3/20/2005

TUNAWASUBIRI WAKOLONI...WAJE HARAKA!

Tarehe 15 mwezi huu nilipata barua ya kusisimua sana toka kwa msomaji wangu ambaye pia ni rafiki yangu, ndugu Mloyi. Aliniandikia baada ya kuandika makala kuhusu kurudisha wakoloni nchini Tanzania. Nilipoisoma nilimtumia rafiki yangu mwingine mpambanaji akaisoma. Akaniambia kuwa nilipoandika makala kuhusu kurudisha wakoloni, nilikuwa natoa dira. Na ndugu Mloyi katika barua yake anatoa mikakati ya utekelezaji. Kwa ruhusa yake ninaanika barua yake wazi muisome:

Ndugu Ndesanjo,
Kabla sijasahau kukuambia, jina langu jipya litakuwa Molly Newman...Je watalipenda? Ninaanza kujitambilisha kwa jina hilo hata kama nitafika miaka sabini bado nitakuwa Newman, New mpaka lini? Labda wapinzani wawaondoe (wakoloni) kwa ujinga wao. Wakoloni watalipenda sana jina hilo, nitatubu mbele kwamba sikujipa jina la zamani, nilipewa na wazazi wangu na watanisamehe kama walivyomsamehe Adam kwa makosa ya Eva au Samsoni kwa makosa ya Delila. Hawawezi kuniadhibu ambaye sikutenda kosa.

Nitakaa nao mbele ya mungu mpya, watajali mama yangu anakula nini. Najua wapigania uhuru waliwafukuza wakoloni kwa sababu walifungwa na nguvu za giza, wao lilileta nuru mpya waliikataa.Utakuwa kiongozi wetu wa maisha, mgombea uraisi wa maisha kwani chama chetu kitakuwa na nguvu ya kugombea uraisi miaka yote. Uhakikishe wakija wasitoke tena, ila ndugu zao wanaowategemea wabaki hukohuko ili waweze kuwatumia fedha kidogo toka kwenye ikulu yetu, maana tutakuwa tumeiga ukarimu wao. Hujui na sisi pia tutakuwa tunawapa misaada zaidi ya wanayotupa wao, kuliko tunavyowapa sasa?

Tutakuwa binadamu wapya wastaarabu na gentle. Tutakuwa tunajiandaa kuwa weupe kama theluji, dhambi zetu zitatakaswa ili tuingie mbinguni. Weupe sio kwa mkorogo bali kwa utakaso wa neno lililo jipya kuliko la wana wa Farao tuliokuwa tunawapenda. Nimejua sasa kwanini nchi hii bendera yake haina rangi nyekundu. Ni mpango wa mungu mkuu. Unajua Mkwawa , Mangi na wengine walimpinga mungu mkuu ndiyo maana walilaaniwa wasikumbukwe kwenye bendera yetu, na wote watakaopinga mpango wetu watasahaulika kama manyani ya porini yanavyosahaulika.

Ndesanjo, lakini jina lako litatutia doa kwanini usiwe Nesto McChair utakuwa na jina linalotamkika hata raisi mpya hata pata tabu kulitamka. Nimeanza mazoezi ya kusahau kiswahili, nimeanza kusahau kuandika maneno ya kiswahili, juzy niliposoma makaler yako ya pili niliona una waopposer wengi sana. Ila ulimi wangu unanitia aibu kila nikijaribu kuongea kama yule buruda wa sunday school, naona niuchonge kabla siku haijafika na weusi uminizidi, nitapata taabu sana kusema mimi ni coloured sio chotara. Nimenunua suti ila joto linanisumbua sana , ila inanibidi nivumilie tu maana najua ninachotaka. Usijali sana tutafanikiwa tu.

Unajua sisi wenyewe bila hawa ndugu zetu hatuwezi kufanya kitu, hata wote tukisoma darasa moja kuanzia nursery hadi college bado tunakuwa na mapungufu, sio wao. Si unaona? Mkapa ana degrii na Schwazeneggar hana lakini uongozi wa Schwaznegger si mzuri kuliko wa Mkapa? Nani anampinga Schwaznegger kama sio uroho wa madaraka tu? Utandawazi utakuwa mzuri kwetu siku hizo sio kama sasa, angalia wazungu waliompinga Bush, na wenye kumuita Kichaka wakome kabla sijawashtaki. Wote sasa wanamuunga mkono, Iraq inajengwa, Iran itakuwa civilized kuliko wote na sisi sasa tutatolewa kwenye viota tufundiswe kuishi kwenye nyumba za kisasa zenye viyoyozi na matanuru ya kuingiza joto, sio utani tunahitaji joto hapa Dar.

Unajua wakija hawa sasa tutapata vitu kwa bei nafuu sana kama bure, angalia kwao maisha yalivyo rahisi sio kama sisi, tutaendelea sana. Tunawasubiri waje watufumbue macho tumechoka kuishi kwenye vibanda. Wapinzani wakijua niko mstari wa mbele kuwapinga si watanitafuta waniue mpaka niombe msamaha na kujiunga nao! Je wewe hautakuwa karibu kunisaidia nisijeingia kwenye laana kuu ya kukataa weupe? Nao watakubali niteseke wakati ni mtu mzuri kwao? Je watakuja na mabinti zao? Tutawaoa kama wao watakavyooa wetu , si unaona South Africa, tutapata jamii ya machotara.

Watoto wangu watakuwa weupe kama theluji hawatahitaji kutubu dhambi maana hawatakuwa nazo kama babu zao upande wa mama yao. Watakuwa na huruma ya hali ya juu, kamwe hawatavumilia kuona watu wanateseka, wengine wanatupwa kwenye bahari waliwe na papa au wengine kwenye minyororo wanapelekwa kufanyishwa kazi. Dunia yetu itakuwa nzuri sana. Hakutakuwa na dhambi, hata malaya hawatakuwapo tena maana watakuwa wamepewa jina jipya zuri. Watanipenda sana hata kama nitapata ajali nikiwahi kufanya ngono nje ya ndoa watasema nilikuwa nakimbia paparazzi kama Diana.
Kwaheri.
***************************************XXX****************************************

Hapo ndipo ukawa mwisho wa barua ya Mloyi.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com