10/07/2005

ConvergeSouth Unaendelea

Mkutano wa ConvergeSouth umenza leo. Asubuhi hii na mchana kutakuwa na mijadala mbalimbali na baadaye jioni kutakuwa na nyama choma nyumbani kwa wanablogu David na Jinni Hoggard na baadaye burudani motomoto. Kesho katika moja ya burudani tutapata uhondo wa muziki wa Alana Davis. Asubuhi hii Sue Polinsky na Ed Cone walikuwa wakiongelea jinsi ambavyo waandishi wa habari na walimu wa uandishi wa habari wanaweza kublogu. Mjadala huu ulikuwa ukifanyika huku waliohudhuria (ambao hawana blogu) wakipewa mafunzo ya papo kwa hapo na hatua kwa hatua jinsi ya kuanzisha blogu. Kwakuwa chumba tulichokuwa tukitumia ni cha Institute for Advanced Journalism, kila kiti kilikuwa kina meza ndogo yenye kioo, ndani ya kioo kuna kompyuta.
Sue Polinsky, ambaye amekuwa akijihusisha na masuala ya kompyuta toka miaka ya 1947 "kweusi", amesema kuwa kama mtu anaanzisha blogu kwa nia ya kuanzisha mijadala na kubadishina mawazo na fikra na wengine, mtu huyo atafurahi sana kwa jinsi teknolojia hii itakavyomsaidia. Ila kama ni kutengeneza manoti pesa, basi ujue umelamba mchanga. Wako wanaoweka manoti mfukoni kupitia blogu ila ni wachache mno.
Ed Cone aliongea jambo moja muhimu sana. Amesema kuwa kuna habari nyingi sana ambazo ziko kwenye ulimwengu wa blogu ambazo ni za maana sana, habari hizi kamwe hazitaweza kupata nafasi kwenye vyombo vya habari. Alitoa mfano wa habari kwenye blogu hii hapa. Amesema kuwa mwenye blogu hiyo ambaye ni mwalimu wa chuo kikuu wa masuala ya kigiriki na kilatini, anaandika (na kuweka picha) juu ya masuala ya ujenzi na mipango miji. Vyombo vingi vya habari havipendi habari kama hizi. Blogu inatoa upenyo kwa watu ambao wana upenzi na utaalamu wa masuala mbalimbali kuandika na kuelimisha jamii nzima badala ya kusubiri vyombo vya habari ambavyo kama habari haihusu Maiko Jakisoni au vita sio habari.
Kati ya jamaa ambao nimekutana nao leo hii ambao ni poa sana ni mwanzilishi wa webu hii hapa inayoendeleza falsafa ya uandishi wa habari wa raia. Tutakutana naye kwa ajili ya chai na kujuana zaidi baadaye.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com