12/10/2005

Blogu za Tanzania, Wowowo, na Mkutano wa Uingereza

Unajua bado siamini amini kuwa siko ndani ya jengo la Reuters nikihudhuria mkutano mkubwa kuhusu blogu. Siamini bado kuwa ndege niliyokuwa niende nayo ilikatisha safari kutokana na hali mbaya ya hewa. Kama nilitaka kung'ang'ania kwenda ingenipasa kuondoka leo na kuwasili Uingereza Jumapili (siku ambayo ndio nilikuwa niondoshe mguu toka hapo kwa Malikia Lizabeti). Huu mkono ulioleta hii nuksi, balaa, mkosi, kisirani, bahati mbaya na kadhalika lazima niutafute. Sijui niende kwa Mandondo Tanga au kwa niende Mlingotini, Bwagamoyo. Hapana, kipindi cha uchaguzi bei za Mlingotini ni kubwa sana sitaziweza. Sitaweza kushindana na pochi ya wagombea ubunge na urais.
Haya, ngoja niweke kejeli pembeni. Jeff Msangi ndiye mwanablogu pekee ambaye namuona akishiriki kwenye mkutano huu tokea Toronto, Canada kwa njia ya "Internet Relay Chat." Kaniuliza swali moja kuhusu idadi ya blogu za Watanzania. Hivi sasa kwa hesabu za haraka kuna blogu 42. Idadi hii inajumuisha blogu za Kiswahili, kiingereza, na zile za lugha zaidi ya moja. Lakini pia kuna blogu zile ambazo haziandikwi mara kwa mara. Halafu kuna blogu nne kuhusu Tanzania zinazoandikwa na Wamarekani walioko vijijini nchini Tanzania.
Chemi Che Mponda naona atazua balaa ndani ya blogu. Kaanzisha mjadala ambao najua utakuwa mtamu sana. Kaandika mada maalum kwa "wapenzi wa matako makubwa." Kanifanya nimkumbuke David Mailu, mwandishi wa Kenya ambaye vitabu vyake tukiwa wadogo tulikuwa tunavisoma huku tukijificha. Chemi anasema kuwa wowowo kubwa ni jambo la kujivunia sana na anatamani kuwa wowowo yake ingekuwa kubwa zaidi! Mija akatoa maoni akimuuliza kama ataandika juu ya matiti makubwa baada ya kuandika juu ya wowowo kubwa. Chemi anadai kuwa mada ya matiti makubwa inakuja. Bonyeza hapa umsome.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com