12/19/2004

JUMAPILI NI JUMASABA?

Leo ni jumapili (hapa Marikani)...wakristo (ukitoa Wasabato) wanadai kuwa leo ni siku ya saba ya juma, kwahiyo ndio siku ambayo mungu wa kiyahudi, yehova, alipumzika baada ya uumbaji. Kwa uelewa wangu wa kiswahili nilijua kuwa jumapili ni siku ya pili maana jumamosi ni siku ya kwanza (yaani mosi = moja/kwanza) na jumatatu yaani kesho ni siku ya tatu. Sasa sielewi jumatatu itakujaje baada ya siku ya mwisho ya juma ambayo ni siku ya saba. Ukifika mwisho wa juma (yaani saba) si unaanza moja? Kama jumapili ni siku ya saba, siku inayofuata ni siku ya kwanza. Sasa kwanini uanze na TATU? Labda ni hili tatizo langu la hisabati, nilizoambiwa na mwalimu Kisanga nikiwa kidato cha kwanza kuwa "mwandiko wangu unaonyesha kuwa hisabati zinanipiga chenga" na pia nilizofeli toka kidato cha pili!
Najua Waislamu wanatabasamu na kusema, "Si unaona. Sisi tunasali ijumaa ambayo ni siku ya saba maana siku inayofuata jumamosi au jumakwanza/jumamoja ni siku ya kwanza." Waislamu wanafurahi kweli mtu ukiwagonga Wakristo, wakristo nao hivyo hivyo, ukigonga waislamu wanatabasamu.

Hii ni moja ya tofauti kati ya dini za asili za Afrika na dini za kuletwa na wakoloni, mabwana biashara utumwa, "mabedui" wenye majambia kiunoni na kurani mkononi, n.k. Imani zetu za asili hazina ushindani. Kwa mfano, imani ya Kichagga haisemi kuwa kwakuwa Msukuma ana imani tofauti basi imani yake ni ya uongo. Wachagga wanaamini imani yao ni ya kweli, na ile ya Wasukuma (ingawa ni tofauti na yao) ni ya kweli pia. Lakini hizi dini za kuja zina mantiki tofauti. Nikiwa mkristo, ninatakiwa kuamini kuwa mwenye dini tofauti na yangu atakwenda motoni. Muislamu naye anatakiwa kuamini kuwa dini yake katika maelfu ya dini na imani duniani ndio ya kweli. Zote zilizobakia ni za uongo. Waafrika hatuna hiyo mambo ya dini za uongo za na kweli. Imani zetu zote (ingawa zinatofautiana kutokana na sababu za kihistoria, na kitamaduni) ni sahihi. Kwanza kuna watu wengi ambao hadi leo hawajui kuwa Waafrika tuna dini za kwetu. Ajabu kabisa. Ndio maana naamini kuwa mfumo wetu wa elimu unatakiwa kufutwa na kuanza upya. Elimu inapaswa kuelimisha sio kupotosha.

Ngoja niwagonge na Waislamu kidogo (tazama Wakristo wanatabasamu!): Ukiweza kutembelea Bwagamoyo, nenda kwenye jumba la watumwa walipokuwa wakirundikwa kabla hawajawekwa kwenye majahazi na kupelekwa Uarabuni kutumikishwa zaidi ya punda. Kisha tambua kuwa waliokuwa wakifanya biashara hiyo ya unyama uliokithiri ya kuuza, kununua na kutumikisha ndugu zako ndio walioleta dini ambayo uko tayari kutoana macho na jirani yako ukiitetea. Wakati ule walichukua ndugu zetu utumwani kimwili, safari hii wanakuchukua kiakili na kisaikolojia. Wamekufanya ukadhani kuwa Uislamu ni Uarabu. Tazama, ili uwe muislamu unachukua jina la kiarabu, unasali kiarabu, unavaa kiarabu ukienda swala, ukisali unaelekeza uso uarabuni, ukimnukuu mungu unabadili lugha toka kiswahili hadi kiarabu (utasikia mtu anasema, "Mnyazi Mungu alisema..." kisha anarukiwa kiarabu. Ina maana anapotamka maneno toka kinywani kwa mungu hawezi kutamka kwa lugha ya kiswahili au ya kabila lake maana mungu wake haongei kiswahili au kinyakyusa. Nasema kama mungu wako hajui lugha yako ya Kimanyema, usithubutu kunihubiria habari zake. SIMTAKI!), mungu kwenye dini yako (uislamu) ana majina 99 na yote ni ya kiarabu, kuhiji unapaswa kuondoka nje ya bara lako lenye maeneo mengi matakatifu unakwenda hadi uarabuni unakobusu jiwe na kumpiga shetani mawe kisha unarudi, manabii zako wote wametoka huko mashariki ya kati...
Bob Marley huyo anaimba: Wont you help me to sing, this song of freedom....Emancipate (jikwamue) yourself from mental slavery, none but ourselves can free our mind....

Ile makala ya Mwafrika Akutana na Muislamu/ Mwafrika Akutana na Mkristo inakuja. Lazima tuongee haya mambo. Hatuna muda wa kupoteza. Hatuna cha kuogopa. Hakuna wa kututisha. Hata wakitutangazia fatwa kama Salman hatuwezi kukaa kimya. Wakristo na waislamu wote wanahubiri kuwa dini zetu za asili ni ushirikina na ushenzi, sisi tukiwasema wao wanakuwa mbogo. Sisi hatutatumia mapanga wala mawe. Hatutakuwa na hasira wala chuki. Tutajadili kwa uwazi, upendo, na ukweli. Historia ni historia.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com