3/09/2005

NIMTUME NANI? - II

Huu ni muendelezo wa Nimtume Nani sehemu ya kwanza ambayo sikuimaliza maana nilirukia kwenye mambo mengine. Nilikuwa nauliza kwa niaba ya mungu: Nimtume Nani? Swali hili linasubiri majibu huko mbinguni. Mwaka 2000 alitumwa Kakobe. Alitumwa na mungu wake anayempa uwezo wa kuponyesha watu ila hampi busara za kwenda kuponyesha mahospitalini badala ya kuwasubiri waende kanisani kwake, ambako pia hupeleka sadaka. Tena ili sadaka ziwe nyingi, waumini wake hawatakiwi kupanda mabasi maana nauli itapunguza mshiko wa mungu.
Unajua zamani nilikuwa nikiamini kuwa ni kweli sadaka zinakwenda kwa mungu. Eti wanasema, "Mtolee Bwana." Wewe nani kakwambia mungu anataka pesa? Kama mungu alikuwa anachukua hizo pesa vitambi na magari ya kifahari ya "watumishi" wa mungu vingepatikanaje? Bila kusahau misalaba mikubwa mikubwa wanayovaa shingoni...sijui inauzwa wapi. Nami nataka wangu. Si tuliambiwa kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe? Kuna walioelewa kuwa Yesu alimaanisha ubebaji wa msalaba ndani ya nafsi zetu, na wengine wakadhani ni kubeba misalaba juu ya kifua. Wahubiri misalaba yao ni mikubwa zaidi ya waumini kumaanisha kuwa wao ni wateule wa mungu.
Nimtume Nani? Mungu wa Waisraeli auliza.
Kwanza, hivi Watanzania wanahangaika na nini na Mungu anayesema kuwa wateule wake ni Waisraeli? Au wewe ndugu yangu Mbena, Mnyaturu, Mmasai, Mkinga, Msukuma, Mchagga, Mzanaki, n.k. umeshakuwa Muisraeli? Kwani si tunaambiwa kuwa Waisraeli hawa wana makabila 12 tu ambayo ndio yenye viti mbinguni na idadi yake, 144,000, imetajwa kabisa kwa mujibu wa kitabu kisichoeleweka vizuri cha Ufunuo? Usishangae idadi ya wateule kuwa ndogo hivyo, njia ya kwenda kule tumeambiwa na watu ambao hawajawahi kufika huko na hawatafika kuwa ni nyembamba! Hivi wewe kabila lako katika 12 ya wateule wa mungu ni lipi? Lazima utakuwa na makabila mawili, la kuzaliwa na hili la kujipenyeza.
Najua Tanzania kuna makabila zaidi ya 120, mbinguni viti ni vya makabila 12...mbona kutakuwa na kasheshe hapo? Mambo ya kuingilia miungu wa wengine na kumtupa wako yatatutokea puani. Amri ya kwanza inasema usiwe na miungu wengine ila mimi. Haiishii hapo. Sababu ya kuwa na mungu huyo na sio wengine inatolewa: "... maana nilikutoa utumwani Misri...."
Huyo mungu hapo haongeni nami maana ninajua historia ya watu wangu. Hatujawahi kuwa utumwani Misri. Lazima anaongea na watu wengine. Jamani, Wachagga tumewahi kuwa utumwani Misri kisha Yehova akatupeleka nchi ya ahadi? Labda makabila mengine Tanzania. Ila Wachagga nimesoma historia yao hatujawahi kuwa na mtu anaitwa Musa. Kwanza jina hilo sio la Kichagga.
Nimtume Nani? Mungu wa wayahudi anauliza. Mwaka 2000 alimtuma Kakobe kutuambia kuwa Mrema atakuwa rais. Uchaguzi ukafanyika Mrema akashindwa vibaya sana. Ahadi ya mungu kupitisha mtumishi wake aendeshaye gari la kifahari huku waumini wake wakitakiwa kutembea kwa miguu haikutimia. Huenda shetani aliingiza mkono wake kwenye uchaguzi. Ndio hoja ya baadhi ya watu. Wanasema, "Shetani anafanya kazi usiku na mchana kuharibu kazi ya mungu." Kwahiyo shetani alitumia wezi wa kura kuharibu unabii wake. Kama nitakubaliana na hoja hii, itabidi nikubali kuwa shetani ana nguvu kushinda mungu maana anaweza kuzuia ukamilisho wa ahadi/unabii wa mungu kwa wanadamu.
Mwaka huu atatumwa nani? Pengo? Sidhani. Pengo anaongoza kanisa linalodai kuwa bikira Maria alikuwa bikira maisha yake yote wakati alizaa watoto (nduguze Yesu). Hawezi kutuma waongo. Pengo yuko kwenye kanisa linalokataza wanawake kuhubiri. Hawezi kutuma wabaguzi wa kijinsia. Pengo yuko kwenye kanisa linalokataza wanaume kuoa na kuwaacha waharibu watoto wadogo wanaopamba mimbara za kanisa. Hawezi kutuma wanaoshindana na kanuni za maumbile na baiolojia.
Au atatumia kanisa la Kiluteri? Majuzi maaskofu wa Kiluteri wametwangana makonde. Kanisa liko kwenye mgogoro mkubwa kuhusu uongozi, mali, teolojia, n.k. Hakuna mtu mwenye nafasi ya kutumwa. Kanisa la Kiluteri linadai kuwa kuna kitu kinaitwa dhambi ya asili...uongo mkubwa huu.
Au labda safari hii atatumwa Muislamu.
Jamaa mmoja kaniambia kuwa tayari mtu keshatumwa. Tena Shekhe. Shekhe Yahya Hussein. Mtabiri mkuu Afrika Mashariki na Kati. Kasema rais mpya atakuwa ni binadamu. Atakuwa na upele (alimaanisha chunisi?). Atachaguliwa Oktoba mwaka huu. Atakuwa na nywele. Atazunguka nchi nzima kupiga kampeni. Atakuwa anajua kusoma na kuandika (basi hatakuwa Mrema!). Atakuwa anapenda kuvaa vizuri....utabiri mkali kweli huu!
Shekhe Yahya huwa ananifurahisha pale anaposema, "Kutakuwa na migogoro ya kisiasa huko Mashariki ya Kati." Jamani, kama huo ni utabiri basi hata mimi basi ninaweza kuwa mtabiri. Ngoja nitabiri: Waafrika wengi watakufa kwa ukimwi, kutakuwa na mgogoro wa kisiasa Lebanoni, Tanzania itafanya uchaguzi mwaka huu, Zanzibar kutakuwa na ghasia za hapa na pale, Marekani itaendelea kuikalia Iraki, Irani na Marekani zitagombana, uhusiano wa Korea ya Kaskazini na Marekani hautakuwa mzuri, "Babu" wa Mlingotini atakuwa na wageni wengi kabla ya Oktoba, wakulima Tanzania wataendelea kutumia jembe la mkono mwakani, Tanzania, Kenya, na Nigeria zitatawaliwa na rushwa...
Swali letu: Nani atatumwa mwaka huu? Kakobe ameshasema akitumwa tena hakubali. Hataki tena kurudia aibu ile ya 2000.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com