10/13/2005

Fide Kaniruhusu: Binadamu ni Sawa au ni Sawasawa?

JIPYA: Fide kaniruhusu kuweka sehemu yote ya waraka wake. Kwahiyo nimeweka sehemu ya mwisho wa waraka wake. Kama ulishasoma hapa. Soma tena maana nimeongeza jambo ambalo ndio msingi wa hoja yake ya binadamu sawa au sawasawa. Pia naomba usome maoni kwenye sehemu ya maoni yaliyotolewa na mwanablogu Idya.
******************************************************************************
Fidelis Tungaraza "Mti Mkubwa" anatueleza kuwa kuna tofauti kati ya "binadamu ni sawa" na "binadamu ni sawasawa." Basi ameandika waraka huo hapo chini, akatuma kwa watu kadhaa. Nami nikabahatika kuupata. Ameandika kufuatia tukio fulani lililotokea nchini ambalo sipendi kulitaja kwa sasa kwasababu fulani fulani. Akinipa ruhusa nitalitaja. Kwahiyo kuna kipengele cha waraka wake ambacho nimekinyofoa hadi akiniruhusu. Hebu msome Fide anayeandika toka Ufini na ujiulize kama uko kwenye binadamu sawa au sawasawa:
Katiba ya Tanzania ninayoijua (Kwa sababu katiba yetu inabadilika kila siku kwa hiyo sijui kama bado inasema hivyo)mimi ilikuwa inaseam kwamba "..Binadamu wote ni sawa. Lakini katiba hiyo haikusema kwamba binadamu wote ni sawasawa kwa sababu sawa si sawa na sawasawa. Tungekuwa binadamu wote ni sawasawa wala kusingekuwa na uhondo wa maisha. Mojawapo ya uhondo wa maisha ni tofauti zetu za kijinsia, kiakili, kimaumbile, kiwajihi, kijamali, kihali, na mali.

Mwanamuziki Julio Eglesias katika kibao chake cha Moonlight Lady anaanza kwa kusema:
"..There were kings and the beggars in the world of magical styles.."
Huu kweli ni ulimwengu wa miujiza wala siyo ulimwengu wa maajabu. Maajabu utabakia kuyastaajabia tu lakini miujiza itakuacha unajiulizajiuliza maswali bila kupata majibu. Sasa katika huu ulimwengu wetu huu wa wafalme na ombaomba tunaona jinsi wafalme wanavyoyastarehe maisha na ombaomba wanavyohenya kutafuta riziki yao ya kila siku. Wafalme wakipita askari anawapigia saluti tena wakati mwingine anawaheshimu wafalme kuliko hata baba yake mzazi. Askari akimuona ombaomba anamtimua kwa marungu, mateke, na magumi aende Gezaulole, Kibugumo, Mkuranga, Chamazi, Msanga, Mwanabilato au kwingineko kokote kwenye mashamba ya vijiji vya ujamaa.

Miye nimepata kuona kwa macho yangu gari la wagonjwa likiwa na mgonjwa ndani likisimama ili mfalme apite. Kama mnafikiri natia chumvi
muulizeni Dennis Londo. Siku ya tukio hilo nilikuwa naye.

Ikifikia siku ya kufa kwa mfalme hata wagonjwa wazimu watajua kwamba kuna tukio la kitaifa. Kwa sababu siku hiyo shughuli zote zingine zitawekwa kando ili kushughulikia msiba wa mafalme. Mapadre, makasisi, mashehe, maimamu wote watahamishia sala, swala, na dua zao kumuombea mafalme kwa Mwenyezi Mungu amuendelezee "goodtime" huko peponi zaidi ya zile alizopata kuzipata akiwa duniani. Nyie wenyewe mliona alipofariki Princess of Wales Lady Diana Spencer. Ile shughuli ilikuwa kubwa sana ukilinganisha na shughuli ya Mtawa mama Theresa wa Culcata. Misiba hii miwili ilikwenda sambasamba lakini ule Mtawa mama Theresa haukunoga kama wa Lady Diana. Mkuu wa mashoga Shoga Sir Elton John alikarabati kibao chake cha Candle in the wind ambacho hata kiziwi alikisikia katika kipindi kile cha msiba. Mtawa mama Theresa hakutungiwa hata shairi. Msiba wa Lady Diana ulihudhuriwa na vingunge na "masebriti" wakali wakali. Kwa Mtawa mama Theresa watu wa kufahamika walikuwa Hilary Clinton na Michael Jackson wengine waliobakia watawa na mapadre wa Kiroma na ombaombawa Kihindi aliokuwa anawapa pakula na pakulala.
Juzi Tanzania amefariki mtoto wa Reginald Mengi. Msiba wake nadhani ni wa pili kwa ukubwa ukifuata ule wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Msiba huu umehudhuriwa na watu wengi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Magazeti yameandika na radio zimetangaza msiba huu kwa umuhimu mkubwa. Mwili wa marehemu Rodney Mengi umesafirishwa kwa ndege ya serikali kupelekwa kwao Moshi kwa maziko. Misa ya Marehemu imeongozwa na Askofu kwa sababu Mchungaji asingetosha kufanya ibada hiyo. Msiba huu ulitimia kila kitu lakini walisahau kutangaza siku arobaini za maombolezo ya kitaifa na bendera nazo zingeshushwa nusu mlingoti.
Hapo chini ni habari toka gazeti la Nipashe ikionyesha baadhi ya mambo anayozungumzia Fide (kama ndege ya serikali, maaskofu, n.k.)

Rodney Mengi kuzikwa leo 2005-10-12 10:02:43
Na Mwandishi Wetu, Moshi

Mwili wa marehemu Rodney Mengi ukishushwa kutoka kwenye ndege katika uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro.(Picha na Mroki Mroki)


Mwili wa marehemu Rodney Mutie Mengi, mtoto wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Bw. Reginald Mengi, uliwasili mjini hapa jana asubuhi kwa ajili ya kuzikwa nyumbani leo. Ndege ya serikali aina ya Fokker 50 namba 5H TGF iliyobeba mwili wa marehemu Mutie iliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ukitokea Jijini Dar es Salaam saa 2:55 asubuhi. Mwili huo ulipokelewa na ndugu na marafiki akiwemo mdogo wa Bw. Mengi, Bw. Benjamin Mengi, kabla ya kuchukuliwa kwenda nyumbani kwake huko Shantytown mjini hapa. Ulipowasili nyumbani hapo, Mkuu wa familia ya Mengi, Mzee Elitira Mengi aliupokea mwili huo na Mchungaji Albert Mongi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) mjini Moshi aliongoza salama maalum ya makaribisho.

Mwenyekiti Mtendaji wa Ipp, Bw. Reginald Mengi akiwa na kaka yake Mzee Elitira Mengi (kushoto) baada ya kufika Moshi jana kwa mazishi ya mwanawe.


’’Mwenyezi Mungu ndiye pekee anayeweza kutupa maelekezo ya sala zetu kwa sababu ndiye anayetusikia na kutujibu’’ alisema Mchungaji Mongi wakati wa sala hiyo. Kwa upande wake, Askofu Mstaafu wa KKKT jimbo la Kaskazini Dk. Erasto Kweka aliwakumbusha umati wa waombolezaji waliokusanyika nyumbani hapo kuifariji familia Bw. Mengi kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha majonzi. ’’Mwenyezi Mungu ndiye pekee anayeweza kukupa nguvu na moyo katika kipindi hiki cha majonzi’’ alisema Askofu Kweka. Baadaye mwili wa marehemu Mutie ulipelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi. Marehemu ambaye alikuwa Mkurugenzi wa the East Africa Television na East Africa Radio alifariki duniani Alhamisi ya wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 31.

Bw. Reginald Mengi (kulia)akiwa ameongoza waombolezaji wa mjini Moshi kubeba jeneza lillilouhifadhi mwili wa marehemu mtoto wake, Rodney Mutie. Kushoto ni mdogo wake Marehemu, Abdiel Mengi.


Ibada ya mazishi itafanyika leo asubuhi katika kanisa la KKKT mjini hapa na baadaye mchana ibada nyingine itafanyika huko Machame Nkuu. Atazikwa leo nyumbani kwa familia ya Bw Mengi huko Nkuu Machame.

4 Maoni Yako:

At 10/13/2005 10:38:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Kwa mtu anayefuata maswala ya Tanzania utajua tukio analozungumzia. Amenikumbusha mama yangu mzazi. Mkibishana anakuambia kwa lafudhi yake ya kichaga:ni sawa lakini si sawasawa. Kumbuka pia matukio ya mabomu ya London ya tarehe saba nwezi wa saba hayakupishana na mapigano ya kikabila yaliyosababisha vifo vya watu karibu 80 huko Kenya. Salamu za rambirambi zikiwemo za Mkapa zilitumwa Uingereza lakini si Kenya kwa jirani zetu. Kuna binadamu na binadamu zaidi. Damu ya waingereza ni bora kuliko ya wakenya

 
At 10/13/2005 02:49:00 PM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Fide, sasa hiki ulichokiongelea hapa ndio utumwa wa akili anaoupigia kelele Ndesanjo kila siku, ni hadi hapo tutakapoamua kubadilisha au kusafisha fikra zetu kwa ajili ya manufaa yetu wenyewe ndio tutakapoweza kuchambua chuya katika mchele, leo hii fedha ni utu zaidi ya utu.....mmh! tumekingwa na wingu linalohitaji kutolewa kwa nguvu ya katrina.

Halafu kingine, raha ya misiba ya namna hii ni mtu ujue kiunagaubaga nini hasa kilichomtanguliza mpendwa wenu....mimi mwenzenu bado sijajua kama kuna anayejua naomba anisaidie.

 
At 10/14/2005 11:12:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Sasa hapo Mija umedodosa chanzo. Sijuhi wale waliosoma vizuri. Mimi sijasikia iliposemwa chanzo cha kutangulia mbele ya haki.

 
At 10/14/2005 12:09:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Nataka kusema jambo lakini napata kwikwi ya ajabu,machoni naona kiza,niendapo sipajui.Kizunguzungu kinataka niweka chini.Dunia gani hii tunaishi?Napata picha ya jeneza langu,rafiki zangu wachache wamelizunguka.Maradhi yote ndio yameniondoa duniani,majirani wote habari wamepewa.Mbona yule hamkusema kifo chake chanzo nini?Unyanyapaa una maana gani hivi?Samahanini wapendwa,kwikwi imenizidia,nitaandika baadaye tena

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com