MSIKILIZE NA KUMJUA MWALIMU NA RAFIKI YANGU: ABDUL ALKALMAT
Mtu aliyenipa msukumo wa kusoma, kutafiti, na hatimaye kufundisha juu ya maingiliano ya jamii na teknolojia mpya za habari na mawasiliano, ni Abdul Alkalmat. Alikalimat ni kati ya watu hapa Marekani ambao kila mara wananifanya nipate huzuni sana. Heshima na upendo walionao kwa Tanzania hakuna mfano. Sababu inayonifanya nihuzunike ni ukweli kuwa Tanzania wanayoizungumzia wanamapinduzi kama hawa imebaki kwenye majivu ya historia. Kwa mfano, katikati ya mwaka huu nilikutana na mshairi Nikki Giovani alipoongea na kusoma mashairi yake mapya hapa Toledo. Tukiwa tunaongea nje ya ukumbi wakati watu wakinywa divai na vitafunio, aliniuliza ninatoka wapi kutokana na lafudhi yangu. Nilipomwambia ninapotoka alitabasamu kwa furaha na kukumbuka alipoitembelea Tanzania na jinsi anavyoipenda. Moyoni nikajisemea, "Angejua Tanzania ya enzi zile imebaki moyoni na akilini mwa wanamapinduzi kama yeye." Niongeze, Nikki Giovani ndiye mwanamama aliyesema maneno haya kuhusu mwanamke mwenye uzuri wa asili: "...if I dreamed natural dreams of being a natural woman, doing what a woman does, when she's natural, I would have a revolution." (Mshairi huyu ana mchoro wa kudumu [tattoo] mkononi unaosema, "Thug Life," kwa kumbukumbu ya Tupac Amaru Shakur. Tupac alikuwa ana mchoro tumboni kwake wenye maneno haya. Hivi sasa Nikki Giovani anafanya kampeni ili picha ya Tupac iwekwe kwenye stampu za Marekani).
Kabla sijapotea njia, nirudi kwenye mada ya msingi. Alkalmat ndiye aliyenifanya nihamie hapa Ohio toka jimbo la Washington mwaka 2002. Baada ya kusoma kazi zake, niliamua kumwandikia barua pepe kumwambia kuwa nataka kusoma chuoni anapofundisha. Nilijua kuwa huyu ndiye mtu ninayetaka kufanya naye kazi hapa Ughaibuni. Nilimwambia kuwa nimetoka Tanzania. Nilijua kuwa nikitaja Tanzania nitakuwa nimemteka. Kama nilivyohisi, alinijibu baada ya dakika chache kwa kunipa namba yake ya simu na kunitaka nimpigie ili tuongee kabisa sio kuandikiana! Nilipompigia maneno ya kwanza toka kinywani kwake yalikuwa ya Kiswahili, "Habari Gani?" Alinisalimu. Kisha akaniuliza kwa kiingereza, "Nikusaidie vipi?" Hapo ndio ukawa mwanzo wa uhusiano wetu. Baada ya kumweleza ninachotaka aliniambia nimpe muda. Hutaamini. Haikupita siku niliandikiwa barua na rafiki yake mwingine ambaye hivi sasa kawa ndugu yangu kabisa (ambaye naye Afrika anaiabudu!) kuniambia kuwa kama nina alama za kutosheleza na barua za walimu toka chuo kikuu cha Dar Es Salaam za kuniunga mkono watanipa skolashipu! Dunia hii bado tuna watu weusi ambao hawajakata tamaa. Nawe usikate tamaa (ninatumia neno "nawe" maana sitegemei kuwa maadui zetu watakuwa wanasoma blogu hii. Kama wapo wakitoe haraka sana. Nikitema mate yakikauka wawe wameishia!)
Nakumbuka siku ya kwanza tunakutana ana kwa ana na Alkalimat, mwezi wa nane mwaka 2002 majira ya asubuhi, jengo la liitwalo chuo, nilikuwa kwenye maabara ya tarakilishi. Naye akawa anapita nje, aliponiona (ingawa hatukuwahi kukutana na wala hakuwahi kuona picha yangu) alisimama na kupunga mkono. Nikamwendea. Akaniuliza, "Wewe ni kaka toka Tanzania?"
Nikajibu, "Ndio. Umejuaje?"
"Huu ni wakati wa mapinduzi. Lazima uweze kumtambua mwanamapinduzi mwenzako. Tusipofahamiana tukiwa vitani tutauana."
Tulipofika ofisini kwake alianza kuwazungumzia akina Abdulrahaman Babu (mtazame Babu akinongonezwa jambo na Malcolm X), Issa Shivji, Mwalimu Nyerere, Wamba dia Wamba, n.k. Alianza kunihubiria juu ya mapinduzi makubwa ya kijamii, kisiasa, kisayansi, kitamaduni, na kitamaduni yanayoletwa na teknolojia mpya za habari na mawasiliano. Kuanzia hapo nikazama kabisa hadi kuja kuibukia kwenye tasnifu yangu iliyoitwa Political Use of New Information and Communication Technologies in Tanzania (ambaye yeye alikuwa mmoja wa wanakamati)...na pia kuibukia kwenye masuala ya blogu! Ukitaka kujua jinsi alivyo na upendo wa damu nyeusi, siku ya kutetea tasnifu yangu (maana alijua kuwa kuna watu walikuwa wamepania kuja kunitwanga maswali) aliniita ofisini kwake kunipa mazoezi. Si hivyo tu, alicheza faulo kidogo lakini katika dhana ya kutetea Uafrika, aliniambia maswali atakayoniuliza! "Nataka ujiandae vyema maana hawa maadui zetu wanatakiwa kujua kuwa hatuko hapa kucheza...tuna kazi ya kuokoa bara zima. Sio suala la mchezo. Lazima tusaidiane maana safari ni yetu wote." Aliniambia.
Ninapenda umfahamu zaidi Dr. Alkalmat ambaye upendo wake kwa watu weusi unanipa nguvu kila ninapokaribia kuanguka kwa majonzi ya jinsi watu wetu wanavyoangamia katika utumwa wa kimawazo na minyororo ya utegemezi. Kuna siku nitajadili kwa kina zaidi juu ya kazi zake zinazoendeleza na kuchangia harakati za watu weusi Ughaibuni na Afrika. Zaidi ya kuwa mwalimu wa masuala ya Afrika, Alkalmat ni msimamizi wa kundi la majadiliano kwenye intaneti kuhusu masuala ya watu weusi la H-Afro-Am ambalo unaweza kujiunga nalo. Ni mhariri wa tovuti za Malcolm X na eBlack Studies. Unaweza kumsoma hapa, na hapa. Kuna kitabu chake kipya hapa.
Ukitaka kumsikiliza, nenda hapa. Ukifika hapo teremka chini ya ratiba ya mkutano kisha utaona picha na jina lake. Kongoli umsikilize akihutubia mkutano wa cybernomads nchini Ujeremani.
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home