3/07/2005

TUWARUDISHE WAKOLONI

Jamani,
Mkiniona Bwagamoyo msishangae. Nitakuwa nafuatilia kizizi kwa "Babu." Unajua tena hii ndio ile miezi yenyewe. Toka sasa hadi Oktoba, "Babu" na watu wengine wanaojiita Masharifu watakuwa na kazi nzito sana. Ila "Babu" wa Mlingotini ndio ana kazi kubwa zaidi.

Kutokana na uchaguzi kukaribia, watu wengi wanakwenda kwa "Babu" Mlingotini ili wapate kizizi cha kushinda uchaguzi. Watu kama hawa wanakwenda kwa ajili ya faida zao binafsi. Mimi ninakwenda kwa sababu tofauti. Ninakwenda kwa faida ya umma. Ninakwenda kwa faida yako wewe Mtanzania. Ninakwenda ili kampeni yangu ya kubinafsisha ikulu na kurudisha wakoloni ifanikiwe. Hakuna kitu tunachohitaji Tanzania na Afrika kwa ujumla zaidi ya wazungu wa kututawala.

Tuamue tu kimoja iishe.

Unajua watu wengi hatujui faida za ukoloni. Ukoloni ulitusaidia sana. Uhuru wa nchi za Afrika ulikuwa ni kosa kubwa sana. Ngoja nikutajie faida za ukoloni: bila ukoloni usingekuwa na jina ulilonalo, bila ukoloni usingekuwa na dini uliyonayo, bila ukoloni usingejua kiingereza ambacho unakipenda sana kuliko hata lugha ya watu wako, n.k. Nadhani unaona mwenyewe.

Kama sio ukoloni usingekuwa unamjua mungu wa kweli hata kidogo. Ungekuwa bado unaamini imani za mababu zako ambazo ni za kishenzi. Kama sio za kishenzi lazima ungezifuata, na kama zimefichwa ungezitafuta. Si unaona huzifuati? Jibu sio gumu: imani hizo ndio za kishenzi na wewe hupendi mambo ya kishenzi. Imani za kuabudu mawe uhangaike nazo ya nini?.

Wakoloni lazima tuwashukuru sana. Daima. Bila wao ungekuwa una jina la ovyo kabisa. Jina lako linaloitwa la "kinyumbani" au "utoto" lingekuwa ndio jina lako rasmi. Si unakumbuka ulivyokuwa unalia au kutaka kupigana ukiitwa jina la "kinyumbani" au "utoto"? Bila wakoloni, ukipata mtoto ingekubidi umpe majina ya kishenzi waliokuachia waliokutangulia. Ungewapa heshima kubwa mababu zako kuliko mababu za wengine. Lakini kutokana na wingi wa rehema wa Wamisionari, walitushawishi hadi tukaamua kuenzi mababu zao vizazi hadi vizazi. Majina ya Kiarabu na Kiuropa ni majina ambayo wao wamerithi toka kwa mababu zao. Ila unajua mababu zao walikuwa wastaarabu na mababu zeti walikuwa washenzi sana.

Kwa ufupi, ukoloni unakupa nafasi ya kumpa mwanao jina zuri kabisa la Kiarabu.

Najua walitudanganya wakatuambia kuwa majina hayo ni ya kidini, yaani ya Kiuropa ni ya kikristo ingawa Yesu hakuwahi kuishi Uingereza, Italia, Ujerumani, Ureno, au Ufaransa. Wala hakuwa anaongea lugha ya nchi hizo.


Wakatuambia pia kuwa majina ya Kiarabu ni ya kiislamu wakati ambapo majina hayo yalikuwepo kabla hata Muhammad hajazaliwa. Kwahiyo Waarabu walikuwa na majina hayo hata kabla hawajaanza kuita jina la Allah. Kabla hakujawa na kitu kinaitwa Uislamu, kwa maana ya dini. Kurani ilikuwa "haijashushwa." Hakukuwa na watu ambao waliuita Uislamu tunaoujua leo kama dini yao, lakini walikuwa na majina ambayo leo unayaita ya kiislamu.
Lakini hakuna ubaya kudanganywa kama jambo lenyewe ni zuri. Mimi mtu akinidanganya lakini nikafaidika kwa namna moja au nyingine na uongo huo, sijisikii vibaya. Ndio maana nafurahi sana wakoloni walivyokuwa wanatundanganya kama watoto. Maadamu kulikuwa na faida za kukubali kudanganywa, naona walifanya jambo sahihi. Kwa mfano huu uongo kuhusu majina. Mimi naona majina yao ni mazuri sana. Yanatamkika vizuri, ladha mdomoni, na yana hadhi ya juu. Kwahiyo naona afadhali walitudanganya. Ndio maana ninawaambieni, tuwarudishe. Tena haraka sana. Tunawarudisha polepole mno hivi sasa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com