NINAKWEPA MIKUKI YA SUMU
Kuna mikuki ya sumu inarushwa kunielekea. Wako wanaorusha kwenye anuani yangu binafsi na wengine wanarusha kupitia kitabu cha wageni. Nadhani kuna hoja ninazotoa ambazo zinawaiingia baadhi yetu kama kisu cha machinjioni. Na kama ni hivyo, basi wajue hiyo ndio gharama ya kujikomboa. Ushauri ambao naweza kuwapa kwa sasa ili wasiwe na ghadhabu kama mkizi, ni huu: Kama kuna jambo hukubaliani nalo, jibu kwa hoja. Hoja kwa hoja. Hoja bin hoja. Nguvu ya hoja. Nipe nikupe. Hakuna mtu yeyote ambaye atanitumia chochote alichoandika kupinga au kusahihisha jambo lolote ninalosema nami niache kuweka wazi kila mtu asome. Kaa chini, andika, nitumie. Nitaweka hapa kila mtu asome. Nawapa uwanja. Kipenga kimelia. Kama kuna haja ya kujibu nitakujibu. Ninaheshimu uhuru wa mtu kutoa maoni. Awe anakubaliana nami au hakubaliani. Sitakutukana, au kutupa kazi yako uliyonitumia jalalani, au kukuita majina ya ajabu ajabu eti kwakuwa sikubaliani na unayosema. Nguvu ninayotumia sio ya misuli, sio ya matusi, sio ya vitisho, bali hoja. Hoja, falsafa, maarifa, elimu, historia...Nawe pambana nami kwa hoja, falsafa, historia, n.k. na sio vitisho au kutukana. Vitisho na maneno machafu ndio naita mikuki ya sumu. Hii nimeikwepa. Changamoto ninayotoa ni hii: usijifiche katika majina ya uongo na mistari miwili, mitatu ya vitisho au maneno machafu kwenye kitabu cha wageni au anuani yangu. Toka nyuma ya mbuyu tupambane kwa hoja. Toka nyuma ya pazia. Kama nimesema 1+1= 5, ukibisha usiseme tu: "Hujui unalosema. Funga mdomo." Hapo unakuwa unapoteza muda muhimu sana maishani. Kaa chini useme kwanini 1+1 sio 5. MMENIELEWA NINYI AKINA NANI HII? Kama mmetumwa, basi waambieni hao wanaowatuma wajipange tena vizuri. Nimeandika haya machache ila mnajua kuwa barua nilizowajibu nimeandika mengi zaidi.
Kuna baadhi ambao wameudhika kwa sababu ya hoja zangu za kisiasa. Hawa tuwaache kwanza. Kuna hawa wameudhika kutokana na maoni yangu kuhusu dini. Hawa ndio wana ghadhabu zaidi. Usiudhike. Bado hujasikia kitu. Ndio mwanzo tu. Kule Moshi enzi za kwenda sinema ukumbi wa Plaza pale Moshi mjini tulikuwa tukiwa na msemo huu, "Hiyo ni trela. Bado picha." Nami nawaambia ndugu zangu waumini wa dini za kuja. Nyie mnapotuita sisi tunaohubiri dini za asili au tusio na dini kabisa kuwa ni wapagani, makafiri na majina mengine ya ajabu, kwani tunawatishia au kuwatukana? Tunajipanga na kuja na hoja. Mnapohubiri na kusema kuwa watu wasioamini hivyo vitabu vyenu viwili watakwenda... sijui mnaita motoni, mbona hatupandishi jinamizi la hasira?
Salman Rushdie alipotumia haki yake ya kutoa maoni yake, mzee mmoja kule Iran akatangaza fatwa. Auawe! Kufuru hiyo! Baadhi ya waislamu Tanzania wakashangilia. Wakataka kitabu kipigwe marufuku kuingia nchini. Kikapigwa marufuku (ingawa kiliingia kwa njia za panya na nilikisoma wakati ule kilipotoka). Lakini sirikali ilipoamua kupiga marufuku kitabu cha Hamza Mustapha Njozi kiitwacho Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania (bonyeza hapa ukisome), waislamu hao hao walioshangilia kutolewa kwa amri ya kuuawa kwa Salman Rushdie na kupigwa marufuku kwa kitabu chake kuingizwa Tanzania, walinyanyuka wakitaka sirikali iruhusu kitabu hiki kuingizwa nchini na kuuzwa. Mkuki kwa nguruwe? Yaani kama kitabu kinaandikwa kinatetea dini yako unakuja juu na kutaka haki za binadamu na kikatiba ziheshimiwe, lakini kitabu kikiandikwa kikiwa na dalili za kupinga imani yako unakuja juu kutaka haki hizo zikanyagwe. Huu ndio tunaita unafiki wahedi. Lazima ukome. Tutaukomesha. Mtusomee ile mistari yenu mnayotumia kutishia watu au mkatusalie huko kwenye majumba ya ibada za unafiki...mfanye lolote. Hatutanyamaza. Kwenye wimbo wa Ride Natty Ride, kuna mstari Bob Marley anasema, "moto unawaka na hakuna wa kuuzima." Ndio kinachotokea hivi sasa. Vijana wanaamka. Wanafungua vitabu vya historia. Wanaongea na mababu zao kabla hawajaaga dunia na kuondoka na hazina ya maarifa. Wanatafiti. Wanaandika. Wanaimba. Wanatunga. Wanaongea. Kwenye wimbo mwingine wa Bob Marley wa Talking Blues anasema, "...sasa tunajua kuwa mhubiri anadanganya." Kweli tunajua hilo. Tunajua, kwa mfano, Kakobe alidanganya nchi nzima mwaka 2000 kuwa kaongea na Mungu. Tunajua mashehe ni waongo. Wanashika tasbihi na kuvaa kanzu na kupaka ndevu hina...wanachanganya uislamu na Uarabu. Uislamu ni unyenyekevu mbele za mungu, hauna maana ya kuiga utamaduni wa Kiarabu. Kuchukua majina yao, staili ya ya mavazi, n.k. Wote hawa wajue moto unawaka na hakuna wa kuuzima. Kwenye wimbo mwingine wa Jah Lives Bob Marley anasema kuwa uongo unaweza kuwa kosa la jinai ila sio dhambi. Kwahiyo mnaweza kwenda kule kwenye mchezo wa kuigiza katika ukumbi wa maonyesho kabambe uitwao bunge, mkaandika sheria za kufanya kusema ukweli ikawa ni kosa la jinai. Lakini mnaweza kuandika sheria ya kufanya ukweli kuwa ni dhambi?
Mimi nasema kitabu cha Salman Rushdie kisomwe na mtu yeyote. Kiuzwe kokote kule. Kitabu cha Njozi kisomwe na yeyote. Kiuzwe Tanzania nzima na hata dunia. Hakuna sababu ya kuzuia vitabu hivi viwili. Bonyeza hapa usome kitabu cha njozi.
Kwahiyo kuna watu hawajazoea kupingwa kwa hoja. Wanataka tu watangaze "ukweli" wao, wakisikia ukweli tofauti na ule wao ulioletwa na majambia na bunduki wanakuja juu. Tuwapa hoja mishipa inawatoka kwa hasira. Tulieni. Ndio mwanzo wa safari ya ukombozi. Kuna watakaolia, kuna watakaoacha midomo wazi kwa mshangao, kuna watakaoshangilia, kuna watakaogutuka, n.k. Tutambue kuwa ukombozi wa nchi na bara letu, iwe ni kwenye nyanja ya uchumi, siasa, michezo, elimu, jamii, sanaa, n.k. lazima uanze kwanza kwenye fikra. Usiende mbali sana. Usianzane na mimi. Usikimbilie kwenye vitabu sijui vitakatifu na vitukufu. Anza kwenye fikra. Anza na wewe binafsi. Fikiria nje ya kasha. Fungua kasha, toka nje. Weka matundu, chungulia nje. Kasha halina kufuli. Mlango uko wazi, wewe tu hutaki kutoka. Kwanini unang'ang'ania kukaa ndani? Ukweli sio ukweli kwakuwa eti watu wengi wanaufuata. Ukweli ni uweli. Hata kama hakuna binadamu yeyote duniani anayeufuata, ukweli unabaki kuwa ukweli. Usiogope kuhoji mambo. Hoji kila kitu. Hoji kila mtu. Hoji dini. Hoji itikadi. Hoji elimu. Hoji historia. Hoji maandiko. Hoji. Ndani ya kasha mmebanana sana. Huoni tabu ya kuhema? Toka nje, jinyooshe, tazama jua, Uko huru. Huu ni wakati wa fikra sahihi. Mtazamo sahihi. Matendo sahihi. Bila fikra sahihi mwili wako unakuwa tu kama gurudumu la gari ambalo linakwenda kule mwendesha gari anakotaka.
Kwa wale wanaoniandama kutokana na makala zangu za hivi karibuni za siasa, nina maneno machache ya kuwaambia: Ujumbe ninaoutoa katika hoja yangu ya kutaka Tanzania itawaliwe tena ni sawa na msemo wa Yesu aliposema, "Nimekuja ili wawe na macho ila wasione. Wawe na masikio, wasisikie..." Hoja yangu hii ya kutaka wakoloni ni fumbo. Werevu wameshafumbua siku nyiiiingi.
0 Maoni Yako:
Post a Comment
<< Home