6/14/2005

JAMES MAPALALA ALIVYONIKARIPIA

Nadhani ulikuwa ni mwaka wa 1993 mwishoni au '94 mwanzoni. Wakati huo nilikuwa ndio ninaandikia gazeti la Bara Afrika chini ya mhariri Joseph Kaseba (bado uko Kigoma?) na Songoro Mnyonge (mara ya mwisho ulikuwa gazeti fulani pale Kariakoo, sikumbuki jina. Magazeti mengi siku hizi...niandikie).
Basi yapata mwendo wa saa tano hivi nikajiondokea kwenda kumhoji ndugu James Mapalala. Sijui nilikuwa nafikiria nini. Siku hiyo gazeti la Bara Afrika lilikuwa limetoa habari ya kumponda Mapalala. Nilipofika nyumbani kwake (na ofisini kwake wakati huo) pale mitaa ya Morocco, jijini Dasalama, tayari yeye na washabiki zake walishanunua Bara Afrika na kulisoma. Basi nafika pale nakutana na Bazigiza (naye sijui yuko wapi siku hizi toka ile misukosuko aliyoipata toka kwa "usalama" wa taifa). Bazigiza alijua kuwa mimi ni mwandishi wa Bara Afrika. Siku hiyo alinitazama kwa namna ya tofauti. Sikushtuka. Hadi leo sijui nilikuwa nafikiria nini kwenda kwa Mapalala baada ya kumponda.
Nikaomba kuoanana na Mapalala. Nikakaribishwa sebuleni. Mapalala akaja. Wacha anisute. Aliongea kweli. Akasema hana muda wa kufanya mahojiano na mimi. Kwanini nisifanye mahojiano kabla ya kumponda? Akasema mambo elfu kumi kidogo kuhusu gazeti lile na waandishi wa habari. Washabiki zake wanatikisa kichwa na kuitikia kwa sauti ili awasikie. Nimewekwa kiti moto. Sikuwa na la kusema. Wala la kujitetea. Nilibaki kimya kama nimemwagiwa maji. Nikabadilika rangi. Mdomo ukanikauka. Akanisuta, akanisuta weee.... kisha akaondoka zake.
Bazigiza akawa na ubinadamu kidogo. Akaongea nami mambo mawili matatu kwa upole kama vile ananifariji kwa chati. Kisha nikaanga.
Sitakaa nisahau. Kilichonikumbusha kisa hiki ni habari hii kuhusu Mapalala kugombea urahisi Tanzania.

2 Maoni Yako:

At 6/16/2005 03:06:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Pole!

 
At 7/04/2006 06:44:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Ndesajo,
Tafadhali fahamu kuwa L K Bazigiza sasa ni marehemu. Alifariki tangu Mei 2003 kutokana na kisukari.

Wasalam wa ughaibuni

Mbongo

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com