6/16/2005

MKUTANO WA G8: JIELIMISHE...

Nitaandika sana kuhusu mkutano wa makabaila uitwa G8 unaofanyika mwezi ujao kule Uskochi. Mkutano huu ni muhimu kwetu kuufuatilia maana moja ya mambo makubwa wanayojadili ni suala la maendeleo Afrika . Mkutano huu ni muhimu kama mkutano huu mwingine utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Uingereza ndio itakuwa mwenyekiti wa mkutano wa mwaka huu wa mabepari. Wakati Marekani imechukua suala la ugaidi na “amani” Mashariki ya Kati kuwa kipaumbele katika sera zake za nje, Uingereza imechukua Afrika na masuala ya mazingira kuwa ndio vipaumbele vyake. Mkutano wa G8 kawaida huwa unajadili masuala ya sera zinazohusu mataifa hayo, ila mwaka huu suala la umasikini Afrika litakuwa mstari wa mbele kutokana na mtazamo wa kisera wa serikali ya Uingereza. Katika kufanikisha azma yake ya kuweka Afrika mbele katika sera zake, serikali hiyo ilianzisha Tume ya Afrika, ambayo rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ni mmoja wa wajumbe.

Mwezi wa tatu mwaka huu tume hiyo ilitoa ripoti yake (baadaye nitawapeni maoni ya watu mbalimbali juu ya ripoti hiyo ya tume ambayo waafrika “tumeundiwa.”


Serikali ya Uingereza pia itachukua ukuu wa Jumuiya ya Ulaya (kwa miezi sita) ambapo serikali hiyo ina nia ya kuweka suala la afrika na umasikini duniani kwenye meza ya majadiliano

Wakati hayo yote yanaendelea, mashirika yasiyo ya kiserikali, watu binafsi, wanaharakati, na vyama mbalimbali vimekuwa katika
kampeni kubwa ya kutaka umasikini duniani utokomezwe na kupinga unafiki, ulafi, na tamaa za nchi tajiri na makampuni makubwa ya kibepari


Huko Uingereza, mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa na kampeni motomoto iitwao “Fanya Umasikini Kuwa ni Historia” (Make Poverty History). Wako wanablogu kama huyu hapa ambao wameweka nembo ya kampeni hii kwenye blogu zao. Kampeni hii inatarajia kushirikisha watu zaidi ya laki mbili kwenye maandamano mwezi ujao huko Uingereza. Hapa kuna habari zaidi juu ya maadamano ya kupinga ubeberu.

Katika harakati hizi za kupinga ubeberu sanaa ya muziki itatumiwa katika miji ya London, Paris, Rome, Philadephia, na Berlin kama njia ya kuonyesha kuwa dunia imechoka na sera za ukandamizaji za mataifa makubwa. Utashangaa kuwa ingawa kampeni hii inafanyika hasa kwa ajili ya Afrika, hakuna mji wa Afrika utakaokuwa na tamasha hili na sijaona jina la mwanamuziki toka Afrika katika orodha ya watakaoshiriki. Kwa sasa niweke mawazo yangu pembeni maana nataka kukupa kwanza picha halisi ya kinachofanyika kisha baadaye tukae chini tujadili, tujiulize maswali, tukosoe, tuunge mkono, n.k.

Suala jingine kubwa litakalojadiliwa kwenye G8 ni mazingira. Katika kampeni zitakazofanyika kule Uingereza, kutakuwa na tukio la kutoa ripoti inayoitwa Afrika Inaungua (Africa is Burning) na masuala ya kampeni dhidi ya ubakaji wa dunia yetu. Katika shughuli zitakazokuwa zikifanyika katika kupinga ubepari na madhara yake kwa masikini na mazingira kutakuwa na kitu
kinaitwa Mbadala wa G8. Na pia kuwakuwa na wanaharakati wa mazingira watakaokuwa na “Tahadhari ya Mazingira.”

Pamoja na mpango wa serikali ya Uingereza kutaka nchi za Afrika zipewe misaada zaidi, ikiwa ni pamoja na kusamehewa madeni na kueleza kuwa nia yake ni kutaka kuona Afrika inaondokana na umasikini, bado sera zake zinazua mabishano, utata, mizozo, n.k. Kwa mfano, shirika la misaada la Action Aid, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, limetoa ripoti inayoonyesha kuwa sehemu kubwa ya misaada ya fedha huwa inaishia kurudi nchi za Magharibi na sio kusaidia nchi changa. Serikali ya Uingereza imepinga ripoti hiyo.

Moja ya mambo ambayo wanaharakati wanasema ni kuwa sera ya serikali ya Uingereza inataka nchi za Afrika zizidi kufungua soko lake na kubinafsisha kila kitu. Madhara na utata mzima wa zoezi la ubinafsishaji unaonyeshwa katika
sakata la kubinafisha maji Tanzania. Ubinafishaji huu ambao umeungwa mkono na Benki ya Wazungu ambao pia huitwa Benki ya “Dunia” umesimamishwa na serikali ya Tanzania

Hapa kuna mabadilishano ya barua kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali Uingereza na mshauri wa kampuni iliyopewa kazi ya kuhodhi maji wakati ambapo maji ni zawadi toka kwa Mola, Ruwa, Ngai, Mulungu, n.k.

Pia gazeti la The Guardian
lina barua ya siri iliyobambwa na waandishi ikielezea kuwa Jumuiya ya Ulaya ambayo inaendesha Mpango wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya nchi za Ulaya na Afrika ikimtaka waziri wa Uingereza anayeshughulikia mambo ya uchumi ya Jumuiya ya Ulaya, Peter Mandelson amshinikize Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, aache kuendeleza sera zinazipa serikali za Afrika haki zaidi za kuamua jinsi ya kuendesha uchumi wa nchi zao.

Habari hiyo imepelekea mabadilishano ya barua kama utakavyoona
hapa na hapa.

Na pia makala kali ya mwandishi matata George Monbiot akidai kuwa serikali ya Uingereza inachofanya kuhusu sera yake ya Afrika ni mchezo wa kuigiza!

Na tena inadaiwa kuwa wakati Uingereza ikidai kuisaidia Afrika, nchi hiyo inaongoza kwa kulinyang’anya bara hilo watumishi wake katika sera ya afya.

Naachia hapa kwa sasa. Itaendelea...


2 Maoni Yako:

At 6/16/2005 04:05:00 AM, Anonymous mshairi said...

Asante, Ndesanjo kwa mambo haya muhimu (and for the mention!). Naona 'Mbadala wa G8' utakuwa kitu muhimu sana - nitafuatilia sana kazi ya hao.

 
At 6/19/2005 09:08:00 AM, Anonymous Anonymous said...

Hii mikutano kweli ina faida zozote kwa masikini? Au ni mchezo tu wa wakubwa?

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com