10/16/2005

Sakata ya Maiti za Watoto wa Matajiri Kubebwa na Ndege ya Sirikali

Kwanza ilianza na uchambuzi wa Fide Mti Mkubwa Tungaraza akiuzungumzia suala la binadamu kuwa sawa na kuwa sawasawa. Akaongelea dunia tunayoishi ya wafalme na ombaomba. Bonyeza hapa usome yote aliyosema. Nami nilidakia hoja za Fide nikihoji kama ndege za sirikali zitaanza kubeba maiti za makabwela. Basi mwanablogu Mloyi wa Motowaka akanijibu. Akaniambia kuwa kwakuwa sisi makabwela hatulipi kodi kubwa hakuna sababu ya ndege ya sirikali kubeba maiti za wanetu au zetu wenyewe. Sasa Fide kaandika kwenye sehemu ya maoni ndani ya blogu. Haya ndio maoni yake:
Kodi? Mmmgh!? Kodi pale nyumbani analipwa nani? Kodi pale nyumbani inalipwa wapi? Pale Samora Avenue au kule karibu na stesheni? Halfu ikishalipwa inafanyiwa nini? Walevi tuliopata kunywa Stelle Artois tulikuwa hatujui kwamba ile bia iliingizwa na muhindi ambaye alisamehewa kuilipia kodi! Waziri Mbilinyi alifukuzwa kazi kwa sababu ya kusamehe kuwalipisha kodi matajiri kadhaa!
Kama ni kodi marehemu bibi yangu kailipa sana kwa kuuzia tena kwa mkopo pamba vyama vya ushirika. Kalipa sana kodi kule Ukerewe kwa mikiki ya wanamgambo na wajumbe wa chama wa kule Ukerewe. Kama unakumbuka polisi, mgambo, na vijana wa chama (TANU Youth League hadi UV-CCM) wamekimbiza sana wananchi kulipa kodi. Msako wa nyumba kwa nyumba umefanywa sana kwa wazawa mijini na vijijini hali kadhalika lakini walikuwa hawabishi hodi nyumba za Wahindi Kisutu kuwauliza mahouse wife na watoto wasio na kazi kama wamelipa kodi!Wapo Watanzania ambao maisha yao yote (mathalani walimu vijijini) wanalifanyia kazi taifa katika mazingira magumu na wanalipa kodi kutoka katika mishahara inayocheleweshwa hata kwa miezi. Watu hawa hata wakifa huko walipoajiriwa maiti zao zinasafirishwa kwa pesa za maskini wenzao, ndugu, jamaa, na marafiki. Hakuna fungu serikalini la kusafirisha maiti za waaajiriwa wa serikali toka sehemu walizoajiriwa mpaka makwao kwa asili!
Marehemu Charles Zawosse (mtoto wa Dakta Hukwe Zawose) alikuwa achomwe moto na Halmshauri ya jiji la Stockholm kwa sababu ya kukosa pesa za kumsafirisha kurudi nyumbani. Ubalozi wa Tanzania Stockholm ulidindisha katakata kwamba hakuna fungu la kusafirishia maiti za Watanzania. Asante nyingi ziwaendee Bwana John Simson wa Real Records na Bi Jaana-Maria Jukkara wa Global Music Center, Helsinki kwa kuchukua jukumu la kumsafirisha Marehemu Charles kwa pesa zao wenyewe.Kama sera ya uwazi na ukweli ni sera ya kweli waturuhusu kuangalia utajiri wa hao matajiri kama ni utajiri wa haki au dhuluma. Kama hao matajiri wana madeni na benki ya zamani NBC au CRDB au benki yoyote iliyokuwa ya serikali na kama wamelipa hayo madeni yao. Ninakuambia tena kwa uhakika tutawakuta na madeni ambayo hayajalipwa na hayajulikani kama yatalipwa.
Mungu Ibariki Tanzania,
Fidelis MtiMkubwa Tungaraza, Helsinki, Finland.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com