10/09/2005

Jina la Kiswahili la Ruby wa Lotus Media na mengineyo

Kumbe yule mwanaharakati wa mtandaoni, Ruby Sinreich, ambaye nilimtaja jana hapa, aliwahi kupewa jina la Kiswahili na rafikiye aitwaye Caroline ambaye ni huyu hapa . Ukisoma aliyoandika hapa utaona akisema kuwa tulipokutana jana alijaribu kukumbuka jina hilo la Kiswahili alilopewa. Baadaye alikumbuka. Aliitwa Kiongozi. Ruby aliongoza mjadala uliohusu matumizi ya intaneti/blogu kwenye harakati za kisiasa. Mtindo alioutumia ulikuwa ni mzuri sana maana ulishirikisha karibu kila aliyekuwa ndani ya ukumbi pale chuo cha A&T. Dave Winer, yule bwana aliyemjia juu Tiffany Brown kwa kudai kuwa wanawake weusi wameachwa pembezoni kwenye ulimwengu wa blogu, aliongoza mjadala wake kuhusu "tools and future" kwa mtindo kama wa Ruby (yaani kusisitiza ushiriki wa kila mtu badala ya mtu mmoja tu kuongea na wengine wote kusikiliza) ila mjadala huo haukuwa na mafanikio sana maana kulikuwa na wakati ilikuwa ni vigumu kujua kinachojadiliwa ni kitu gani. Kila mtu alikuwa akiongelea jambo lake na Dave alichofanya ni kusikiliza tu na kuuliza maswali ya hapa na pale. Alituambia wazi, "Sikuandaa chochote cha kuwaonyesha au kuwaambia na wala sijaja na majibu yoyote. Nataka ninyi muamue mnataka kujadili nini." Basi hapo ikawa ni vurugu mechi.
Dave Winer sikujua kuwa ni matata namna hii. Basi alipotuambia kuwa hana lolote aliloandaa akatuuliza, "Kuna mwenye swali lolote?" Jamaa mmoja akamuuliza, "Zile dola milioni mbili umefanyia nini?" Dola hizi alizoulizia jamaa huyu zinatokana na kuuzwa kwa Weblogs.com ya Dave Winer kwa kampuni ya Verisign. Basi kila mtu akakaa vizuri kwenye kiti akisubiri jibu. Dave akajibu, "Umekosea, sio dola milioni mbili bali ni milioni mbili na laki tatu! Lakini kama unataka kujua nimefanyia nini hizo hela, nimeziweka benki!"
Kama hukusoma niliyoandika juu ya Dave Winer na mjadala alioongoza Tiffany kuhusu wanablogu wa pembezoni soma hapa na hapa. Dave anazungumzia kidogo mjadala huo kwenye blogu yake hapa. Utaona anasema kuwa alikwenda kumsikiliza Jimmy Wales kwa dakika tano tu. Kisa? Eti kwakuwa Jimmy alikuwa anaendesha mjadala kuhusu wikipedia kwa kuongea na wahudhuriaji wakimsikiliza badala ya kuwa msimamizi tu wa mjadala ambapo angeruhudu kila mtu mwenye kutaka kuchangia achangie. Basi Dave akaaandika kwenye blogu yake, "Kama kazi yangu ni kusikiliza tu basi sina haja ya kuwepo hapo." Anasema alijisikia kama vile mtu anayesikiliza podikasiti (au redio).
Kuhusu harakati za mtandano, mjadala alioongoza "Kiongozi" (jina la Kiswahili la Ruby), ukienda hapa utaona viungo kadhaa ambavyo kaviweka kuhusu harakati za mtandaoni.
Kama alivyosema Ruby hapa akijibu niliyoandika kwenye blogu yake (nenda sehemu ya maoni) nadhani kuna mambo mengi mimi na yeye na pia mpenziye, Brian Russel wa Audioactivism tutafanya kwa pamoja siku za usoni. Brian na Ruby ndio watu wa kwanza ninaowajua ambao wana mpango wa kuoana kwa dhana mpya ya "open-source marriage." Dhana ya "open-source" tunaitumia zaidi kwenye masuala ya teknolojia kama inavyoelezwa hapa. Tazama hiyo "open-source marriage" ya hawa wanaharakati mtandaoni. Binya hapa.


1 Maoni Yako:

At 10/09/2005 03:01:00 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Ahsante kaka,
Naamini umejifunza mengi kwenye mkutano huo.Mara nyingi nimekuwa mkorofi sana mkutano unapomalizika bila maafikiano rasmi.Unaweza ukatudokeza kidogo kuhusu maafikiano ya mkutano huu?Kutakuwa na mkutano kama huu mwakani?Utafanyikia wapi?Masharti ya kuhudhuria ni yapi?Na je waligusia masuala ya lugha za kigeni kama kiswahili?

 

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com