6/28/2005

Nimewasili kwa Bibi

Niko kwenye mgahawa wa Copacabana nje ya hoteli ninayokaa katika mtaa wa Southampton. Ninaandika haraka kidogo maana muda si mrefu tutaondoka na waandishi wengine, ambao wanakunywa chai sasa, kwenda ofisi za Panos.
Niliwasili jana asubuhi hapa kwa Malikia Lizabeti, au kama vijana wa kijiweni wanavyopaita, 'kwa bibi.' Nimekutana na waandishi wengine walioko kwenye mpango huu wa shirika la Panos wa G8 Media Fellowship: Kamau, Machrine, na Maura. Salamatu toka Sierra Leone anawasili leo.
Jana tulipelekwa kutambulishwa kwa wafanyakazi wa Panos na baada ya mlo wa mchana tulihudhuria kikao cha wafanyakazi wa shirika hili, ambapo kulikuwa na ripoti kuhusu ushiriki wa Panos katika mkutano wa dunia wa masuala ya jamii-habari (world summit on information society). Baadaye tulikwenda ofisi za bunge kuoana na mbunge wa jiji la York, Hugh Bayley, ambaye ni mwenyekiti wa Africa All Party Parliamentary Group. Alitueleza kwa kifupi juu ya kazi na mafanikio ya kundi hili. Nitatoa maelezo yake kadri siku zinavyokwenda.
Leo tutakuwa na mjadala kuhusu agenda ya kundi la nchi nane (G8) na pia kutazama yaliyomo katika vyombo vya habari vya Afrika na Uingereza kuhusu mkutano wa G8 utakaofanyika mwezi ujao, ambapo moja ya agenda kuu ni suala la maendeleo ya Afrika. Tutakwenda katika ofisi za gazeti la Metro, ambalo liko mbioni kuanzisha blogu. Kuna watu kadhaa ambao kuna uwezekano wa kukutana nao leo, au siku nyingine, kutegemea na ratiba itakavyokuwa: Aubrey Meyer wa Global Commons Institute, John Hilary wa kundi la Chatham House, na waziri wa masuala ya maendeleo ya kimataifa, Hilary Ben.
Mchana nitakwenda kufanya mahojiano na mmoja wa wakurugenzi walitimuliwa nchini Tanzania, Cliff Stone, wa kampuni ya City Water iliyokuwa imepewa jukumu la kusambaza maji jijini Dar Es Salaam. Tutakutana katika ofisi za kampuni mama ya City Water iitwayo BiWater.
Ila tukio kubwa nadhani ni kesho tutakapozindua blogu mpya inatakayoendeshwa na waandishi toka Afrika. Anuani yake siwezi kuianika hapa sasa hadi izinduliwe rasmi.
Mengine baadaye.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com