3/07/2005

NIMTUME NANI?

Mwaka 2000 alitumwa Mhubiri Kakobe. Hatujui kilichotokea. Hatujui kama mungu alibadili mawazo akasahau kumwambia Kakobe au kutuma mtumishi mwingine. Hatujui kama Kakobe hakusikiliza ujumbe kwa makini. Tunachojua kwa uhakika wa asilimia 600 ni kuwa Augustine Lyatonga Mrema hakuwa rais wa Tanzania.

Nakumbuka nilikutana na wananchama wa TLP wakaniambia kuwa Mrema atakuwa rais. Nikawauliza, "Mmejejuaje?" Wakasema kuwa Kakobe ametangaza. Na kwa kuwa Kakobe ni mtumishi wa mungu mwenye miujiza mingi, lazima ana mawasiliano ya moja kwa moja na mungu. Na mungu huyo ambaye anaponyesha wagonjwa pale Mwenge, jijini Dasalama huku wagonjwa wa matatizo ya akili wakiteseka Muhimbili...wagonjwa hawa kwakuwa wanaumwa akili hawawezi kuamua kwenda kwa Kakobe. Kwanza wengi wao wanaamini kuwa sio wagonjwa. Sasa unawategemea watafunga safari hadi Mwenge kutibiwa? Kutibiwa nini wakati wanajua kuwa ni wazima?

Unajua hawa watu wanaojifanya kuponyesha kwa miujiza wananishangaza sana. Mhubiri anatoka Marekani hadi Tanzania kuponyesha wagonjwa. Anakwenda kufanya miujiza hiyo Dasalama. Badala ya kwenda hospitali ya barabara ya baharini (Ocean Road) ambako kuna wenzetu wanaumwa kansa na wanasubiri kuaga dunia. Anakwenda ukumbi wa Diamond Jubilee utafikiri kuna onyesho la Twanga Pepeta.

Badala ya kwenda muhimbili ambako wagonjwa wanateseka bila dawa, anakwenda viwanja vya Jangwani wakati muhimbili ni mwendo wa dakika kumi kwa miguu mwendo wa haraka toka Jangwani. Anatoka nchi ya mbali anaenda kuhubiri kwenye kiwanja ambacho wengi waliokwenda hapo hawahitaji kuponywa magonjwa.

Najua hoja wanayotumia kujibu hili, wanasema kuwa mtu akiwa na imani atakwenda katika eneo kwenye miujiza. Imani inayowapeleka hapo ndio inawaponyesha.

Kuna majibu mawili ya haraka ya hoja hii. Kwanza, kama mtu anaponywa na imani yake hahitaji mtu kutoka Marekani kumponyesha maana dawa ni imani yake mwenyewe na sio ya mtu mwingine. Na imani yake haiko mikononi mwa huyu mhubiri anayejifanya kuponyesha. Imani anayo nafsini mwake. Kwahiyo mponyaji wake hatoki Marekani bali moyoni mwake.

Hoja yangu ya pili ni kuwa kama mtu mwenye imani ndio anaponyeshwa, je kichaa anaweza kuponyeshwa kwa jina la Bwana? Kwani kichaa anaweza kuelewa maana ya kuwa na imani? Anaweza kuelewa maana ya kuombewa? Kwanza kitendo cha kuwa kichaa kinamfanya asijue kuwa anaumwa.

Na watoto je? Watoto wachanga walioko hospitali wanatakiwa kuamka kwenda viwanja vya Jangwani? Au kama wazazi wao hawana imani basi watoto hao wanatakiwa wabaki na magonjwa yao na kuteseka kwa makosa ya wazazi? Lakini Bwana anayeponyesha sio ndio alituambia kuwa kama hatuna imani kama watoto hatutaingia ufalme wake? Si yeye alisema kuwa ufalme wa Bwana ni kwa ajili ya watoto? Sasa mhubiri anapokwenda Tanzania toka nchi ya mbali kama Marekani kisha anaacha kwenda kuponyesha watoto katika wodi za watoto zisizo na dawa za kidunia, tumwelewe vipi? Kwani Jangwani kuna nini? Wagonjwa si wako hospitali? Wameshaomba ruhusu toka serikalini kwenda kuponyesha mahospitalini wakakataliwa? Kwanza wahubiri wanatoa huduma za "kiroho" hospitalini. Kwahiyo haitakuwa mara ya kwanza kwao kwenda kuombea wagonjwa kule waliko.

Tunataka tuamke siku moja tuone kwenye vichwa vya habari vya magazeti:
1. WAGONJWA WODI YA VICHAA WAPONYWA WOTE KWA UWEZO WA MUNGU
2. WODI YA WATOTO YABAKI TUPU: NI BAADA YA MHUBIRI TOKA MAREKANI KUWAOMBEA KWA JINA LA BWANA ALIYE MKUU

Nilikuwa nauliza juu ya atakayetumwa mwaka huu. Nimerukia mambo kibao. Naona nikae chini niandike kabisa makala ndefu juu ya hoja ninazojenga hapa. Au mnaonaje?

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com