Waacheni Wenye Lugha Yao!
Hii inanikumbusha enzi zile nikisoma gazeti la Uhuru.
Majuzi nilitangaza kuwa kuna mwanablogu mpya aliyekuja kwa nguvu na kutishia wale wote wanaotaka kujichukulia cheo cha u-malenga. Nikampiga dongo Kasri La Mwanazuo. Kama hukusoma tangazo hilo lisome kwa kubofya hapa.
Basi Kasri hakusita, akarudisha dongo kwangu na Mkwinda kwa shairi hili hapo chini:
Ndesanjo acha udhia, kidole ninyooshea
Gange umemgusia, vitisho kumtupia
Kasri limechimbia, mizizi imarishia
Itakuwa songombingo, kutaka libomolea.
Wazo la kulijengea, asili mbali anzia
Nikali bado tambua, Baba Mama ungania
Pumzi ilinambia, Kasri kwenda jengea,
Itakuwa songombingo, kutaka libomolea.
Mkwinda mwana fikia, Kasirini jifunzia
Fikira kutafunia, Fasihi kufahasia
Kisha weledi jazia, gange bora patilia
Itakuwa songombingo, Kasri libomolea.
Ndesanjo nanyamazia, karatasi kushikia
Kesho napaswa ketia, mtihani kufanyia
Nikisha kumalizia, Mkwinda ntamchapia
Kasri jumba la ghali, kicheko kubomolea!
*********************************************
Hakuishia hapo. Baada ya kuona Mkwinda kawa kimya akafyatua shairi jingine:
Sina ajizi fyatua, bomu nilolizindua
Awali nilidhania, muda bado kufikia
Kumbe mwanichungulia, kwa lengo kunilipua
Nataja hali hatari, Kasri kulilindia.
Ugaidi sikujua, waweza kunifikia
Hima sipendi jutia, tahadhali naanzia
Ijapo sitasemea, Walinzi naandalia
Hii ni hali hatari, Kasirini sogelea.
Nilisema nakimbia, kurasa kutazamia
Bado sijamalizia, ni mbili zilobakia
Moja itashika tama, leo napoifutia
Nikirudi hadithia, Kasri mtazamia.
Mkwinda u wapi kaka, utata umezulia
Umechupa kwa haraka, kisa watu nitishia
Tambua sijatishika, cheche ninakutemea
Kama wataka ingia, balaghashia vulia.
********************************************************
Mkwinda akasema isiwe tabu. Akaandika shairi fupi akitutisha kwa kalamu yake (mimi na Makene). Hili hapa:
Ya mja ada unene, nimepata makene,
Katu si vyema ujivune,kauli pasi mapene,
Kalamu iwe ni nene,andiko lionekane,
Ndesanjo nawe makene, kalamu vyema tumieni.
******************************
Mtembee Kasri la Mwanazuo kwa kubonyeza hapa na bofya hapa umtembelee Mkwinda.
1 Maoni Yako:
waarabu wa pemba hao wanajuana kwa vilemba vyao
Post a Comment
<< Home