12/23/2005

Mbona Kasheshe Bloguni?

Majuzi nilikuwa nafanya mahojiano kuhusu blogu zetu za Kiswahili. Jambo moja ambalo nilisema kuwa napenda kuona likitokea ni kuwepo kwa blogu za watu wenye fikra mbalimbali zinazotofautiana. Kujadiliana na watu wanaofikiri kama wewe ni sawa ila unaweza usikue kifikra na pia usipate changamoto ya kuhoji fikra zako mwenyewe na kutafuta maarifa zaidi. Sio vyema tukiwa na blogu za watu wote wanaokubaliana. Kwahiyo nchi kama Irani (ambayo ina blogu zaidi ya laki moja) na Marekani ambapo zipo blogu za wananchi wenye fikra za mrengo wa kushoto, katikati, kulia, n.k. Hapo utakuta mawazo ya watu wanaotetea mfumo na mambo yalivyo hivi sasa na blogu zenye kunyooshea kidole mfumo wa utawala, utamaduni, elimu, n.k. Utakuta pia blogu za vichekesho na kejeli, blogu za fasihi, n.k. Pia unakuta zipo blogu za picha, za video, za sauti (podikasiti), n.k. Unaweza pia kuona kuna blogu nyingine za kufundishia, za kutangazia biashara, za wasafiri, wanamichezo, n.k.
Chemi Che Mponda alipoandika juu ya matako makubwa nikaona kuwa huenda huo ndio mwanzo wa blogu zinazozungumzia masuala ambayo hatupendi kuyazungumzia hadharani. Bonyeza hapa usome. Ndugu Swai naye alianzisha blogu yake akawa anaandika masuala kwa staili yake na masuala ambayo wanablogu wengine hatuandiki. Lakini amekuwa kimya kwa muda. Bonyeza hapa uone blogu yake.
Sasa amekuja mwanablogu wa picha ambaye bado sijamuelewa hasa mwelekeo au nia yake. Pia hajaandika jina lake na anasema anaishi "cybercity." Yaani mji wake uko kwenye mtandao wa kompyuta. Utaona kuwa huyu bwana ni mtu wa utani sana. Hii ni staili nyingine ya blogu (naamini kuwa waliopigwa picha wametoa ruhusu picha zao kutumia. Katika mwongozo mpya wa wanablogu wapya ninaoandika, ninazungumzia masuala ya kisheria kuhusu blogu zetu hizi. Nitagusia kuhusu matumizi ya picha) ya picha tofauti na ile blogu ya kwanza ya picha ya Issa Michuzi. Itazame hapa.
Huyu bwana nimeanza kuhisi kuwa ni nani. Ila kwakuwa hajapenda kujitangaza jina sio vizuri kumtaja hata kama unamfahamu. Katika mwongozo ninaoandika, ninaongelea pia kuhusu namna ya kublogu kama hutaki ujulikane kuwa wewe ni nani. Kuna mbinu za kiufundi ambazo unatakiwa kutumia maana hata usipotumia jina lako, ni rahisi mtu kujua kompyuta unayotumia na huduma za intaneti unazipata toka kwa nani. Kila kompyuta ina namba ambayo ni rahisi sana kuipata. Njia hii imetumiwa majuzi huko China kumtia jela kwa miaka 10 mwandishi wa habari wa China. Yahoo! iliisaidia serikali ya China kumtambua mwandishi huyu. Bonyeza hapa usome habari hiyo.
Bonyeza hapa umuone mwanablogu mpya wa picha.
*****************************
Ninasafiri kwa siku mbili tatu hivi kimapumziko. Nitakuwa nachungulia mtandaoni kwa chati. Nadhani jumatatu ndio nitaweza kuandika tena nikiwa nimetulia. Kama nitaandika kabla ya hapo itakuwa ni juujuu au jambo la muhimu sana.
********************************
Wakati huo huo: ninajiandaa kusherehekea sikukuu ya Kwanzaa. Sikukuu hii husherehekewa kwa kukumbuka na kuenzi nguzo saba. Bonyeza hapa uzione. Zaidi juu ya sikukuu hii baadaye. Kwa sasa bofya hapa usome kuhusu sikukuu hii.

4 Maoni Yako:

At 12/26/2005 02:56:00 AM, Blogger Christian Bwaya said...

Ndesanjo, sijajua vizuri wewe ni muumini wa dini gani manake hii sherehe sijawahi kuisikia tangu nimehamishiwa duniani. Unaonaje ukiwa muwazi zaidi, tuanze kusherehekea wote. Au sio?

 
At 12/26/2005 06:55:00 AM, Blogger Kaka Poli said...

Ninaungana na mawazo ya Kaka Macha, ila suala ni kwamba udadisi kunatokana na mtu kuhitaji kufahamu undani haswa wa jambo fulani. Kwa bahati mbaya wengi miongoni mwetu, kutokana na kubeba utamaduni hasi kutoka upande wa pili kumetufanya tuishie pabaya. Hatudadisi tena, tumebaki kulishwa tu na watu wa ulaya na marekani!

 
At 12/26/2005 06:57:00 AM, Blogger Kaka Poli said...

Kaka macha naomba unisaidie kuitambulisha blogu yangu ya www.mawazo-huru.blogspot.com, ni Mtandao wa Mawazo Huru na Habari Chanya.

 
At 12/29/2005 04:05:00 AM, Blogger Christian Bwaya said...

Bwana Macha siku moja nilikuwa nafikiri hivi mbona inakuwa wanablog wote ni wapinzani wa utawala? Kila wazo la unayemsoma unakuta anakosoa na kujaribu kurekebisha anayoona yanaenda isivyo.
Nikajisemea mwenyewe, hivi ingekuwaje kama tungekuwa na wanblog ambao wanapendezwa na mfumo wa utawala uliopo, wana CCM mathalani, ingekuwaje? si pangekuwa patamu?
Sasa kuhusu kuwa na mitizamo tofauti, hilo ni sawa kabisa. Tatizo nafikiri bado ni mapema. Watu wengi bado hawajajiunga na Blog. Kwa vyovyote vile, ogezeko nadhani ni lazima lingeendana na ongezeko la fikra tofauti tofauti.
Nilisoma siku moja Blog yako ukatupa idadi ya wanaBolg wakati huo ikiwa chini ya 50, watu ambao nadhani ni wachache bado.
Na ni kweli kujadili kitu na mtu ambaye tayari anakuwa na mtazamo kama wako, hapo inakuwa si mjadala, ni kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa.
Kingefanyika kitu kimoja. Kwa sababu faida za Blog ziko dhahiri, watu wenye nafasi kwenye magazeti yetu, kama Makene na wewe mngewaelimisha watanzania umuhimu wa kushiriki kwenye midahalo ikiwamo hii ya kwenye Blog. Nadhani wataongezeka, na hapo tutaona sura tofauti zaidi.
Halafu, Bwana Macha usisahau kuwa wapo watu ambao kwao kukosolewa ni matusi. Ukimkosoa anaona kama unampinga, wakati si mara zote mtu unakubaliana na mawazo unayosoma. Huo ndio mchango wangu.
Jana bwana nimefuatilia sikukuu ya Kwanzaa kwenye mtandao, nikafumbuaka macho. Kumbe ni sikukuu ya kiafrika kabisa? Unajua nini, nikajisemea kumbe kuna watu wanasiku ya kusherehekea Uafrika wetu? Ni maendeleo hayo ingawa haijulikani hapa Tanzanaia. Umenifungfua macho Mzee, umuhimu wa Blog huo.

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com