3/21/2005

MAENDELEO YA VYOMBO VYA HABARI

Vyombo vya habari vya Marekani vimeendelea sana kama vile vya Tanzania. Habari za vyombo hivi ni za muhimu sana kwa maisha ya binadamu. Kawaida, maendeleo ya vyombo vya habari yanapimwa kwa vigezo vingi sana, kimojawapo ni kutazama umuhimu wa habari zinazotolewa katika maisha ya binadamu kwa ujumla. Tazama habari kwenye gazeti kisha jiulize, hivi habari hii ndio iliyotusaidia tukajenga shule ya Mapinduzi ambayo jiwe lake la msingi limewekwa juzi? Je habari hiyo kama hatuna tutashindwa kupambana na rushwa kikamilifu? Je habari hiyo inasaidia binadamu waweze kuishi kwa utu zaidi?
Ukipima kwa kipimo hicho utajua kuwa vyombo hivi katika nchi za Marekani na Tanzania vimeendelea sana. Kwa mfano, dakika 35 zilizopita vyombo vya habari hapa Marekani vimetupa habari nzito kuliko zote katika siku hii ya leo. Habari hii ni muhimu mno. Umuhimu wake ndio umenifanya niseme ninayosema. Nimeamua nikugawie na wewe habari yenyewe kwani itakusaidia sana katika harakati zako za kupata elimu, kazi, huduma bora za afya, kutaka barabara nzuri hadi vijijini, na kudai uwajibikaji. Usipoipata, vyombo vya habari hapa vinatuambia, utakuwa umekosa jambo moja kubwa sana maishani. Vyombo hivi na vile vya Tanzania ni kama pacha. Sijui nani kajifunza kwa mwenzie.
Kila mtu nchi nzima (yaani Tanzania) anajifanya kuwa ni mfuasi wa hizi dini za kuja. Anajifanya kuwa anatii Amri Kumi za huyo mungu wake. Lakini Mtu huyo huyo habari anazopenda sana kuzisoma ni zile zinazohusu watu wanaovunja amri za mungu wake kuliko habari za watu wanaotii amri za huyo mungu. Ndio maana nikisema kuwa Tanzania watu hawana dini wengine mnanijia juu. Nadhani kuna faida fulani ya waislamu na wakristo kutokutii amri kumi wanazodai kuzifuata. Kama wangetii amri hizo nani, kwa mfano, angeua wezi? Wezi wangetumaliza maana wasingekuwa na woga. Hivi sasa wanaiba kwa woga maana wanajua kuwa mkiwakamata, ingawa dini zenu zinakataza msiue, lazima mtawaua. Mtawapiga hata kama hamna ushahidi. Mtawachoma moto. Kisha mtaondoka zenu kuelekea kwenye mazoezi ya kwaya, misa ya jioni, au sala ya alasiri. Mkifika huko mnadai mungu anasema katika Amri ya sita: Usiue.
Nadhani kuna mistari ilifutika kidogo katika amri hiyo. Labda karatasi ililoana. Mistari iliyofutika inasema, "Usiue labda awe kijana masikini mwizi wa elfu kumi. Wale wezi wa mamilioni, kwa jina langu, muwasamehe na kuwafanya wawe viongozi wenu. Wanayofanya ni mambo mazuri sana kiasi kwamba mnataka wao watangulie nyie mtawafuata. Wao ndio wanajua njia.
Na ile Amri ya Nane isemayo usiibe nasikia kuna maneno yaliyofutika pia. Ilikuwa inasema, "Iba ili mradi usikamatwe. Na ukishaiba usisahau kunijengea mimi bwana wa majeshi makanisa na misikiti kwa fedha hizo za wizi."
Mkristo au muislamu akienda kununua magazeti, kukawa na gazeti moja linasema, "Fahamu kurani na biblia inasemaje kuhusu vyakula vifaavyo kutunza hekalu (mwili) la bwana," na jingine linasema, "Kondomu zinazoongeza raha kwa mwanamke zagunduliwa." Unadhani watanunua gazeti jipi? Najua kwakuwa ni waumini wa dini mbili "kuu duniani" watachagua lile gazeti la mambo ya mungu wao. Je kama kuna habari kuhusu mjadala wa wabunge kuhusu muswada wa marekebisho ya katiba na gazeti jingine lina habari ya mbunge aliyekuwa amelala wakati wa mjadala huo, unadhani Watanzania wengi watanunua lipi? Acha kudharau Watanzania, yaani unafikiri wengi watanunua lenye habari ya mbunge kulala? Una maana pia kuwa hawatanunua habari kuhusu kurani au biblia bali habari kuhusu kondomu? Nakataa.
Narudi Marekani. Nilisema kuwa kuna habari imetokea dakika 35 zilizopita ambayo ndio namba moja kwa siku. Sitaki uikose. Nayo ni hii: MAIKO JAKISONI AMECHELEWA KWENDA MAHAKAMANI.
Huoni nisingekwambia maisha yako yangeharibika? Ndio kuendelea kwa vyombo vya habari.
Tafuta maana ya yote niliyosema. Au kulalamika. Kuna jamaa wanasema kuwa eti mimi napenda kulalamika na sio kuchambua. Tunatakiwa kulalamika. Tukilalamika wote itakuwa kelele. Kelele hiyo itamtoa chatu pangoni kwa woga. Kulalamika ni kupinga. Kulalamika ninakozungumzia hakuna maana ya kulia kama mtoto. Kulalamika kwa kuelimisha na kuamsha. Kwa kila lalamiko, maarifa. Kila lalamiko, historia. Kila lalamiko, ukweli. Kila lalamiko, falsafa. Kila lalamiko upinzani wa kitamaduni. Kila lalamiko, utaifa. Kila lalamiko, uafrika. Kila lalamiko, mwamko. Mapinduzi. Ya dhati.
Kila ninapoandika neno mapinduzi kuna watu akili zao zinakimbilia kwenye silaha. Sijui kwanini baadhi ya watu ni rahisi kufikiria silaha na vita namna hiyo. Yaani tutumie vita, tuangamize uhai, kwa ajili ya kutetea uhai? Mbona wanadamu tuna akili na maarifa tele ya kuondoa udhalimu wa njia na mikakati isiyohitaji silaha? Fungua vitabu vya historia. Fuata nyayo za waliokutangulia.
Wengine wakisikia neno mapinduzu wanaanza kufikiria idadi ya watu. Wanajiuliza, "Mapinduzi hayo ni lini wakati kila mtu amepotea? Itachukua muda gani watu wote kufumbua macho?" Usithubutu kufiria namna hiyo. Mabadiliko makubwa ya jamii huletwa na watu wachache ambao wanakuwa kama vile wa ugonjwa wa kuambukiza. Isitoshe kuna kanuni ambazo ni za wazi kuhusu jinsi ya kuleta mabadilikobila kumwaga damu, kuhitaji pesa, kuhitaji nguvu za dola, vyombo vya habari, n.k.
Wanaharakati wengi ninaoshauriana nao wanalalamika kuwa hawana uwezo wa kuwa na vyombo vya habari. Wanataka wapate chombo cha kuwasiliana na taifa zima. Ninawauliza mifano ya vyombo wanavyozungumzia, wanataja magazeti, redio, luninga, webu, n.k. Nawauliza, "Kuna chombo cha habari kikubwa kuliko mdomo? Kwa siku unasoma maneno mangapi na mangapi unasikia toka kinywani mwa mtu?" Nawaambia kuwa midomo yao na midomo ya wengine kama wao ndio vyombo vya habari.
Wengine wananiuliza, "Unajua kaka mimi nina mawazo mengi napenda wananchi wenzangu wayajue lakini sina upenyo wa kuyatoa. Unaweza kunisaidia nipate safu kwenye gazeti lolote?" Nawauliza kama wamehawai kuandika hayo mawazo yao yakasomwa na marafiki zao wa karibu, majirani, vijana wenzie kijiweni, wanafunzi wenzake, waumini, ndugu zake na hata wazazi wake. Wanasema kuwa hao watu watawasomaje wasipotolewa gazetini. Nawauliza, "Je masomo shuleni unaandika wapi?" Wanasema kwenye daftari. Hapo ndio tunakuwa tumefika kwenye kilele cha mazungumzo. Kama mtu anaweza kuandika mambo kwenye daftari na yakasomeka, kwanini asitafute daftari zuri akaandika hayo anayotaka kuandika magazetini ili waliomzunguka waelimike? Kwanini asubiri hadi apewe safu gazetini? Asipopewa safu mawazo yake ndio yanapotea? Je kila mwelimishaji lazima awe na safu ili mawazo yake yawe na faida kwa binadamu?
Anzisha safu ya mtaani kwenu. Kanunue daftari dukani. Andika, wape watu wasome. Mabadiliko ya nchi hayatokei ghafla. Ni mabadiliko yanayoanzia mtaani ndio yanayobadili taifa. Ni kitu gani kinakuzuia kufanya unayotaka kufanya kwa Watanzania wote kwa wakazi wa mtaani kwenu? Kwanini unataka kuanza na nchi? Taifa letu lina mtazamo wa ajabu kabisa wa maendeleo. Unaona tuliowachagua ndio huwa wanaamua maendeleo ni kitu gani. Sio tunawachagua ili watekeleze kile sisi tunachoamini kuwa ni njia ya kuleta maendeleo. Wanataka sisi ndio tutekeleze wanachoona kuwa ndio njia ya kumkomboa Mtanzania. Hii ni demokrasia ya kushushwa kama aya za manabii wanazotuambia wameshushiwa. Demokrasia ya kweli inaanza chini inakwenda juu. Ni pale mimi na wewe tunapoweza kufanya mwenyekiti wa mtaa atimize wajibu wake. Na aogope nguvu ya wana mtaa maana anajua kuwa asipotimiza kazi zake hatachaguliwa tena. Mkiweza kuwa na serikali ya mtaa inayofanana na sirikali kuu mnayoitaka, hapo ndipo mnaweza kuanza kuzungumzia kubadili mfumo wa sirikali kuu. Lakini kama mwenyekiti wa mtaa ni mzembe, mwongo, mbadhirifu, na mla rushwa na mnaendelea kumchagua maana anawapa pilau, usitarajie utaweza kuleta mabadiliko huko juu.
Nitaendelea...

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com