6/29/2005

Kutoka London: Nasaha za Tariq Ali na wenzake

Jana, mimi na John Kamau wa Sunday Standard (Kenya) tulifanya mahojiano na Cliff Stone, mkurugenzi wa City Water aliyetimuliwa nchini. Mahojiano hayo yalipangwa na taasisi ya Panos London. Dhumuni kuu lilikuwa ni kupata taarifa toka kinywani mwake kuhusu mgogoro wa kampuni aliyokuwa akiiongoza na serikali ya Tanzania. Hatukumaliza mahojiano yenyewe, tutaendelea. Siku haijapangwa.

Katika mambo yote tuliyofanya jana, kubwa ni pale tulipokwenda ukumbi wa New Theatre wa London School of Economics kwenye mhadhara ulioitwa Make the G8 History. Nlifurahi sana kumsikiliza na kukutana na Tariq Ali, mwandishi wa habari, mtunzi, na mhariri wa jarida la New Left Review. Tariq ni mwandishi wa kitabu kiitwacho The Clash of Fundamentalisms. Wengine waliozungumza kwenye mhadhara huo ni mwandishi George Monbiot, na Mark Curtis.

Tariq Ali alizungumzia mada iliyoitwa Power and Resistance. Haya ni baadhi ya mambo aliyosema:
- Afrika haitakaa iondoke kwenye dimbwi la umasikini kwa kutumia misaada toka nchi za Magharibi
- Wanasiasa wa mrengo wa kulia na kushoto wana tofauti ndogo sana. Ukiwachambua kwa undani unakuta lao moja
- Marekani ni kati ya nchi zinazoongoza kwa rushwa duniani!
- Ili kuondokana na uchumi tegemezi Afrika iache kukimbilia nchi za Magharibi na ianze kushirikiana na nchi za Amerika ya Kusini
- Waafrika waache kutegemea tabaka la wasomi na matajiri wa Afrika na wanasiasa wa Magharibi

Mark Curtis alisema yafuatayo:
- Nia ya Uingereza katika mpango wake wa Afrika sio kuondoa umasikini bali kutengeneza njia kwa ajili ya makampuni ya Magharibi kuwekeza na kuiba utajiri wa Afrika
- Anashangaa sana waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, anaonekana kama vile ni mwokozi wa Afrika
- Ni ajabu kuwa Uingereza inajifanya ghafla kuwa inaipenda Afrika wakati ilikaa kimya wakati wa mauaji ya Rwanda, iliunga mkono ubaguzi wa rangi Afrika Kusini kwa miaka 50, ilimuunga mkono dikteta Idd Amin kwa mwaka mmoja na nusu, ina historia chafu sana kutokana na mateso ya Kinazi iliyowafanyia mashujaa wa kundi la Maumau nchini Kenya, na kitendo cha serikali ya Uingereza kukaa kimya wakati makampuni ya mafuta ya Uingereza yananyonya utajiri wa Nigeria na mabenki ya Uingereza yakificha fedha za watawala wala rushwa wan chi hiyo

George Monbiot alisema:
- Mwanamuziki Bob Geldof anashangaza baada ya kuwaambia wanamuziki wanaoshiriki kwenye tamasha la Live 8 kuwa wasimsakame mwizi namba moja duniani ambaye ni raisi wa Marekani, Joji Kichaka
- Wazungu nane (viongozi wa G8) wanajifanya kuwa wana uwezo wa kuondoa matatizo ya dunia nzima

2 Maoni Yako:

At 6/30/2005 12:19:00 AM, Anonymous Anonymous said...

I wish I had been able to attend that meeting! Lakini asante sana kwa ripoti hii.

 
At 6/30/2005 02:24:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Hawa watu ndio wanajua wanachoongea. Sasa hiyo tume ya Blair iliyokuwa na marais wa nchi na maprofesa hivi hawajuhi historia? Kweli Afrika tutabaki nyuma milele

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com