Watakujia juu, "Haiwezekani!"
Haiwezekani. Kivipi. Hawatakubali. Mishipa itawatoka. Maswali watakurushia. Utashangaa, iweje hawaelewi jambo rahisi namna hii?
"Haiwezekani mtu asiwe na dini!" Watakwambia huku wakijiweka tayari kwa ubishi. Ubishi. Wanabisha jambo linalohusu nafsi yako. Wewe unawaambia kuwa nafsini mwako huamini kitu kinachoitwa dini. Na huna dini, sio muislamu wala mkristo (maana dini kwao ni hizi mbili tu).
Wanakataa. Haiwezekani. Kila binadamu ana dini.
"Hawezekani kivipi wakati mimi ni binadamu na sina dini?" Unawauliza.
Wanajibu, "Acha kutuhadaa, kila binadamu ana dini. Ina maana huamini kuwa kuna mungu?"
Wakiuliza swali hili lazima nicheke kwanza. Hapo wanakuwa wamekwenda ninapotaka. Ndipo ukombozi wa akili toka kwenye mtazamo ulioletwa na dini za kuja unapotakiwa kuanza. Watu wengi wanadhani kuwa ukiwa huna dini basi humwamini mungu.
Mahesabu yake:
binadamu+ dini = imani juu ya mungu (yaani mungu yupo)
binadamu- dini = mungu hayupo
Hawajui kuna tofauti kubwa sana kati ya dini na kumwamini mungu. Wakati wengi wetu tunadhani kuwa dini kazi yake ni kutufanya tumjue mungu, kumwamini na kumtii, ukweli ni kuwa dini nyingi zinatuwekea ukuta wa chuma usionekana ambao unatuzuia tusimjue mungu. Ukiwa hutaki kumjua mungu, nitakushauri uwe na dini. Ukiwa unataka kumjua mungu, acha nazo. Najua sentenso hiyo ya mwisho inaweza kukufanya ujiulize kama "zimenitoka" au bado "zipo."
Dini inakufanya umjue mungu kupitia mawazo na mitazamo ya watu wengine (karibu wote ni wanaume) ambao wanavaa kanzu na majoho wakiongea kwa utaratibu ili uone kuwa wana tofauti sana na wewe na kuwa wana ukaribu na mungu. Werngine hudiriki kutuambia kuwa huongea na mungu. Ila ukiwaambia wakuite saa wanaongea naye ili usikilize au kushiriki, watakwambia kuwa kama huna roho safi huwezi kuongea naye. Lakini ninaposoma busara za Yeshua (Yesu/Isa) nakuta akisema kuwa mungu anatafuta wale waliopotea. Na ndio maana Yeshua alikuwa akishinda vijiweni na wacheza kamari na wachakaramu wengine. Miyahudi ikamjia juu, "He, wewe mbona unajumika na wenye dhambi?" Unajua aliwajibu nini? Kasome kitabu unachoamini kuwa ndio ramani na dira yako hapa dunini ingawa kinakusanya vumbi. Kila siku unahangaika na magazeti ya ushambenga lakini kitabu unachodai kimeandikwa na mungu mwenyewe hukisomi...turudi kwenye hoja ya msingi.
Kwahiyo unachojua kuhusu dini ni mawazo ya viongozi wa dini yako. Mawazo yao hayo ndio yanakuwa dira yako wewe ambaye una akili na uwezo wa kujitafutia ukweli mwenyewe. Dini inakufanya uwe mvivu. Hutasoma biblia au kurani kwasababu kuna viongozi wa dini yako ambao kazi yao ni kusoma vitabu hivyo na kukutafsiria mara moja kwa juma. Au wakati mwingine mara moja kwa mwaka...kama wewe ni wale wanaoenda kanisani misa ya usiku au siku ya krisimasi.
Dini inakufanya udhani kuwa kuna mashindano kati yako wewe mkristo wa kilutheri na mkristo wa kiangikana, au shahidi wa yehova dhidi ya mkatoliki, au mashindano kati ya muislamu wa sunni na yule wa shia, au mashindano kati ya muislamu na mkristo...mashindano ya kwenda mbinguni. Dini inakufanya uamini kuwa watu wote wasio na imani kama yako watakwenda unakoita motoni. Wewe na wenzako ndio mnajua hiyo njia nyembamba iliyozungukwa na malaika weupe (ndio malaika weupe, hakuna mweusi) wenye mavazi meupe ya kuelekea kwenye uzima wa milele. Pengine ndio maana tunajichubua ili tufanane na hao malaika.
Kuna watu ambao huniambia kuwa dini huleta amani. Jamani, hivi Rwanda watu hawana dini? Je Sudan? Je Kashmir? Je Iraki? Serikali ya Marekani inayopenda vita kama sijui nini inaongozwa na watu wasio na dini? Tuache nchi hizo, twende kule zilikozaliwa dini zinazoitwa "kuu" duniani: uislamu, ukristo, na uyahudi. Twende kule walikotokea manabii wa dini hizi. Kule walikotembea na kufundisha. Twende kule mnakotumia mamilioni kwenda kuhiji. Twenda Mashariki ya Kati. Twende Palestina. Twende Yerusalemu. Huko kila mtu ana dini. Kama sio mkristo, basi ni muislamu, kama sio muislamu basi ni myahudi.
Dini moja inafundisha amani (uislamu), nyingine upendo (ukristo) na nyingine kushika amri kumi. Twende huko tutazame jinsi ambavyo dini inaleta amani!
Nyooshea kidole nchi yenye amani kutokana na watu wake kuwa na dini. Tazama Indonesia, nchi inayoongoza kwa idadi kubwa ya waislamu, je inaoongoza pia kwa amani? Tazama Ufilipino, karibu kila mtu ni mkatoliki, je wanaongoza kwa upendo aliohubiri Yesu? Hivi Kongo hawana dini? Kama dini inaleta amani, nchi zenye watu wachache wenye dini zingekuwa zinaongoza kwa vita. Lakini ajabu ni kuwa nchi zenye watu wachache wanaojihusisha na mambo ya dini zinaonekana kuwa na amani zaidi ya nchi ambazo karibu wananchi wake wote wana dini. Au tuseme wanajifanya wana hiki kitu kiitwacho dini.
Kwahiyo watu wengi wanaamini kuwa kama binadamu wasingekuwa na dini, wangekuwa watu wabaya na waovu sana. Mimi hujiuliza, binadamu anaweza kuwa mwovu zaidi ya alivyo sasa? Kuna uovu gani uliobakia? Au mnadhani yanayotokea Palestina, Iraki, Sudani, Kongo, yaliyotokea Rwanda, Cambodia, Vietnam, Aghanistan, Ujerumani ya Hitler ni hadithi? Maovu makubwa kabisa kwenye historia tunayoijua yametokea katika kipindi ambacho wanadamu wana hiki kitu mnaiita dini.
Biashara ya utumwa ya Atlantiki miaka zaidi ya 400. Ile ya waarabu ilichukua miaka mingi zaidi maana ilianza kabla hii ya Atlantiki. Mauaji ya wayahudi na Hitler. Bomu la atomiki huko Japani. Ubaguzi wa rangi Marekani na Afrika Kusini. Vita vya Wazungu vya Kwanza na vya Pili (wengine mnaviita vita vya dunia...wazungu (na baadhi ya waasia) vita vyao wanataka kubebesha lawama dunia nzima kwa kuiita vita vya dunia. Nanyi mnakubali. Yaani hawataki tugawane mali waliyotuibia bali tugawane historia ya damu.) Mauaji ya halaiki Rwanda. Ukoloni. Yote haya yamefanyika katika kipindi ambacho wanadamu wengi wanasema kuwa wana dini.
Hivi wezi wanaoiba sirikalini na wengine kuuza nchi hawana dini? Wananchi wenye hasira kali wanaoua binadamu wenzao bila huruma kwa kuwa wamedaiwa kuwa wezi, hawana dini? Wala rushwa na wana magendo, hawana dini?
Najua moja ya hoja inayotolewa ninaposema mambo haya ni hii, "Vita na maovu hayo hayajaletwa na dini." Nakubaliana kwa kiasi fulani. Nasema kwa kiasi fulani kwakuwa historia iko wazi juu ya maovu yaliyoletwa na dini. Ila hata kama maovu hayo hayakuletwa na dini, tunaweza kujiuliza: kama dini inaleta amani iweje mambo hayo yote yanayoharibu amani yatokee?
Tukichimba zaidi hoja hii tunaweza kwenda kwenye hoja nyingine ambayo sitaiingilia kwa undani. Hoja hiyo ni kuwa huenda watu "wenye dini" ukweli ni kuwa "hawana dini."
Kwa upande mwingine unapochunguza sana kitu tunachoita dini unagundua kuwa dini ni pazia. Linakuzuia usimjue mungu wako wala manabii zako. Hapa ninazungumzia Waafrika.
Hivi wewe na akili zako zote unadhani Afrika nzima haijawahi kuwa na manabii?
Kwanini sina dini? Kama wewe ni mwafrika, huhitaji dini. Uafrika ni utamaduni. Utamaduni huu unatupa mwongozo kwa kila jambo, yakiwemo masuala ya kiroho. Wewe unaweza kuyaita dini. Kwahiyo uafrika una misingi na falsafa yake kuhusu mungu unayedhani kuwa simwamini kwakuwa nasema kuwa sina dini. Falsafa na miongozo kuhusu mungu iliyoko katika utamaduni wa Mwafrika, kwa mtazamo wangu, vinatosheleza. Hakuna kitu kipya ambacho uislamu, ukristo au uyahudi unaweza kunifundisha. Kwanza amri kumi ambazo ni msingi wa dini hizi zinazoonekana kuwa ni "bora" zaidi ya nyingine zilikuwa Afrika miaka mingi kabla Musa, aliyesema kuwa kapewa mlimani na yehova, hajazaliwa. Ngoja nirudie ili usidhani nimekosea: NINASEMA KUWA AMRI KUMI "ZA MUSA" ZILIKUWEPO AFRIKA KABLA MUSA HAJAZALIWA! Ni kati ya amri 147 zilizokuwa zikitawala maisha ya Waafrika katika bonde la mto Nile (Misri ya zamani, Nubia, Ethiopia, n.k.).
Soma historia. Sio ile unayodanganywa shuleni na walimu waliodanganywa shuleni kama wewe na vyuo vya ualimu. Tafuta historia yeu.
Wakati dini yako inakupa amri isemayo, "Mpende jirani yako kama nafsi yako," utamaduni wa Afrika unakupa falsafa hii: Mtu sio mtu bila watu (Kwa Ki-Xhosa, "Umtu Ngumtu Ngabantu). Kwa maneno mengine tunaambiwa tupendane. Falasafa hiyo ndio inakupa ujamaa, harambee, n.k. Marasta wao wanakuja na dhana kama hiyo wanaposema, "I and I."
Unadhani kanuni ya mtu sio mtu bila watu imetoka kwa shetani?