10/30/2005

Blogu za Kiswahili katika Blogu ya Sauti za Dunia

Hivi sasa kila alhamisi, kutakuwa na makala fupi kuhusu yazungumzwayo katika baadhi ya blogu za Watanzania/Kiswahili katika blogu ya Sauti za Dunia (Global Voices).

Bonyeza hapa usome makala ya wiki iliyopita. Bonyeza hapa usome ya wiki ile nyingine.

TANGAZO: MUHIMU NA HARAKA SANA

Kuna nafasi za kuhudhuria warsha kuhusu matumizi ya programu huria za kompyuta kwa wanaharakati wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya wanawake. Barua pepe iliyonitaarifu kuhusu warsha hii sikuifungua mapema. Washiriki wa warsha hii (hasa wanawake) watagharimiwa kila kitu. Tarehe ya mwisho kuomba kushiriki ni tarehe kwanza/mosi mwezi wa 11 (Novemba). Ingawa siku zimebaki chache, fomu yenyewe inauliza maswali machache sana.
Kama uko kwenye shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya wanawake au unafahamu mtu yeyote, tafadhali chukua hatua ya kuomba au kutaarifu wanaohusika. Muda ni kidogo hivyo fanya hima.
Taarifa za warsha hiyo na fomu ya maombi bonyeza hapa.
Au nenda kwenye anuanni hii:

Mwendo wa kinyumenyume na viatu vya juujuu...

Sikujua kuwa naweza kwenda mwendo wa kinyumenyume nikiwa nimevaa viatu vya juujuu. Mmoja wa waanzilishi wa mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices) , Ethan Zuckerman, ndivyo anavyosema. Ethan ambaye tulikuwa naye kwenye mkutano wa teknolojia wa Pop!Tech ameandika juu yangu. Pambazuko ndio kanikumbusha juu ya makala hiyo. Bonyeza hapa uisome.

Hivi ukawapa watoto vijijini kompyuta bila mafunzo itakuwaje?

Mradi wa The Hole in the Wall ndio unachofanya. Hawa jamaa wanachukua kompyuta, wanakwenda maeneo ambayo watu hawajui na hawajawahi kuona kompyuta, kisha wanawapa watoto kompyuta bila kuwapa mafunzo yoyote. Swali ni kuwa ukimpa, kwa mfano, mtoto wa kijijini kompyuta, ataifanyia nini? Bonyeza hapa uone yanayotokea unapowapa watoto kompyuta bila kuwaambia cha kufanya.

10/29/2005

Fide anashangaa waliombeba Livingstone bado wapo

Fide Tungaraza anasema kuwa alidhani kizazi cha Watanganyika (ambao pia huitwa Wadanyanyika) walibeba maiti ya Dakta Livingstone toka Kigoma hadi Bwagamoyo kwa miguu kilikwisha. Kwanini anasema hivyo? Soma waraka wake hapo chini:
Mimi nilifikiri kizazi cha wale Watanganyika waliombeba Dr Livingstone tena akiwa kafa kilikwisha! La hasha! Kumbe wajukuu zao bado tupo na tunaendeleza waliyoyafanya! Nilipokuwa Chuo cha Sanaa Bagamoyo nilikuwa nikienda kanisani na kutazama pale mahala waliposimama wale Watanganyika waliombeba mfu Dr Livingstone na kuwaambia wazungu wenziye kwamba "..Bwana amefariki.." Nilikuwa sipati majibu kwamba: Wale Watanganyika walikuwa na utu sana? Au walifanya vile kwa sababu walikuwa wanataka walipwe mishahara, marupurupu, mafao na pensheni zao kwa kukileta kidhibiti cha maiti? Au walimpenda sana Hayati Dr Livingstone? Au walikuwa wafanyakazi watiifu na waaminifu kwa mwajiri wao? Au walikuwa kama Waswahili wasemavyo mafala? Au walikuwa wapumbavu kupindukia? Au kama uchawi upo walikuwa wamelogwa?

Siku zilizopita nilikarahishwa na habari kama hii kwenye gazeti la Dar Leo
(http://www.bsctimes.com/). Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari ASKARI WA KIINGEREZA WAUA CHANGUDOA. Habari hiyo niliituma kwa baadhi yetu na kwa Mheshimiwa Waziri Omar Mapuri na Balozi Abdulkadir Shareef ili kwamba ichukuliwe hatua. Sijui kama kuna hatua iliyochukuliwa. Leo nimekumbana tena na habari za kabila hiyo hiyo yenye kichwa cha habari MCHINA AMTWANGA 'HEDI' MBANTU NA KUZIRAI. Kuna tusi limenijia lakini nalihifadhi, hivi ingekuwa MBANTU KAMPIGA 'HEDI' MCHINA NA KUZIRAI ndani ya mitaa ya Beijing huyo Mbantu angekuwa hai mpaka saa hizi? Leo imenipasa kusema kwamba wajukuu wa wale Watanganyika bado tupo baada ya kukumbana na taarifa hii kwenye gazeti la Nipashe (

Wawekezaji, waezekaji na "nunueni vya nyumbani"

Bwana mmoja kanitumia makala moja kiboko. Anazungumzia hadithi ambayo Watanzania tumekuwa tukipigiwa na wezi wa kalamu. Wezi wa kalamu ni watawala. Fela Kuti ana wimbo anasema kuwa wezi wanaotumia silaha wasitutishe kama wezi wa kalamu. Unajua mwizi wa silaha anaweza akaenda dukani kwa Mangi akaiba na kuua watu wawili. Wezi wa kalamu walioko madarakani wizi wao unaua taifa zima.
Basi makala hiyo inazungumzia hadithi ya toka mwaka 1973 ya kuhamia "makao makuu" Dodoma. Makala hiyo itatoka kwenye blogu mojawapo za Kiswahili karibuni kwahiyo sitaizungumzia. Nilichotaka kusema ni kuwa ndani ya makala hiyo huyu bwana hataki kuita wakoloni wapya "wawekezaji." Anawaita "waekezaji." Anasema kuwa kazi yao wakoloni hawa, wanaoshirikiana na akina Mangungo wa Msovero wa siku hizi ambao wanaishi kwenye jengo lenye kuta nene kuliko gereza la Ukonga, ni kuezeka kwani Watanzania tayari tumejenga. Kwahiyo jina lao ni waekezaji.
Makala hii imezungumzia suala la Watanzania kutopenda vitu vyao. Hii inanikumbusha jambo moja linalokera sana. Utasikia wakati fulani Rais Mkapa akiwataka Watanzania kujenga tabia ya kununua bidhaa za Tanzania. Ajabu ni kuwa wakati Mkapa anasema hivyo kila kitu mwilini mwake kuanzia anjifu/leso, tai, viatu hadi nguo ya ndani (kinasa) vimetoka kwenye nchi za viongozi anaopenda sana kupiga nao picha. Ukienda pale ikulu huoni vitu vya Tanzania, hata mapambo...sasa anapotuambia tununue vya Tanzania anakuwa anatutania au? Sio Mkapa tu anayefanya hivyo, hotuba za kuwataka Watanzania wanunue bidhaa zao hutolewa mara kwa mara na watu mbalimbali.
Huenda watawala hawa wanaohubiri wasichofanya wanaiga kwa wahubiri wa kidini wanaosema, "Fuata ninayohubiri sio ninayotenda." Unafiki wa-hedi!

10/26/2005

Napumua

Baada ya siku kadhaa za pilikapilika za mkutano katika mji huu mdogo (pichani) wa Camden, ninapumua. Mji huu wa ajabu sana. Siku ya mwisho ya mkutano wa Pop!Tech (ambao hufanyika kila mwaka, kwa miaka tisa sasa), hoteli, migahawa, lojingi, n.k. hufungwa. Mimi na rafiki yangu, Denver Hopkins wa ThoughtFarm, tulikwenda kula chakula cha mchana hoteli moja siku ya mwisho wa mkutano. Tunafika pale tunakuta wenye hoteli na wafanyakazi wanajichana. Wakatukaribisha na kutuambia kuwa siku hiyo ni mwisho wa biashara hadi baada ya miezi sita kipindi cha baridi kitakapomalizika. Ninapokaa mimi na anapokaa Denver napo wanatia kufuli. Hoteli nyingine walitia kufuli toka asubuhi. Mji huu hasa ni wa jamaa wenye nazo wanaokuja kupumzika kipindi cha majira ya joto. Jamaa mmoja wa Google ambaye nyumbani kwake kila jioni kulikuwa na tafrija ya kukata na shoka, yeye hukaa kwenye nyumba yake hiyo mwezi mmoja kwa mwaka. Camden ni ile miji Marekani ambayo imejaa watu wenye siasa za mrengo wa kulia, wenye pesa, wenye kupenda kuchangia pesa zao kwenye miradi ya maendeleo. Ni miji ile isiyo na uhalifu...sikuona polisi hata siku moja. Ni miji ambayo iko kama vile kisiwa, ukikaa hapo unaweza kudhani kuwa Marekani ni mbinguni...toka kidogo uone.

Napumua.


10/22/2005

Pop!Tech: Siku imemalizika

Siku imamelizika hapa katika mkutano wa Pop!Tech. Kilichobaki sasa ni kwenda kwenye tafrija. Tafrija hiyo inafanyika hapa. Ninachofurahi ni kuwa leo hawajaleta ule mchezo wa kutuambia eti tuvae suti nyeusi.

Pop!Tech: Wamarekani wanaamini kwamba...

Zaidi ya asilimia 70 ya Wamarekani wanaamini kuwa Saddam Hussein na Osama bin Laden wana uhusiano wa damu! Anayesema hayo ni Robert Trivers. Anasema kuwa binadamu wanapenda sana kudanganywa na kujidanganya.

Pop!Tech: Falsafa na mengineyo

Watu wametoka kwenye pumziko. Sasa tunapata dozi ya falsafa toka kwa mwanafalsafa na mwanahesabu, Nassim Taleb. Sijui kama nitaweza kusikiliza vyema. Kuna mengi yanaendelea. Ninatazama teknolojia ya kufundishia mtandaoni toka kwa mwalimu mmoja hapa pembeni yangu. Bonyeza hapa uone shirika analofanya kazi. Anaandaa kompyuta yake ili aniingize kwenye darasa lake (liliko mtandaoni). Nimekuwa namuona kila dakika yuko bize akiandika. Nikamuuliza, mbona? Nilidhani ni mwanablogu kumbe mwenzangu tuko wote hapa lakini wakati huo huo anafundisha wanafunzi waliotapakaa sehemu mbalimbali duniani! Mwanablogu wa Kenya, Ory (Kenyan Pundit) yuko mbele yangu upande wa kulia akihojiwa na Renee Blodget (ambaye ameishi Tanzania na hata kulala lupango!). Anamuhoji Ory kwa ajili ya blogu yake hii hapa. . Kesho asubuhi Waafrika wote 12 tulioko hapa tutakuwa kwenye kiti moto kwa ajili ya kipindi cha luninga kituo cha PBS. Tulikuwa na mkutano kabla ya chakula cha mchana kujadili jinsi ambavyo kiti moto kitakavyoendeshwa. Mwendeshaji wa kiti moto atakuwa ni David Kirkpatrick ambaye ni mhariri wa masuala ya intaneti wa jarida la Fortune. David ni kati ya wazungu wachache ambao wameweza kutamla jina langu inavyopaswa bila kuketishwa chini na kufundishwa kwa kiboko. Labda ni kwakuwa aliwahi kuishi Afrika (Nigeria) na ametembelea nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania.
Huyu mwanafalsafa naona anawaacha wengi nje...wanaoanza kusinzia ni wengi. Wapiga miayo nao wamo...wanafalsafa wakati mwingine...anakuwa kama anaongea mwenyewe.
Baadaye.

Pop!Tech: Susan Blackmore na "meme"

Anaongea sasa Susan Blackmore:
-Dhana ya "memetic" imezungumziwa katika kitabu cha The Selfish Gene cha Richard Dwarkin
-tafsiri ni kuwa meme ni kitu ambacho kinaigwa, kinajirudia, kinaambukiza...
- inaweza kuwa ni nyimbo, teknolojia, hadithi, mitindo, tabia, nembo
-ni kitu gani kinafanya vitu au mawazo au tabia fulani kuigwa zaidi ya nyingine?

** Anaonyesha mfano wa zile barua (zamani zilikuwa barua za posta siku hizi ni barua pepe) tunazotumiwa inayokwambia kuwa unatakiwa kutuma kwa watu wengine 10 au 20 ili upate bahati na usipofanya hivyo utakumbwa na balaa
- anaelezea sababu inayofanya barua hizi kufanikiwa na kuzunguka dunia mara nyingi: authority, ahadi za mambo mazuri, kuna vitisho kwenye barua hizo (mfano, usipoituma majanga yatakukumba), n.k.

** Anachekesha kidogo:
- nimetafiti Kurani nikakuta kuwa wanaume wanaokufa wakitetea uislamu wanapewa mabikira mbinguni. Lakini sikuona zawadi wanayopewa wanawake. Mimi binafsi nisingependa kupata wanaume mabikira. Nataka wanaume wanaojua majamboz!
- Mto Ganges unaaminiwa kuwa unatakasa waumini wa dini ya Kihindu. Tatizo ni kuwa mto huu ni kati ya mito michafu kuliko yote duniani. Ila waumini wanaamini kuwa nafsi zao zinatakaswa

**Siwezi kumsikiliza huyu mama hadi mwisho. Nakwenda kuongea na bwana mmoja ambaye anaondoka hapa Camden muda sio mrefu hivyo lazima tuongee sasa.

abPop!Tech: Sam Harris na Tatizo la Dini

Anaongea Sam Harris:
- dunia imejaa imani ambazo hazikubaliani
- dini kuu zimetokana na vitabu vilivyoandikwa na watu
- nitaongea mambo kadhaa ambayo yanaweza kukera baadhi ya watu
- najua kuwa watu asilimia 90 wanamwamini mungu, asilimia 93 wanaamini kuwa Yesu alifufuka, kwahiyo lazima nitaudhi baadhi ya watu maana nitaongea mambo makali sana dhidi ya dini na imani
- asilimia 22 ya Wamarekani wanaamini kuwa Yesu atashuka toka mawinguni na kuokoa dunia hii hivi karibuni
- Wamarekani wanaamini kuwa Israeli ni nchi iliyotengwa na mungu kwa ajili ya waisraeli
- asilimia zaidi ya asilimia 50 wanaamini kuwa binadamu wanaamini kuwa ni kweli kabisa kuwa tuliumbwa toka kwenye udongo, wanaamini kisa cha nyoka kuongea na kumshawishi Hawa kula tunda
- chukua mfano huu: eti matumizi ya kondomu ni kinyume na mapenzi ya mungu. Nenda Afrika katika vijiji ambavyo mamilioni wanakufa, nenda huko ukasambaze imani hii. Huu ni ujinga na kosa la jinai
- ninachosema ni kuwa lazima fikra na imani potofu zipewe changamoto. Sitaki kukataza watu kuwa na imani hizo au kupitisha sheria dhidi ya imani hizi. Ninachotaka ni watu kuhoji imani na fikra hizo
- tatizo la dini ni kuwa dini hazitaki hoja au ushahidi
- ndio unaona tofauti ya sayansi na dini, kwenye sayansi lazima kuwe na ushahidi. Unaona wakristo wenye siasa kali Marekani wanasema kuwa shambulio la Septemba 11 linatokana na ghadhabu ya mungu kutokana na Marekani kuwa na mashoga na kuruhusu utoaji mimba
- hivi wako wapi magaidi wa kujitoa mhanga wa Kibudha? Unatakiwa kufanya kazi kubwa sana kupata watu wa kujitoa mhanga katika imani ya Kibudha
- nashindwa kuelewa kwanini watu wenye siasa za kushoto hawataki kukubali kuwa uislamu una itikadi inayofanya rahisi kwa waumini wake kujitoa mhanga na kuua wasio na hatia
- kwenye uislamu kuna imani kuwa wanaojitoa mhanga wanapata maisha ya raha ya milele
- vitabu vya dini havifundishi uvumilivu wa dini na imani tofauti na yako. Vinafundisha ukereketwa na siasa kali. Hakuna kitabu cha dini kinachosema dini zote zina haki sawa
- wakristo waliokuwa wakichoma watu moto
- "Mtakatifu" Aquinas alisema kuwa wanaopinga ukristo hawana budi kuuawa. "Mtakatifu" Augustine alisema kuwa wateswe vikali sana
Maswali:
Anaulizwa anafikiria nini kuhusu "intuition"
- anajibu na kusema kuwa tunazungumzia "intuition" pale tunaposhindwa kuelezea hisia fulani
Anaulizwa swali kuhusu maendeleo ya binadamu na imani ya dini
- anajibu kwa kusema kuwa ukitazama ripoti ya Umoja ya Mataifa ya Maendeleo inayotolewa kila mwaka inaonyesha kuwa nchi ambazo zina maisha bora zaidi (kwa vipimo kama afya, elimu, vitendo vya uhalifu, vifo vya watoto, usawa wa jinsi, n.k) ni zile ambazo zina watu wengi wasio waumini wa dini (Mawazo yangu: huenda huyu bwana kasoma makala zangu maana hii ni hoja yangu!)
Mwisho***

Pop!Tech: Bunker Roy wa Barefoot College

Tunayemsikiliza sasa ni mtu ambaye ninamuheshimu mno mno. Huyu ni mkurugenzi na mwanzilishi wa chuo cha mguu peku, Barefoot College, ndugu Bunker Roy.
Msikilize:
- nilipomaliza shule nilijiambia kuwa nataka kuanzisha chuo kwa ajili ya watu masikini, watu wasio na elimu hata kidogo
- alianzisha chuo katika kijiji cha Tilonia ambapo ni jangwa. Kuna wakati hawapati mvua kwa miaka 6
- Sababu ya kuita chuo "barefoot" ni kuwa watu wengi duniani wanaotembea bila viatu wana maarifa na uwezo mkubwa
- chuo hiki ni sehemu ambayo walimu na wanafunzi wanajifunza
- chuo hiki hakikubali watu wenye vyeti vya shule au vyuo lakini zaidi ni kuwa hata wanaohitimu chuo hiki hawapewi vyeti
-** Anatuonyesha nyumba zilizojengwa na mwanafunzi wa chuo hicho ambaye hajui kusoma wala kuandika
- paa la chuo hicho lilijengwa na wanawake kwa kutumia teknolojia ya India ambayo imekuwa ikitumika zaidi ya miaka 100
- kijiji cha Tilonia kimeshaingia karne ya 21: wana teknolojia ya mtandao usiwaya, wanauza bidhaa zao mtandaoni (http://www.tilonia.com/), n.k.
**anatuonyesha teknolojia ya kukusanya maji ya mvua.
- teknolojia hii inasaidia kuwapatia wanavijiji maji na hivyo kuwapa watoto muda wa kwenda shule (maana hutumia masaa mengi kutafuta maji) na pia kuwapa wazazi wao muda wa kufanya mambo mengine badala ya kutembea mwendo mrefu kutatufa maji. Baada ya kuanza kutumia teknolojia hii katika mashule vijijini, idadi ya watoto wanaokwenda shule iliongezeka!
- wahandishi wa kisasa ni wajinga sana...elimu yao imeshindwa kabisa kutatua matatizo makubwa ya masikini na watu vijijini
- alikwenda kwa waziri wa maji kumwambia kuwa serikali ijihusishe na mradi wa kukusanya maji ya mvua mlimani, waziri akasema: Hutaweza maana mhandishi mkuu amesema haiwezekani. Bunker akamwambia waziri: nipe ruhusu nijaribu. Mradi huo ulifanikiwa na sasa vijiji vingi vinatumia teknolojia hiyo
* Anatuonyesha picha ya vibao vinavyokusanya nishati ya jua. Teknolojia hii iliwekwa na inakarabatiwa na mtu ambaye amehudhuria shule kwa miaka 6 tu maishani mwake.
- tumevipa vijiji zaidi ya 6000 teknolojia ya nishati ya jua
- anatuonyesha picha ya mhandisi wa kwanza wa teknolojia ya nishati ya jua ambaye ni mwanamke wa nchini Afghanistan
- asilimia 60 ya watoto vijijini India hawaendi shule maana wanachunga mifugo. Lakini wana uwezo wa kwenda shule usiku, ila hakuna taa. Sasa tumetengeneza taa zinazotumia nishati ya jua kwahiyo kuna shule vijijini ambazo wanafunzi wanakwenda shule usiku
** anatuonyesha picha ya dakitari wa kijijini.
- huyu bwana mnavyomuona ni mlemavu na hakuwa na elimu hata kidogo. Tulikumta barabarani tukamsimamisha tukamwambia, "Twende chuoni kwetu na baada ya miezi sita utakuwa dakitari!" Hivi sasa anafanya kazi kwenye zahanati vijijini akipima watu damu, choo, anatoa dawa, n.k.
- anaseme kuna kijiji Ethiopia ambapo watoto wanatembea zaidi ya saa moja kwwenda shule wakiwa wamebeba maji kwa matumizi shuleni wakati kwa teknolojia rahisi sana shule hizo zinaweza kukusanya maji ya mvua
- wanafunzi wanaokubaliwa katika chuo chake lazima wawe wametoka vijijini, wachaguliwe na kijiji, na mafunzo wanayopata yanaendana na mahitaji ya kijiji wanachotoka na lazima warudi kijijini kwao
- moja ya sababu inayowafanya chuo hiki wasitoe vyeti ni kuwa ukishampa mtu cheti basi ujue atakimbilia mijini wakati nia ya chuo hiki ni kufunza wahandisi, wanasayansi, na wataalamu mbalimbali kwa ajili ya wakazi vijijini
- alipoanza kuishi kijijni baada ya kumaliza chuo wanakijiji walimuuliza kama amefanya kosa mjini na anawakimbia polisi. Wanakijiji walidhani hivyo maana mfumo wa elimu ya kisasa unawaondoa wasomi vijijini, wanakijiji hao hawakuamini kuwa Bunker amekwenda kijijini hapo kuishi nao. Ameishi hapo kwa miaka 35 sasa
- Anamaliza kwa nukuu toka kwa Mahtma Gandhi: Kwanza wanakudharau, kisha wakucheka, kisha wanapambana nawe, kisha unashinda!

Makofi wa! wa! wa! waaaaaaa

Pop!Tech: Huyu jamaa anaongelea kitu gani?

Tumetoka kwenye chai na mandazi ya kizungu. Neil Gershenfeld wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachussetts (MIT). Sielewi kabisa anaongelea kitu gani. Ninajisikia kama vile niko darasa la Fikizia la mwalimu Mashingia pale sekondari ya Mawenzi. Mashingia ni yule mwalimu aliyetazama mwandiko wangu siku moja na kusema, "Wewe kijana mwandiko watu tu unaonyesha kuwa hesabu zinakupiga chenga." Da, hapo ni kidato cha pili. Maneno yake yalikuwa ni kama unabii kwani kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili nilipata 11 kwenye hisabati. Nkya, usicheke!
Haya, Neil anaongea. Labda ili uelewe kwanini sielewi, soma kuhusu utafiti anaofanya pale MIT kwa kiingereza, sitaki wala kujaribu kutafsiri):
"His unique laboratory investigates the relationship between the content of information and its physical representation, from molecular quantum computers to virtuosic musical instruments."
Labda pia majina ya vitabu alivyoandika vitakupa picha ya tabu ninayopata kumwelewa anazungumzia mdudu gani. Hivi ndio vitabu vyake:
When Things Start to Think, The Physics of Information Technology, na The Nature of Mathematical Modeling (hasa hiki cha mwisho!!!).
Pale MIT anapofanya kazi kuna watu wanafanya utafiti ambao ukielezwa unaweza usiamini. Katika maabara za MIT, wana msemo mmoja. Wanasema kuwa kama jambo linasemekana kuwa haliwezekani, basi jambo hilo ndio watataka kulifanyia utafiti na majaribio.

Pop!Tech: Jamaa wa Architecture for Humanity

Anaongea Cameron Sinclair. Huyu ni mwanzilishi wa shirika la Architecture for Humanity.
Shirika lake lina miradi sehemu mbalimbali duniani. Shirika hili linabuni na kujenga makazi katika maeneo yenye maafa, kwa mfano, wamejenga zahanati zinazomfuata mgonjwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ukimwi Kusini mwa Afrika, makazi ya wakimbizi wanaorudi makwao, majengo ya michezo.

Haya ndio anayosema:
- wanajenga uwanja wa mpira wa miguu kwa wanawake nchini Afrika Kusini
- ramani ya uwanja hiyo ilibuniwa na vijana walioshiriki kwenye mashindano ya kuchora ramani ya uwanja huo. Aliyeshinda ni kijana toka Singapore mwenye miaka 20
- sababu kubwa ya kujenga uwanja huo ni kuwa wanawake katika kitongoji cha Somkhele, KwaZulu Natal hawana maeno ya kupumzika na kujishusisha na michezo. Pia idadi ya walioathirika kwa ukimi ni kubwa sana. Ili kuepusha vitendo ambavyo vinaweza kuwaweka kwenye hatari ya kupata ukimwi, wakazi wa kitongoji hicho waliamua kuwa eneo la michezo kwa wanawake ni muhimu
** Anatuonyesha picha na video za miradi yao katika nchi mbalimbali duniani
Anaonyesha picha ya nyumba ambayo inaweza kuangushwa na kisha kujengwa kwa dakika 45! Nyumba hii haiwezi kuteketea kwa moto. Anaonyesha picha nyingine ya shule iliyojengwa kwa fedha zilizotokana na mandazi yaliyouzwa na watoto wa shule. Shule hi imejengwa kwa teknolojia ambayo inakusanya maji ya mvua kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

*** Anaonyesha video: inaanza na kauli toka kwa mtu anayesema kuwa Bush hapendi watu weusi. Video ina wimbo wa rap na picha za maafa ya Katrina. Wimbo huu wa rap ni kuhusu maafa ya Katrina. Sijawahi kuusikia. Una maneno makali sana.

** Anaonyesha picha ya nyumba za bei nafuu ambazo wamezibuni kwa ajili ya wakazi wa New Orleans.

(Bwana anaongea haraka kweli!)
- anasema kuwa mtu mmoja katika saba duniani anaishi kwenye makazi yasiyofaa kabisa kuishi kwa mwanadamu.

Pop!Tech: Nyimbo toka mashairi ya Rumi

Jina la mwanamuziki huyu sikulikia vizuri. Ni binti mmoja mrembo na nywele zake ndefu. Anaimba mashairi ya mshairi ambaye lazima usome mashairi yake kabla hujaondoka hapa duniani. Mshairi huyo ni Rumi. Bonyeza hapa umsome. Binti sauti nyororo kabisa ya kutoa nyoka, mapanya, panyabuku, vichakoro, na viumbe wengine walioko mapangoni au darini. Anapiga gitana halafu kuna jamaa anapiga matwali (matwali ni aina ya ngoma zipigwazo nchi za kiarabu). Ukumbi mzima mdomo wazi...acha tu. Matwali haya yananikumbusha sikukuu za idi pale mtaani kwetu (nyumbani kwetu ni dakika mbili kwa miguu toka ulipo msikiti wa dini ya kiarabu, uislamu).

Pop!Tech: Msanii wa picha za video, satelaiti

Asubuhi nyingine. Ingo Gunther ni msanii ambaye anatumia zana mbalimbali kama vile video, satelaiti, kompyuta, n.k. katika kazi zake. Anasema dhumuni kubwa la kazi zake ni kuonyesha mabadiliko na mambo mbalimbali duniani kama vile mazingira, siasa, utamaduni, n.k. Bonyeza hapa uone moja ya kazi zake iitwayo "World Processor." Kazi yake nyingine inaitwa Refugee Republic ambayo utaiona ukibonyeza hapa. Kazi zake na bahari zake zaidi bonyeza hapa.
Kabla ya Ingo aliongea Robert Newirth. Kutokana na kuchelewa kulala nilichelewa kuamka na nikachelewa kufika hapa nikakuta ndio anamaliza kuongea. Bwana huyu anazunguka nchi mbalimbali duniani katika makazi ya masikini katika miji mikubwa.

10/21/2005

Pop!Tech: Bart Depram anaongea

Bart Depram anajihusisha na mradi wa kutengeneza zana za kusaidia watu kutumia mtandao wa kompyuta kama sehemu ya kujenga mahusiano. Anasema wafanyabiashara wanataka kufanya webu kuwa ni kama soko moja kubwa. Yeye na wenzake wanataka kufanya webu iwe ni sehemu ya maingiliano, mahusiano, n.k.
Naandika anayosema bila kusahihisha:
- tazama webu yao ya www.flock.com
(nimetazama pembeni nikapitwa. Ameitaja tovuti hii: http://secondlife.com/ ila sijui kwanini ameitaja maana sentensi za awali zikuzisikia. Sasa anaonyesha teknolojia wanayotengeneza ambayo inakusanya habari mbalimbali toka kwenye tovuti mbalimbali. Kwa teknolojia hii huna haja ya kwenda kwenye tovuti hizo)
**************
Sasa wazungumzaji wote wameketi jukwaani wanaulizwa maswali. Kiti moto.
Negroponte akijibu swali kuhusu wakazi wa vijijini na watoto wa shule watakavyotunza kompyuta hizo: anasema wamefanya majaribio huko Cambodia na kukuta kuwa watoto wakiona matumizi ya kompyuta hizo watazitunza.
Negroponte anaulizwa je mtu akitokea mtu akitaka kununua kwa dola 300?
Anajibu kuwa kompyuta hizo hazitauzwa kwa kila mtu. Ni kwa ajili ya kusaidia watoto katika nchi zinazoendelea.
(Ninaacha kusikiliza ili nikaongee na jamaa fulani. Wakimaliza tunakwenda kula mlo wa jioni).

Pop!Tech: Negroponte na kompyuta za dola 100

Nitakuwa naandika haraka anayosema Nicholas Negroponte:
- ukitaka kubadili maisha ya watu badili mfumo wao wa elimu
- nia yake ni kujenga kompyuta ya mapajani ya dola 100
- asilimia 50 ya bei ya kompyuta za mapajani inakwenda kwenye mambo ambayo hayahusiani na utengenezaji wa kompyuta hizo.
- mwanzoni walitaka badala kuweka kioo kwenye kompyuta hizo ili kupunguza gharama watumie aina ya karatasi ngumu!
- kompyuta hizo zitakuwa pia ni kitabu
- wamekwenda nchi hizi kutangaza mradi wao: China, Brazil, India, Thailand na wanaongea na Afrika Kusini na Nigeria
- watu wengi wanamwambia kuwa yeye ni mwalimu wa chuo kikuu hajui masuala ya uzalishaji wa bidhaa. Anadai kuwa amekuwa kwenye bodi ya kampuni ya Motorola kwa muda mrefu kwahiyo anafahamu kwa kiasi fulani masuala ya uzalishaji wa bidhaa
- Anaweza kuwa wanaweza kushinda kutimiza ndoto yao ila kushindwa kwao hakutamaanisha kuwa kompyuta hizo hazitatengenezwa bali labda watazitengeneza kwa dola 125, kitu kama hicho ila sio kutozitengeneza
- wanaanza kuzitengeneza mwezi wa pili mwakani
(anatuonyesha picha za kompyuta hizo zitakavyokuwa)
- Kompyuta hizo zitakuwa zikitumika kama tunavyotumia kompyuta hivi sasa na pia kama kitabu. Yaani kama unavyoshika kitabu mkononi kukisoma, utaweza kuishika kompyuta hiyo kama kitabu
- wataonyesha kompyuta hizo mwezi ujao kule Tunisia kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Jamii-Habari
** Amemaliza. Maswali baadaye.

Pop!Tech: Magwiji wako jukwaani

Hivi sasa tuko kwenye kipindi kiitwacho "Participation Revolution." Magwiji wawili wataongea. Hawa ni kati ya watu ambao nimekuja kuwasikiliza. Hawa ni Yochai Benkler ambaye ni mwalimu wa sheria pale Yale. Mwingine atakayekuja nyuma yake ni Nicholas Negroponte. Negroponte anajihusisha na mradi wa kutengeneza kompyuta za mapajani ambazo zitauzwa kwa dola 100 au chini ya hapo kwa ajili ya nchi zinazoendelea. Tazama kuhusu mradi huo hapa.

Pop!Tech: Unataka kuangusha serikali za wezi kwa amani?

Ivan Marovic, ambaye nimemzungumzia hapo awali (bonyeza hapa), anaamini kuwa michezo ya kompyuta inaweza kusaidia sana wanaharakati wanaopambana ili kuangusha tawala wezi. Mchezo uitwao A Force More Powerful, ambao amehusika kuutengeneza, una nia ya kukusaidia ili ujue jinsi ya kuangusha watawala wa kijeshi, madikteta, na wala rushwa. Bonyeza hapa.

Pop!Tech: Davy Rothbart muokota barua barabarani

Jukwaani anapanda Davy Rothbart. Davy ni mwanzilishi wa gazeti la Found Magazine. Gazeti hili linachapisha vitu kama barua, kadi za heri ya kuzaliwa, karatasi za bili ya simu, tiketi, n.k. ambavyo watu wameokota. Dakika hii anasome baadhi ya barua ambazo wasomaji wameokota na kuwatumia. Kasoma barua moja ambayo mwanamke mmoja anamwandikia "mpenziwe" baada ya kugundua kuwa wana uhusiano wa damu! Anasema kuwa ukikuta karatasi imetupwa barabarani, ichukue. Itazame. Isome. Utashangaa mambo watu wanayoandika au kuandikiana. Anaonyesha kitabu ambacho amekichapa hivi karibuni chenye barua na karatasi zilizookotwa sehemu mbalimbali.
Kamaliza kusoma barua inayohuzunisha sana. Kila mtu kimya. Barua hii iliokotwa makaburini. Imeandikwa na mtoto aliyemwandikia barua mama yake ambaye amefariki. Anamweleza mama yake kuwa amempenda msichana. Anamwambia, "Ungekuwa hapa nawe ungempenda sana."

Pop!Tech: Ivan Marovic na mwamko wa umma dhidi ya wezi

Toka Ivan Marovic, ambaye bado anaongea katika mkutano huu wa Pop!Tech, aongoze vuguvugu lililomlazimisha Milosevic kujiuzulu, amekuwa akisaidia na kutoa ushauri kwa makundi mbalimbali duniani namna ya kuondoa watawala wezi madarakani. Alikuwa na mchango mkubwa wakati wa mapinduzi kule Ukraine. Amekuwa akishauri kampuni ya BreakAway Games kutengeneza michezo ya kompyuta na video inayofundisha jinsi ya kuangusha serikali bila kwa njia za amani.
Mapema leo wakati wa mlo wa mchana, Waafrika wote tulikuwa na majadiliano yaliyokuwa yakirekodiwa na kituo cha luninga cha PBS. Majadiliano hayo yalikuwa ni kati yetu na Bunker Roy, mwanzilishi na mkurugenzi wa chuo cha miguu peku (Barefoot College). Chuo hiki hutoa mafunzo tu kwa wale watu ambao wanaishi vijijini na wana elimu ndogo kabisa. Nitaeleza baadaye juu ya chuo hiki. Sitaki kupitwa na yanayoendelea. Mwingine aliyekuwepo ni Robert Neuwirth, ambaye hutafiti na kuandika kuhusu watu wanaoishi katika maeneo masikini katika miji mikubwa.

Pop!Tech: Tunamsikiliza Ivan Marovic

Tunamsikiliza Ivan Marovic ambaye ni mwanaharakati na mwanzilishi wa vuguvugu la Otpor huko Serbia lililokuwa likimpinga Milosevic. Anatuonyesha filamu fupi kuhusu vuguguvu hilo. Vuguvugu hilo lilihamasisha vijana wadogo kabisa kuamua kupambana dhidi ya dhuluma na udikteta. Kuhusu Otpor nenda hapa.

Pop!Tech: Rebecca wa Global Voices anaongea

Rebecca ndio kamaliza na tunakwenda kula. Baadhi ya aliyosema ambayo nimeandika kwa haraka haraka ni haya:
China watu 60 wako ndani kwa kupinga serikali mtandaoni.
Tovuti ya mashirika kama Human Rights Watch huwezi kuzipata ukiwa China.

Yahoo! walishirikiana na serikali ya China kutoa taarifa za mwanaharakati wa China aliyekuwa akitumia barua pepe kueneza habari za kupinga serikali. Mwanaharakati huyu ametiwa ndani. Atasota huko kwa miaka 10.

Simu za mkono zinatumika kama watu nchi nyingine wanavyotumia kompyuta. Watu wengi China, hasa vijijini, wanatumia simu zao za mkono kusoma blogu, kuandika barua pepe, na mambo mengine ambayo unaweza kufanya ukiwa na kompyuta.

Tatizo anasema ni kuwa kampuni kubwa kama Microsoft na Yahoo! zinashirikiana na serikali ya China kutumia teknolojia za kuchunguza wananchi wa China wanafanya nini mtandaoni. Anasema tabia hii ni hatari sana maana kama makampuni yanawekeza mamilioni kujenga mitandao na teknolojia za habari na mawasiliano lakini wakati huo huo teknolojia hizo zinatumika kuzima upinzania. Uhusiano huu wa makampuni ya biashara na serikali zisizopenda upinzani unatisha.

Sasa anajibu maswali. Anasema kuwa Intaneti ilipoingia China, watu wengi walianza kusema kuwa teknolojia hii ndio italeta mwamko wa kuiangusha serikali ya kikomunisti ya China.
******
Soma aliyosema hapo awali kwa kubonyeza hapa.

Pop!Tech: Rebecca wa Global Voices anaongea

Hivi sasa anaongea Rebecca Mackinnon wa mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices) anaongea hivi sasa. Mjadala wake unaitwa How the Internet is Changing China. Blogu yake hii hapa.

Anaongelea kijiji kimoja huko China kilichojenga tovuti hii: www.pusalu.com mwaka 1999. Tovuti hii ilitokana na madai kuwa kijiji hicho kimekuwa kikitembelea na viumbe toka sayari nyingine. Kijiji hicho kimepata umaarufu kiasi ambacho utalii kijijini hapo umekuwa ni sehemu kubwa ya kuwapatia fedha. Anasema serikali ya China inatumia mamilioni ya dola hivi sasa ili kusaidia vijiji nchini humo kuwa na mitandao ya Intaneti.

Akizungumzia jinsi ambavyo mtandao wa kompyuta unabadili mambo huko China, Rebecca anatoa mifano kadhaa. Mfano wa kwanza unahusu mwanablogu maarufu China ambaye umaarufu wake unatokana na urahisi wa watu binafsi kutoa habari mtandaoni. Mwanablogu huyu ni binti mmoja mrembo ambaye anaandika masuala mbalimbali kuhusu maisha yake. Mamilioni ya wasomaji hutembelea blogu yake.

Mfano mwingine unahusu mwalimu mmoja ambaye alikuwa anaishi maisha ya kawaida hadi pale aliporekodi wimbo na kuuweka mtandaoni. Wimbo unaitwa: Mice Love Rice. Wimbo wake umesikilizwa na watu zaidi ya milioni 100 mtandaoni. Tayari amepata mkataba wa kurekodi na anazunguka kila mahali akitumbuiza.

Anaendelea...

Pop!Tech: Ijumaa Asubuhi

Leo asubuhi kuliwa na wazungumzaji wawili katika mjadala ulioitwa: People, Place, and Planet. Nilipata matatizo ya mtandao usiwaya. Kwahiyo sikuweza kuandika mambo yalivyokuwa yanatokea. Walioongea ni Suketu Mehta mwandishi wa kitabu cha Maximum City. Tovuti yake hii hapa. Mzungumzaji mwingine alikuwa ni Mark Lynas ambaye alikuwa akizungumzia mabadiiko ya hali ya hewa. Tazama picha za mjadala wake hapa. Picha nyingine ziko hapa. Tovuti yake hii hapa. Siwezi kuongea kwa undani waliyosema maana mkutano unaendelea na kuna wengine wanaongea. Ila tovuti zao zinaweza kuwapa picha fulani ya mambo ambayo wamezungumzia.

10/20/2005

Pop!Tech: Mkutano umefikia tamati kwa leo

Watu tunatawanyika kwa leo. Waafrika tuliokaribishwa kwenye mkutano huu tunatakiwa kwenda kula chakula cha usiku na waandaaji. Nimefurahi hawajafanya lile jambo linaloniudhi sana. Unajua kuna hizi sherehe unakribishwa, kisha kwenye kadi wanaandika kuwa unatakiwa kuvaa suti nyeusi. Kama unanikaribisha, nikaribishe sio eti unipangie hadi namna nitakavyovaa. Yaani unakuja hadi kwenye kabati langu la nguo kunichagulia nivae nini?
Sasa mimi nilivyo na kiburi...ingawa siku hizi kimepungua. Kiburi kikipungua wanasema ni dalili ya uzee! Nasema nilivyo na kiburi mimi huvaa kinyume na wanavyotaka. Kwa mfano, kule Helsinki waliponipa ile kadi ya chakula cha usiku na kutaka nivae suti nyeusi...unajua nilivaa nini? Nilivaa kanzu nyeupe ya toka Ghana! Leo naona hawajataka kuleta hii habari ya kutuchagulia nguo. Usinikaribishe hata siku moja na kunipangia nivae nini...unasikia?

Baadaye wandugu. Pop!Tech inaendelea kesho.

Pop!Tech: Carolyn Porco Kamaliza, sasa maswali

Carolyn Porco kamaliza kunzungumzia utafiti wa anga za mbali. Hapa mwisho mwisho nimempata na hata kumpigia makofi alipomaliza. Na kama unanijua na ubishi wangu, nikikupigia kofi langu basi inabidi ukatambikie. Basi kamaliza kwa kusema kuwa utafiti wa "maajabu" ya anga za mbali kwake ni kama dini. "Jinsi vile waumini wanavyofarijika nafsini kwa kwa imani zao, ndivyo hivyo nami ninavyofarijika." Utafiti huu kwake ni kama vile dini.
Ameongeza kusema kuwa anaamini kuwa utafiti kama wake utaonyesha dunia kuwa hakuna sababu ya kuwa na migongano kati ya sayansi na dini. Sayansi inatufunza mengi sana kuhusu dunia yetu hii. Mengi ya mambo hayo binadamu tusingeyafahamu bila sayansi.
Naamini moja ya migongano anayozungumzia ni huu wa somo la mabadiliko ya polepole toka kwa Darwin. Waumini wa kikristo wa mrengo wa kulia Marekani wanasema kuwa wanafunzi waanze kufundishwa kitu wanachokiita kwa kiingereza, "Intelligent design." Hebu soma habari hii hapa. Tazama na hii hapa.
Mwanamama Porco anasema kuwa atafurahi siku moja wanadamu watapoweza kutazama video za moja kwa moja zikitumwa toka sayari zote. "Watu tuwe tunazitazama kama tunavyotazama Oprah..."
Muda wa maswali sasa. Peter, Marcia, na Carolyn wanapewa maswali kwa pamoja na pia wanabishana wao kwa wao kwa chati.

Pop!Tech: Carolyn Porco

Aliyeko jukwaani sasa ni Carolyn Porco, mtafiti wa masuala ya sayari na anga za mbali. Anatuonyesha picha ya chombo kinachokwenda kufanya utafiti angani chenye ukubwa sawa na basi la kutoka Mwenge kwenda Kariakoo. Saa ni picha ya sayari ya Zohari na ule mkanda ulioizunguka.

Nimepitwa na mambo anayoongelea Carolyn, nimehama nikaingia kwenye ukurasa wa kamusi elezo ya Kiswahili kutafuta kama tuna majina ya sayari, nikajikuta nimeanza kuhariri kamusi hiyo. Sijui anachoongelea hivi sasa maana kaniacha mbali kweli. Lakini ngoja nisikilize kwa makini nijue kafika wapi.

Kwakuwa nimegusia kuhusu kamusi elezo ya Kiswahili. Niliomba tusaidiane kuijenga kamusi hii. Tutakuwa tunalalamika kila siku kuwa historia yetu inaandikwa na watu wengine wakati ambao tuna nafasi ya kuiandika wenyewe kwa kusaidia lakini hatutumii nafasi hiyo. Hivi sasa hakuna kamusi duniani zenye kutumiwa na watu wengi, mashuleni, vyuoni, watu binafsi kama kamusi huru (wikipedia). Utashangaa: watu wengi ambao wanaijenga kamusi elezo ya kiswahili hivi sasa ni wazungumzaji wa Kiswahili ambao wamejifunza ukubwani maana wametoka nchi za Magharibi.

Kamusi elezo ni ya ajabu sana. Unaweza ukajikuta umeandikwa au ukakuta jina la babu yako. Ni kamusi inaandikwa na watu na sio kundi dogo la wanazuoni wanaojifanya kuwa eti wanajua kila kitu. Unadhani kama sio hivyo pombe ya mbege ingekuwa kwenye kamusi elezo? Tazama hapa.

Narudi kwa mama Carolyn, kaniacha pale kwa Alfonsi, katikati ya majengo na kiboriloni wakati ndio anaitazama Chalinze...

Pop!Tech: Marcia na utafiti chini ya habari

Marcia McNutt anaongea hivi sasa kuhusu utafiti chini ya bahari. Anasema utafiti wa sayari za mbali una faida kadhaa ambazo ni changamoto kwa watu wanaotafiti chini ya bahari. Kwa mfano, anasema mawasiliano chini ya bahari ni magumu zaidi ya mawasiliano kati ya dunia na watafiti walioko sayari za mbali. Pia anasema utafiti angani unafaidika kwa nishati ya jua wakati ule wa chini ya bahari unatumia zaidi betri. Hivi sasa anatuonyesha chombo kiitwacho Autonomous Underwater Vehicle. Chombo hiki anasema ndio macho, mkono, masikio na kila kitu kwa wanasayansi wanaotafiti yaliyoko chini ya ardhi. Chombo hiki kinajiendesha chenyewe, kina kamera zenye uwezo wa kuona kila kitu, kina mikono, n.k.

(Mawazo Yangu: Sijui kwanini wanafanya utafiti wa mamilioni chini ya bahari...hivi hawajui chini ya bahari kuna nini? Chini ya bahari kuna chunusi na majini mengine kama jini mahaba...)!

Anaongelea viumbe vipya ambavyo vimegunduliwa kutokana na utafiti wao. Anasema kuna aina ya funza ambaye hana mdomo, tumbo, wala mfumo wa kusaga chakula. Anazungumzia viumbe vingine ila tuache utani hapa anaanza kuniacha nje. Majina tu ya viumbe hao na mimea chini ya ardhi...acha tu. Sijui kwanini nilikuwa nakwenda kujificha nyuma ya chooni na Richard Shilangale na Ramadhani Isa wakati wa kipindi cha baiolojia pale shule ya Mawenzi. Naamini ningejua kidogo anayozungumzia.

Pop!Tech: Peter Diamandis na Ndege za Kwenda Anga za Mbali

Peter Diamandis anaongea dakika hii ninayoandika hapa. Huyu bwana kampuni yake inajihusisha na utengenezaji wa ndege za kibiashara za kibinafsi za kurusha watalii kwenda sayari za mbali. Mwaka 2001 Dennis Tito alikuwa ndio mtalii wa kwanza wa sayari za mbali. Safari za aina zinaelezewa kirefu katika kamusi elezo ya kiingereza. Bonyeza hapa.

Mkutano wa Pop!Tech Moja kwa Moja Mtandaoni

Unaweza kusikiliza mkutano huu kupitia kompyuta yako. Bonyeza hapa.

Pop!Tech: Camden Nimewasili na Nitarudi Tena!

Hivi unajua ili miji unayotembelea na kujisema kimya kimya kuwa lazima urudi siku moja. Basi kamji haka kadogo ka Camden ni kati ya miji hiyo. Nilichelewa kufika. Kama nilivyowahi kusema wakati fulani nadhani natakiwa kuoga na maji ya magadi. Nkya sijui kama una magadi kidogo unitumie babangu! Basi ndege ikaniacha. Nikachukua nyingine, nilipowasili uwanja wa ndege hapa Maine, jamaa aliyekuwa anichukue kaondoka. Basi kulala hotelini hadi leo asubuhi. Kuchukuliwa saa tatu, mwendo wa masaa mawili hadi hapa Camden. Kufika hotelini, kuoga, kubadili na kuja mkutanoni. Naingia tu hivi nakutana na Ethan (ambaye ameandika kwa kirefu na picha pia kuhusu matukio ya leo) na Ory. Furaha na vicheko.
Basi kwakuwa nilisahau disketa ambayo ina kazi niliyotakiwa kutuma kwenye mradi wa Sauti za Dunia, imenibidi nikache mlo wa mchana na matukio mawili ya mchana huu ili kuandika upya kazi hiyo ambayo nitaipandisha hapa baadaye. Sasa watu wametoka nje kupumzika. Chai, vitafunio, kisha tunarudi ndani. Tunakwenda kumsikiliza huyu, huyu, na huyu.
Ratiba yote ya mkutano huu wa Pop!Tech itazame hapa.

10/18/2005

Nakwenda Mkutano wa Pop!Tech kule Camden

Kila mwaka, shirika lisilo la kiserikali, Pop!Tech, huandaa mkutano mkubwa unaojumuisha wafanyabiashara, waandishi wa habari, wanazuoni, wataalamu wa teknolojia mbalimbali, wanaharakati, watunga sera, n.k. Mkutano wa kwanza ulikuwa ni mwaka 1997. Katika mkutano wake wa mwaka huu huko Camden, Maine, Pop!Tech kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Michezo kwa ajili ya Amani na Maendeleo na kampuni ya teknolojia ya Sun Microsystems wamechagua Waafrika 12 (Pop!Tech/Sun Africa Fellows) ambao kwa njia moja au nyingine wanajihusisha na juhudi za kunyanyua bara la Afrika katika nyanja za teknolojia na jamii.
Katika Waafrika hao 12 kuna Watanzania wawili. Mmoja wa Watanzania hao waliochaguliwa ni Neema Mgana. Neema ni mwanaharakati wa masuala ya Ukimwi nchini Tanzania. Yeye ni mmoja wa wanaharakati wanawake 1000 waliochaguliwa kwa ajili ya Nishani ya Nobeli ya Amani. Soma habari hiyo hapa. Na kuhusu Nishani ya Nobeli kwa wanawake 1000 soma hapa.
Mtanzania mwingine aliyechaguliwa ni jamaa moja mwenye "rasta" anaitwa Ndesanjo Macha.
Kati ya waliochaguliwa pia yumo yule mwanablogu wa mstari wa mbele wa Kenya, Kenyan Pundit.
Orodha kamili ya Waafrika hao bonyeza hapa.
Na kuhusu mkutano huo bonyeza hapa. Tazama orodha ya watakaozungumza na masuala watakayozungumzia. Orodha hii ina watu ambao nawafuatilia sana kazi zao. Bonyeza hapa uwaone.
Kwa mtaji huo kesho jioni ninaondoka kwenda Camden, mji wa kihistoria ambako ndipo mkutano huo utafanyika. Na ninataandika juu ya mkutano huo hapa nikiwa huko.

Maoni ya Watanzania Wanaokunwa na Uozo: Mkapa Kafanya Makubwa?

Kayonko Jumaa kaandika nasaha zake kuhusu nchi yetu ambayo naambiwa kuwa iliposwa na kuolewa siku nyingi sana. Nasaha za Kayonko kazitoa kwenye ukurasa wa majadiliano wa Watanzania walioko Japan (TIJA). Naweka ujumbe wake wote na baadaye nitaweka nasaha za washiriki wengine katika mjadala huu kuhusu nchi yetu (yetu?). Ndugu Kayonko mimi simfahamu na waraka huu hajanipa yeye. Na ruhusu sijamuomba. Nimepewa na mzalendo mwingine ambaye anaamini kuwa Kayonko hatatia unaa kwa kuweka waraka wake kwa Watanzania hapa. Haya msome:
Watanzania wenzangu mmeutonesha Moyo wangu juu yaTanzania! Kuna siku huwa nasema Mungu ambaye kwa hakika nakilikusema alitupendelea na Tanzania yetu, yawezekana akatuingiza motoni watanzania wote kwa kushindwa ku-appreciate utajiri wa kila kitu alicho tupa. Naomba mnivumilie, nahisi hii barua pepe yangu itakuwa ndefu kwa sababu nadhani naongea kwa watu wenye uchungu na TZ yetu, walio free na siasa za kimangimeza, mchumia tumbo au ambao wanadhani FutureYetu ipo WEST.
Mimi huwa si waelewi watu ambao huwa wanasema eti Mkapa kafanya mambo makubwa kwa TZ, karudisha heshima yaTaifa kimataifa n.k. Hao ni wale ambao hawajui walisemalo daima milele lakini kama watapewa TuitionClass wakaelewa, wasubiri muda si mrefu udhaifu wa uongozi wa awamu ya tatu na sisiemu kwa ujumla utaonekana muda simrefu. Unajua mtu mwenye njaa yamuda mrefu ambaye hata ratiba yake ya kura haieleweki(yaani yeye kifungua kinywa cha viazi ndo lunch, na dinner ndo breakfast na siku zingine ni deshi) ukimpa msaada kidogo, si ajabu akakufuru kwa kukuita weweMungu. Mmeandika mengi sana kuhusu vibweka vya uongozi wetu, sasa mimi nitapita humo humo ni paraphrase na kusherehesha. Mwaka jana katika ukumbi wa AICC kule Arusha, nikiwa pamoja na wenzangu wa UDASM, Makerere na Nairobi varsity kwenye mafundisho ya "Future EastAfrican Leaders", hii ni Summer School ambayo hutolewana East African Uongozi Institute. Si kuamini macho na masikio yangu kwa majibu ambayo Kikwete (Huyu mgombeaUrais kupitia Sisiemu) nilipomuliza swali: Je, kamakweli nia ni kuondoa/kupunguza umasikini TZ mpaka mwaka 2025, hiyo 3% as royalty na 97% kwa wawekezaji itasaidia nini? (Na kwa taarifa yenu kama mjuavyo uzembe wetu (rushwa, ufisadi, kujuana n.k, hata hiyo3% ni namba tu si ajabu tunabaki na ziro point something %).
Kikwete alijibu kwamba: Ni mfumo tuliouchagua eti wa Market Economy na kama hatuwezi kuwavutia wawekezaji eti watajiondokea!!!!!. Kwa ufupi toka siku hiyo nilianza kuwa na wasiwasi juu ya uwezo wake kuliongoza taifa toka lindi la umasikini. Mpaka sasa wasiwasi huo bado ninao. Hajui hata hao wawekezaji ni watoto wa walewale wakoloni ambao walichota na kujenga nchi zao na kwamba kilichopo sasa ni muendelezo wa "BLOOD FED SYSTEM:NEO-COLONIALISM/GLOBALISATION. Hakuna siku mzungu atakaa akupe bure wewe mbongo, ili iweje? Akikupa shilingi moja ujue atachukua sh. 3 hata baada ya miaka mitano. Sumaye wakati akitafuta kura ili agombee urais alisema moja ya malengo yake ni kulinda wawekezaji walioletwana awamu ya tatu wasiondoke nchini!!! Moja ya vitu ambavyo Wapambe wa Mkapa wanavyojivuniani miundo mbinu hasa barabara. Hiyo ni kweli imeboreka lakini lengo hasa ni kama lile la wakati wa ukoloni "All the roads and railways ran from the interior to the coast", nadhani mnajua reli ya kati haijajengwa kumsaidia Muha wa Kigoma bali kumbeba kama MANAMBA akazalishe kwenye mashamba ya mkonge, pia reli hiyo ilisafirisha mali (madini n.k) lukuki toka Congo.
Sasabarabara za Mkapa ni kwa ajili ya kuvutia WAWEKEZAJI nchini "Conducive Environment for Foreign Investors". Kwa hiyo mtanzania wa kawaida anafaidi by chance tu. Barabara nyingi zinaelekea kuliko na madini ili hao wawekezaji wavune pasina mwenyewe kwa gharama nafuu. Hoja nyingine ni eti Mkapa ameweza kukusanya kodi kwaufanisi sana kuliko miaka iliyipita!. Hapa pia ni kweli mapato ya kodi yameongezeka ila kwa mtu ambaye upo CRITICAL and CURIOUS hupaswi kulipongeza hilo kwa nguvu zote. Naomba mjue kwamba TZ na Afrika kwa ujumla tusingehitaji misaada toka nje kama kungekuwa na FAIRNESS katika International Systems. Hebu fikiria, tumeprivatise mashirika ya umma kwa bei za kutupa, tunatoa tax holidays za miaka mitano, wawekezaji wakofree sana kufanya watakalo e.g wanatuletea hadi mayai, matunda toka south africa. Kuku toka nje. Hivi mnajua kama kuna Wachina wanauza karanga katika mitaa ya soko la kariakoo? eti nao wawekezaji! Hoja yangu hapa ni kwamba ongezeko la mapato ya kodi linatokana na ujinga wetu au ukipofu wetu; hivi nani anaweza kushindwa kulipa kodi wakati faida ni ya kuzoa kutokana na kupewa mashirika na migodi bure? Yaani hii haihitaji kuandika research proposal ili ufanye utafiti. Kwa jinsi mambo yalivyo hapa TZ ni justifiable kusema "bila hata kufanya utafiti una haki ya kusema? angalau ktk maongezi ya kawaida. Hivi mnajua kwa nini Mkapa anawekwa kwenye majukwaa yakimataifa (e.g Kukaa katikati ya Bush na Blair kule Gleneagles, Scotland pia Uenyekiti wenza waUtandawazi?), nawauliza tena mnajua au na nyie ni kama watanzania wengi?. Kwa taarifa yenu kwa ufupi ni kwamba "THE MAN HAS VEHEMENTLY SOLD US". Na je mnajua kama BUSH baba ni sehemu ya BARRICK GOLD MINING CO.ambayo inamiliki mgodi wa Kahama? Halafu wanatupoza kwa viji misaada ambavyo kamwe havitotutoa ktk umasikini wetu bali ASPRIN tu za kutupoza maumivu.
Hivi Gadaff wa LIBYA ana nini zaidi ya mafuta ambayo na sisi tunayo? Jamaa yule amegeuza jangwa kuwa kijani, anazalisha mpaka anatoa food aids nje. Anatoa unemployment benefits kwa raia wake. Sisi tuna madini lukuki lakini hayana faida kwetu. Gasi ya songo songoilitoka moja kwa moja hadi Dar leo hii ndo wanafikilia kuwapa umeme wenyeji wanaozunguka mradi. Ni ajabu na kweli, na inahuzunisha. Kama haya madini na rasili mali tulizonazo hayawezi kututoa ktk umasikini huu, faida yake ikatuwezesha ku-import "Appropriate Technology", yakatufanya tujenge strong infrastructures both social and physical, tukaweza kujenga mfumo imara wa elimu, pia tukajenga strong industrial base, basi kamwe maendeleo angalau ya kama nchi za Asian Tigers itakuwa ni ndoto na badala yake itakuwa ni vita baina yetu kama ilivyokuwa Angola, Ivory Coast, DRC n.k. Hii siyo kitu cha kuombea ila it is a material fact of which both the contemporary and ancient historical observationsin many parts of the world reveals. Si kwamba watu wanapenda vita ila kuna wakati hiyo inakuwa ndo the only way to reach their desired Destination and future. Ongea au fuatilia historia ya Rais mpya waBurundi, Peter Nkurunziza. Burundi na hata Rwanda si kwamba ni ukabila tu, uchumi wa kibaguzi daima hauvumiliki. Mimi nimesoma historia, hata hizo nchi za zilizoendelea zinajua lakini, la msingi kwao ni kupora tu. Wala amani tuliyonayo si kitu cha kujivunia sana kwani wao muhimu sana, angalia DRC na zamani Angola uporaji ulikuwa wa juu sana hata watu wakiwa wanauana tena kwa silaha toka Majuu! Kwetu sisi hapa TZ amani inakuwa muhimu zaidi kwa ajili ya DIRECT FOREIGN INVESTMENTS(DFI) otherwise mzungu hajashindwa kuchukua anachokitaka popote Africa iwepo amani au vita yeye hajari, kwa sababu yeye anacho kifanya ni ku-sustain vita huku akipora. USA ana uzoefu wa kufaidika na vita nje ya ardhi yake. Vita zote kuu mbili za dunia zilimpa uchumi imara na kuchukua nafasi ya UK, the former "Workshop of the World". Hata hizi DFI hazina faida sana kwa uchumi wetu. Mojatumeamini kwamba duniani kuna kitu kinaitwa FREE TRADEor OPEN ECONOMY na hivyo tumeshindwa kuwalindawazalishaji wa ndani, hatuna STRONG PROTECTIONISM POLICY ambayo kila taifa lililoendelea duniani lazima liwe nayo. Mmesikia juzijuzi jinsi ambavyo Marekani alikuwa anahaha kuhakikisha China anapunguza supply ya bidhaa za nguo huko Asia! Ili DFI ziwe na faida kwa local economy lazima zi-stimulate domestic economy na kutoa ajira zaidi angalau kwa kujenga viwanda vya vipuri nchini. Siyo kila spare-part lazima itoke ulaya. Nimeandika sana ingawa siwezi maliza yote kwani upuuzi ni mwingi sana Afrika hasa TZ linapokuja suala la maendeleo. Hebu tuone aibu jamani nchi kama Ivory Coast pamoja nakuwa na vita tayari watakuwa Ujerumani kwenye WORLD CUP sisi na amani yetu tu? Kwa nini haitusaidii kufanya lolote la kimaendeleo?
Wachache matajiri wengi masikini, amani amani; hii ni amani feki. Niongee kidogo kuhusu uchaguzi maana upo karibu. Kuna kila dalili kwamba kama uchaguzi utakuwa huru na waHaki, basi wabunge na madiwani wa upinzani wataongezeka, na hiyo itakuwa ni hatua muhimu ktk kuelekea kupata viongozi wanaojali na pia utawala bora. Kwani hao ndo tunawakosa hapa TZ. Binafsi sijali kiongozi ni wa CCM au Upinzani la msingi kwangu ni Maslahi ya Taifa. Mungu ibariki Tanzania, pia utusaidie tuwe na amani yakweli kwani hii tuliyonayo ni ya nta.
Kayonko Juma.

10/17/2005

Blogu nyingine ya Mtanzania hiyooooo....

Nakuapia vile...hakya nani vile...kila anapotokea mwanablogu mpya ninajisikia furaha isiyo kifani. Haya, kuna mwanablogu mpya Mtanzania. Huyu ni Fatma Karama. Ni mwanafunzi wa sheria pale kwa Bibi Lizabeta, Uingereza. Kwao Arusha. Ameanza kublogu kwa kiingereza, ingawa ataingilia pia na Kiswahili. Kama kawaida tunamtembelea na kumkaribisha. Bonyeza hapa umsome. Kuna somo ametoa ambalo nimelipenda sana (ingawa sikuelewa kwanini ametumia neno "superstition." Nadhani naweza kusema kuwa naelewa lakini pia sielewi...kama umenipata nasema nini). Somo hilo bonyeza hapa.

10/16/2005

Suala la HakiElimu na sirikali yetu

Kama kosa kubwa la HakiElimu ni tabia yao ya kukosoa na kutosema jambo lolote zuri kuhusu mfumo wa ujinga (watwawala wanauita mfumo wa elimu) nchini Tanzania, basi kwa mantiki hiyo hiyo viongozi wa sirikali ambao husifu sirikali bila kukosoa hata siku moja nao wanafanya makosa. Kama HakiElimu walipaswa kusema mazuri na mabaya, mbona akina Mkapa na majang... (malizia hili neno mwenyewe. Mimi sijasema) wenzake huwa hawasemi mazuri na mabaya?

Zisome Fikra za Nyerere

Oktoba 14 mwaka jana niliweka kiungo cha mahojiano kati ya mwanaharakati na mwanazuoni Ikaweba Bunting na Mwalimu Nyerere (ambaye aliwahi kuwa baba mkwe wake Ikaweba) yaliyotolewa ndani ya gazeti la the New Internationalist. Kwa kumbukumbu ya mzee wetu naomba usome niliyoandika mwaka jana. Bonyeza hapa.

Sakata ya Maiti za Watoto wa Matajiri Kubebwa na Ndege ya Sirikali

Kwanza ilianza na uchambuzi wa Fide Mti Mkubwa Tungaraza akiuzungumzia suala la binadamu kuwa sawa na kuwa sawasawa. Akaongelea dunia tunayoishi ya wafalme na ombaomba. Bonyeza hapa usome yote aliyosema. Nami nilidakia hoja za Fide nikihoji kama ndege za sirikali zitaanza kubeba maiti za makabwela. Basi mwanablogu Mloyi wa Motowaka akanijibu. Akaniambia kuwa kwakuwa sisi makabwela hatulipi kodi kubwa hakuna sababu ya ndege ya sirikali kubeba maiti za wanetu au zetu wenyewe. Sasa Fide kaandika kwenye sehemu ya maoni ndani ya blogu. Haya ndio maoni yake:
Kodi? Mmmgh!? Kodi pale nyumbani analipwa nani? Kodi pale nyumbani inalipwa wapi? Pale Samora Avenue au kule karibu na stesheni? Halfu ikishalipwa inafanyiwa nini? Walevi tuliopata kunywa Stelle Artois tulikuwa hatujui kwamba ile bia iliingizwa na muhindi ambaye alisamehewa kuilipia kodi! Waziri Mbilinyi alifukuzwa kazi kwa sababu ya kusamehe kuwalipisha kodi matajiri kadhaa!
Kama ni kodi marehemu bibi yangu kailipa sana kwa kuuzia tena kwa mkopo pamba vyama vya ushirika. Kalipa sana kodi kule Ukerewe kwa mikiki ya wanamgambo na wajumbe wa chama wa kule Ukerewe. Kama unakumbuka polisi, mgambo, na vijana wa chama (TANU Youth League hadi UV-CCM) wamekimbiza sana wananchi kulipa kodi. Msako wa nyumba kwa nyumba umefanywa sana kwa wazawa mijini na vijijini hali kadhalika lakini walikuwa hawabishi hodi nyumba za Wahindi Kisutu kuwauliza mahouse wife na watoto wasio na kazi kama wamelipa kodi!Wapo Watanzania ambao maisha yao yote (mathalani walimu vijijini) wanalifanyia kazi taifa katika mazingira magumu na wanalipa kodi kutoka katika mishahara inayocheleweshwa hata kwa miezi. Watu hawa hata wakifa huko walipoajiriwa maiti zao zinasafirishwa kwa pesa za maskini wenzao, ndugu, jamaa, na marafiki. Hakuna fungu serikalini la kusafirisha maiti za waaajiriwa wa serikali toka sehemu walizoajiriwa mpaka makwao kwa asili!
Marehemu Charles Zawosse (mtoto wa Dakta Hukwe Zawose) alikuwa achomwe moto na Halmshauri ya jiji la Stockholm kwa sababu ya kukosa pesa za kumsafirisha kurudi nyumbani. Ubalozi wa Tanzania Stockholm ulidindisha katakata kwamba hakuna fungu la kusafirishia maiti za Watanzania. Asante nyingi ziwaendee Bwana John Simson wa Real Records na Bi Jaana-Maria Jukkara wa Global Music Center, Helsinki kwa kuchukua jukumu la kumsafirisha Marehemu Charles kwa pesa zao wenyewe.Kama sera ya uwazi na ukweli ni sera ya kweli waturuhusu kuangalia utajiri wa hao matajiri kama ni utajiri wa haki au dhuluma. Kama hao matajiri wana madeni na benki ya zamani NBC au CRDB au benki yoyote iliyokuwa ya serikali na kama wamelipa hayo madeni yao. Ninakuambia tena kwa uhakika tutawakuta na madeni ambayo hayajalipwa na hayajulikani kama yatalipwa.
Mungu Ibariki Tanzania,
Fidelis MtiMkubwa Tungaraza, Helsinki, Finland.

Blogu Toka Washington DC

Nimesikiliza matangazo niliyorusha jana toka kwenye Vuguvugu la Mamilioni Zaidi. Sikupenda ubora wake hata kidogo. Simu niliyotumia haikuweza kudaka vizuri. Baadhi nitazitoa. Hizi ni zile ambazo huwezi kusikia chochote. Na nyingine, ingawa nazo hazisikiki vizuri, nitazibakiza na kuweka vichwa vya habari. Nitakachofanya ni kuandika mambo ya msingi yaliyotokea na kuzungumziwa. Kwahiyo samahani kwa mapungufu ya sauti.

Blogu Mpya ya Kiswahili, Washington, na kadhalika

Ni saa tisa alfajiri (au bado usiku?). Nilipanga kusikiliza matangazo niliyorusha kwa simu toka Washington DC na kuweka vichwa vya habari kabla ya kulala. Ila mwili umekataa. Kwahiyo nitafanya nikiamka. Bahati mbaya simu iliisha nguvu za betri. Nilisahau kuipatia nishati kabla ya kuondoka. Kwahiyo kuna mengi niliyoshindwa kutuma. Na niliyotuma mimi mwenyewe sijasikiliza kwahiyo sijui ubora wa sauti uko vipi. Kingine ni kuwa wakati nilikuwa naita tukio la DC maandamano, kumbe sio maandamano. Ni vuguvugu. Millions More Movement. Utamsikia Wyclef Jean katika moja ya matangazo niliyotuma akiimba, "We are building a movement..." Wyclef achana naye kabisa. Kesho nitaanza kusaka tikiti za maonyesho yake. Nilikuwa nampenda ila jana ndio kanimaliza kabisa. Iwapo hufahamu ninazungumzia tukio gani, bonyeza hapa.
Mwanablogu Mloyi kanipa somo kidogo. Kaniambia kuwa niache kulalamika kuwa watoto wa matajiri wakifariki wanabebwa na ndege za sirikali. Kasema kuwa matajiri wanalipa kodi kubwa zaidi yetu sisi makabwela! Fide umeipata hiyo?
Haya. Kabla sijaupumzisha mwili napenda kutangaza blogu mpya ya Kiswahili. Blogu hii inaitwa Kasri la Mwanazuoni. Mwanablogu Boniphace Makene ni Mtanzania anayefundisha na kusoma Texas nchini Marekani. Pia huandika safu za kila wiki za gazeti la Mwananchi nchini Tanzania. Mtembelee na kama kawaida yetu tumkaribishe kwa shangwe. Bonyeza hapa.
Sasa kuna wanablogu wawili wa Kiswahili toka Texas. Mwingine ambaye huchanganya na Kichagga huyu hapa.

10/15/2005

Msikilize Mhubiri Farrakhan

this is an audio post - click to play

Msikilize Mhubiri Farrakhan

this is an audio post - click to play

Erykah Badu akimwaga maarifa

this is an audio post - click to play

Nasaha za Erykah Badu

this is an audio post - click to play

Huyu ni Erykah Badu

this is an audio post - click to play

Wyclef akiimba: We are building a movement...united state of Africa!

this is an audio post - click to play

Wyclef na wimbo wa heshima ya wakazi wa New Orleans

this is an audio post - click to play

Msikilize Wyclef Jean akitumbuiza

this is an audio post - click to play

Nasaha za Mchungaji machachari Al Sharpton

this is an audio post - click to play

Kisanga cha Rapu za Matusi: Mwana Rapu Atolewa Jukwaani

this is an audio post - click to play

Mwanazuoni Cornel West Anaongea

this is an audio post - click to play

Hii haisikiki vizuri...Wimbo wa Bob na picha za mashujaa

this is an audio post - click to play

Sauti za Wamarekani wa Asili

this is an audio post - click to play

Toka "Millions More Movement": Ngoma Nazo zilikuwepo

this is an audio post - click to play

10/14/2005

Ndio Naondoka hivyo

Nitakapoweka kituo katika ukurasa huu nitanyanyua begi la mgongoni, huyoooo...kuelekea kwenye Maandamano ya Mamilioni na Ushee. Nawahi ili nikake viti vya mbele! Nikirudi nataka tuendeleze mjadala alioanzisha Fide. Je ndege ya sirikali inabeba maiti za watoto wa matajiri tu au hata wakeshanjaa? Nitapenda tuanze kujadili jinsi ya kuipiga sirikali marufuku. Kumbuka nitakuwa naripoti mambo yanavyokwenda katika maandamano haya makubwa ya watu weusi.
Baadaye.

Erykah Badu na Maandamano ya Mamilioni na Ushee

Mmoja wa wanamuziki ambao wamekuwa wakizunguka nchi nzima kuhamashisha watu kushiriki katika maandamano Washington DC hapo kesho ni Erykah Badu. Bonyeza hapa umsikilize akipiga kampeni. Pia sikiliza CD maalumu kwa ajili ya maandamano haya. Bonyeza hapa.

Usisahau kuwa nitakuwa nakuletea vipande vya hapa na pale. Unachotakiwa kuwa nacho ni kompyuta yenye spika. Tulia. Bonyeza kisha sikiliza. Hiyo kesho.

Wakati huo huo...

Wakati huo huo sikujua kuwa meneja wa Oakland Athletics in ndugu yangu. Itabidi nianze kumtembelea! Kama huamini soma habari hii hapa na utazame jina lake.

Maandamano ya Mamilioni na Ushee

Hapo chini utaona nimeblogu kwa simu. Nilikuwa nafanya majaribio kwa ajili ya kesho. Kama hujui nazungumzia nini bonyeza hapa usome. Pia Yahoo! wameweka habari hii kuhusu maandamano hayo ya kesho kule Washington D.C muda sio mrefu. Baadaye nakwenda kununua maji, matunda, na vitu vingine tayari kwa maandamano hayo.

Majaribio ya kublogu kwa simu kwa ajili ya kesho

this is an audio post - click to play

Fujo Zenji, Binadamu Sawa na Sawasawa

Kule Zanzibar sijui mwisho wake utakuwa nini. Tuna sirikali ambayo kawaida inapenda sana kukalia matatizo. Kwa muda mrefu sirikali imekuwa ikijifanya kuwa mambo Zanzibar ni shwari. Sasa kila asubuhi nasikia watu kadhaa wamepata ngeu, wamelazwa hospitali, mikutano inavunjwa. Ndio matunda ya kukalia mzozo na kujifanya kuwa kila kitu salama. Lakini nasema kuna siku mawe na mapanga hayataelekezwa tena kwa wananchi wa kawaida bali watawala "twawala" wa sirikali yetu "tukutu."
Pale Bara tumeona sirikali yetu ya "uwazi na ukweli" haitaki kukosolewa. Sirikali yetu inataka mashirika yasiyo ya kisirikali yawe ni kama kwaya za kuimba nyimbo za sifa kwa sirikali. Shirika la HakiElimu eti limepigwa marufuku kwakuwa linatoa taarifa za uongo kuhusu hali ya elimu Tanzania. Nasema: kama kutoa taarifa za uongo adhabu yake ni kupigwa marufuku, basi sirikali yetu ndio hasa inatakiwa ipigwe marufuku. Sirikali hii imejaa uongo, unafiki, na rushwa. Nani asiyejua kuwa mfumo wa elimu Tanzania ni mfumo wa ujinga?
Kwanini HakiElimu ipoteze muda wake kusifia sirikali. Sirikali ina vyombo vyake vya habari na mawaziri na taasisi mbalimbali, vyote hivi viwe vinasifu. HakiElimu wao wameamua kuonyesha mapungufu ili sirikali na wananchi tujifunze. Ni sawa na baadhi ya watu huwa wananiambia, "ndesanjo wewe unakosoa kila siku..." Ndio nakosoa. Wako watu ambao wanasifia. Mimi naamua kukosoa. Ni kama tunagawana kazi. Au wote tusifu tuwe kama magazeti ya chama na sirikali? Wengi hatujui kuwa kukosoa kuna faida nyingi sana. Kazi tunayofanya ni kama ile ya dakitaria anayetazam afya yako. Kuna watu katika harakati tunafanya kazi kama madakitari. Hivi ukienda kwa dakitari kupima afya, unataka akwambie kuhusu sehemu za mwili zinazofanya kazi sawasawa au unataka akwambie kuhusu sehemu za mwili ambazo zinahitaji tiba?
Tunaona sirikali yetu ya "uwazi na ukweli" inataka mashirika yasiyo ya kisirikali yanayoisifia. Nadhani muda si mrefu hata vyama vya upinzania vitapigwa marufuku maana vinakosoa sirikali. Huwezi kuamini kuwa mwaka 2005 kukosoa sirikali Tanzania ni kosa. Unajua "watwawala" wetu wamezoea kupigiwa saluti, kufunguliwa mlango, kupishwa barabarani, kupigiwa makofi kwenye hotuba zao hata kama wanayosema ni upuuzi, n.k. Ikitokea watu wakawakosoa wanaudhika sana sana.
Jamani kwanini tusiipige sirikali yetu marufuku?
Soma habari kuhusu yanayoendelea kule Zanzibar hapa.
Ile habari niliyoandika jana toka kwenye waraka wa Fide bado naifiria. Ni hili suala la je binadamu ni sawa au ni sawasawa? Kama hukuisoma isome hapa. Pia soma maoni ya wasomaji chini ya habari hiyo kwa kubonyeza kidude cha maoni. Amenikumbusha Idya alipokuja na suala la "mkumbokrasia."

Sikiliza Maandamano ya Mamilioni Zaidi hapa Jikomboe

Haya. Miaka kumi iliyopita waliitwa wanaume milioni moja katika yale maandamano yaliyoitwa: Maandamano ya Wanaume Milioni Moja. Bonyeza hapa usome kuhusu maandamano hayo.
Sasa kwa ajili ya kumbukumbu ya maandamano yale ya kihistoria, jumamosi hii (tarehe 14 oktoba) kutakuwa na maandamano yanayoitwa Maandamano ya Mamilioni Zaidi. Na nitabahatika kuwepo miongoni mwa watu hao milioni na ushee. Nawe utabahatika kusikia yanayoendelea kwani nitablogu kwa sauti na sio maneno. Kwa maana hiyo utaweza kusikia sehemu za hotuba mbalimbali na burudani kemkem zitakazotawala Washington D.C hiyo kesho. Najua Joji Kichaka hatakuwepo kwenye lile kasri jeupe. Lazima aukimbie mji.
Binya hapa utembelee tovuti kuhusu maandamano hayo. Kuna taarifa kuhusu vyama vya watu weusi vinavyoshiriki, viongozi watakaongea, wanamuziki watakaokuwepo na kutumbuiza na pia video za kutazama.
Usikose kuja hapa kusikiliza kwa masikio yako mwenyewe maandamano ya mamilioni na maneno ya busara toka kwa watu mbalimbali.

10/13/2005

Fide Kaniruhusu: Binadamu ni Sawa au ni Sawasawa?

JIPYA: Fide kaniruhusu kuweka sehemu yote ya waraka wake. Kwahiyo nimeweka sehemu ya mwisho wa waraka wake. Kama ulishasoma hapa. Soma tena maana nimeongeza jambo ambalo ndio msingi wa hoja yake ya binadamu sawa au sawasawa. Pia naomba usome maoni kwenye sehemu ya maoni yaliyotolewa na mwanablogu Idya.
******************************************************************************
Fidelis Tungaraza "Mti Mkubwa" anatueleza kuwa kuna tofauti kati ya "binadamu ni sawa" na "binadamu ni sawasawa." Basi ameandika waraka huo hapo chini, akatuma kwa watu kadhaa. Nami nikabahatika kuupata. Ameandika kufuatia tukio fulani lililotokea nchini ambalo sipendi kulitaja kwa sasa kwasababu fulani fulani. Akinipa ruhusa nitalitaja. Kwahiyo kuna kipengele cha waraka wake ambacho nimekinyofoa hadi akiniruhusu. Hebu msome Fide anayeandika toka Ufini na ujiulize kama uko kwenye binadamu sawa au sawasawa:
Katiba ya Tanzania ninayoijua (Kwa sababu katiba yetu inabadilika kila siku kwa hiyo sijui kama bado inasema hivyo)mimi ilikuwa inaseam kwamba "..Binadamu wote ni sawa. Lakini katiba hiyo haikusema kwamba binadamu wote ni sawasawa kwa sababu sawa si sawa na sawasawa. Tungekuwa binadamu wote ni sawasawa wala kusingekuwa na uhondo wa maisha. Mojawapo ya uhondo wa maisha ni tofauti zetu za kijinsia, kiakili, kimaumbile, kiwajihi, kijamali, kihali, na mali.

Mwanamuziki Julio Eglesias katika kibao chake cha Moonlight Lady anaanza kwa kusema:
"..There were kings and the beggars in the world of magical styles.."
Huu kweli ni ulimwengu wa miujiza wala siyo ulimwengu wa maajabu. Maajabu utabakia kuyastaajabia tu lakini miujiza itakuacha unajiulizajiuliza maswali bila kupata majibu. Sasa katika huu ulimwengu wetu huu wa wafalme na ombaomba tunaona jinsi wafalme wanavyoyastarehe maisha na ombaomba wanavyohenya kutafuta riziki yao ya kila siku. Wafalme wakipita askari anawapigia saluti tena wakati mwingine anawaheshimu wafalme kuliko hata baba yake mzazi. Askari akimuona ombaomba anamtimua kwa marungu, mateke, na magumi aende Gezaulole, Kibugumo, Mkuranga, Chamazi, Msanga, Mwanabilato au kwingineko kokote kwenye mashamba ya vijiji vya ujamaa.

Miye nimepata kuona kwa macho yangu gari la wagonjwa likiwa na mgonjwa ndani likisimama ili mfalme apite. Kama mnafikiri natia chumvi
muulizeni Dennis Londo. Siku ya tukio hilo nilikuwa naye.

Ikifikia siku ya kufa kwa mfalme hata wagonjwa wazimu watajua kwamba kuna tukio la kitaifa. Kwa sababu siku hiyo shughuli zote zingine zitawekwa kando ili kushughulikia msiba wa mafalme. Mapadre, makasisi, mashehe, maimamu wote watahamishia sala, swala, na dua zao kumuombea mafalme kwa Mwenyezi Mungu amuendelezee "goodtime" huko peponi zaidi ya zile alizopata kuzipata akiwa duniani. Nyie wenyewe mliona alipofariki Princess of Wales Lady Diana Spencer. Ile shughuli ilikuwa kubwa sana ukilinganisha na shughuli ya Mtawa mama Theresa wa Culcata. Misiba hii miwili ilikwenda sambasamba lakini ule Mtawa mama Theresa haukunoga kama wa Lady Diana. Mkuu wa mashoga Shoga Sir Elton John alikarabati kibao chake cha Candle in the wind ambacho hata kiziwi alikisikia katika kipindi kile cha msiba. Mtawa mama Theresa hakutungiwa hata shairi. Msiba wa Lady Diana ulihudhuriwa na vingunge na "masebriti" wakali wakali. Kwa Mtawa mama Theresa watu wa kufahamika walikuwa Hilary Clinton na Michael Jackson wengine waliobakia watawa na mapadre wa Kiroma na ombaombawa Kihindi aliokuwa anawapa pakula na pakulala.
Juzi Tanzania amefariki mtoto wa Reginald Mengi. Msiba wake nadhani ni wa pili kwa ukubwa ukifuata ule wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Msiba huu umehudhuriwa na watu wengi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Magazeti yameandika na radio zimetangaza msiba huu kwa umuhimu mkubwa. Mwili wa marehemu Rodney Mengi umesafirishwa kwa ndege ya serikali kupelekwa kwao Moshi kwa maziko. Misa ya Marehemu imeongozwa na Askofu kwa sababu Mchungaji asingetosha kufanya ibada hiyo. Msiba huu ulitimia kila kitu lakini walisahau kutangaza siku arobaini za maombolezo ya kitaifa na bendera nazo zingeshushwa nusu mlingoti.
Hapo chini ni habari toka gazeti la Nipashe ikionyesha baadhi ya mambo anayozungumzia Fide (kama ndege ya serikali, maaskofu, n.k.)

Rodney Mengi kuzikwa leo 2005-10-12 10:02:43
Na Mwandishi Wetu, Moshi

Mwili wa marehemu Rodney Mengi ukishushwa kutoka kwenye ndege katika uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro.(Picha na Mroki Mroki)


Mwili wa marehemu Rodney Mutie Mengi, mtoto wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Bw. Reginald Mengi, uliwasili mjini hapa jana asubuhi kwa ajili ya kuzikwa nyumbani leo. Ndege ya serikali aina ya Fokker 50 namba 5H TGF iliyobeba mwili wa marehemu Mutie iliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ukitokea Jijini Dar es Salaam saa 2:55 asubuhi. Mwili huo ulipokelewa na ndugu na marafiki akiwemo mdogo wa Bw. Mengi, Bw. Benjamin Mengi, kabla ya kuchukuliwa kwenda nyumbani kwake huko Shantytown mjini hapa. Ulipowasili nyumbani hapo, Mkuu wa familia ya Mengi, Mzee Elitira Mengi aliupokea mwili huo na Mchungaji Albert Mongi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) mjini Moshi aliongoza salama maalum ya makaribisho.

Mwenyekiti Mtendaji wa Ipp, Bw. Reginald Mengi akiwa na kaka yake Mzee Elitira Mengi (kushoto) baada ya kufika Moshi jana kwa mazishi ya mwanawe.


’’Mwenyezi Mungu ndiye pekee anayeweza kutupa maelekezo ya sala zetu kwa sababu ndiye anayetusikia na kutujibu’’ alisema Mchungaji Mongi wakati wa sala hiyo. Kwa upande wake, Askofu Mstaafu wa KKKT jimbo la Kaskazini Dk. Erasto Kweka aliwakumbusha umati wa waombolezaji waliokusanyika nyumbani hapo kuifariji familia Bw. Mengi kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha majonzi. ’’Mwenyezi Mungu ndiye pekee anayeweza kukupa nguvu na moyo katika kipindi hiki cha majonzi’’ alisema Askofu Kweka. Baadaye mwili wa marehemu Mutie ulipelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi. Marehemu ambaye alikuwa Mkurugenzi wa the East Africa Television na East Africa Radio alifariki duniani Alhamisi ya wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 31.

Bw. Reginald Mengi (kulia)akiwa ameongoza waombolezaji wa mjini Moshi kubeba jeneza lillilouhifadhi mwili wa marehemu mtoto wake, Rodney Mutie. Kushoto ni mdogo wake Marehemu, Abdiel Mengi.


Ibada ya mazishi itafanyika leo asubuhi katika kanisa la KKKT mjini hapa na baadaye mchana ibada nyingine itafanyika huko Machame Nkuu. Atazikwa leo nyumbani kwa familia ya Bw Mengi huko Nkuu Machame.

10/11/2005

Blogu Mpya ya Motowaka ya Ndugu Mloyi

Mshikaji Mloyi ni kati ya watu ambao barua zao pepe wanazonitumia huwa kama vile nasoma riwaya fulani. Nimefurahi kuwa amenza kublogu. Na hili ni shairi aliniandikia akinitaarifu juu ya blogu yake hiyo:

Karibuni nawaalika,
sijui nitaishi mpaka lini,
kifo kikinipata,
nitashukuru kwa mazuriyangu,
Mabaya yotenitaomba niende nayo,
karibuni kwangu,
naomba pawe pazuri,
nyuki wangurumena maua yachanue,
vipepeo wajae kama tutamaniko kwenda sote,
kaibuni kwangu kwa wingi mjongee,
maisha marefu naombea,
nyumba yangu imepata jina,
itawasha moto wa heri,
motowaka ndilo jinale.
blogspot mbeba wake,
karibu motowaka.blogspot.com,
kibarazani kwake kuna heri
hakuna wacheza kamari,
na hata karata tatu,
upatu nao hauruhusiwi.
karibuni kwa heri,
hapa shwari hamna shari.
***************************

Soma hapa chini moja ya barua zake pepe ninazozungumzia:

Huku tumezoea wagombea uraisi wa maisha, sasa pia wapo wabunge wa maisha wanaong'ang'ania ubunge kama vile ndiyo dawa ya kifo...wengine kuambiwa na wananchi ubunge basi, wameasi kauli zao zote za kidumu chama cha mapinduzi!!! na kuhamia vyama vya upinzani. Nipe kura yako nami nitakuletea maendeleo! labda maendeleo toka mbinguni, sijui, wao wanaweza kuwa watakatifu wenye roho nyeupe kama theluji na wapendwa wa bwana hivyo wataweza kumshauri mungu amalize umasikini alioukodolea macho ukue tangu siku alipoumba dunia hadi sasa umekithiri!
Sala zote za watu wa mungu hazijawahi kusikilizwa leo kuna mkombozi anayedai anaweza kuzuia umasikini kwa kushirikiana na IMF. Labda kwanza mungu awe mwehu au alale usingizi.
Haya blogu ya Mloyi hii hapa.

10/09/2005

Jina la Kiswahili la Ruby wa Lotus Media na mengineyo

Kumbe yule mwanaharakati wa mtandaoni, Ruby Sinreich, ambaye nilimtaja jana hapa, aliwahi kupewa jina la Kiswahili na rafikiye aitwaye Caroline ambaye ni huyu hapa . Ukisoma aliyoandika hapa utaona akisema kuwa tulipokutana jana alijaribu kukumbuka jina hilo la Kiswahili alilopewa. Baadaye alikumbuka. Aliitwa Kiongozi. Ruby aliongoza mjadala uliohusu matumizi ya intaneti/blogu kwenye harakati za kisiasa. Mtindo alioutumia ulikuwa ni mzuri sana maana ulishirikisha karibu kila aliyekuwa ndani ya ukumbi pale chuo cha A&T. Dave Winer, yule bwana aliyemjia juu Tiffany Brown kwa kudai kuwa wanawake weusi wameachwa pembezoni kwenye ulimwengu wa blogu, aliongoza mjadala wake kuhusu "tools and future" kwa mtindo kama wa Ruby (yaani kusisitiza ushiriki wa kila mtu badala ya mtu mmoja tu kuongea na wengine wote kusikiliza) ila mjadala huo haukuwa na mafanikio sana maana kulikuwa na wakati ilikuwa ni vigumu kujua kinachojadiliwa ni kitu gani. Kila mtu alikuwa akiongelea jambo lake na Dave alichofanya ni kusikiliza tu na kuuliza maswali ya hapa na pale. Alituambia wazi, "Sikuandaa chochote cha kuwaonyesha au kuwaambia na wala sijaja na majibu yoyote. Nataka ninyi muamue mnataka kujadili nini." Basi hapo ikawa ni vurugu mechi.
Dave Winer sikujua kuwa ni matata namna hii. Basi alipotuambia kuwa hana lolote aliloandaa akatuuliza, "Kuna mwenye swali lolote?" Jamaa mmoja akamuuliza, "Zile dola milioni mbili umefanyia nini?" Dola hizi alizoulizia jamaa huyu zinatokana na kuuzwa kwa Weblogs.com ya Dave Winer kwa kampuni ya Verisign. Basi kila mtu akakaa vizuri kwenye kiti akisubiri jibu. Dave akajibu, "Umekosea, sio dola milioni mbili bali ni milioni mbili na laki tatu! Lakini kama unataka kujua nimefanyia nini hizo hela, nimeziweka benki!"
Kama hukusoma niliyoandika juu ya Dave Winer na mjadala alioongoza Tiffany kuhusu wanablogu wa pembezoni soma hapa na hapa. Dave anazungumzia kidogo mjadala huo kwenye blogu yake hapa. Utaona anasema kuwa alikwenda kumsikiliza Jimmy Wales kwa dakika tano tu. Kisa? Eti kwakuwa Jimmy alikuwa anaendesha mjadala kuhusu wikipedia kwa kuongea na wahudhuriaji wakimsikiliza badala ya kuwa msimamizi tu wa mjadala ambapo angeruhudu kila mtu mwenye kutaka kuchangia achangie. Basi Dave akaaandika kwenye blogu yake, "Kama kazi yangu ni kusikiliza tu basi sina haja ya kuwepo hapo." Anasema alijisikia kama vile mtu anayesikiliza podikasiti (au redio).
Kuhusu harakati za mtandano, mjadala alioongoza "Kiongozi" (jina la Kiswahili la Ruby), ukienda hapa utaona viungo kadhaa ambavyo kaviweka kuhusu harakati za mtandaoni.
Kama alivyosema Ruby hapa akijibu niliyoandika kwenye blogu yake (nenda sehemu ya maoni) nadhani kuna mambo mengi mimi na yeye na pia mpenziye, Brian Russel wa Audioactivism tutafanya kwa pamoja siku za usoni. Brian na Ruby ndio watu wa kwanza ninaowajua ambao wana mpango wa kuoana kwa dhana mpya ya "open-source marriage." Dhana ya "open-source" tunaitumia zaidi kwenye masuala ya teknolojia kama inavyoelezwa hapa. Tazama hiyo "open-source marriage" ya hawa wanaharakati mtandaoni. Binya hapa.


FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com