10/07/2005

Farai Chideya, Blogu, Rebecca, Wikipedia, Mwendwa na Ocholi

Nadhani moja ya mambo makubwa ninayofanya ninapokwenda katika mikutano ni "kuhubiri" juu ya blogu, hasa kwa Waafrika. Nakumbuka mwezi wa saba mwaka huu tuliongea kirefu juu ya blogu na ndugu John Kamau. Muda si mrefu akaanza kublogu hapa. Hivi majuzi tulipokutana na Muhiddin Michuzi hakuweza kujizuia baada ya kumuuzia maneno. Akaanza kublogu. Sasa pale kwenye mkutano wa We Media niliongea kirefu na waandishi wawili toka Kenya ambao hivi sasa ni watafiti katika Taasisi ya Kettering kule Ohio. Ndugu hawa wawili ambao ni Martin Wanjala Ocholi na John Mwendwa, wataanza kublogu kwa nguvu sana hivi karibuni. Nitawapeni taarifa watakapoanza.
Tukiacha "mahubiri" yangu kuhusu blogu, nimeanza pia kupiga debe kuhusu ile kamusi elezo ya Kiswahili (wikipedia ya Kiswahili). Kwahiyo jinsi ninavyojitahidi kushawishi Waafrika kutumia teknolojia ya blogu kupashana habari, kujenga mitandao, kuonyeshana picha, kuelimishana, n.k. ndivyo hivyo nimeanza kushawishi wazungumzaji wa Kiswahili kuchangia kujenga kamusi hii.
Ukiacha mazungumzo yangu na bwana Mwendwa na Ocholi ambayo yalinitia furaha sana moyoni (bwana Ocholi alinishangaza sana na uelewa wake wa vyombo vya habari Tanzania...huyu bwana anafahamu karibu waandishi wote nchini Tanzania!), nilifurahi sana sana kukutana na dada Farai Chideya. Farai, kama jina lake linavyoonyesha, ana asili ya Zimbabwe (ingawa alizaliwa Marekani). Chideya alipoongea saa tatu ya asubuhi wakati wa mjadala uliopewa jina We Media, nywele zilinisimama. Kidogo nisimame juu ya meza kupiga mbinja.
Farai ni mwanzilishi na mhariri wa webu ya habari ya PopandPolitics na pia anablogu hapa.
Farai alisema kuwa visa vya watu masikini huwa havipewi kipaumbele na vyombo vya habari. Teknolojia inaweza kuwasaidia watu hao kuwa na vyombo vyao vya habari ila bado masuala ya upatikanaji wa zana hizo yanahitaji mjadala. Akasema kuwa hata ukitazama wahudhuriaji wa mkutano wa We Media utaona kuwa kuna hatari ya kujenga vyombo vya habari vya matajiri na weupe huku tukiviita "we media."
"Tazama tulioko hapa ndani...karibu wote ni wazungu, wenye uwezo, wenye umri wa kati..." Hapo baadhi ya watu wakajigusagusa kwenye viti na kukohoa. Nikatazama ukumbini, watu weusi, kwa mfano, tulikuwa kama watano hivi. Mkutano wenyewe ukidaiwa kuwa unajumuisha "wana dunia." Farai alieleza kuwa kuna umuhimu wa kujenga kitu alichoita "peer to peer journalism" na "in-group discussions." Yaani watu ni vyema tuanze kuongea sisi kwa sisi kisha ndipo tuanze kuongea na wengine. Nikiongea naye baadaye nilimwambia kuwa sisi tunaoblogu kwa Kiswahili tunaamini kuwa watu wenye historia moja, wanaoishi katika mazingira yanayofanana kwa kiasi fulani, wenye lugha moja, utamaduni unaofanana, na wakati mwingine hata umri unaokaribiana, wakianza kujadiliana wao kwa wao kisha wakahami kweny mijadala na wengine toka tamaduni, nchi, historia tofauti, basi mjadala huo utakuwa na uzito zaidi.
Mtu mwingine akataja "glocalisation." Tunaanza "local" kisha tuaamina "global" na kurudi "local." (samahani kwa kutumia maneno hayo ya kimombo."
Farai baadaye aliniambia kuwa anachotaka hivi sasa ni sisi watu wenye asili ya Afrika kuwa na mikutano kama We Media maana kama tulivyoona ile We Media ilijaa ngozi nyeupe! Hata hivyo alisema kuwa tutakuwa tukijidanganya kama tutaacha kwenda kwenye mikutano kama hiyo. Alisema "hii yote ni mchezo fulani, lazima ujue jinsi ya kuucheza."
Furaha ya kukutana na ndugu Wakenya, kumsikiliza na kuongea na Farai, iliongezwa na kukutana na Rebeca Mackinnon, mtafiti wa Kituo cha Intaneti na Jamii cha Berkman. Rebecca ni mmoja wa waanzilishi wa mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices). Hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza kukutana ingawa tumekutana mtandaoni mara kwa mara. Rebecca aliniambia kuwa naye alifurahi sana kumsikia Farai na amekuwa "mshabiki" wake kwa muda mrefu. Rebbeca alitoa hoja kumuunga mkono Farai wakati wa mjadala akasema kuwa kuna hatari ya kujenga vyombo vya habari shirikishi (participatory media) kwa ajili ya matajiri (tena weupe...hii nimeongeza mimi.)





0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com