3/20/2005

NIMERUDI: MAENDELEO NI SAYANSI

Nilipotea kidogo bila taarifa. Nilikabiliwa na mambo mbalimbali (safari, mikutano, ulezi, n.k.). Sasa nimerudi. Nina makala zaidi toka kwa Freddy Macha, Padri Karugendo na zangu. Nitaziweka. Pia kuna barua kadhaa toka kwa wasomaji ambazo nitaziweka hapa mzisome. Kuna mengi mapya, mishale ya sumu bado ninaikwepa. Waafrika tumepoteza kabisa nafsi zetu kiasi ambacho akitokea mtu kutuonyesha njia anaonekana kuwa ni adui. Tunataka kunyanyua mapanga kutetea manabii toka nchi za mbali huku tukiwa hatujui hata manabii toka kwenye vijiji vyetu. Kwanza huu ugonjwa wa akili lazima tuutafutie dawa. Ugonjwa wa kudhani kwamba Afrika nzima hakuna manabii. Manabii wanatoka tu Uyahudini na Uarabuni. Ugonjwa wa kudhani kuwa Afrika nzima haina maeneo "matakatifu" ndio maana watu wanatumia mamilioni kwenda kubusu jiwe Uarabuni au kuhiji Yerusalemu au Roma. Ugonjwa wa kudhani Abdalah ni jina la Kiislamu na George (ambaye huitwa Joji) ni jina la Kikristo. Ugonjwa wa kuamini hekaya za Kiyahudi kuwa dunia ilianza kati ya miaka 5000 - 7000 iliyopita. Lazima tukomeshe gonjwa hili baya kabisa linaloharibu akili na nafsi za Waafrika ambao hadi leo tumeshindwa kabisa kujitawala kutokana na kutojijua. Sirikali zetu zimejaa wezi. Wanachojua ni kuomba. Wanaita "misaada." Hivi sasa Afrika nzima viongozi wamejiunga na kwaya inayoimba pambio la "utandawizi" na "soko holela." Hawa nao lazima waondolewe. Bara limejaa huzuni. Ukimwi unatumaliza. Ujinga unaongezeka. Mauaji yasiyo na mbele wala nyuma yanasikika kila kukicha. Visima vinakauka. Watoto hawaendi shule kwa kukosa ada. Vifo vya magonjwa yanayotibika vinaongezeka. Umri wa kuishi unazidi kupungua. Ni tabu tupu. Ni kilio. Yote haya lazima yakome. Wako wanaodhani kuwa Afrika haitakaa iende mbele. Hawa ni wale wanaodhani kuwa maendeleo ni muujiza. Sio muujiza. Ni sayansi. Sayansi hii inaanza kwa kusafisha fikra zetu na kusafisha viambaza vya utawala vilivyojaa wezi ndani ya suti na majina ya kuazima. Kazi hii ni yangu na yako.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com