10/14/2005

Fujo Zenji, Binadamu Sawa na Sawasawa

Kule Zanzibar sijui mwisho wake utakuwa nini. Tuna sirikali ambayo kawaida inapenda sana kukalia matatizo. Kwa muda mrefu sirikali imekuwa ikijifanya kuwa mambo Zanzibar ni shwari. Sasa kila asubuhi nasikia watu kadhaa wamepata ngeu, wamelazwa hospitali, mikutano inavunjwa. Ndio matunda ya kukalia mzozo na kujifanya kuwa kila kitu salama. Lakini nasema kuna siku mawe na mapanga hayataelekezwa tena kwa wananchi wa kawaida bali watawala "twawala" wa sirikali yetu "tukutu."
Pale Bara tumeona sirikali yetu ya "uwazi na ukweli" haitaki kukosolewa. Sirikali yetu inataka mashirika yasiyo ya kisirikali yawe ni kama kwaya za kuimba nyimbo za sifa kwa sirikali. Shirika la HakiElimu eti limepigwa marufuku kwakuwa linatoa taarifa za uongo kuhusu hali ya elimu Tanzania. Nasema: kama kutoa taarifa za uongo adhabu yake ni kupigwa marufuku, basi sirikali yetu ndio hasa inatakiwa ipigwe marufuku. Sirikali hii imejaa uongo, unafiki, na rushwa. Nani asiyejua kuwa mfumo wa elimu Tanzania ni mfumo wa ujinga?
Kwanini HakiElimu ipoteze muda wake kusifia sirikali. Sirikali ina vyombo vyake vya habari na mawaziri na taasisi mbalimbali, vyote hivi viwe vinasifu. HakiElimu wao wameamua kuonyesha mapungufu ili sirikali na wananchi tujifunze. Ni sawa na baadhi ya watu huwa wananiambia, "ndesanjo wewe unakosoa kila siku..." Ndio nakosoa. Wako watu ambao wanasifia. Mimi naamua kukosoa. Ni kama tunagawana kazi. Au wote tusifu tuwe kama magazeti ya chama na sirikali? Wengi hatujui kuwa kukosoa kuna faida nyingi sana. Kazi tunayofanya ni kama ile ya dakitaria anayetazam afya yako. Kuna watu katika harakati tunafanya kazi kama madakitari. Hivi ukienda kwa dakitari kupima afya, unataka akwambie kuhusu sehemu za mwili zinazofanya kazi sawasawa au unataka akwambie kuhusu sehemu za mwili ambazo zinahitaji tiba?
Tunaona sirikali yetu ya "uwazi na ukweli" inataka mashirika yasiyo ya kisirikali yanayoisifia. Nadhani muda si mrefu hata vyama vya upinzania vitapigwa marufuku maana vinakosoa sirikali. Huwezi kuamini kuwa mwaka 2005 kukosoa sirikali Tanzania ni kosa. Unajua "watwawala" wetu wamezoea kupigiwa saluti, kufunguliwa mlango, kupishwa barabarani, kupigiwa makofi kwenye hotuba zao hata kama wanayosema ni upuuzi, n.k. Ikitokea watu wakawakosoa wanaudhika sana sana.
Jamani kwanini tusiipige sirikali yetu marufuku?
Soma habari kuhusu yanayoendelea kule Zanzibar hapa.
Ile habari niliyoandika jana toka kwenye waraka wa Fide bado naifiria. Ni hili suala la je binadamu ni sawa au ni sawasawa? Kama hukuisoma isome hapa. Pia soma maoni ya wasomaji chini ya habari hiyo kwa kubonyeza kidude cha maoni. Amenikumbusha Idya alipokuja na suala la "mkumbokrasia."

1 Maoni Yako:

At 10/14/2005 11:08:00 AM, Blogger Indya Nkya said...

Tatizo ni kuchanganya mambo Macha. Hivi ukikosolewa si inatakiwa na wewe utafute takwimu uwaonyeshe wanaokukosoa kwamba ni waongo? Wapi? Tanzania ni tofauti kabisa. Nilikuwa nasoma gazeti jingine kwamba majuzi Sumaye alibishana na balozi wa Ubeligiji nchini pale balozi huyo alivyosema sekta ya elimu tanzania bado inakumbwa na matatizo mengi. Jamaa akasimama akasema si kweli. Sijuhi matatizo yameisha? Kila siku unasikia serikali inafanya uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya fedha za elimu kwa mfano. Mwaka jana Sumaye aliunda tume kuchunguza madai ya kuliwa kwa fedha. sasa hiyo ni nini? Si ndiyo matatizo hayo? Wanataka nini sasa?

 

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com