Nafasi ya Fasihi Andishi, Simulizi katika Blogu za Kiswahili
Kama unatazama blogu za Kiswahili kwa karibu, utagundua kuwa kuna jambo moja zuri sana linajitokeza. Blogu zinakuwa sio tu eneo la kujadili masuala ya kisiasa, kiutamaduni, na kijamii bali pia ukumbi wa kutoa kazi za fasihi andishi: riwaya, tamthilia, visa, mashairi, n.k. Hili ni jambo kubwa sana. Nimelizungumzia majuzi kwenye muhtasari niliouandika kwenye blogu ya Sauti za Dunia. Bonyeza hapa uusome. Katika muhtasari huo nilisema hivi (kwa Kiingereza):
It is a common practice among Swahili poets to challenge each other using various poetry techniques and deep Swahili. For example, one poet writes a poem and another poet responds to that poem through a poem of his/her own. This practice has long been associated with Uhuru, the only Tanzanian newspaper that for many years provided a space for Swahili poets to publish their work. Two poet bloggers, Kasri la Mwanazuo and Fasihi za Ufasaha are moving this practice to cyberspace through their blogs.
This is a particularly interesting moment in the Kiswahili blogosphere. The possibility that blogging can become one of the ways in which Tanzanian writers and poets can bypass problems related to cost of publication and economics of distribution is an exciting one. For example, because of limited distribution, Swahili novels are mostly read in Tanzania and Kenya. If Swahili literary works are available online in digital format, making them globally accessible, Swahili speakers in Oman, India, the US, China, Mexico, South Africa and elsewhere will be able to read them. Utilizing this opportunity, Kasri la Mwanazuo is planning on releasing his first novel on his blog.
Utaona kuwa katika muhtasari huo ninasema kuwa kazi za fasihi andishi hata fasihi simulizi za Kiswahili (tukianza kutumia blogu za sauti [podikasiti]) ambazo kawaida husomwa Afrika Mashariki tu (hasa nchi mbili, Kenya na Tanzania) zinaweza kuanza kusomwa na wasomaji zaidi ya milioni 100 wa Kiswahili ambao wametapakaa sehemu mbalimbali duniani. Kwa kuwa mzungumza Kiswahili anayependa fasihi ya Kiswahili anayeishi India au Oman hawezi kununua vitabu vilivyoko pale TPH, mtaa wa Samora, kazi hizi za fasihi zikipatikana katika mtandao wa Intaneti (kupitia blogu, podikasiti, fasihi pepe, n.k.) mtu huyo ataweza kujisomea. Kwa maana hiyo fasihi ya Kiswahili haitakuwa ni fasihi ya kikanda bali ya dunia. Tunajua kuwa wachapishaji wetu wanakabiliwa na tatizo la mtaji wa kuweza kusambaza kazi za Kiswahili duniani.
Jambo jingine ni kuwa kuna watu wengi ambao ni watunzi wazuri sana wa riwaya, mashairi, au tamthilia lakini kutokana na gharama kubwa za kuchapa vitabu, kazi zao zinabaki kwenye shajara au madafatari yao binafsi. Wanazisoma wenyewe. Teknolojia ya blogu inaweza kusaidia, kwa kiasi fulani, baadhi ya watunzi hawa kwa kuwapa eneo la kuchapa kazi zao kwenye mtandao wa Intaneti. Hata kama mtunzi mwenyewe hana utaalamu wa masuala ya kompyuta anaweza kutumia ndugu au marafiki au wakereketwa ili waweke kazi zake mtandaoni.
Upo pia uwezekano wa kazi za fasihi zilizotolewa mtandaoni kutolewa katika muundo wa vitabu kwa ajili ya wasomaji wasio na mtandao wa Intaneti au wanaotaka kusoma kazi hizo katika vitabu. Kwa mfano, mwablogu Salam Pax wa Iraki amechapisha yaliyoko kwenye blogu yake kwenye kitabu ambacho kimepata umaarufu sana. Bonyeza hapa uone kitabu chake na hapa ili usome habari zake.
Kama ulifuatilia tuzo, ambayo niliitangaza hapa, ya blogu duniani utakumbuka kuwa aliyeshinda (ukiacha blogu ya Sauti za Dunia ambayo ilishinda kwa upande wa Kiingereza) kwa blogu za lugha zote zilizoshiriki ni blogu ya kifasihi ya Kihispania ambayo inaelezea maisha ya familia moja. Blogu hiyo inaitwa, Heshima Kidogo, Mimi ni Mama Yako. Bonyeza hapa uone tangazo la kushinda kwake. Bonyeza hapa uone blogu yenyewe.
Kwahiyo kama mnafahamu watunzi ambao wanatafuta njia ya kuweka kazi zao mikononi mwa wasomaji ila hawana namna, waelezeni kuwa blogu ni moja ya njia ambazo hazihitaji gharama kubwa. Sio mwanzo na mwisho ila ni moja ya upenyo.
Ninawaombeni pia mufuatilie kazi zilizopo hivi sasa mtandaoni za fasihi. Majuzi nilimtangaza mwanablogu mshairi Ustaadh, Rashid Mkwinda(ngominenga)(Malenga wa Kilwa). Nikamrushia dongo mshairi mwingine, Makene, kuwa akae chonjo. Bonyeza hapa usome tangazo hilo. Makene, mzee wa Kasri la Mwanzuo, akajibu kwa mashairi mawili ya haraka haraka katika sehemu ya maoni. Nami nikaweka shairi fupi la Ustaadh Mkwinda jibu kwa Makene na mimi. Bonyeza hapa usome mashairi hayo. Makene hakuishia hapo, akakaa chini na kumkaribisha Mkwinda kwa shairi. Bofya hapa usome shairi hilo. Mkwinda naye akamwandikia Makene. Bofya hapa na pia tazama sehemu ya maoni kwa mashairi la Makene. Mkwinda akaandika pia shairi jingine kwa Makene na mimi. Bofya hapa. Nadhani nitamjibu Mkwinda kwa Kichagga!
Mkwinda kaandika shairi, baada ya mchezo wa kuigiza wa uchaguzi Tanzania, akiuliza kama ulikuwa ni uchaguzi au uchakuzi. Lisome hapa. Makene kabla hajaondoka kwenye Kanada aliandika shairi la salamu kwa wanablogu wa Kiswahili. Bofya hapa ulione. Kinachotokea katika mashairi haya ya nipe nikupe ni sawa na hali ambayo imekuwepo kwa miaka mingi katika ukurasa wa mashairi wa gazeti la CCM, Uhuru. Bonyeza hapa uone ukurasa huo, Uga wa Malenga.
Huko nyuma Mwandani aliwahi kuandika mshairi kadhaa (ninatafuta viungo vyake...Tunga unavyo haraka haraka unipatie?). Ukiacha mashairi kuna kazi nyingine za kusisimua kama aliyoandika Jeff hivi karibuni. Kazi yake hii: Nyerere Yuko Wapi?, nimeipenda sana. Isome kwa kubonyeza hapa. Makene naye ana kazi yake iitwayo Safari ya Mashua. Bonyeza hapa kwa sehemu ya kwanza na hapa kwa sehemu ya pili. Jana ameandika kisa kilichomtokea ndotoni. Bofya hapa. Kasri la Mwanazuo tuliongea siku si nyingi juu ya kufungua ukurasa wa Fasihi Pepe za Kiswahili (Makene, sijasahau nilichokuahidi!).
Kwangu mimi mambo haya ni kile kitu ninachopenda kuita, "ishara ndogo za mambo makubwa." Hizi ni ishara ndogo za mambo makubwa yanayokuja mbeleni. Ninatazama mambo haya ninatabasamu. Tunafanya jambo moja kubwa sana bila wenyewe kujua. Au pengine tunajua...
2 Maoni Yako:
Ndesanjo,
Nakubaliana na wewe kabisa kuhusu ukuaji,umuhimu huu wa fasihi za aina zote.Nikiiangalia jamii yetu ya sasa siwezi kubisha kwamba mambo yameenda kombo.Ndio maana kila siku unasikia ile parapanda ya "kuporomoka kwa maadili".Nadhani fasihi ni jambo ambalo lilitujenga sisi siku za nyuma.Nakumbuka zama zile tukiambiwa kwamba tusikojoe vichakani kwa sababu mama zetu watakatika matiti,tukakubali na kuweka mazingira yetu safi.Dhana hizo mara nyingi tulikabidhiwa na babu na bibi zetu.Mparang'anyiko wa jamii kiuchumi,kijamii na kisiasa umepelekea fasihi kupewa kisogo.Lakini mathalani tumegundua kwamba fasihi ni mojawapo ya misingi yetu katika kujenga upya jamii bora basi tutumie nafasi kama hizi kuamsha tena hisia zile zile.Huu ni uandishi mpya wa historia yetu na mustakabali wetu.Naamini tutafika!
mwamko, mwamko. Nami naliona hilo linakuja, bila papara.Nitapachika mashairi zaidi, tatizo langu nina vijikaratasi vingi kwenye kila mfuko wa suruali vingine nasahau halafu navifua, basi ninapoteza mengi.
haidhuru, tuko kwenye njia sawa.
Post a Comment
<< Home