6/07/2005

KUTOKA MKUTANO WA COMMONS-SENSE: MJUE "BABA" WA CREATIVE COMMONS

Ndivyo watu wanavyomwita, "Baba" wa vuguvugu la creative commons. Creative Commons, ambayo tawi lake nchini Afrika Kusini lilianzishwa rasmi tarehe 25 Mei katika hafla niliyohudhuria ndani ya ukumbi wa hoteli ya Rosebank, ilianzishwa nchini Marekani na mwalimu wa sheria chuo kikuu cha Stanford, Larry Lessig. Creative Commons imejengwa juu ya dhana inayofanana na tamaduni za Afrika hasa falsafa ya ubuntu na ujamaa: mtu sio mtu bila watu. Creative Commons ni mfumo mbadala wa sheria ambao unawapa haki watunzi, wasanii, waandishi, wanazuoni, n.k. kuruhusu kazi zao kutumiwa na watu wengine bila wao kuombwa ruhusa au kulipwa. Mfumo wa sasa wa hakimiliki unasema "haki zote zimehifadhiwa" wakati ambapo Creative Commons inasema, "Baadhi ya haki zimehifadhiwa" au "Hakuna haki zilizohifadhiwa." Kabla ya kuingia kwa undani juu ya mfumo huu mpya na kutoa mifano mbalimbali duniani ya watu na mashirika yanayotumia nembo ya Creative Commons (kazi ndani ya blogu hii ziko chini ya creative commons), napenda kumzungumzia mwanzilishi wa vuguvugu hili. Lessig ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Code and Other Laws of Cyberspace. Kinyume na utaratibu uliozoeleka wa uandishi wa vitabu, toleo la pili la kitabu hiki linaandikwa na kuhaririwa na watu mbalimbali duniani. Kawaida waandishi wa toleo la kwanza huwa ndio wanaoendelea kuandika matoleo yanayofuata. Mtu yeyote, hata wewe (tena dakika hii!!), anaweza kushirikia kuandika toleo la pili la kitabu chake. Lessig kwa kutumia teknolojia mpya ya "wiki" anabadilisha kabisa maana ya uandishi tuliyokuwa tumeizoea. Uandishi unakuwa ni kazi ya jumuiya, kazi ya kijamaa. Kazi ya ushirikiano. Kuandika kitabu sio lazima iwe ni shughuli ya kibinafsi ya kujifungia chumbani. Kutokana na toleo hili la pili kuandikwa na watu toka sehemu mbalimbali duniani, sehemu ya kuandika jina la mwandishi katika kitabu hikiitaandikwa: Larry Lessig na Ninyi. Nenda hapa utazame na ukitaka ushiriki kuandika kitabu hiki. Lessig ameandika pia kitabu kiitwacho Free Culture. Kitabu hiki kinapatikana bure. Watu wengi walishangazwa na uamuzi wa wachapaji wakubwa wa vitabu kama Penguin kukubali kutoa kitabu bure na kwa leseni yaCreative Commons. Zaidi ya hilo na wasomaji wanaruhusiwa kukitumia, kukibadili, kukiandika upya, kukisambaza, kukitafsiri…kufanya lolote watakalo (isipokuwa kwa matumizi ya kibiashara) bila kuomba ruhusa toka kwa mwandishi wake au wachapishaji. Kitabu chake kingine ni hiki hapa. Unaweza kusoma makala yake video yake alipohojiwa hivi majuzi nchini Afrika Kusini.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com