3/20/2005

MSOMAJI KANIAMBIA: YOU ARE A LEGEND "ON" YOUR OWN EYES

Kati ya wanaonirushia mishale ya sumu kuna bwana mmoja ambaye kama wengine anajificha nyuma ya mbuyu: hatoi jina lake halisi. Huyu bwana kaniachia ujumbe mara mbili kwenye kitabu changu cha wageni. Sijui kwanini kila mara anakuja kwenye blogu hii wakati anadai kuwa ninamkumbusha mwanafunzi wa kidato cha tano ambaye ndio wa kwanza kijijini kwao kwenda kidato cha tano na sita. Huyu bwana katumia Kiswahili na Kiingereza kunirushia mishale hiyo. Huenda alitaka kuonyesha kuwa naye yumo. Ndio wale wale. Unakuja kwenye blogu ya kiswahili, unaniandikia ujumbe mimi ninayeongea kiswahili unaingiza kiingereza cha hapa na pale. Labda alikuwa anaweka msisitizo maana kuna wanaodhani kuwa jambo likizungumziwa kwa kiingereza linakuwa na nguvu zaidi. Lakini jambo nisiloelewa ni hili: huyu bwana hiki kiingereza chenyewe kinampa tabu lakini bado anaking'ang'ania. Jamani, kwanini Waafrika tuko hivi? Ngoja niweke sentensi zake za kiingereza alizoniandikia na kumfundisha jinsi hii lugha ya watu wasiomthamini inavyotumiwa.
Maneno yake: You consider yourselves as legends, but you are legends on your own eyes.You reminds me of those form five students who were the first from their village to attend high school, and thterefore thought the journey ends there.
Uchambuzi wangu: kama ananizungumzia mimi basi hana haja ya kusema "yourselves" au kusema "legends." Pia sio sahihi kusema "you reminds," hakuna haja ya kuweka "s" kwenye neno "remind." Angeweka "s" kama angetumia He/She au It. Hii ni sawa na mtu kusema, "You goes to school." Halafu ni vyema kusema, "...a legend in your own eyes," yaani angetumia "in" badala ya "on," pale aliposema, "...legends on your own eyes."
Kama ningekuwa na anuani yake ningemwandikia ili iwe siri yake. Lakini kwakuwa sina anuani yake inabidi niweke hapa maana najua atarudi. Na pia kwakuwa hajaacha jina, hakuna atakayejua anayekosolewa ni nani. Kwahiyo huyo mtu asijisikie vibaya. Ningekuwa na anuani yake ningempa somo zaidi la lugha hii kutokana na makosa mengine kwenye ujumbe wake ambayo sina muda wa kuyajadili.
Kingine alichonishangaza huyu bwana ajifichaye nyuma ya mbuyu ni kuwa ameanza ujumbe wake kwa kusema, "Inaonekana waafrika wakioa wazungu au waarabu wanasahau uafrika wao." Nimeshindwa kuelewa anamzungumzia nani hapo. Kama ananizungumzia mimi basi nitapenda kumfahamisha kuwa mimi sijaoa mzungu au mwarabu. Kuhusu Waafrika kusahau Uafrika wao, kusahu huko kunaanza pale unapowasiliana na Mwafrika mwenzako ambaye mnazungumza lugha moja (Kiswahili), lakini unakimbilia Uingereza kwenda kuokota maneno ya kiingereza ya kuwasiliana na nduguyo.
Nitapenda kurudia kusema kuwa watu wanaonirushia mikuki ya sumu nimewapa uwanja. Badala ya kuweka mistari miwili, mitatu kwenye kitabu cha wageni au kwenye anuani yangu ya barua pepe, waandike kwa mapana na marefu hoja zao. Mpambano wa fikra ni mtamu sana. Hasa tunapokuwa tunazungumzia masuala ya nchi yetu na bara letu, utaifa, uzawa, utamaduni wa Mwafrika, ukoloni mamboleo, dini za uongo za kuja, ubeberu, umuhimu wa Kiswahili, haki za binadamu, n.k.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com