Afrika haki zaidi za kuamua jinsi ya kuendesha uchumi wa nchi zao.

Habari hiyo imepelekea mabadilishano ya barua kama utakavyoona
hapa na hapa.

Na pia makala kali ya mwandishi matata George Monbiot akidai kuwa serikali ya Uingereza inachofanya kuhusu sera yake ya Afrika ni mchezo wa kuigiza!

Na tena inadaiwa kuwa wakati Uingereza ikidai kuisaidia Afrika, nchi hiyo inaongoza kwa kulinyang’anya bara hilo watumishi wake katika sera ya afya.

Naachia hapa kwa sasa. Itaendelea...


Waafrika Walivyowambwa Mtini Marekani

Bunge la Marekani ambalo lina historia ya kupinga zaidi ya miswada 200 iliyokuwa na nia ya kuondoa sheria zilizoruhusu watu weusi kuuawa kwa kuwambwa mtini, sasa linaomba msamaha kutokana na makosa yake. Sikuwa najua kuwa zaidi ya mara 200 bunge hili lilikataa kuzuia mauaji haya ya kinyama kabisa kwenye historia ya mwanadamu. Mauaji haya yanaitwa kwa kiingereza lynching. Tazama aliyoandika mwanamama Ida B. Wells aliyekuwa mstari wa mbele kupinga unyama huu wa wazungu. Mwanamuziki Billie Holiday aliimba wimbo uitwao Strange Fruit akimaanisha kuwa miili ya watu weusi iliyotundikwa mitini wakati wa mauaji hayo ni sawa na matunda ya ajabu. Wimbo huo uliandikwa na mwanamuziki Lewis Allen. Haya ni baadhi ya maneno ya wimbo huo unaosikitisha sana:
Southern trees bear strange fruit,
Blood on the leaves and blood at the root,
Black bodies swinging in the southern breeze,
Strange fruit hanging from the poplar trees

Kuna sinema iitwayo Strange Fruit ambayo inaonyesha kwa kina unyama huu dhidi ya binadamu ambao kosa lao ni rangi yao.
Je msahama huu watu weusi wanauonaje? Soma maoni haya. Wachambuzi wa masuala ya watu weusi wanadai kuwa unyama huo unaendelea hivi sasa kwa sura nyingine, sura hiyo ni magereza ya nchi hii ambayo yamejaza watu weusi masikini. Kwahiyo Marekani ya leo mfumo wake wa magereza ni sawa na miti iliyokuwa ikitundika miili ya watu weusi wasio na hatia.

6/14/2005

JAMES MAPALALA ALIVYONIKARIPIA

Nadhani ulikuwa ni mwaka wa 1993 mwishoni au '94 mwanzoni. Wakati huo nilikuwa ndio ninaandikia gazeti la Bara Afrika chini ya mhariri Joseph Kaseba (bado uko Kigoma?) na Songoro Mnyonge (mara ya mwisho ulikuwa gazeti fulani pale Kariakoo, sikumbuki jina. Magazeti mengi siku hizi...niandikie).
Basi yapata mwendo wa saa tano hivi nikajiondokea kwenda kumhoji ndugu James Mapalala. Sijui nilikuwa nafikiria nini. Siku hiyo gazeti la Bara Afrika lilikuwa limetoa habari ya kumponda Mapalala. Nilipofika nyumbani kwake (na ofisini kwake wakati huo) pale mitaa ya Morocco, jijini Dasalama, tayari yeye na washabiki zake walishanunua Bara Afrika na kulisoma. Basi nafika pale nakutana na Bazigiza (naye sijui yuko wapi siku hizi toka ile misukosuko aliyoipata toka kwa "usalama" wa taifa). Bazigiza alijua kuwa mimi ni mwandishi wa Bara Afrika. Siku hiyo alinitazama kwa namna ya tofauti. Sikushtuka. Hadi leo sijui nilikuwa nafikiria nini kwenda kwa Mapalala baada ya kumponda.
Nikaomba kuoanana na Mapalala. Nikakaribishwa sebuleni. Mapalala akaja. Wacha anisute. Aliongea kweli. Akasema hana muda wa kufanya mahojiano na mimi. Kwanini nisifanye mahojiano kabla ya kumponda? Akasema mambo elfu kumi kidogo kuhusu gazeti lile na waandishi wa habari. Washabiki zake wanatikisa kichwa na kuitikia kwa sauti ili awasikie. Nimewekwa kiti moto. Sikuwa na la kusema. Wala la kujitetea. Nilibaki kimya kama nimemwagiwa maji. Nikabadilika rangi. Mdomo ukanikauka. Akanisuta, akanisuta weee.... kisha akaondoka zake.
Bazigiza akawa na ubinadamu kidogo. Akaongea nami mambo mawili matatu kwa upole kama vile ananifariji kwa chati. Kisha nikaanga.
Sitakaa nisahau. Kilichonikumbusha kisa hiki ni habari hii kuhusu Mapalala kugombea urahisi Tanzania.

Eti Wametusamehe madeni

Eti wazungu wametusamehe madeni...wametusamehe kivipi wakati sisi ndio tunawadai. Wametuibia miaka mingi. Wameiba sio maliasili tu bali waliiba hadi watu kwa miaka 400 (biashara ya utumwa). Na wanaendelea kutuibia. Sasa wanakuja na mchezo huu wa kuigiza eti wametusamehe madeni, watawala wezi Afrika na wananchi tunashangilia. Hebu nipisheni nipite...

6/13/2005

VITA VYA PILI VYA DUNIA NDIO VITA GANI HIVYO?

Jamaa yangu mmoja ananijia na historia yake ya Afrika aliyosoma toka vitabu vya wazungu. Wakati ananiuliza uliza maswali juu ya watawala wa Afrika akinionyesha kuwa analifahamu bara langu, alitaja vita vya pili ya "dunia."
Nikamuuliza, "Vita gani hiyo umeitaja mbona siijui?" Akatoa macho kwa mshangao, "Yaani hujui vita vya pili vya dunia?"
"Sifahamu." Nikamjibu.
"Ni ajabu sana kama hujasoma habari za vita hivyo shuleni."
"Kama vita hivi viko kwenye vitabu vyenu vya historia ni ajabu sana kuwa sivijui maana historia tunayofundishwa Afrika asilimia kubwa ni historia yenu na kidogo tunachojifunza kuhusu Afrika ni ninyi mmetuandikia." Namwambia.
Baada ya hapo alitumia dakika kadhaa kunieleza juu ya vita hivyo. Alipomaliza nikamuuliza, "kwanini unaita vita vya dunia wakati maelezo yako yanaonyesha kuwa ugomvi ulikuwa ni wenu wazungu Ulaya na Marekani?"
Akashtuka kidogo. Akataka kufungua mdomo akaacha. Sasa anaona historia kwa jicho jingine.
Nikachukua nafasi hiyo kumpasha sawasawa. Kuna wakati unachoka kabisa kufundisha watu kila dakika. Ukikutana na nduguzo toka Afrika unakuta wamekwenda shule ila wamedanganywa toka vidudu hadi chuo kikuu, basi inabidi uanze kuwafundisha taratibu. Ukikutana na hawa jamaa zake Karl Peters nao unakuta wanaogelea kwenye uongo uitwao historia.
Kwanini vita vya kwanza na vya pili vya wazungu vinaitwa vya "dunia"? Hawa mabwana wamechukua historia yao na uzoefu wao kuwa ni historia na uzoefu wa dunia. Vita yao wanafanya ni vita vya dunia nzima. Vita vya kwanza na vya pili vya dunia vilijaa unyama usioelezeka. Sasa wanataka tugawane lawama na hatia ya vita hivyo. Vita vile havikuwa vya dunia. Dunia nzima haikuwa inapigana. Kama ni vya dunia, je Tanzania tulikuwa tumegombana na nani katika vita vya kwanza na vya pili? Je Kambodia ilikuwa ikipambana na nani? Je Brazili, Venezuela, Paraguay, n.k.? Kuna watu katika nchi hizi waliopigana katika vita hivyo ila hawakuwa wanatetea maslahi yao, walikuwa wakitetea maslahi ya wazungu, maslahi ya wakoloni. Walikuwa wakipigana kwenye ugomvi wa wazungu. Havikuwa vita vyetu vile, havikuwa vita vya dunia.
Kwahiyo ninakushauri kama nilivyomwambia huyu bwana, usije hata siku moja ukasema vita vya kwanza au vya pili vya "dunia." Kama ni mwanafunzi, usikubali hata kidogo mwalimu akudanganye kwa kukwambia kuwa kuna vita vinaitwa vya dunia. Dunia haijawahi kupigana. Jiulize nini kilikuwa kinagombaniwa, maslahi yalikuwa ya nani, n.k. Jiulize sikukuu za kukukmbuka ushindi wa vita hivi zinafanywa wapi?
Nchi za Ulaya zilikuwa na magomvi yao, sasa wanatumia uongo uitwao historia kufanya kuwa vita vile ni vya dunia nzima...usikubali. Sema vita vya kwanza vya wazungu (au Ulaya) au vita vya pili vya Ulaya na Marekani.
Ndivyo nilivyomwambia jamaa yangu. Nikamuonya.
Wakati tunaagana aliniacha akitikisa kichwa. Aliniuliza, "Hivi nchi yenu ilipata uhuru lini tena?"
Nikamjibu, "Bado tunatafuta uhuru!" Kuna watu wanaamini kabisa, na siwalaumu, kuwa nchi za Afrika ziko huru. Kama unadhani uko huru, utaona vipi minyororo?

MADENI...WALIKOPA LINI?

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kati ya mwaka 1970 hadi 2002, Afrika ilipokea mikopo yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 540. Katika kipindi hicho, Afrika ililipa wazungu waliotukopesha dola bilioni za Kimarekani 550. Hadi mwaka 2002, Afrika ilikuwa na madeni ya dola za Kimarekani 295.
Nadhani mmeona vichwa vya habari kuhusu nchi 14 za Afrika zilizosamahewa madeni asilimia 100, Tanzania ikiwa ni mojawapo. Tanzania ilikuwa ikitumia asilimia 12 ya pato lake kulipia madeni. Watawala wa nchi zilizosamehewa madeni wanadai kuwa serikali zao sasa zitaweza kutumia fedha hizo kwa maendeleo ya wananchi.
Mimi hadi hivi sasa kuna jambo moja sijaelewa. Kwanini tunasamehewa madeni? Kwani tulikopeshwa lini? Mbona hizo hela mimi sijaziona? Kama fedha tulizokopa ziliingia kwenye mifuko ya watawala wanaotupa takrima kisha tunawapa kura, fedha zitakazopatikana kutokana na msamaha huu ndio wataamua kuzipeleka kwa Hadija, Matayo, Buruani, na Msechu?
Kusamehewa madeni huku wezi wakiwa wamekalia viti vya uongozi kutasaidia nini? Swali hilo.

MAREKANI INAHITAJI MSAADA KUONDOA NJAA!

Nimeamua kuwasiliana na wanamuziki wa Afrika ili wafanye onyesho la kuchangisha fedha za kusaidia watoto wanaokumbwa na baa la njaa Marekani. Si mnakumbuka wao walitusaidia tulipokumbwa na baa la njaa kule Ethiopia? Basi nasi lazima turudishe fadhila. Kama unashangaa iweje Marekani, nchi "tajiri" kuliko zote duniani ambapo wananchi wake wamejaza mapesa mfukoni, iwe na tatizo la njaa...nenda hapa. Kisha watembelee hawa jamaa.

TANZANIA KATIKA "MSAHAMA" ASILIMIA 100 WA MADENI

Eti wazungu wamefuta "madeni" wanayotudai kwa asilimia 100. Kati ya nchi 18 za Afrika "zilizofutiwa" madeni, Tanzania imo. Madeni hayo ni yale tunayodaiwa na benki ya wazungu ambayo watu huuita Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, na Shirika la Fedha Duniani. Waziri wa Fedha, ndugu Mramba, anasema haya kuhusu kufutiwa madeni hayo. Gazeti la Uhuru linatuambia kuwa eti kufutiwa madeni huko kunatokana na juhudi za Mkapa.

MKAPA AZINDUA RIPOTI YA TUME TULIYOUNDIWA NA WAZUNGU

Rais Mkapa mwishoni mwa wiki iliyopita alizindua ripoti ya Tume ya Afrika tuliyoundiwa na wazungu. Wakati wa uzinduzi huo alisema haya.

6/12/2005

Silaha huweza kuota kama miti?

Kumbe silaha za maangamizi zinazotengenezwa na nchi za Magharibi na kuuzwa nchi masikini kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe huweza kuota kama miti!

UNESCO na Matumizi ya Lugha Mbalimbali Mtandaoni

Ule mkutano wa shirika la umoja wa mataifa la Kielimu, Kisayansi, na Kiutamaduni, UNESCO, African Academy of Languages (ACALAN), Agence Intergouvernementale de la Francophonie, (AIF) na serikali ya Mali kuhusu matumizi ya lugha mbalimbali duniani kwenye mtandao wa kompyuta uliofanyika nchini Mali tarehe 6 na 7 mwezi jana ulifikia maazimio haya. Maazimio haya yanaendana kabisa na vuguvugu tunaloanzisha sisi wanablogu tunaotumia lugha za Kiafrika. Sisi tunaoamini kuwa titi la mama litamu ingawa la mbwa.

WANABLOGU CHINA WANATAKIWA KUJISAJILI SERIKALINI

Kati ya nchi ambazo watawala wake wanasumbuliwa sana na jinsi teknolojia ya mtandao wa kompyuta inavyotumiwa na wapinga serikali ni Uchina. Sasa nchi hiyo imeamua kuwa wanablogu lazima wasajiliwe, wajulikane ni akina nani, wanaishia wapi, n.k. Fuatilia zaidi habari hiyo hapa. Mwanablogu maarufu wa Uchina, Mao, anahojiwa kuhusu sakata hilo.

Mzee Madibaa kwenye tamasha la 46664 Norway

Mzee Mandela amehudhuria na kuongea katika tamasha kwa ajili ya janga la Ukimwi barani Afrika. Tamasha hilo lenye jina ambayo ndio namba aliyokuwa amepewa Mzee Madiba alipokuwa jela, 4664, liko kule Norway. Hotuba yake pamoja na habari zaidi za kampeni hii ya Mzee wetu nenda hapa.

6/11/2005

CD ya Ushairi wa Kikuyu

Garua wa Mbugwa ni mshairi anayetumia lugha ya Kikuyu. Unaweza kupata CD yake iitwayo Maitũ nĩ Ma Itũ Kerĩ(Mama Yetu Ndio Ukweli Wetu). Nenda hapa.


MAFUNZO KUHUSU UANDISHI WA MTANDAONI

Uandishi wa mtandaoni (blogu, wiki, n.k.) unakua kwa kasi hasa mataifa ya magharibi. Kama wewe ni mwandishi wa habari, mtunzi, mchambuzi, n.k. nenda hapa kuna mafunzo kuhusu aina hii ya uandishi.

Mkutano wa vyombo vya habari-husisha

Mkutano kuhusu vyombo vya habari-husisha huko New Orleans ulikuwa na jopo kuhusu mjadala wa blogu dhidi ya uandishi wa habari. Halafu Robert Niles anaongelea kuhusu uandishi wa mtandaoni.

UNAKUMBUKA ENZI ZA UTUMWA?

Burning Spear ana wimbo mmoja uitwao Days of Slavery. Kwenye wimbo huu anakuuliza: Unakumbuka walivyotupiga,
walivyotufanyisha kazi ngumu,
walivyotutumia,
na walivyotelekeza?

Mradi wa UNESCO unatukumbusha.

6/10/2005

Umeiona tovuti ya Chadema?

Niliwahi kutoa tovuti za vyama vya CCM na CUF. Hivi ndivyo vyama vya kwanza kuwa na tovuti rasmi Tanzania. Sasa Chadema nao wana tovuti. Inafurahisha jinsi vyama hivi (hasa CCM na Chadema) vinavyoenzi lugha ya taifa mtandaoni tofauti na serikali au bunge.SHAIRI LA UASI TOKA KWA MSOMAJI

Carlos Majura ni mshairi, mwanahistoria, na mwanaharakati kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaishi Nyakato, Mwanza. Shairi hili kuhusu uasi dhidi ya mfumo hasi kaandika yeye. Lisome:

Ikipatikana sababu na nafasi,
Kila mmoja huwa ni mwasi,
Pia huwa muasisi,
Katika kupigania salama ya nafsi.

Nafahamu kuwa wewe ni mwasi,
ulieasi kanuni na sheria za kibeberu.
Sasa umeshika kasi katika kuondoa nuksi,

nalaana za ukaburu.

Mimi pia ni mwasi,

ninapambana na mfumo HASI wa utawala.


WANAOIUA DUNIA....

Wanaoiua dunia wana majina na anuani. Hapa.

6/08/2005

TAMASHA LA "LIVE 8": WAAFRIKA NI WATAZAMAJI TU?

Bob Geldoff anakumbukwa kwa kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya waliokumbwa na baa la njaa Afrika miaka 20 iliyopita. Kampeni hiyo iliitwa Live Aid. Hivi sasa Geldoff, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Tume ya Afrika, anaongoza kampeni nyingine iitwayo Live 8. Katika kampeni hii, kutakuwa na matamasha ya muziki katika miji mbalimbali huku Ughaibuni. Tofauti na Live Aid, kampeni hii haitafuti fedha bali inakusanya sauti za watu wanaoamini na kusema kuwa “sasa imetosha.” Msikilize Mandela akiongea kuhusu mradi wa Live 8.
Katibu mkuu wa Pan African Movement yenye makao yake makuu Kampala, Uganda, Dk. Tajudeen Abdul Raheem, anasema kuwa kampeni hii ni mfano wa harakati mbalimbali duniani za kuwasaidia Waafrika ambazo haziwahusishi Waafrika. Anasema kuwa Live 8 ni sawa na kinyozi anayenyoa nywele huku anayenyolewa akiwa hayuko. Soma uchambuzi wake hapa.


WAMEAMUA HADI KUBINAFSISHA MAJI!

Hivi maji katengeneza au kaumba nani? Yanatoka wapi? Dunia ya kesho itakuwa dunia ambayo itakuwa ni rahisi zaidi kwa masikini kugharamia unywaji soda kuliko unywaji maji. Kuna msukumo mkubwa uliojengwa juu ya mantiki ya ubepari na soko wa kubinafsisha maji. Soma hapa kisa cha kampuni iliyonunua maji ya Watanzania. Na barua katika gazeti la Guardian la Uingereza juu ya kisa hicho. Hapa. Ukienda katika jarida hili utapata habari zaidi kuhusu ubinafsishaji wa maji. Tafuta matoleo ya nyuma kwa kuweka maneno haya kwenye kisanduku cha kusaka habari kwenye tovuti yao: Privatisation of Water. Nenda pia hapa na hapa.

MAFUNZO TEKNOLOJIA BURE

Ukitaka kuwa na blogu ya video, kuna mafunzo ya bure hapa. Hapa napo kuna mafunzo ya bure ya matumizi ya teknolojia mpya ya mawasiliano na habari.

6/07/2005

KUTOKA MKUTANO WA COMMONS-SENSE: FAIDA ZA KUTOA VITABU BURE MTANDAONI

Hakuna ambaye hakushawishika baada ya kumsikiliza mwanamama Eve Gray ambaye alizungumzia umuhimu wa wachapishaji barani Afrika kuanza kutoa vitabu vyao bure kwa njia ya mtandao wa Intaneti na teknolojia nyingine za kisasa. Mada yake iliyotolewa siku ya kwanza ya mkutano wa Commons-Sense ilitokana na utafiti alioufanya kwa ajili ya jamaa hawa Hapa. Utafiti wake unaonyesha kuwa kuna uwezekano wa wauza vitabu kuongeza mauzo wakitoa vitabu vyao bure mtandaoni. Mwanzoni watu wengi tulijiuliza, "Utaongezaje mauzo kama utakuwa ukitoa vitabu bure? Mauzo hayo yatatokana na kumuuzia nani? Jibu ukitaka soma mada yake kamili hapa. Mwanauchumi wa Pambazuko soma kwa undani uniambie.
Moja ya mambo aliyosema Gray yaliyoshtua washiriki wengi na kuwafanya kuona umuhimu wa teknolojia rahisi za kupeana na kuhifadhi habari na maoni kama blogu ni kuwa mambo yote yaliyoko katika mtandao wa intaneti asilimia 0.4 tu ndio inatoka Afrika. Ukiondoa Afrika Kusini mchango wa Afrika unabaki kuwa ni asilimia 0.02!

KUTOKA MKUTANO WA COMMONS-SENSE: MJUE "BABA" WA CREATIVE COMMONS

Ndivyo watu wanavyomwita, "Baba" wa vuguvugu la creative commons. Creative Commons, ambayo tawi lake nchini Afrika Kusini lilianzishwa rasmi tarehe 25 Mei katika hafla niliyohudhuria ndani ya ukumbi wa hoteli ya Rosebank, ilianzishwa nchini Marekani na mwalimu wa sheria chuo kikuu cha Stanford, Larry Lessig. Creative Commons imejengwa juu ya dhana inayofanana na tamaduni za Afrika hasa falsafa ya ubuntu na ujamaa: mtu sio mtu bila watu. Creative Commons ni mfumo mbadala wa sheria ambao unawapa haki watunzi, wasanii, waandishi, wanazuoni, n.k. kuruhusu kazi zao kutumiwa na watu wengine bila wao kuombwa ruhusa au kulipwa. Mfumo wa sasa wa hakimiliki unasema "haki zote zimehifadhiwa" wakati ambapo Creative Commons inasema, "Baadhi ya haki zimehifadhiwa" au "Hakuna haki zilizohifadhiwa." Kabla ya kuingia kwa undani juu ya mfumo huu mpya na kutoa mifano mbalimbali duniani ya watu na mashirika yanayotumia nembo ya Creative Commons (kazi ndani ya blogu hii ziko chini ya creative commons), napenda kumzungumzia mwanzilishi wa vuguvugu hili. Lessig ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Code and Other Laws of Cyberspace. Kinyume na utaratibu uliozoeleka wa uandishi wa vitabu, toleo la pili la kitabu hiki linaandikwa na kuhaririwa na watu mbalimbali duniani. Kawaida waandishi wa toleo la kwanza huwa ndio wanaoendelea kuandika matoleo yanayofuata. Mtu yeyote, hata wewe (tena dakika hii!!), anaweza kushirikia kuandika toleo la pili la kitabu chake. Lessig kwa kutumia teknolojia mpya ya "wiki" anabadilisha kabisa maana ya uandishi tuliyokuwa tumeizoea. Uandishi unakuwa ni kazi ya jumuiya, kazi ya kijamaa. Kazi ya ushirikiano. Kuandika kitabu sio lazima iwe ni shughuli ya kibinafsi ya kujifungia chumbani. Kutokana na toleo hili la pili kuandikwa na watu toka sehemu mbalimbali duniani, sehemu ya kuandika jina la mwandishi katika kitabu hikiitaandikwa: Larry Lessig na Ninyi. Nenda hapa utazame na ukitaka ushiriki kuandika kitabu hiki. Lessig ameandika pia kitabu kiitwacho Free Culture. Kitabu hiki kinapatikana bure. Watu wengi walishangazwa na uamuzi wa wachapaji wakubwa wa vitabu kama Penguin kukubali kutoa kitabu bure na kwa leseni yaCreative Commons. Zaidi ya hilo na wasomaji wanaruhusiwa kukitumia, kukibadili, kukiandika upya, kukisambaza, kukitafsiri…kufanya lolote watakalo (isipokuwa kwa matumizi ya kibiashara) bila kuomba ruhusa toka kwa mwandishi wake au wachapishaji. Kitabu chake kingine ni hiki hapa. Unaweza kusoma makala yake video yake alipohojiwa hivi majuzi nchini Afrika Kusini.

UANDISHI WA JUMUIYA

Nimewahi kuweka viungo na pia kuzungumzia juu ya aina ya uandishi unaojitokeza kutokana na zana mpya za mawasiliano kama blogu. Uandishi huu una majina mengi: uandishi wa umma, uandishi shirikishi, uandishi wa wananchi, n.k. Inatabiriwa kuwa ifikapo mwaka 2021 asilimia 50 ya habari zitakuwa zikiandikwa na wananchi wa kawaida (na sio waandishi wa habari). Soma kitabu hiki.

6/06/2005

MSOME PADRI KARUGENDO

Nimepata muda wa kutundika makala za Karugendo. Kazi kwako. Makala zenyewe ni: Je Hili ni Kosa Lenye Heri?, Kiswahili Lugha Yetu, Kiswahili Lugha ya Afrika, Teolojia ya Ukombozi, na Viongozi wa Dini Wametukwaza. Makala zake nyingine ziko kwenye kona yake iitwayo: Kalamu Ya Padri Karugendo, mkono wa kulia chini ya makala zangu na za Freddy Macha.

UPINZANI NA MAANDAMANO DHIDI YA MKUTANO WA G8

Ukienda hapa utakuwa ukipata habari mbalimbali kuhusu upinzani dhidi ya mkutano wa G8 huko kule Edinburgh mwezi ujao. Halafu kuna hawa jamaa wanaitwa Dissent!:
Na wale wanaosema kuwa dunia mpya inawezakana. Bila kusahau jamaa wa Stop the War Coalition.

G8 SUMMIT KUJADILI AFRIKA

Kama ambavyo baadhi wanavyojua, Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, anasema kuwa moja ya kazi zake kubwa ni kuhakikisha kuwa bara la Afrika linanyanyuka toka katika dimbwi la umasikini, migogoro, ukimwi, n.k. Kwahiyo moja ya mada kuu katika kikao cha viongozi wa nchi tajiri 8 duniani unaofanyika huko Uingereza mwezi ujao ni Afrika. Soma hapa. Blair ni mwenyekiti wa Kamisheni/Tume ya Afrika ambayo mmoja wa makamishna wake ni rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa. Tume hii imetoa ripoti yake inayopatikana hapa. Ukienda hapa unaweza kuona na kusikiliza yaliyosemwa wakati wa uzinduzi wa ripoti yenyewe.
Ukiacha Mkapa, kamishna mwingine toka Tanzania ni mama Anna Tibaijuka. Makamishna wengine hawa hapa.
Hapo awali viongozi wa G8 waliunda NEPAD kule Kanada. Haya ndio madhumuni ya NEPAD. Tunajua tunakokwenda?
MKUTANO WA G8 NCHINI UINGEREZA

Wale wakuu wa nchi tajiri duniani wanakutana Edinburgh tarehe 6-7 mwezi ujao. Kwanza kabisa kuna historia ya mkutano huu ambao kawaida huwa unaandamwa na upinzania wa nguvu kabisa na wanaharakati wanaoamini kuwa mfumo wa kiuchumi na kisiasa unaosukumwa dunia nzima na nchi hizi nane sio bora kwa watu na nchi masikini na pia haujali mantiki ya maendeleo endelevu. Kabla ya kuwa G8 ilikuwa G6. Nenda hapa uone ilivyobadilika. Tazama habari za mkutano wa mwaka huu hapa na pia habari zaidi juu ya G8 kwa ujumla hapa.

HATA DAKITARI AKIKUANDIKIA DAWA YA KUTUMIA "LILE JANI" UKIKAMWATWA, NDANI!

Mahakama kuu hapa Marekani imekataza matumizi ya jani (au bangi) kwa sababu za kimatibabu. Kesi ilifunguliwa na wagonjwa hawa. Katika uchaguzi wa mwaka jana, kati ya maeneo 20 yaliyokuwa na kipengele kinachohusu ulegezaji wa sheria kuhusu jani, maeneo 17 yalikuwa na kura nyingi zilizounga mkono ulegezaji. Hapa.

Independent Media Center na vuguvugu la uandishi huru

Moja ya mafanikio makubwa ya upinzani dhidi ya dubwana WTO kule Seattle mwaka 1999 ni kuanzishwa kwa vuguvugu la uandishi huru chini ya mwavuli Independent Media Center. Vuguvugu hili ilikuwa ni hatua za mwanzo za kitu ambacho Dan Gillmor anaita: We The Media, kama lilivyo jina la kitabu chake ambacho kinapatikana bure hapa.

Mahakama ya Kimataifa na Mauaji ya Darfur

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inatazama suala la mauaji ya halaiki huko Darfur. Hapa. Kwa habari zaidi juu ya Darfur nenda kwenye blogu hii.

6/05/2005

MASHINDANO YA HADITHI YA SEKUNDE SITINI

Tazama video za mashindano ya riwaya ya sekunde sitini kwa video.

Tovuti ya Wanafunzi Tanzania

Tembelea mradi wa tovuti ya wanafunzi Tanzania. Nimefurahi sana wanaheshimu titi la mama.

AFRIKA KUSINI, HISIA, MAJINA, N.K.

Nitakuwa nikiandika mambo kadhaa juu ya nchi ya Afrika Kusini. Baada ya kurudi toka kwa Mzee Madiba, nimekuwa nikiifikiria sana nchi ile. Nchi ilinipa hisia za ajabu ajabu sana. Nilifurahi mno kuwa Afrika, kuwa miongoni mwa watu wangu. Lakini wakati huo huo nchi ile ilinipa huzuni kubwa. Utajiri usio na kifano na umasikini wa kutisha vinatazamana uso kwa uso. Hakuna anayemwelewa mwenziye. Nadhani toka kuzaliwa kwangu sijawahi kuona utajiri namna ile (hata ukiiweka Marekani) na ufukara wa kutisha. Sina maana kuwa Afrika Kusini ndiko kwenye ufukara kuliko nchi nyingine duniani, nina maana katika nchi nilizotembelea sijawahi kuona ufukara kama ule.
Lakini kuna mambo ambayo yalinipa furaha. Moja kubwa ni ufahari walionao Waafrika Kusini juu ya utamaduni na historia yao. Ukienda mahakama ya katiba unakuta meza kuu ya majaji imepambwa na ngozi ya ng'ombe. Sherehe za kitaifa zinafunguliwa sio kwa sala za kikristo na kiislamu tu kama Tanzania, bali pia kwa sala toka kwa viongozi wa dini zetu za asili. Watambaji mashairi ya sifa hutumika katika matukio mbalimbali ya kitaifa (kwa waliofuatia sherehe za kuapishwa serikali mpya ya Mandela wanaweza kukumbuka). Timu yao ya taifa wanaiita Bafana Bafana (timu ya taifa ya Tanzania inaitwa Taifa Stars...neno "stars" sijui linafanya nini hapo!).
Baada ya kuondolewa kwa mfumo wa kinyama wa ubaguzi nchini Afrika Kusini, wananchi wa nchi hiyo waliamua kubadili baadhi ya majina ambayo yamebeba historia ya kibaguzi na unyama wa makaburu. Jiji la Pretoria ambapo ndipo makao makuu ya serikali mwishoni mwa mwaka huu litabadili rasmi jina lake na kuitwa Tshwane (ukitamka usitamke herufi "h". Inatamkwa "Tswane). Hili ni jina la mto unaokatiza katika jiji hilo. Inasemekana kuwa jina Tshwane lilitokana na jina la mtoto wa Chifu Mushi aliyekuwa akiishi maeneo hayo mwanzoni mwa miaka ya 1800. Neno hili linamaanisha, "Sisi ni ndugu." Jina "Pretoria" lilitokana na jina la kiongozi wa kikaburu, Andries Pretorius.
Jiji nililokuwa, Johannersburg, linajulikana pia kwa jina la eGoli. Neno hili la Kizulu linamaanisha, "Mahali penye dhahabu." Sijasikia kama kuna hatua za kutumia jina eGoli kama jina rasmi la jiji hili. Watu wengine hupenda pia kuliita jiji hili "Jozi."
Miji mingine ambayo iko mbioni kubadilishwa majina ni Durban: eThekwini. Jina hili linamaanisha ghuba. Pietersburg itakuwa Polokwane.
Kitongoji cha Alexandra nadhani kinatakiwa kubadili jina lake mapema iwezekanavyo. Jina hili linatokana na jina la mke wa kaburu Papenfus ambaye aliamua kuita eneo hili kwa jina la mkewe! Kitongoji hiki visa vyake hutavimaliza. Jina la kitongoji maarufu cha Soweto ambacho kina wakazi zaidi ya wakazi wote wa jiji la Dar Es Salaam linatokana na ufupisho wa jina lake la awali: South Western Township. Hefuri mbili za mwanzo katika maneno hayo matatu ndio zilizaa Soweto.SIKILIZA MAHOJIANO YANGU REDIO UFARANSA

Nimemaliza kufanya mahojiano kwa njia ya simu na Radio France Internationale, idhaa yake ya kiingereza, kuhusu vuguvugu la kujenga blogu za Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika. Mwanamama aliyenihoji, Cordelia Hebblethwaite, kanitumia maelezo ya kuwasaidia wale watakaopenda kusikiliza mahojiano hayo redioni au kwenye mtandao wa kompyuta. Ujumbe wake huo hapo chini. Tafsiri ya Kiswahili ni ya kwangu:
"Nenda hapa. Vipindi vyote viko mkono wa kulia. Mahojiano yatarushwa katika kipindi kimoja kati ya vinne vya asubuhi vinavyokwenda kwa jina la "English to Africa." Saa ni hizi: 04.00 GMT, 05.00 GMT, 06.00 GMT, 07.00 GMT. Vipindi vya jumatatu vitakuwa mtandaoni kwa masaa 24 kisha nafasi yake itachukuliwa na vipindi vya siku ya jumanne. Vipindi vya asubuhi huanza kwa habari, kisha baada ya kama dakika 15 mahojiano mbalimbali huanza kurushwa. Sehemu hiyo ndipo mahojiano yako yatakuwepo."

Blogu za Tanzania kwenye Wiki

Nimemaliza kuweka blogu mpya za Tanzania katika ukurasa wa "wiki" wa mradi wa Sauti za Dunia.

MAHOJIANO YA MWANABLOGU SOKARI EKINE

Fuatilia mahojiano kati ya Ethan Zuckerman na Sokari Ekine anayeblogu hapa na hapa.
YALIYOJIRI BLOGU ZA KISWAHILI

Nimemaliza kutundika, kwa ufupi, yanayojiri ndani ya baadhi za blogu za Kiswahili katika tovuti ya mradi wa Sauti za Dunia. Nilikuwa sijafanya hivyo kwa muda kutokana na kutingwa. Hapa. Nimejaribu kuweka blogu zilizoandikwa karibuni.

BLOGU MPYA YA KIINGEREZA TOKA TANZANIA

Jana nilitangaza blogu hii ya kiingereza toka Tanzania. Leo naitangaza nyingine ya ndugu Mongi. Hapa.

MANIFESTO YA SAUTI ZA DUNIA

Hii ni tafsiri ya Kiswahili (isiyo rasmi) ya manifesto hii ambayo ndio dira ya mradi wa Global Voices.
MANIFESTO YA SAUTI ZA DUNIA
Tunaamini kauli huru, haki ya kujieleza, na haki ya kusikiliza. Tunaamini haki ya upatikanaji wa zana za mawasiliano na habari kwa watu wote.

Kufanikisha hayo, tunaazimia kumwezesha kila anayetaka kujieleza awe na njia za kujieleza, na kwa kila anayetaka kusikiliza awe na njia za kusikiliza.

Kutokana na faida za zana mpya za mawasiliano na habari, kujieleza hakutawaliwi tena na wanaomiliki njia za uchapishaji na usambazaji, au serikali zinazozuia uhuru wa fikra na mawasiliano. Hivi sasa kila mmoja anaweza kuwa na nguvu za vyombo vya habari. Kila mmoja ana uwezo wa kuelezea simulizi zake kwa dunia nzima.

Tunaazimia kujenga maelewano penye utengano ili tuweze kufahamiana kwa undani zaidi. Tunaazimia kufanya kazi pamoja kwa ufanisi na kuchukua hatua kwa nguvu zaidi.

Tunaamini nguvu za mahusiano ya moja kwa moja. Udugu kati ya watu toka tamaduni mbalimbali ni wa karibu, kisiasa, na wenye nguvu. Tunaamini majadiliano bila kujali tofauti zetu ni muhimu kwa ajili ya dunia ya kesho ambayo ni huru, ya haki, ustawi na endelevu…kwa wananchi wote wa sayari hii.

Wakati tukiendelea kufanya kazi na kuongea kama watu binafsi, tunaazimia kutambua na kuendeleza maslahi na malengo yetu ya pamoja. Tunaahidi kuheshimu, kusaidia, kufundisha, kujifunza, na kusikilizana.

Sisi ni Sauti za Dunia.

6/03/2005

BLOGU MPYA TOKA TANZANIA

Mhandisi wa kilimo, ndugu Isaria Mwende, anablogu kwa kiingereza toka Tanzania. Mtembelee hapa.

6/02/2005

TAMASHA LA NCHI ZA JAHAZI

Tamasha hili lilianza kama mchezo, sasa limekuwa tamasha kubwa. Mwezi ujao ukiweza nenda pale Zanzibar ukafurahie na kujielimisha. Kongoli hapa.

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com