10/16/2005

Blogu Mpya ya Kiswahili, Washington, na kadhalika

Ni saa tisa alfajiri (au bado usiku?). Nilipanga kusikiliza matangazo niliyorusha kwa simu toka Washington DC na kuweka vichwa vya habari kabla ya kulala. Ila mwili umekataa. Kwahiyo nitafanya nikiamka. Bahati mbaya simu iliisha nguvu za betri. Nilisahau kuipatia nishati kabla ya kuondoka. Kwahiyo kuna mengi niliyoshindwa kutuma. Na niliyotuma mimi mwenyewe sijasikiliza kwahiyo sijui ubora wa sauti uko vipi. Kingine ni kuwa wakati nilikuwa naita tukio la DC maandamano, kumbe sio maandamano. Ni vuguvugu. Millions More Movement. Utamsikia Wyclef Jean katika moja ya matangazo niliyotuma akiimba, "We are building a movement..." Wyclef achana naye kabisa. Kesho nitaanza kusaka tikiti za maonyesho yake. Nilikuwa nampenda ila jana ndio kanimaliza kabisa. Iwapo hufahamu ninazungumzia tukio gani, bonyeza hapa.
Mwanablogu Mloyi kanipa somo kidogo. Kaniambia kuwa niache kulalamika kuwa watoto wa matajiri wakifariki wanabebwa na ndege za sirikali. Kasema kuwa matajiri wanalipa kodi kubwa zaidi yetu sisi makabwela! Fide umeipata hiyo?
Haya. Kabla sijaupumzisha mwili napenda kutangaza blogu mpya ya Kiswahili. Blogu hii inaitwa Kasri la Mwanazuoni. Mwanablogu Boniphace Makene ni Mtanzania anayefundisha na kusoma Texas nchini Marekani. Pia huandika safu za kila wiki za gazeti la Mwananchi nchini Tanzania. Mtembelee na kama kawaida yetu tumkaribishe kwa shangwe. Bonyeza hapa.
Sasa kuna wanablogu wawili wa Kiswahili toka Texas. Mwingine ambaye huchanganya na Kichagga huyu hapa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com